Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI ya Mwaka: Heri za Mlimani
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanapaswa kutambua kwamba, wana heri kwa sababu wao ni watoto wateule wa Mungu. Heri za Mlimani ni chemchemi ya furaha ya upendo aminifu wa Mungu inayobubujikia maisha ya waamini! Hii ni furaha endelevu ambayo hakuna mtu wala mazingira yanaweza kuwapokonya wateule wa Mungu. Katika Zab. 49:16- 18 tunasoma neno hili, lakini Mungu ataiopoa roho, atanichukua kutoka kuzimu. Usihangaike, ukimwona mtu anatajirika, mali za nyumba yake zikiongezeka. Kwani atakapokufa hatachukua hayo yote, wala mali zake hazitashuka pamoja naye. Katika masomo yetu ya leo tunaona pengine jambo au wito ambao si rahisi kuamini au kuelewa – heri maskini na ole wao matajiri.
Tofauti kati ya Mwinjili Luka na Mwinjili Mathayo katika Mafundisho ya Heri za Mlimani ni hivi: Mathayo anawaandikia Wayahudi Wakristo haja ya mtazamo mpya, juu ya Ufalme wa Mungu, haja ya badiliko la akili na moyo, habari juu ya ufalme wa Mungu. Luka, mwongofu mpagani anaandika kwa ajili ya waongofu wapagani, watu waliookoka, maskini na watu wa kizazi cha chini. Watu hawa anaowaandikia Luka waliuchagua ukristo na wakapata mateso zaidi. Katika somo la kwanza tunaona au kusikia ole wake anayeweka matumaini yake kwa watu. Mwandishi anatambua uwepo wa ufalme wa Mungu na mwisho wa nyakati na haja ya kutoa majibu. Ufahamu huu unatuwajibisha na kutualika kuutafuta. Mwandishi wa somo la pili anatambua uwepo wa vitu hivyo na haja ya kuwa navyo lakini anatukumbusa haja ya kutambua kuwa ni kwa ajili ya matumizi tu na si mwisho wa yote.
Mtume Paulo katika 1Tim. 6:17 – anaandika - ‘uwaonye matajiri hapa duniani wasijidai, wala wasitegemee utajiri usio salama, bali wamtegemee Mungu atupaye vyote kwa wingi ili tuvidumishe.’ Mtume Paulo anatuangalisha na hatari ya mali. Mt. Jerome anasema ni tajiri wa kutosha yule aliye maskini katika Kristo. Ushuhuda huu ni mkubwa sana kwani Kristo ndiye mwana mrithi wa Mungu aliye Muumba wa yote na yule amfuataye Kristo atapata yote yaliyo yake Mungu. Ndugu zangu dhana ya heri/utajiri/mali/furaha na/au umaskini inaweza ikapata maana na sura mbalimbali pengine kadiri ya mila, desturi, mahali na wakati na pengine mahitaji ya watu.
Mtazamo huu unaweza pia kugusa uelewa wetu juu ya utajiri na umaskini wa kiroho. Katika injili Matayo tunasikia habari juu ya heri, heri maskini wa roho – Mt. 5:1. Tukisoma mahali pengine katika injili tunasikia habari ya jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia mbinguni – Mt. 19:16-30. Je utajiri na umaskini wa kweli ni upi? Biblia yatuambia nini? Jibu la kibiblia kuhusu utajiri wa kweli liko wazi. Tajiri wa kweli na mwingi wa fadhila ni Mungu Baba peke yake. Yote tuliyo nayo yatoka kwake na ni mali yake. Kwa tabia ya kibinadamu kila mmoja wetu angetamani kuwa na vitu zaidi na pengine kwa ajili yake mwenyewe. Kila mtu anatafuta au kutaka kupata furaha. Ila njia ziko tofauti. Kwa uhakika ulimwengu una majibu tofauti kuhusu furaha ni kitu gani na ole ni kitu gani. Pale Yesu asemapo heri maskini wa roho, ulimwengu ungesema heri walio tajiri na ole wao maskini. Kama ingeundwa kamati kulinganisha kati ya heri zake Yesu na heri za ulimwengu tungepata majibu ya ajabu na yanayotofautiana kabisa.
Mwandishi mmoja kwa jina Anon anasema kama huna au huwezi kuwa na kila kitu, basi tumia vizuri kile ulichonacho. Hili ni fundisho fupi na lenye maana kubwa. Mungu ametuumba kwa mfano na sura yake. Sisi ni warithi pamoja na Mwanae. Hakuna heri kubwa zaidi ya nafasi hii aliyotujalia Mungu kwamba sisi ni warithi wa ufalme wa Mungu pamoja na Mwanae. Kinyume chake ni ole. Furaha ya kweli kama anavyotaka Yesu ni ile ya kuurithi uzima wa milele. Neno lingine mbadala wa furaha ya kweli na inayodumu ni heri. Ni hali ya kimbingu ambayo ulimwengu hauwezi kutoa. Hii hupatikana tu kama tukipata fadhila za kimbingu. Hizi heri katika injili ya leo ni mwongozo wa kufika mbinguni.
Kadiri ya Biblia, umaskini huonekana kama njia ya kumtumainia Mungu na si kitu cha thamani kwa chenyewe jinsi kilivyo. Yer. 17:5 – ‘ole wake mtu anayemwaninia mwanadamu, aliyemfanya mtu kuwa tegemeo lake.’ Ieleweke wazi kuwa lengo la Luka katika heri au uelewa wake uko kwenye hitimisho la heri ya mwisho – kwa ajili ya mwana wa mtu. Kwa uelewa huu, wale watakaofuata mambo yao na si wito wa Mwana wa Mtu basi watakuwa wamepotea. Hatari inayojitokeza hapa ni kule kuona mali kama mwisho wa kila kitu. Hatari ya mali au kukumbatia mali na Mungu anafuata baadaye.
Tunaambiwa kuwa fundisho hili la Yesu katika injili ya Luka litaeleweka tukielewa hali ya maisha ya wakati ule Mwinjili Luka akiandika Injili hii. Luka aliandika Injili wakati wa mateso ya kijamii na kidini ya wakati ule yaliyowakuta wafuasi wa kwanza wa ukristo. Aliyeongokea ukristo alipoteza hata hadhi ya kifamilia, mali yake ilifilisiwa na kutengwa na sinagogi. Mmoja alipoteza haki ya urithi na ushiriki huru katika jamii. Kwa hali hii wengi ya wale waliotaka kuwa wakristo waliuza kwanza mali yao yote ili wasinyanganywe na viongozi dhalimu. Kama tungesoma sehemu iliyotangulia injili ya leo tungesikia habari juu ya wito wa wale kumi na wawili – Lk. 6:12-16. Mwandishi mmoja anasema wewe ungejisikiaje kama ungeitwa wakati huu ambapo wakristo wanapata mateso mengi, hata kupoteza mali yao? Bila shaka ndipo katika mazingira kama haya Yesu anasema; Lk. 6:20-23 … wenye heri ninyi mlio maskini …
Kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele cha ‘Ufunuo’ tunaambiwa kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, aweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Hakika fundisho hili lamtaka mwanadamu kuutambua ukuu wa Mungu na uweza wake. Hakika yule anayefahamu hilo basi katika maisha yake atakiwa kumchagua Mungu. Kwa kutumia akili aliyojaliwa na yenye uwezo wa kujua na kufahamu basi anaweza kumchagua huyo ambaye ni asili na chanzo cha utajiri wote na heri ya kweli.