Tafuta

Sifa kuu za Nabii: Kuitwa na kutumwa na Mungu; Pili, ni jukumu zito na nyeti! Tatu: Uhakika wa uwepo wa Mungu katika maisha na utume huu! Sifa kuu za Nabii: Kuitwa na kutumwa na Mungu; Pili, ni jukumu zito na nyeti! Tatu: Uhakika wa uwepo wa Mungu katika maisha na utume huu! 

Sifa kuu za Nabii: Kuitwa, Kutumwa na Kupambana kweli kweli!

Sifa kuu za Unabii: Kuitwa na kutumwa na Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Nabii Yeremia. Pili: Unabii ni wito mzito unaoweza kumweka mtu hatarini hasa kwa kutangaza na kushuhudia ukweli. tatu: Unabii una changamoto pevu, lakini daima Mwenyezi Mungu yupo kati pamoja na watu wake wanapomlilia anawasikiliza na kuwategemeza!

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. – Vatican.

Masomo yetu ya dominika hii ya leo, yanasisitiza juu ya nafasi ya nabii katika kufikisha Nano la Mungu kwa watu.   Katika somo la kwanza, Nabii Yeremia anatusimulia jinsi alivyopata jukumu la kuwa nabii. Tunaona mambo muhimu matatu katika maisha yake. Jambo la kwanza, Yeremia hakujituma mwenyewe wala hakutumwa na mtu mwingine bali alitumwa na Mungu mwenyewe. Hili linadhihirika pale ambapo Mungu anasema, “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua…. nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa… ukawaambie maneno yote niliyokuamuru.”

Kumbe wito wa unabii, kama jinsi ilivyo miito mingine, hutoka kwa Mungu mwenyewe. Wito fulani si mastahili ya mtu binafsi bali ni zawadi itokanayo na upendo wa Mungu mwenyewe. Kwa kuwa nabii anatumwa na Mungu basi anapaswa kuwa na uhusiano wa pekee na Mungu. Anapaswa kumsikiliza Mungu ili kwamba ujumbe atakaoupeleka kwa watu usiwe ujumbe wake binafsi bali ujumbe wa Neno la Mungu. Kabla ya kumtuma, Mungu alimtakasa Yeremia, yaani alimtakatifuza, akamtia wakfu kwa ajili ya kufanya kazi hiyo maalum ya unabii.

Jambo la pili, jukumu la Unabii si lelemama, ni jukumu gumu na lina uzito wake. Mungu alimtahadharisha Yeremia na kumtaka ajifunge mkanda ili kukabiliana na upinzani mkali. Wakati Yeremia anatumwa na Mungu kuwa nabii, utawala wa Kaskazini yaani Israeli ulikuwa umeshaanguka kutokana na mashambulizi ya Mfalme wa Assiria. Kadhalika, katika utawala wa kusini yaani Yuda kulikuwa na maanguko makubwa ya kimaadili na kidini mbali ya juhudi kubwa za wafalme Ezekia na Yosia za kuleta marekebisho. Katika mazingira haya Yeremia anawakaripia watu kumuasi Mungu, rushwa, ukiukwaji wa haki katika jamii na juu ya manabii wa uongo. Haikuwa rahisi kwa watu hao kupokea ujumbe wa Mungu kupitia nabii Yeremia. Yeremia hakusita kusema ukweli japo alipata upinzani mkali na mateso hata kwa ndugu zake wa karibu.

Jambo la tatu, Mungu kwa kumpa jukumu la unabii alitambua changamoto zilizopo ikiwa ni pamoja na hatari ya kupoteza maisha. Ndiyo maana Mungu anamhakikishia kuwa atakuwa naye. Mungu anamhakikishia hili kwa kumwambia, “Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe ili nikuokoe”. Ndiyo ahadi anayompa yeyote ambaye yuko tayari kuifanya kazi ya Mungu.

Nguvu ya Historia ya maisha ya nabii Yeremia inajirudia katika maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika utume wake hapa duniani alitambua kuwa alitumwa na Baba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Dominika iliyopita tulimsikia Yesu akilitambua hili pale aliposema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri masikini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao…”. N amara nyingi Yesu alibaki na uhusiano wa karibu na Mungu Baba na ndiyo maana anadiriki kusema, “…neno mnalolisikia si neno langu bali la Baba aliyenituma.” (Yohane 14: 24). Yesu hakusita kufikisha ujumbe wa Mungu kwa watu hata kama kufanya hivyo kulimgharimu maisha yake.

Leo tumesikia katika Injili kwamba akiwa ndani ya sinagogi la kijijini kwake, kati ya kati ya watu wanaomfahamu, anapata upinzani mkali, hawakubali maneno yake na zaidi sana wanampeleka mpaka ukingoni mwa kilima, wapate kumtupa chini kwa lengo la kumuua ili asirudi tena katika mitaa yao. Upinzani huu alioupata mwanzoni mwa umisionari wake hapa duniani ulikuwa ni utangulizi wa matukio mengi ya upinzani aliyoyapata katika utume wake hadi kufa Msalabani.

Nguvu ya unabii inaonekana pia katika somo la pili ambapo mtume Paulo anawafikishia waamini wa Korintho ujumbe wa Injili ukilenga katika kushughulikia tatizo kubwa lililokuwepo katika jumuiya hiyo changa ambayo aliianzisha mwenyewe. Karama na vipaji mbalimbali walivyokuwanavyo waumini hao vilikuwa ni chanzo cha migogoro, mivutano, utengano, ubaguzi na kuvunjika kwa umoja ndani ya jumuiya hiyo. Katika kupinga hali hii Dominika iliyopita tulimsikia Paulo akiwaasa waumini hao juu ya umuhimu wa umoja na ushirikiano katika jumuiya.

Wakristo wanapaswa kuwa na umoja kwakuwa vipaji na karama mbalimbali walizonazo zinatoka kwa Roho Mtakatifu na havipaswi kutumika kwa ajili ya sifa au faida ya mtu binafsi bali kwa ajili ya faida ya jumuiya nzima. Katika Dominika ya leo Paulo anaendelea pale alipoishia Dominika iliyopita. Anatoa siri au njia inayoweza kuunganisha vipaji na karama walizonazo waumini kwa ajili ya manufaa ya wote. Ijapokwa mtume Paulo anatambua umuhimu wa vipaji na karama hizi anasisitiza waziwazi kwamba vipaji na karama hizi bila upendo hazifai chochote, hazina maana. Haziwezi kuleta matunda yaliyokusudiwa na Mungu mwenyewe ambaye ndiye mtoaji wa vipaji na karama hizi.

Bila upendo wa dhati, karama na vipaji hivi vitageuka kuwa ni sababu ya uwepo wa kiburi, dharau, chuki, wivu, majivuno, na utengano ya kila aina. Kinyume chake endapo vipaji na karama hizi vitatumika katika msingi wa upendo basi jumuiya itavuna matunda ya umoja, kuvumiliana, na ushirikiano katika jumuiya. Mtume Paulo anapoongelea juu ya Upendo haongelei upendo wa jumla kama wengi wanavyouelewa bali analenga ule upendo wa Yesu Kristo uliomfanya ayatoe maisha yake kwa ajili ya wengine.

Tunapotafakari ujumbe wa leo tukumbuke kwamba mfuasi wa kweli wa Yesu ni yule aliye tayari kutumia vipaji na zawadi zote alizojaliwa na Mungu kwa ajili ya manufaa ya wengine na si kutafuta faida yake pekee. Huu ndiyo upendo wa kikristo. Yesu anatukumbusha akisema, “…Mmepewa bure, toeni bure.” (Mt. 10:8). Zaidi sana sisi sote tuliobatizwa, tumepewa cheo cha unabii. Je, maisha yetu kama wakristo yanatoa unabii gani katika jamii inayotuzunguka? Tumwombe Mungu atujalie ili tuweze kujenga uhusiano wa karibu na Mungu ili Neno lake liweze kuzaa matunda ndani yetu na ndani ya jamii nzima. 

Jumapili 4 ya Mwaka

 

01 February 2019, 14:47