Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili V ya Mwaka C: Kwa neno lako!
Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. – Vatican.
Masomo yote matatu Dominika hii ya tano ya mwaka yanaongelea juu ya wito wa kwenda kulitangaza Neno la Mungu. Ni wito wa kuwa wamisionari kwenda kuwainjilisha watu. Tunaweza kujiuliza, Je, kuwainjilisha watu maana yake ni nini? Ni kuwapelekea Neno la Mungu lenye kuwaweka huru na kuwaokoa (Rejea Yohane 8: 32; Warumi 1:16; 1 Korintho 1:18). Ni kuipeleka Injili katika mioyo ya watu na kuwafanya waishi kadiri ya tunu za Injili katika nyanja mbalimbali za maisha yao. Wakiongozwa na tunu hizi waweze kubadilika toka ndani ya mioyo yao na kufanywa upya (Rejea Ufunuo 21: 5; 2 Korinto 5: 17; Wagalatia 6: 15). Upya huu unatokana na namna yao ya kufikiri, kuchagua na kutenda kadiri ya Injili (Rejea Wa Efeso 4: 23-24; Wakolosai 3: 9-10).
Tunatambua kuwa jukumu la kuinjilisha ni la kila mbatizwa. Hivyo kila mbatizwa anaitwa kuwa wamisionari na kulipeleka Neno la Mungu kwa watu wote. Hata hivyo masomo yote matatu yanatusimulia jinsi watu mbalimbali walivyoitwa kwa namna ya pekee kulitangaza na kulishuhudia Neno la Mungu. Katika somo la kwanza tunamkuta nabii Isaya anayepokea wito toka kwa Mungu akiwa ndani ya Hekalu la Yerusalemu. Alijaliwa kupata maono na kuuona utukufu na ukuu wa Mungu kwa kushuhudia malaika wakiimba na kukiri utakatifu na ukuu wa Mungu. Mara moja Isaya anajitambua kuwa ni mwenye dhambi na anaishi miongoni mwa jamii ya wenye dhambi. Hata hivyo Mungu mwenyewe anamtakasa na anamtuma. Alipewa ujumbe mkali wa kutangaza adhabu kwa waisraeli kutokana na kuishi katika njia yao mbaya na kumwasi Mungu. Hata hivyo unabii wake uliishia kwa maneno ya faraja na matumaini kwa watu.
Yesu katika maisha yake ya utume hapa duniani alikuwa na wafuasi wengi wake kwa waume. Hata hivyo aliwachagua wafuasi 12 wawe karibu zaidi naye na waliandamana naye katika maisha yake ya kila siku ya utume. Katika Injili ya leo tunaona ni jinsi gani na ni katika mazingira yepi Yesu aliwaita mitume wake wa kwanza. Miongoni mwa mitume hawa alikuwa Simoni Petro ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa mitume wengine. Baada ya kufanya kazi usiku kucha katika ziwa la Genezareti bila kupata chochote, Simoni na wenzake walikuwa tayari wameshaiacha mitumbwi yao na walikuwa wakizitengeneza nyavu zao kuziandaa kwa kazi ya siku nyingine.
Yesu akiwa katika maeneo hayo ya ufukwe wa Ziwa anajikuta akiwa amezungukwa na watu wengi amabao walitaka kusikiliza Neno la Mungu. Watu walitaka kumsikia kwa kuwa huko nyuma walimsikiliza na wakatambua kuwa hakuongea kama waalimu wengine bali kama mtu mwenye mamlaka na alikuwa amegusa mioyo yao. Naye Yesu hakuwaacha bali akapanda katika mtumbwi wa Simoni na kumwomba aupeleke mbali kidogo ya pwani. Naye akaaanza kuwafundisha watu habari njema. Baada ya kumaliza anamuamuru Simoni atweke mpaka kilindini na ashushe tena nyavu zao wapate kuvua samaki. Kwa namna walivyohangaika usiku kucha na kwa sababu ilikuwa tayari mchana ilikuwa ni vigumu kwa Simoni na wenzake kukubali agizo la Yesu.
Tofauti na watu wa Nazareti ambao hawakumwamini Yesu, Simoni anafanya jambo kubwa la imani na utii anapomwambia kwa Yesu, “lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu.” Hapo tunaambiwa kuwa ulitokea muujiza mkubwa kwa wingi wa samaki waliowavua. Simoni akatambua kuwa hakuwa amekutana na mtu wa kawaida. Alimtambua mara moja kuwa lazima Yesu atakuwa ni mtakatifu, akamuabudu kwa kupiga magoti. Akijitambua kuwa yeye ni mwenye dhambi alimwambia Yesu, “Ondoka kwangu, kwakuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana.” Badala yake Yesu anamtia matumaini na kumwambia, “Usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu.” Yesu alikuwa amemwalika katika kazi nyingine tofauti lakin muhimu zaidi. Alimwalika kufanya kazi kwa ajili ya ukombozi wa roho za watu. Kisha, Simoni na wenzake wakaacha kila kitu wakamfuata Yesu.
Katika somo la pili tunamkuta mtume Paulo akiwahubiria Wakristo wa Korintho Habari Njema yenye kuwaokoa. Anawasimulia juu ya Yesu Kristo Mkombozi aliyekufa na kufufuka na kuwatokea mitume na watu mbalimbali. Paulo naye alibahatika kutokewa na Yesu na kukutana huko kukawa ndiyo chanzo cha kuongoka kwake. Kisha Paulo alipokea toka kwa Yesu wito wa kwenda kuwatangazia mataifa habari njema. Kwa unyenyekevu Paulo anatambua kuwa wito alioupokea ni neema tu na si mastahili yake binafsi (Rejea Wagalatia 1: 15; 2: 9; 1 Kor 3: 10; 6: 4; 11: 23; Rum 1: 5; 13: 2; 15:15). Kwa sababu hiyo, Paulo aliheshimu kwa namna ya pekee wito huo na aliamini kuwa ili kuokoka watu wanapaswa kumtambua Yesu kuwa ni Bwana.
Aliamini pia kwamba imani ni zawadi toka kwa Mungu ambayo msingi wake ni kusikiliza Neno la Mungu. (Rejea Warumi 10: 13-15). Mungu alimwita ashiriki mpango wake wa kuwakomboa watu (Wagalatia 1: 1). Alijitambua kama mtumishi wa Kristo na kwamba amefanywa kuwa balozi na mwakilishi wa Kristo ( Rejea 2 Wakorintho 5: 20; Wagalatia 4:41). Kazi ya umisionari wa Paulo katika historia ya Kanisa ni ya pekee na Kanisa linampa heshima ya kuwa na hadhi sawa na ya wale mitume wengine. Historia na mang’amuzi ya wito wa Nabii Isaya, Mitume wa kwanza na ya Mtakatifu Paulo kama tulivyoyasikia katika masomo yetu yanatusaidia kutafakari juu ya wito wetu wenyewe.
Mungu kabla ya kutuita daima anajifunua kwetu ili tuweze kumjua na kukiri ukuu na utakatifu wake. Tunaweza kumjua Mungu kwa kupitia maandiko matakatifu na hasa kwa kumtazama Kristo ambaye ndiye kielelezo halisi cha Mungu asiyeonekana. Tujiulize ni kwa kiasi gani Neno la Mungu linachukua nafasi katika maisha yetu? Mungu hatuiti kwa sababu sisi ni watakatifu bali kila mmoja wetu katika wito wake anataka amtakatifuze kupitia wito huo. Ametuachia na nyenzo mbalimbali za kututakatifuza ikiwa ni pamoja na Neno lake na Sakramenti hasa kitubio na Ekaristi Takatifu. Tujiulize ni kwa jinsi gani tunatumia nyenzo hizi kujipatia utakatifu. Kadiri tunavyojiweka mbali na sakramenti hizi ndivyo ambavyo tunajiweka mbali na Mungu na kadiri tunavyozitumia vema sakramenti hizi ndivyo ambavyo maisha yetu yanakuwa karibu na Mungu.
Japo Mungu anamuita kila mbatizwa kuwa mmisionari, Mungu anawaita wengine kwa namna ya pekee ili wajitolee maisha yao yote kwa ajili ya kuujenga Ufalme wa Mungu na kwa ajili ya ukombozi wa roho za watu. Wanaoitikia wito huu lazima waitikie kwa hiari kwa kutambua kuwa ni jukumu muhimu sana na wawe tayari kumtii Kristo na kuacha yote ili kuweza kuitenda vema kazi hii bila kutafuta faida yao binafsi. Kanisa linapitia katika kipindi kigumu ambacho miito ya upadre na utawa inazidi kupungua. Dunia inawaaminisha wengi umuhimu wa fedha, utajiri wa haraka haraka na umaarufu, hivyo hata watoto wengi siku hizi wanaandaliwa kufanya kazi zenye kuwaingiza kipato tofauti na kujitolea kumtumikia Mungu. Tuzidi basi kumwomba Mungu aamshe ndani ya vijana wengi tamaa ya kumtumikia yeye wakiwa kama mapadre, watawa na watu wa ndoa na familia, msingi wa miito yote ndani ya Kanisa!