Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili VI: Heri na Ole!
Na Padre Walter Milandu, C.PP.S. – Vatican.
Siku moja Yesu aliwaambia wanafunzi wake akisema, “Mimi ndiye njia, ukweli na uzima”. (Yohane 14:6). Ni yule tu anayeweka imani na matumaini kwa Yesu na anayeyapokea na kuyaishi mafundisho yake ndiye atakayeingia katika Ufalme wa Mungu. Katika Dominika hii ya VI ya Mwaka C wa kanisa, sote tunaalikwa kuchagua kati ya hekima itokayo kwa Mungu na hekima ya kidunia. Bwana wetu Yesu Kristo anatupatia mwongozo unaopaswa kuongoza maisha ya kila mkristo. Mwongozo huu unafupishwa katika heri kuu nne anazotufundisha Yesu kadiri ya masimulizi ya Mwinjili Luka.
Mafundisho ya Yesu kupitia heri hizi nne yanatoa picha halisi ya jinsi mtazamo na mtindo wa maisha wa kila mfuasi wa Yesu hapa duniani unavyopaswa kuwa. Heri hizi zinahusu mahusiano yetu na Mungu na wenzetu. Heri anazotufundisha Yesu zina msingi wake katika hekima itokayo kwa Mungu na kwa sababu hiyo zinapingana moja kwa moja na mtazamo na hekima ya kidunia. Sisi kama wakristo tunaalikwa kuchagua heri anazotufundisha Bwana wetu Yesu Kristo ili kuweza kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu na warithi wa Ufalme wa Mungu.
Injili ya leo ina msingi wake katika Agano la kale ambapo Manabii waliwaalika Waisraeli kuchagua kati ya laana au baraka, maisha au kifo. Katika somo la kwanza la leo, Nabii Yeremia, kama ilivyokuwa kwa manabii wengine kabla yake, anakaripia ukosefu wa imani kwa Mungu kutokana na taifa la Israeli kufanya maagano na mataifa mengine yenye nguvu mfano Asiria, Misri na Babilonia ili kupata ulinzi wao. Kwa kufanya hivyo, Waisraeli walilivunja Agano lao na Mungu, wakataka kuwa kama mataifa mengine. Walikubali kupokea imani na ibada ya miungu ya kipagani.
Matokeo yake walipoteza kitambulisho chao cha kuwa taifa teule la Mungu. Watawala hawakutawala tena kadiri ya mapenzi ya Mungu bali kadiri ya mitazamo yao ya kidunia. Jumuiya ikakosa misingi ya haki, ikatawaliwa na tamaa na ubinafsi. Mambo yote hayo yalipelekea kuanguka kwa taifa la Israeli. Kwa sababu hiyo, nabii Yeremia anaweka bayana kuwa maisha ya mtu anayejiweka mbali na Mungu na kutegemea nguvu za kidunia ni sawa na mti uliopandwa jangwani au katika ardhi yenye chumvi ambako hakika hunyauka na hatimaye kufa.
Kinyume chake amebarikiwa mtu ambaye anamtumainia Mungu. Maisha yake ni sawa na mti uliopandwa kandokando ya mto. Husitawi siku zote; iwe ni katika kipindi cha mvua au wakati wa kiangazi maana hautegemei mvua bali mizizi yake hushuka chini ya ardhi mpaka kwenye chemchemi ya maji. Ni katika mantiki hiyo kwamba mzaburi wa Zaburi ya kwanza anasema kwamba heri mtu yule aliyemfanya Mungu kuwa tumaini lake akilitafakari neno lake usiku na mchana na akijiepusha na watu wasio haki.
Utimilifu wa hekima hii unajionyesha katika heri anazozitangaza Yesu. Mafundisho haya Yesu aliyatoa kwa ajili ya watu wa mataifa yote na ndiyo maana wale waliokuwa wakimsikiliza walikuwa wametoka katika pande mbalimbali; Uyahudi, Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Hivyo wale waliokuwa wakimsikiliza hawakuwa Waisraeli tu bali pia wapagani. Kwa mafundisho haya Yesu alitaka wafuasi wake waishi tunu za Injili ili waweze kuishi katika uhusiano mzuri na Mungu na wengine.
Leo tunatafakari heri na kwanza ambayo Yesu anaifundisha. Yesu anasema, “Heri ninyi mlio masikini, kwa sababu ufalme wa Mungu ni wenu.” Bwana wetu Yesu Kristo hapendi kuona umasikini ukiendelea katika jamii zetu. Kinyume chake anatualika sisi sote kumtokomeza adui umasikini kwani unaweza kusababisha madhara na kumweka mwanadamu chini ya hadhi na heshima aliyompa Mungu. Kwahiyo sisi kama wakristo yatupasa kumpiga vita adui huyu kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na pia kwa kugawana na wenzetu wenye shida yale tuliyojaliwa na Mungu kama ambayo tunavyoshauriwa katika kitabu cha matendo ya Mitume. (Rejea Matendo 2: 44-45).
Hata hivyo Yesu anasifu ile hali na moyo walio nao masikini, wakiweka imani na matumaini yao yote kwa Mungu. Mtu masikini hutambua kuwa bila Mungu yeye hawezi chochote. Hivyo, huishi kwa kumtegemea Mungu kila siku na kila wakati. Masikini hutambua kuwa yale anayoyapata ni majaliwa ya Mungu na haachi kamwe kumshukuru Mungu. Zaidi ya hayo masikini daima yuko tayari kugawana na wengine wenye kuhitaji. Wanasema kuwa pale wanapoishi masikini pamoja hakuna anayekufa na njaa.
Katika Biblia tunaona watu mbalimbali maskini jinsi walivyo na moyo wa kutoa. Mfano, katika Kitabu cha kwanza cha Wafalme 17: 7-16, tunamkuta mjane wa Sarepta ambaye alikuwa tayari kumtayarishia nabii Eliya mkate uliotokana na unga wa mwisho aliokuwa nao. Kadhalika Bwana wetu Yesu Kristo katika Injili anamsifu mjane kwa moyo wake wa kutoa sadaka mpaka senti ya mwisho. (Rej. Mk 12: 43). Waswahili pia husema kuwa kutoa ni moyo na si utajiri. Mkristo anayeishi moyo wa kimaskini ni yule ambaye hubaki karibu na Mungu akitambua kuwa bila Mungu yeye hawezi kitu. Hudumu katika mahusiano ya karibu na Mungu. Hata akipatwa na magumu tegemeo lake ni Mungu na daima humkimbilia yeye. Katika muungano huu na Mungu, mkristo huyu hubaki katika furaha na amani ya kweli.
Kinyume cha heri ya umaskini, Yesu anatoa ole kwa matajiri. Hata hivyo Yesu hana nia ya kuwaalaani matajiri kwa sababu ya utajiri wao bali anakemea mtazamo wa kidunia unayowaaminisha watu kwamba fedha au utajiri ndicho kitu muhimu zaidi katika maisha. Katika zama hizi zetu, mtazamo huu unazidi kushika kasi na kuteka mawazo na mioyo ya walio wengi. Taratibu Mungu anapoteza nafasi yake ya kwanza katika maisha ya watu. Si ajabu kwamba watu wengi hukosa nafasi ya kumwabudu na kumshukuru Mungu kwa kujihusisha na utafutaji wa fedha. Fedha inapochukua nafasi ya Mungu katika moyo wa mtu na katika jamii kwa jumla hatari yake kubwa ni kwamba hata wengine hasa masikini na wanyonge hukosa thamani yao katika jamii. Ndiyo maana jamii zetu zinakumbwa na matukio mbali mbali ya uvunjwaji wa haki, unyang’anyi na kila aina ya dhambi kwa ajili ya kujipatia pesa.
Kama jinsi ilivyokuwa wakati wa Nabii Eliya, wengi wamejaribiwa katika imani kwa kumwasi Mungu na kujihusisha na ibada za kipagani na ushirikina kwa ajili ya kujipatia madaraka na fedha. Ndugu yangu tutambue kuwa fedha haiwezi kamwe kumpa mtu furaha ya kweli maana mwanadamu ameumbwa ili aungane na Mungu aliye chanzo cha furaha na uzima wa milele. Furaha ya kweli ya mwanadamu hupatikana katika uhusiano wake mzuri na Mungu na wengine. Wewe na mimi tunapaswa kujiuliza endapo kweli Mungu ana nafasi ya kwanza katika maisha yetu ya kila siku. Tumwombe Mungu atujalie kiu ya kumtafuta na kuungana naye daima katika maisha yetu.