Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili VI: Tumaini kwa Mungu!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 6 ya Mwaka C wa Kanisa. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Yer. 17:5-8) ni kutoka kitabu cha Nabii Yeremia. Nabii anaeleza aina mbili za watu: kwanza yule anayeweka tumaini lake kwa mwanadamu na pili yule anayeweka tumaini lake kwa Mungu. Na anasema moja kwa moja kuwa amelaaniwa yule awekaye tumaini lake kwa mwanadamu bali amebarikiwa yule anayeweka tumaini lake kwa Mungu. Katika somo hili Nabii Yeremia anaonesha kuwa katika maisha ya mwanadamu hapa duniani kuna namna ya kuishi ambapo mtu anayajenga maisha yake na anaweka hatima ya maisha hayo katika vigezo na vipimo vya kiulimwengu tu.
Kutoka hapo anaonesha kuwa ipo namna nyingine ya kuyajenga maisha na kuweka hatima yake kwa Mungu, namna anayowaalika watu kuifuata. Zaidi ya kupata baraka za Mungu, Nabii Yeremia anaonesha kuwa kuyajenga maisha katika tumaini kwa Mungu ni kuyajenga maisha katika misingi inayodumu. Kitu ambacho anayeishi kwa kumtegemea mwanadamu hana uhakika nacho, tena kuishi kwa kumtegemea Mungu humuondoa mwanadamu katika hofu na wasiwasi mwingi katika maisha.
Somo la pili (1Kor 15:12, 16-20) ni Waraka kwa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho. Katika somo hili Mtume Paulo anazungumza kuhusu ufufuko wa wafu, suala ambalo jumuiya ya wakorinto walikuwa na mashaka nalo. Walikuwa na mashaka kuhusu ufufuko wa wafu lakini hawakutilia shaka fundisho kuwa Kristo alikufa na akafufuka. Ndiyo maana Paulo anaanza kuelekezea kutoka pale wanapoamini, yaani ufufuko wa Kristo. Na anawaonesha waziwazi kuwa Kristo ndiye kielelezo halisi cha wote waliolala katika imani naye. Na kama Yeye alivyokufa na kufufuka ndivyo na wafu watakavyofufuliwa.
Somo hili linaonesha ugumu ambao hata sisi wakati mwingine tunakuwa nao katika mafundisho ya imani yetu. Kwamba tunayapokea mafundisho na kuyakariri kwa kichwa lakini pale inapofika wakati wa kutafsiri hali fulani ya maisha yangu kupitia mafundisho ninayoamini inakuwa ni kitu kigumu kweli kweli. Ni somo linalotukumbusha pia kuwa kweli za kiimani tunazokiri sio nadharia, ni kweli zinazogusa maisha yetu wenyewe zikilenga kuyapa maelekeo ya kimungu.
Injili (Lk 6:17, 20-26) Injili ya leo inaleta sehemu ya kwanza ya mafundisho ya hadhara ya Yesu kwa wafuasi wake. Nayo ni mafundisho yanayofahamika kama mafundisho ya heri na ole kadiri ya mwinjili Luka. Mafundisho haya yanaanza kwa tangazo la baraka za Mungu kwa watu wake: kwa maskini, kwa walio na njaa na kwa wale wanaoshutumiwa, wanaotengwa na kushutumiwa kwa ajili yake. Hawa wanatangaziwa baraka ya kuurithi ufalme wa Mungu, baraka ya kufurahi na kuwa na thawabu mbinguni. Tangazo la pili ni lile la ole – laana kwa wale walioshiba sasa – waliojitosheleza, wale wanaofurahi sasa na kusifiwa kwa umaarufu, hao watapata hukumu yao.
Katika Injili hii ya Luka ni jambo la pekee kwamba mafundisho ya heri na ole ameyaweka si katika mazingira ya kiroho tu bali pia katika mazingira ya kijamii. Mwinjili Luka awali ya yote anatuonesha kuwa Mungu anashughulikia ustawi wa kiroho na wa kimwili wa watu watu wake; Mungu anayealika ujengaji wa jamii iliyo na haki na usawa. Katika mafundisho ya leo anawazungumzia walio masikini hasa wa kipato na wa hadhi katika jamii, anawazungumzia walio na njaa, yaani mateso mbalimbali na wale wanaowekwa pembezoni katika jamiii. Yesu anatoa mwongozo mpya ambao unageuza mwono wa mambo na maisha mazima katika ulimwengu. Wale ambao muundo wa kiulimwengu hauwapi nafasi ndio walio na nafasi ya pekee kwa Mungu na ndio wanaotangaziwa baraka. Wale ambao ulimwengu unawapata nafasi ya kufurahi, kushiba na kuwasifu ndio wanaotangaziwa ole, laana na hukumu machoni kwake.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo yetu ya leo yanatualika tutafakari juu ya ustawi wa maisha ya mwanadamu. Ni hitaji asilia tulilo nalo kama binadamu kuwa ndani yetu na kichocheo cha kushughulikia ustawi na maendeleo yetu katika maisha. Leo tunaoneshwa kuwa zipo mbele yetu njia mbili za kuchagua kupita katika kushughulikia ustawi wetu. Ipo njia ya mwanadamu na ipo njia ya Mungu. Lakini pia katika hali ya kawaida si mara zote inakuwa rahisi kupambanua ni ipi njia ya kimungu ya kufuata na ni ipi njia ya kibinadamu ya kuiepuka. Kwa jinsi hii tumejikuta tukikwama katika ile inayotuonesha mafanikio, inayotupa furaha na kuridhika. Masomo yetu yote matatu ya dominika ya leo yanakutana katika kutuonesha kuwa njia ya kimungu ni ile inayokwenda zaidi ya hapo. Ni ile yenye kutufikisha katika kutupatia misingi ya kudumu; ni ile yenye uthabiti.
Papa Francisko katika mafundisho aliyoyatoa katika Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa huko Dublin, nchini Ireland, alitualika tuwe makini sana katika utamaduni unaojengeka kwa kasi katika maisha yetu siku hizi; utamaduni wa mambo yasiyodumu kama alivyouita Papa mwenyewe. Katika utamaduni huu tuna vitu vingi kwa mfano tunavyovitumia kwa muda mfupi tu, vinaisha wakati wake na utamaduni huu huu unatudai tutafute vingine vinavyoendana na wakati. Ndivyo inavyojionesha katika mavazi, vifaa vya kielektroniki na kadhalika. Katika utamaduni huu, aliongeza Papa, ni rahisi kutoka katika vitu na kuhamia katika tunu zingine za maisha na kujikuta tunayajenga maisha yetu katika utamaduni wa mambo yasiyodumu na hayo wakati mwingine kuyapa kipaumbele ilhali kuyaona yadumuyo kama yasiyo na maana.
Njia yenye uthabiti ndiyo anayotualika nabii Yeremia katika somo la kwanza anapotuonesha kuwa anayeishi kwa kumtegemea Mungu atakuwa kama mti uliopandwa karibu na maji, uenezao mizizi yake katika mto. Njia ya uthabiti ndiyo anayoifundisha Mtume Paulo kwa wakorintho, kutokuyaona maisha ya mwanadamu kuwa yanaishia hapa duniani tu bali kutoka katika imani ya ufufuko wa Kristo kutambua kuwa maisha yanaendelea hadi kufikia uzima wa milele. Njia ya uthabiti ndiyo njia ya heri anazofundisha Kristo katika injili. Heri ambazo huinua tumaini la mwanadamu kuelekea mbingu kama kuelekea katika nchi ya ahadi. Ni heri ambazo zinaonesha njia ya kupitia majaribu yanayowangoja wafuasi wa Yesu lakini kwa mastahahili ya mateso yake, Mungu anawalinda katika “tumaini lisilotahayarisha”, tumaini hakika na thabiti (Rej. KKK 1820).