Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Mwaka C wa Kanisa: Kanuni ya Dhahabu! Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili VII ya Mwaka C wa Kanisa: Kanuni ya Dhahabu! 

Liturujia ya Neno la Mungu Jumapili VII: Kanuni ya dhahabu!

Njia hii ya kuushinda uovu kwa wema ndiyo iliyokuwa katika moyo wa Daudi. Pale ambapo kibinadamu alikuwa na uwezo wa kumwangamiza Sauli adui yake na yeye kubaki kama mfalme wa Israeli, hakufanya hivyo. Hakutaka kumaliza uadui kwa kumwangamiza adui yake na wala hakutaka kujipatia madaraka kwa njia ya kumwaga damu. Hii ndiyo njia anayoifundisha Kristo Yesu!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 7 ya Mwaka C wa Kanisa. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Sam 26:2, 7-9, 12-13, 22-23) ni kutoka kitabu cha Samweli. Linaeleza mazingira ambapo kulikuwa na uadui mkubwa kati ya mfalme Sauli na Daudi. Uadui ulikuwa mkubwa kwa sababu Sauli alidhamiria kumuua Daudi na alimfuatia yeye pamoja na watu wake ili amuue. Katika harakati hizi Daudi akiwa na Abishai wanamkuta mfalme Sauli akiwa amelala pamoja na maaskari wake. Abishai anamwambia Daudi Bwana amemleta adui yako mikononi mwako, niruhusu nimwangamize. Abishai anasukumwa na kanuni ya “jino kwa jino”, kanuni ya “akuanzae mmalize”, kanuni ya “dawa ya moto ni moto” lakini Daudi anamzuia. Anamzuia kwa kutambua kuwa Sauli ni mpakwa mafuta wa Bwana, ni mwekwa wakfu. Kunyoosha mkono juu ya mwekwa wakfu wa Bwana ni kujitafutia hatia mbele ya Bwana. Kinyume na Abishai, Daudi anatambua kuwa kuwa daima kuna njia ya amani ya kutatua matatizo na kuna suluhu ya amani pale palipo na uadui.

Somo la pili (1Kor 15:45-49) ni waraka kwa kwanza wa mtume Paulo kwa wakorinto. Paulo anaendeleza fundisho kuhusu ufufuko wa wafu, msamiati ambao ulikuwa ni mgumu kueleweka kwa wakorinto. Anaeleza Paulo kuwa yupo Adamu wa kwanza na yupo Adamu wa mwisho. Adamu wa kwanza alikuwapo kwa jinsi ya mwili, Adamu wa mwisho yupo kwa jinsi ya roho. Kwa jinsi ile ile tulivyochukua asili ya mwili kutoka kwa Adamu wa kwanza ndivyo hivyo hivyo tutachukua asili ya roho kutoka kwa Adamu wa mwisho. Sasa Adamu wa mwisho si mwingine bali ni Kristo, naye amekwishaonesha asili mpya, asili ya roho kwa ufufuko wake. Hili ni tumaini kuwa hata wale waliokufa wakiwa na imani naye watashirikishwa naye ufufuko wake. Katika fundisho hili Mtume Paulo anabainisha kuwa mwanadamu anayo asili ya mwili inayoishia hapa duniani lakini pia anayo asili ya roho ambayo inavuka maisha yake ya duniani, hii ni asili inayoishi milele.

Injili (Lk 6:27/34) Injili ya leo inaleta sehemu ya pili ya mafundisho ya hadhara ya Yesu kwa wafuasi wake. Sehemu ya kwanza ilikuwa ni ile ya mafundisho ya heri na ole ambayo tuliitafakari dominika iliyopita. Katika sehemu hii ambayo pia inaendeleza dhamira ya kubadilisha mwono wa kuishi wa mwanadamu, Yesu anafundisha kuhusu upendo kwa adui. Mwinjili Luka anaanza kwa kutoa fundisho la Yesu: wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wanawalaani ninyi na waombeeni wale ambao wanawaonea ninyi. Baada ya fundisho hilo anatoa baadhi ya mifano halisi ya kuonesha namna ya kuwapenda adui zetu. Anaonesha katika mifano hiyo kuwa kumpenda adui ni kutokuishi naye kwa kisasi – akupigaye shavu moja mgeuzie la pili, ni kujifunza kuwachukulia katika mapungufu yao– akunyangànyaye joho mpe na kanzu pia, ni kuishi nao kwa ukarimu – akuombaye mpe, na ni kuwa kwao hatua mbele zaidi katika upendo hata kama wao hawatuoneshi – usitake akurudishie. Hiyo ndiyo namna mpya ya wafuasi wa Kristo, namna inayozidi ile ya ulimwengu.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo yetu ya leo yanatualika kufanya mapinduzi katika nafsi zetu ili kujenga mahusiano ya kindugu yanayosimikwa juu ya msingi wa mafundisho ya Kristo. Ni masomo yanayogusa mazingira ya mwanadamu yanayozungukwa na magomvi, uhasama, uadui kati ya mtu na mtu, familia na familia na hata ukoo na ukoo. Yanatualika pia tuyaangalie mazingira ambapo mwanadamu kufikia lengo lake yuko tayari kutumia njia yoyote ile hata kuwaangamiza wengine; kuwaangamiza kwa kuwachafua lakini hata kwa kuwaondolea uhai. Na kwa bahati mbaya, mtindo huu kwa kiasi fulani unaonekana kuwa ndio hali ya kawaida na inayokubalika katika maisha. Masomo ya leo yanatuambia hapana. Sisi kama wafuasi wa Kristo njia yetu ni njia ya upendo. Na upendo huu unatualika kuushinda uovu kwa wema.

Njia hii ya kuushinda uovu kwa wema ndiyo iliyokuwa katika moyo wa Daudi. Pale ambapo kibinadamu alikuwa na uwezo wa kumwangamiza Sauli adui yake na yeye kubaki kama mfalme wa Israeli, hakufanya hivyo. Hakutaka kumaliza uadui kwa kumwangamiza adui yake na wala hakutaka kujipatia madaraka kwa njia ya kumwaga damu. Hii ndiyo njia anayoifundisha Kristo katika mafundisho yake ya kimapinduzi. Kinyume na hapo, anasema Kristo, ni kuishi maisha yasiyo na fadhili. Anaweza kabisa mwanadamu kuchagua njia ya kisasi na  njia ya jino kwa jino lakini haitamletea fadhili na hata ule utulivu anaodhani ataupata hataupata kwa sababu ni njia iliyo nje ya mpango wa baraka wa Mungu.

Njia ya Kristo ya kuushinda uovu kwa wema katu sio njia inayoendekeza kushamiri kwa ukandamizaji wala si mwono wa woga wa kukabiliana na ukosefu wa haki katika maisha. Ni njia inayotualika kutambua kuwa katika kupambana na hali hizo zinazofifisha hadhi ya mwanadamu daima tuongozwe na njia za amani. Zipo njia za amani kusuluhisha magomvi, uhasama na uadui kati yetu. Historia ya ubinadamu wenyewe inatuonesha kuwa njia za amani zinapotumika kutatua matatizo, huacha amani ya kudumu ila kisasi na mabavu hayajawahi kuleta amani ya kudumu. Tuupokee mwaliko wa Kristo, tufanye mapinduzi katika fikra na maisha yetu tuuishi upendo wake kati ya adui zetu, tuushinde uovu kwa wema.

Liturujia J7

 

23 February 2019, 15:03