Neno la Mungu Jumapili V ya Mwaka: Wito wa Mkristo!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 5 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Is 6:1-2, 3-8) ni kutoka katika kitabu cha nabii Isaya na linazungumzia wito wa nabii Isaya mwenyewe; namna alivyopokea wito wake wa kuwa nabii. Isaya anauelekezea wito wake katika kipindi maalumu cha muda – mwaka aliokufa mfalme Uzia. Kwa hili anapenda kutuambia mwito wake ni kitu halisi kilichotokea, sio habari ya kutunga. Katika mwito huu wa nabii Isaya tunaweza kuainisha mambo manne.
Jambo la kwanza, Mungu anajionesha kwa Isaya akiwa katika utukufu wake. Isaya anamwona Bwana akiwa ameketi katika kiti chake cha enzi, akiwa na maserafi wakisema Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu. Ndiyo kukiri utakatifu wa hali ya juu kabisa wa Mungu. Jambo la pili ni woga wa nabii Isaya. Udhaifu wa ubinadamu unapokutana na utakatifu wa Mungu, hisia ya kwanza ni woga. Na Isaya anasema, “ole wangu… kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu nami nimekaa kati ya watu wenye midomo michafu na macho yangu yamemwona Bwana wa majeshi”.
Jambo la tatu ni utakaso. Na hatua ya kwanza ya kupokea utakaso ni mwanadamu kukiri udhaifu wake mbele ya utakatifu wa Mungu. Isaya aliyekuwa anakaa kati ya watu wenye midomo michafu anatakaswa kwa kaa la moto. Ni alama kuwa sasa anatengwa kutoka watu wenye midomo michafu, anawekwa wakfu. Jambo la nne ni kutumwa na kupokea utume. Isaya anasikia sauti ikisema “nimtume nani” naye anasema “mimi hapa, nitume mimi”. Wito wa Nabii Isaya unatufafanulia kwa namna iliyo wazi zaidi ni nini Mungu anachotenda kwa mwanadamu pale anapomwita katika wito wowote ule: anajifunua kwake, anamwondolea hofu, anamtakasa na ndipo anampa utume wa kutekeleza.
Somo la pili (1Kor 15:1-11) ni waraka kwa kwanza wa mtume Paulo kwa wakorinto. Katika somo hili, Paulo anajitaja kuwa yeye ni kama chombo kinachobeba Habari Njema. Na habari hiyo njema ni kuwa Kristo akikufa kwa dhambi zetu, alizikwa na siku ya tatu alifufuka. Habari hii njema Paulo anasema aliipokea na sasa na yeye anawatolea wengine. Alirithishwa kwa njia ya neema na sasa na yeye anawarithisha wengine kwa njia ya utume. Katika somo hili, Paulo pia anaelezea mwito wake wa kuwa mtangazaji wa habari njema. Huyu Kristo anayemtangaza ndiye aliyemtokea kama alivyowatokea wengine wengi kabla yake baada ya kufufuka. Alimtokea na akambadilisha kutoka kuwa mtesaji wa Kanisa hadi kuwa mtetezi na mhubiri wa mafundisho yake ya imani.
Injili (Lk 5: 1-11) katika injili ya leo, mwinjili Luka anatuletea mwito wa mtume Simoni Petro pamoja na Yakobo na Yohane. Ni mwito ambao kama ulivyokuwa ule wa Nabii Isaya, na wenyewe unaanza kwa kuonesha utukufu wa Mungu. Simoni, Yakobo na Yohane wakiwa wavuvi wa samaki wanajaliwa kuvua samaki wengi mno kimiujiza. Mbele ya muujiza huo Petro anakumbwa na woga mkubwa kwamba yeye ni mtu mwenye dhambi na sasa amekutana na Mungu. Kama ilivokuwa katika mwito wa nabii Isaya, Kristo anamwondolea hofu zake na anampa utume “usiogope, tangu sasa utakuwa ukivua watu”
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News masomo yetu ya leo yanatualika tutafakari juu ya wito. Kwa wengi kila wanaposikia tafakari au mazungumzo kuhusu wito, moja kwa moja hufikiri kuhusu upadre au utawa. Kwa jinsi hiyo dhana ya wito inakuwa imefinywa na kujikuta inawaacha wengi wakiwa nje na wakati mwingine kujihisi kuwa hawahusiki kabisa na suala zima la wito wa kimungu. Kumbe jambo la kwanza tunalopenda kusisitiza leo ni kwamba wito ni kwa wote.
Sote tunaitwa kumfuasa Kristo, tunaitwa kuuitikia wito wa kumtumikia Mungu na kuwahudumia watu wake katika kila namna na mfumo wa maisha anaotujalia, iwe ni katika upadre, iwe ni katika utawa, iwe ni katika maisha ya wakfu, iwe ni katika Ndoa Takatifu. Kwa nini Mungu anaita? Mungu anaita kwa sababu hupenda kutumia watu kufanya kazi zake. Hutumia midomo ya watu kutangaza ujumbe wake, hutumia mikono ya watu kutekeleza mipango yake, hutumia miguu ya watu kuwafikia watu hutumia watu kufanya kazi zake.
Katika masomo yetu ya leo, kwa njia ya mwito wa watu watatu Isaya, Mtume Paulo na Mtume Petro, tunaona vipengele viwili muhimu vya kutafakari kuhusu mwito wa Mungu. Kipengele cha kwanza ni kwamba kwa njia ya wito anaotujalia Mungu anapenda kutuokoa sisi kwanza. Isaya alipokutana na utakatifu wa Mungu alikiri kuwa na udhaifu, akasema ana midomo michafu na anakaa katika watu wenye midomo michafu. Mtume Paulo alikiri pia kuwa alikuwa mtesaji na muuaji wa Kristo alipokutana na Kristo Mfufuka. Na hatimaye Mtume Petro baada ya muujiza huo wa samaki anamwambia Yesu “ondoka kwangu maana mimi ni mwenye dhambi”. Katika wote hao, wito unakuwa ni mwanzo wa wongofu wao binafsi, mwanzo wa kutakaswa na kufanywa wapya. Hapa ninajiuliza, wito wangu ni upi? Je ninaona ndani ya wito wangu mwaliko wa wokovu wangu binafsi?
Kipengele cha pili ni kwamba: mwito wa Mungu hutualika tuyatumie mazingira yale tuliyomo kuitenda kazi ya kimungu. Nabii Isaya kutoka kuwa mtu mwenye midomo michafu anapokea wito wa kuwa mtangazaji wa ujumbe wa Mungu: Mtume Paulo kutoka kuwa mtesi na muuaji anakuwa mtetezi na mmoja wa wale wale aliowatesa: Mtume Petro kutoka kuwa mvuvi wa samaki anakuwa mvuvi wa watu. Na hapa najiuliza, ninatumia nafasi nilizonazo: kazi zangu, biashara na kadhalika kuwasogeza watu kwa Mungu au natenda kinyume chake? Ninatumia nafasi hizo kama fursa Mungu aliyonipa ya kufanya utume au ninaziona zipo mbali kabisa na ukristo wangu? Mungu Mwenyezi anayetuita na kututumia katika kufanya kazi zake atuimarishe katika miito aliyotuitia kwa ajili ya wokovu wetu na wa ulimwengu mzima.