Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Madhara ya Dhambi! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Madhara ya Dhambi! 

Tafakari ya Neno la Mungu, Kwaresima III: Madhara ya dhambi!

Ujumbe wa dominika hii Kristo ameutamka wazi katika injili akisema msipotubu mtaangamia milele, hivyo tunaalikwa kufanya toba ya kweli kila mmoja kwa nafsi yake ili tusiangamie milele bali tuuridhi ufamle wa Mungu. Somo la kwanza linaelezea jinsi Mungu alivyomtokea Musa katika kijiti cha moto, akamwita na kumtuma ili kuwakomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, katika dominika ya tatu ya kipindi cha kwaresma mwaka C wa Kanisa. Ujumbe wa dominika hii Kristo ameutamka wazi katika injili akisema msipotubu mtaangamia milele, hivyo tunaalikwa kufanya toba ya kweli kila mmoja kwa nafsi yake ili tusiangamie milele bali tuuridhi ufamle wa Mungu. Somo la kwanza linaelezea jinsi Mungu alivyomtokea Musa katika kijiti cha moto huko Horebu, akamwita na kumtuma ili akawaokoe na kuwatoa ndugu zake wana wa Israel katika utumwa wa Misri. Mungu anamwita Musa kwa jina lake halisi, kisha anamtaka Musa avue viatu, yaani atubu makosa yake kwanza aliyofanya akiwa misri na kukimbia ili aweze kupokea utume ujumbe wa Mungu.

Kisha Mungu anajitambulisha akisema Mimi niko ambaye niko yaani yeye ni wa milele yote, mwanzo na mwisho wa yote, yeye ni Mungu wa wanaoishi sio Mungu wa wafu, ni Mungu anayewajali watu wake, hafurahii mateso bali anaona uchungu watu wake wanapoteseka. Mungu anayesikiliza kilio cha watu wake wanapomlilia na kuomba msaada kwani yeye amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa rehema na fadhili. Katika somo la pili Mtume Paulo anawaasa Wakorinto kwamba wafanye mageuzi ya kiroho, kwani walikuwa wameanza kwenda kinyume na amri na maagizo ya Mungu kwa kuzama katika uasherati, ushirikina kwa kuabudi miungu mingine, chuki baina yao, mafarakano na wivu.

Anawakumbusha kuwa kama Waisraeli walivyookolewa toka utumwani na kupitia Musa, wakapita kati ya bahari, wakala chakula na kunywa kinywaji kile kile cha roho, lakini baadhi yao walipopotea na kumwasi Mungu waliangamizwa wao nao waliobatizwa na kumpokea Kristo katika Ekaristi waache njia zao mbaya wamrudie Mungu wasije nao wakaangamizwa. Katika Injili Kristo anatoa mafundisho makuu mawili: kwanza anaweka wazi madhara ya kutokutubu dhambi kuwa ni kuangamia milele. Pili ni kwamba si kila anayeteseka au kufa ni mdhambi kuliko wengine. Wayahudi waliamini kwamba maafa, magonjwa au kifo viliwapata wadhambi ndiyo maana Elifazi alimwambia Ayubu, “Kumbuka, tafadhali: ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia?” (Ayu 4:7).

Yesu anaweka wazi kuwa sio kweli. Anawaambia wasidhani kwamba wale waliouawa kwa amri ya Pilato au walioangukiwa na mnara huko Siloamu kuwa walikuwa wadhambi kuliko wote waliobaki. Kisha anawaonya akisema; lakini nawaambia msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Mzaburi katika wimbo wa katikati ametuambia kuwa Bwana amejaa huruma na neema, si mwepesi wa hasira ni mwingi wa rehema na fadhili. Mungu anaona uchungu watu wake wanapoteseka na wakimwita na kuomba msaada daima atawasikiliza na kuwaokoa. Ukweli huu anaudhihirisha Mungu wenyewe katika somo la kwanza akisema; “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nimesikia kilio chao, nami nimeshuka ili niwaokoe, niwapandishe kutoka nchi ile niliyowaahidia baba zao”.

Mungu anaona dhahiri kabisa tunavyoteseka katika dhambi, tunahangaishwa na kuburuzwa na shetani, anaona uchungu, anatuhurumia, anatamani tutoke huko tuishi maisha mapya, maisha ya furaha na amani, maisha ya utulivu, upendo na mshikamano. Lakini sharti ni moja tu, kutubu dhambi zetu. Ili kilio chetu kifike machoni pa Mungu sharti tuwe safi nafsini mwetu ndiyo maana alivyomwambia Musa vua viatu vyako,  anatupatia muda na nafasi ya kufanya toba, hataki na hapendi kabisa tuangamie katika dhambi anatupatia nafasi ya pili. Ukweli huu Yesu anavyoudhihirisha kwa mfano wa mtini akisema; uuache hata mwaka huu nao, niutilie samadi na kama hautazaa basi ndipo uukate na kuuteketeza”.

Tunapotenda dhambi Mungu hatuadhibu mara, ametuacha hata mwaka huu. Ametupatia kwaresima hii ili tufanye toba ya kweli na tusipofanya hivyo tutaangamia milele. Kwanini Mungu anatuacha na kutupatia nafasi ya pili? Kwa kuwa huruma yake ni ya milele ndiyo maana kile kijiti alichokiona Musa kiliwaka moto, nacho hakikuteketea maana yake Huruma ya Mungu haiteketei, huruma ya Mungu haiishi ni ya milele yote. Kwani Mungu anasema “Mimi Niko ambaye Niko”, Mungu ni yule yule Jana, Leo na hata Milele, hapungui katika huruma yake. Mungu anatualika tusafishe roho zetu, tutubu kweli, tufanye toba na upatanisho wa kweli. Mwaliko wa “Vua viatu” ambao Musa anaambiwa na Mungu ni alama ya kuacha dhambi, ndiyo maana Mungu anaongezea “kwa sababu mahali hapa uliposimama ni nchi takatifu”.

Ni kitu gani kisichotakiwa patakatifu kama sio dhambi? Musa alipaswa kuacha chuki na hasira aliyokuwa nayo juu ya wa Misri hata akaweza kutenda dhambi ya kuua na hivyo akakimbilia mbali. Ni mwaliko wetu sote wa kuvua kwa nguvu rohoni mwetu yale yote yanavunja urafiki wetu na Mungu hata ikibidi kutoa sadaka ili tusije kuangamizwa. Paulo ametuambia katika somo la pili “Lakini wengi sana katika wao Mungu hakupendezwa nao, maana waliangamizwa jangwani”. Hao ndio waliokataa kuvua viatu ndiyo maana Kristo anasisitiza “Msipotubu nanyi mtaangamia kama wao”. Anaposema “msipotubu mtaangamia” hamaanishi kuwa itafika wakati Mungu ataishiwa na huruma bali kuwa sisi tutamkataa jumla jumla na kukosa nafasi ya kutubu siku atakapomtuma mjumbe wake kutuita turudi tulikotoka yaani baada ya kifo hakuna tena nafasi ya kutubu, wakati uliokubalika ndiyo sasa, tufanye hima tujipatanishe na Mungu kabla ya kifo.

Njia tuliopewa sisi Wakatoliki ya kujipatanisha na Mungu ni kupitia Sakramenti ya Kitubio. Maswali ya kujiuliza juu ya Sakramenti hii muhimu katika maisha yetu ya kiroho. Je, niliungama mara ya mwisho lini? Je, naungama mara kwa mara? Kama sio, Je, sababu ni zipi? Je, sizioni dhambi zangu au sina? Lakini Yohane anatuonya akisema, “Tukisema kuwa hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe na wala kweli haimo kabisa ndani mwetu.” (1Yn:1:8). Inawezakuwa hatuzioni kwa sababu tumezizoea na zimekuwa sehemu yetu kiasi cha kutokuzitambua kama waswahili wasemavyo mtu hawezi kunusa harufu yake mwenyewe au pengine tunajifanya kutokuziona au kwa sababu ya kiburi kwamba tumemaliza siku nyingi bila kuungama na hatujaangamia au tunajilinganisha na wengine wanaoteseka na majanga tukawa na mtazamo kama Wayahudi kuwa sisi tusioteseka hatuna dhambi, Yesu anatuambia tusipotubu tutaangamia.

Wengine tunaogopa kwenda kuungama na kuona haya kujitaja na kujishtaki kuwa tu wadhambi pengine watu wengine, baba, mama, watoto, mume, mke, walezi au walele watanionaje au watafikiri nina dhambi gani. Hata kama ni hulka ya mwanadamu kukwepa mashtaka na kujitetea kuwa hatuna hatia umuhimu wa kitubio uko pale pale na tunapaswa kuwa na ujasiri wa kujiambia ukweli kuwa tu wadhambi tumekosa, tunahitaji huruma na msamaha wa Mungu la sivyo tutaangamia. Katika ulimwengu wetu wa sasa wapo wanaohoji je, ni lazima kuungama kwa Padre? Bila kigugumizi chochote jibu ni ndiyo.

Tufahammu kuwa NENO linasamehe, linaponya na kufanya upya maisha. Katika mahusiano ya kawaida tunataka watu watuambia “Nakupenda” wakinyamaza tu hatuwezi kujua na kutambua kuwa wanatupenda pia ili tumsamehe aliyetukosea tunahitaji atamke wazi kuwa “ninaomba msamaha” na tuliokosa tunahitaji kusikia nimekusamehe, vivyo hivyo katika sakramenti ya kitubio tunahitaji kusikia “umesamehewa dhambi zako nenda na amani.” Maneno haya nami kwa mamlaka niliyopewa na Kanisa nakuondolea dhambi zako au “Nenda na amani dhambi zako zimeondolewa” yanatupatia uhakika wa kile tulichokipata na haya maneno hayawezi kutamkwa na yeyote yule isipokuwa na Padre anayefanya hivyo katika nafsi ya Kristo mwenyewe. Hivyo tunahitaji kuungama kwa Padre ili tupate hakikisho la msamaha wetu kwa kusikia maneno haya.

Tunahitaji kuungama kwa Padre ili tupate ushauri wa kupambana na vishawishi baada ya kuungama. Tunapoungama kwa Padre licha ya malipizi tunayopewa ambayo ni ya muhimu sana, tunapata pia ushauri wa namna ya kupambana na vishawishi vilivyotuuangusha dhambini visitushinde tena. Ili tukue kiroho tunahitaji sana sakramenti ya kitubio kwani Kristo kwa kujua umuhimu wake aliiweka hii sakramenti akisema; “Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa.” (Yoh. 20:23). Tunahitaji Kitubio ili kutunza dhamiri zetu ziwe hai kwani dhambi huu dhamiri.

Ndiyo maana mzaburi anatuambia “Dhambi huongea na mtu mwovu ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya.” (Zab.36:1-4). Tunapozoea dhambi tunazivuruga dhamiri zetu hivyo haziwezikutambua tena lipi jema lipi baya. Mwishowe dhamiri zinatuacha tutende tupendavyo. Na hapo ndipo tunapoangamia. Ndiyo maana tunapoanza kutenda dhambi fulani mwanzoni tunaogopa lakini baadaye tunazoea inakuwa ni kawaida. Tukipokea Kitubio tunaifundisha tena dhamiri kuwa kile tulichokiona kuwa kizuri kumbe ni kibaya.

Basi dhamiri inaanza tena kutuonya tunapokaribia kutenda dhambi hiyo. Ukitaka kuogopa dhambi pokea kila mara Sakramenti ya kitubio. Kitubio kinatusaidia kurudisha urafiki wetu na Mungu. Dhambi ni kumkataa Mungu, na kumkataa Mungu ni kupoteza neema ya utakaso. Ni kitubio peke yake kinaweza kuturudishia Neema hii ya Utakaso, yaani uwepo wa Mungu ndani yetu. Kitubio kinasaidia kurudisha urafiki wetu kwa wengine. Bila kitubio hatuwezi kupatana na wale tuliokoseana nao. Kwa sababu tunajiona wema, hatukubali makosa yetu. Tunaona kuwa sisi tunaonewa tu.

Tunapokwenda kuungama ina maana tumejikubali kuwa sisi tuna makossa, tunadhambi hii inatusaidia kuomba msamaha na kupata na wale tuliokosana nao, kwani katika kitubio tunajazwa neema na baraka za Mungu na hivyo tunakuwa na nguvu ya kujipatanisha na wengine. Kitubio ni muhimu sana. Tuombe ituwie rahisi kuungama, tufanye toba ya kweli, tuvue kweli viatu ili tuweze kusimama mahali patakatifu na kusherekea vyema fumbo la wokovu wetu Pasaka.

Kwaresima J3
22 March 2019, 17:43