Jumatano ya Majivu: Tubuni na kuiamini Injili!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, katika siku ya jumatano ya majivu tunapoanza kipidi cha kwaresma. Leo ni Jumatano ya Majivu, Siku ya kwanza ya Kwaresma siku rasmi ambapo tunaingia katika kipindi cha Kwaresima. Siku hii huitwa Jumatano ya Majivu kutokana na tendo la kupakwa majivu katika paji uso na wakati huo Padre au mhudumu wa tendo hili takatifu la kiroho anasema maneno haya “…Mwanadamu kumbuka, U mavumbi wewe na mavumbini utarudi”.
Jina hili yaani Jumatano ya Majivu, lilianza kutumika rasmi mwaka 1099 na Papa Urbano II: mwanzoni iliitwa “Mwanzo wa Mfungo”. Majivu yatumikayo hutokana na matawi yaliyobarikiwa Jumapili ya Matawi ya mwaka uliopita. Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za kufunga, kusali, kutafakari Neno la Mungu na kufanya matendo ya huruma. Ni kipindi kinachotualika kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa upendo, kwa kufunga na kuwasaidia maskini zaidi. Kipindi hiki cha Kwaresima ni safari ambayo kilele chake ni adhimisho la fumbo la ukombozi wetu yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News; kusali, kujitoa sadaka kwa ukarimu kwa wahitaji na kufunga, ndizo nguzo kuu tatu za kipindi cha Kwaresima, kipindi tunachokianza leo hii, siku ya Jumatano ya Majivu. Leo linafanyika tendo la kupakwa majivu katika paji la uso la kila mkristo mkatoliki anayekiri kuwa ni mdhambi na anahitaji huruma ya Mungu Baba kwani ni ukweli kuwa tunapopakwa majivu tunakubali kuwa sisi ni jumuiya ya wakosaji tunaohitaji huruma, msamaha, kutakaswa na kufanywa upya watoto wa Mungu na wa kanisa. Tendo hili la kiroho la kupakwa majivu katika paji la uso ni ishara ya toba ya kweli, ishara ambayo imekuwa ikitumika kwa maelfu ya miaka iliyopita.
Katika siku za Agano la Kale na pia katika Agano Jipya, kama tulivyosikia katika Maandiko Matakatifu ya kuwa ikiwa mtu alikuwa ametenda dhambi, alivaa nguo za magunia na kujipaka majivu katika mwili wake (Rej. Yer 6:26). Tendo hili tunalofanya leo la kupakwa majivu, linatokana na desturi hiyo ya kiroho ya kufanya toba. Katika ulimwengu wa wayahudi majivu yalikuwa ni alama ya huzuni, masumbuko, uchungu au uduni (Rej. Ayubu 2:8, 30:19; Zab 102:10). Baadaye utamaduni huu wa kupakana majivu ulitumiwa na wakristo wa kwanza kama alama ya toba.
Mwaka 600 hivi, Papa Gregory Mkuu aliifanya siku ya Jumatano ya Majivu kuwa siku ya kwanza ya Kwaresima na akaongeza urefu wa kipindi hiki cha toba hadi siku arobaini. Miaka ya 800 hivi, baadhi ya makanisa yaliadhimisha ibada ya Jumatano ya majivu kwaajili ya wadhambi waliokubuhu katika dhambi na waliojulikana. Sasa pale walipoamua kufanya toba ndio walipakwa majivu. Hivi wakati huu si wote walipakwa majivu ila tu wale waliokuwa wadhambi waliojulikana wazi, kama vile Malaya, wauaji, waasi n.k. Kuanzia karne ya 11, Kanisa lilipanua ibada hii na kuwahusisha waamini wake wote na si wadhambi waliokubuhu tu.
Tendo hili liliambatana na matendo mbalimbali ya kufunga, kusali, kutoa sadaka, kuonesha mapendo kwa wengine na matendo mengineyo ya huruma. Leo hii mwenyezi Mungu kwa kinywa cha Nabii Yoeli, anatuita tumrudie Yeye kwa mioyo yetu yote, kwa kufunga na kwa kulia na kwa kuomboleza. Tunaambiwa tuirarue mioyo yetu, na siyo mavazi yetu. Katika siku za Agano la Kale, watu walikuwa na desturi ya kurarua mavazi yao kama ishara ya kufanya toba. Hata hivyo, walikuwepo wengine waliokuwa wakiyararua mavazi yao kama ishara ya nje tu, na kumbe ndani ya mioyo yao hawakuwa na nia ya kufanya toba ya kweli. Mioyo yao ya ‘jiwe’ haikuweza kubadilika! Watu hawa hawakuwa wameyaacha mambo ya kiulimwengu na kuanza kuyaishi maisha mapya, maisha ya kumcha Mungu.
Nabii Yoeli, anatutaka sisi waamini kumrudia Mungu. Katika hili Nabii Yoeli haiti mtu mmoja mmoja, bali anatoa wito kwa watu wote, akisema, “Pigeni tarumbeta katika Sayuni, takaseni saumu, kusanyikeni kusanyiko kuu; kusanyikeni watu, litakaseni kusanyiko, kusanyikeni wazee kusanyeni watoto na hao wanyonyao maziwa” (Rej. Yoe 2:15). Mtakatifu Paulo, katika Waraka wake wa pili kwa Wakorintho, anatusihi tukubali kupatanishwa na Mungu kwa njia ya Kristo. Mungu Baba alimtuma Mwanawe wa pekee, Yesu Kristo, aje kutukomboa kwa kuteswa na hata kufa msalabani. Mungu asiyejua dhambi alimfanya Yesu Kristo kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (Rej. 2Kor 5:21).
Yesu Kristo hakujua dhambi, lakini alifanywa kuwa dhambi; vivyo hivyo sisi tusio haki tunafanywa kuwa haki katika Yeye. Sisi wadhambi tulistahili kifo hiki cha aibu nakutisha, kifo cha msalaba lakini Yesu Kristo kwa Upendo aliokuwa nao akakubali kutoa Maisha yake kufa msalabani kwa ajili yetu. Katika Injili Yesu anatuonya kuhusu unafiki wa mafarisayo yaani mtindo wa kufanya matendo mema ili kuonekana machoni pa watu wengine. Yesu anasema ya kuwa Mafarisayo hao wamekwisha kupokea thawabu yao kwa njia ya hao watu wengine wanaowatazama na kuwastaajabia, na pia kuwasifia. Watu wa namna hii, anasema Yesu, hawatapokea tena thawabu mbele ya Mungu Baba aliye Mbinguni. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, matendo yetu mema yasiwe yale yanayolenga kujionesha hadharani au kwa watu wengine, bali yawe ni mawasiliano binafsi kati yetu na Mungu yaani kujenga muungano na Mungu wetu Mtakatifu sana kwa sala, sadaka na kufunga.
Tutembee wakati wote na Kristo katika maisha yetu katika kila dakika ya siku, kuanzia asubuhi wakati wa kuamka hadi wakati tuelekeapo kulala, wakati wa usiku. Leo tunapoianza rasmi safari yetu ya siku arobaini za mfungo mtakatifu wa kwaresma, kama Yesu Kristo ambaye alifunga chakula kwa siku arobaini akaona njaa lakini mfungo huu uliompatia nguvu ya kuanza utume wake pamoja na magumu yaliyomkabili, matumaini ya mfungo wetu hayana budi kujengeka katika njaa na kiu ya muungano na Mungu wetu mtakatifu sana. Muungano huu unawezekana tukiwafungulia mlango wenzetu hasa wahitaji na kuwapatia yale tutakayojinyima.
Ni katika mfungo ndipo tunaweza kuiga mfano wa Msamaria mwema, anayejitolea kumsaidia mhitaji bila kuangalia tofauti zao. Mfungo unaoambatana na huduma kwa wahitaji ni njia ya kushinda tofauti zetu na vishawishi vinavyoambatana na tofauti hizo. Kwa hiyo, tunaalikwa katika kila hali tuliyonayo tushiriki mfungo huu wa Kwaresima kwa malengo zaidi ya maisha yetu ya kiroho. Tutofautishe kipindi hiki na mazoea tuliyojijengea ya kujikatalia chakula pengine kwa sababu tu za kibinafsi. Mfungo wetu hauna budi kuambatana na majitoleo mbalimbali (sadaka na huduma) kwa wahitaji. Zaidi sana, wakati huu wa Kwaresima ni wakati wa kutubu na kuiamini Injili.
Tunakumbushwa leo namna sahihi ya kufanya mfungo. Tendo la kufunga chakula lisiwe na mwelekeo zaidi wa Mafarisayo, ambao walitekeleza mfungo kwa kutimiza sheria tu bila uhusiano wowote na maisha yao ya kiroho, tena roho zao zikiwa mbali na Mungu. Tumwombe Mwenyezi Mungu, ili kwa neema zake, mfungo wetu uweze kutusaidia zaidi kushindana na kila hali inayotuzuia kutekeleza mapenzi Yake. Hali kadhalika, mfungo huu tunaofanya uweze kuwa ni sehemu ya toba ambayo itatusaidia kuushinda ubinafsi wetu. Hatua za kuchukua ili tuweze kufanya vema mapinduzi ya kiroho, toba na kubadilika.
Tukubali kwamba sisi ni wadhambi. Tusipokubali kuwa sisi ni wadhambi hatutaona hitaji la kufanya toba na kubadilika. Ndio maana leo tunapakwa majivu ikiwa ni alama ya kukubali kuwa sisi ni wadhambi hatuna thamini mbele ya Mungu, na hivi tunahitaji kutubu. Hivi kila atakayepakwa majivu leo anakubaliana na ukweli huu. Sala, kufunga na matendo ya huruma ni mambo matatu ambayo tunahimizwa kuyafanya katika kipindi hiki cha Kwaresma. Haya ndiyo mambo ambayo Bwana wetu Yesu Kristo anayaweka bayana katika Injili ya leo. Yesu anatuangalisha kuwa, ili tuweze kufaidika kutokana na sala, matendo yetu ya huruma, na kufunga kwetu, tuondokane na unafiki.
Kuna hatari ya kuingia kipindi hiki cha Kwaresima kwa mazoea. Tukifanya hiyo hatutafaidika lolote kiroho. Wito kwetu sote: kila mmoja akiingie kipindi hiki cha Kwaresma kama vile ni cha kwanza na cha mwisho katika maisha yake. Tuitumie kwaresma hii kana kwamba hakuna tena Kwaresma nyingine. Kwa hakika hakuna hata mmoja mwenye uhakika wa kuiona Kwaresma nyingine. Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kipindi cha Kwaresma ndio wakati ulikubalika, siku ya wokovu ndiyo sasa. Tusisubiri wakati mwingine. Tukitumie vema kipindi hiki. Nawatakieni nyote mwanzo mwema wa kipindi cha Kwaresima. Tumsifu Yesu Kristo.