Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili VIII: Fumbo la maisha!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 8 ya Mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Dominika hii inatuandaa kuingia katika kipindi cha Kwaresima, kipindi cha kutafakari: huruma, upendo na wema wa Mwenyezi Mungu; ni kipindi cha, kuongeza nguvu katika sala, kufunga, kujitakasa, kufanya toba, kuungama na kufanya mabadiliko ya maisha ya kiroho kwa ajili ya maandilizi ya Sherehe ya Fumbo la Pasaka.
Katika somo la kwanza, Yoshua bin Sira anatuonyesha umuhimu wa majadiliano katika maisha yetu ya kila siku. Majadiliano huleta muafaka, hutatua matatizo au migogoro kati ya pande mbili zinazolumbana kwa njia ya amani. Ni katika majadiliano mtu hutoa yaliyo ndani ya nafsi yake na kuyaweka wazi na bayana. Kiuhalisia kinachoka ndani ya moyo wa mtu katika kinywa ndicho kinachoonesha na kudhihirisha tabia yake. Ndivyo anavyotuambia Kristo katika Injili kuwa mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu.
Kwa kuwa kinywa cha mtu hunena yale yaujazayo moyo wake. Kwa hiyo ili tufahamu yaliyo ndani ya nafsi ya mtu, Yoshua bin Sira anatuasa na kutushauri kumpa kwanza nafasi ya kuongea na kujieleza, tumsikilize ndipo tumhukumu kwa haki kwa yaliyotoka kinywani mwake. Hali kadhalika kabla ya kupokea au kuunga mkono jambo, hoja au mtu lazima tusikilize kwanza ili tuweze kutambua uzuri na ubaya wake hapo tutakuwa sawa kuliongelea na kulipigania inapobidi. Haya yote yanawezekana kama kuna utamaduni wa majadiliano na kusikilizana!
Mtume Paulo katika somo la pili anatueleza kuwa hali ya mwili wetu wa sasa ni ya kufa na kuoza. Mungu anataka tuwe katika hali hii kwa muda, ikiwa ni mapito kuendea hali yakutokufa, hali ya uzima wa milele. Kwa kifo na ufufuko wake, Yesu ametutayarishia hali hiyo ya kutokufa. Kwa hiyo Maisha ni kufa na kuishi. Tunaishi ili tufe na tunakufa ili tuishi milele. Katika injili mwinjili Luka anatupatia misemo ya hekima na busara za Yesu juu ya viongozi au walimu wanavyopaswa kuwa.
Katika hali ya kawaida mwalimu anapaswa kuwa na uwezo wa kuona, kutambua, kuhukumu na kutenda vyema ili awe mfano mwema kwa mwanafunzi. Kama mwalimu ni kipofu, yaani hawezi kuona, kusoma na kutambua alama za nyakati ili atoe maelekezo yanayostahili ni hatari kwa kuwa anaweza kuwapoteza wanafunzi wake. Yesu anasisitiza umuhimu wa kuona, kusikiliza, kutambua na kuongoza kuliko kwema na sahihi. Pia anatuonya tusiwe wepesi katika kuwahumu wengine, maana hata sisi nasi tuna maboriti katika macho yetu, yaani tuna makosa, hatuko wakamilifu, tu wadhaifu, tu wadhambi mbele za Mungu na tunahitaji msamaha. Kilicho cha maana ni kuonyana na kusaidiana katika kuepuka nafasi za dhambi. Hivyo tuepuke maisha ya unafiki, tuwe wakweli na wema mbele za watu na mbele za Mungu.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunakaribia kuanza kipindi cha kwaresma, kipindi cha toba, kipindi cha kujinyima kwa ajili ya wahitaji, kipindi cha maandalizi ya kusherehekea Fumbo la wokovu wetu, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo yaani Pasaka, tutafakari ukweli huu aliotudokeza mtume Paulo katika somo la pili: Maisha ni kufa na kuishi. Tunaishi ili tufe na tunakufa ili tuishi. Kwanini tutafakari ukweli huu ambao ni mgumu kupokeleka? Kwa sababu ni ukweli na uhalisia wa maisha yetu kwamba tunaishi na tutakufa na baada ya kufa tutaendelea kuishi na pili tumekaribia kipindi kitakatifu cha Kwaresima tujiweke tayari kufa kuhusu dhambi na kuishi maisha ya kitakatifu ili tuwe na muungano zaidi na Mungu wetu aliye mtakatifu.
Kifo ni ukweli ulio mgumu kuupokea na kuukubali. Hivyo kifo hakizoeleki, licha ya kuwa kila siku watu wanakufa nasi tunashuhudia, lakini kifo kinabaki kuwa tishio na hofu kubwa kwa mwanadamu. Watu wengi hawapendi kujua wala kusikia habari za kifo; hawa ndio wale wasio na matumaini na imani juu ya ukweli wa maisha yajayo maisha ya ufufuko. Ni wale wasio kuwa na imani juu ya uwepo wa Mungu na hivyo hawaoni thamani ya maisha ya sasa wala yajayo. Lakini hata sisi tulio na matumaini na imani, bado tunakiogopa kifo kwa kuwa hatukeshi, hatujiandai kumpokea mjumbe wa Mungu atakapokuja kutuchukua na hatujui ni lini atakuja.
Hali yetu ya kuishi katika dhambi, kuwa mbali Mungu, kukosa muunganiko na Mungu wetu aiye mtakatifu sana ndiyo sababu pekee ya kuwa na hofu, mashaka na woga wa kufa. Kifo ni matokekeo ya dhambi ya asili, dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva ya kutotii amri na maagizo ya Mungu, hivyo tupende, tusipende, tukubali tusikubali lazima tutakufa na habari ndio hiyo. Ndiyo maana Paulo Mtume katika Waraka wake wa kwanza kwa Wathesalonike 1Thes. 4:13-17, anasema “ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini”. Kumbe kila nafsi itaonja mauti na hii ndiyo njia pekee ya kurudi nyumbani kwa Baba.
Hata hivyo hatupaswi kuwa na mashaka, tujiandae kwa kutubu vyema dhambi zetu na kujipatanisha na Mungu, tukubali kufa kuhusu dhambi ili tuishi katika Kristo na hivyo tutakuwa na ujasiri wa kutamka maneno ya mtume Paulo akisema mimi kuishi kwangu ni Kristo na kufa ni faida hana mashaka kabisa juu ya ujio wa kifo. Nasi pia hatupaswi kuogopa, kwani kwa kifo cha Kristo Msalabani kifo chetu kimepata maana mpya, ambapo kwayo maisha mapya yanazaliwa. Maisha ni suala la uhai na kifo. Huu ni uhalisia na ukweli usiopingika kuwa; Kifo ni mabadiliko kutoka hali fulani, kuingia hali nyingine. Mtu anayekufa, lazima amekuwa anaishi, na anakufa ili aishi tena.
Sisi binadamu tangu kutungwa mimba tumekuwa tukifa mara nyingi pasipo kutambua ndiyo maana Paulo kwa kulitambua hilo anasema kutwa kuchwa twakikabili kifo. Katika safari ya kukua, kutoka mimba, mimba inakufa mtoto mchanga anazaliwa, uchanga unakufa, utoto unazaliwa; utoto unakufa, na ujana unazaliwa; ujana unakufa, utu uzima unazaliwa na utu uzima unakufa, na uzee unazaliwa; na mwisho wa yote, maisha huingia kifo na kifo huingia maisha, kama usiku unavyoupisha mchana, kifo nacho hupisha maisha.Kwa hiyo tunaweza kusema, ni katika kuishi tunakufa na katika kufa tunaishi; lakini mwisho wa yote, kifo kitaangamizwa na uzima utatawala, kama anavyosema Nabii Isaya, “Bwana atakiangamiza kifo milele,” (Isa. 25:8); naye Nabii Hosea anauliza, “Ewe kifo, yako wapi maafa yako? Ewe kuzimu yako wapi maangamizi yako? (Hos.13:14); kwani “Kisha kifo na kuzimu vitatupwa ndani ya ziwa la moto,” (Ufu. 20:14). Kwa hiyo kifo kitaangamizwa na uzima utatawala.
Kwa asili yake kifo ni sehemu tu ya mpangilio wa maisha yetu ya hapa duniani. Kifo ni lile tukio la Roho na Mwili kutengana; lakini maisha yanaendelea baada ya utengano huu yaani maisha yenye muunganiko na Mungu wetu Mtakatifu. Mwili na roho vikitengana ndipo mwanadamu anakufa, lakini mtu anaendelea kuishi, akiwa amevaa mwili mwingine wa kiroho, wenye uzuri wa pekee tofauti na ule aliokuwa nao kwanza ndiyo kusema anakuwa na muungano na Mungu Baba huko mbinguni ambako malaika na watakatifu wanafurahi milele yote.
Katika mabadiliko haya, Mungu anatusindikiza daima na anatembea nasi bega kwa bega katika mabadiliko haya, maana Paulo anatuambia “kama tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana, na tukifa tunakufa kwa ajili ya Bwana,” (Rum.14:18). Kwahiyo Mungu anakuwa nasi katika kila hatua ya maisha. Na kwa namna hiyo, Mzaburi anasema, “Nijapopita katika bonde la giza kuu, sitaogopa mabaya wala hatari yeyote, maana wewe ee Mwenyezi Mungu u pamoja nami; gongo na fimbo yako vyanilinda”. Mt. Francisko wa Assisi, anasema, “Usifiwe, ee Bwana wangu, kwa ajili ya huyu dada yetu kifo cha mwili, ambapo hakuna mwanadamu yeyote, aweza kumkwepa. Ole wao watakao kufa katika dhambi ya mauti! Heri wale watakaokutwa katika mapenzi yako, kwani, kifo cha pili hakitawadhuru KKK 1014”.
Mtakatifu Yahane Paulo II, aliwahi kusema kuwa “ninapata amani tele ninapofikiria kuhusu wakati, ambapo Bwana ataniita kutoka maisha kwenda maisha.” Maana yake, anapata furaha na amani tele anapofikiria siku yake ya kufa, ambapo Mungu atamwita kutoka maisha haya ya duniani kuelekea Mbinguni kwenye maisha ya umilele. Mt. Theresa wa Avila, anasema, “nataka kumwona Mungu, nakumwona Mungu, lazima nife.” Tunapojiandaa kuanza kipindi hiki kitakatifu sana cha Kwaresima tukumbuke kuwa hapa duniani tu wapitaji. “Sisi ni Raia wa Mbinguni,” (Fil. 3:20). Huko ndiko tulikotoka, kwa maana tulitoka kwa Mungu na “Mungu wetu yuko mbinguni” (Zab.115:3a), kama tulitoka kwa Mungu aliye mbinguni, basi kumbe nasi tunapaswa kurudi mbinguni.
Huku duniani tuliko ni ugenini tu, kama tunavyosali katika sala ya salamu Malkia, “Mama mwenye huruma, uzima tulizo na matumaini yetu salamu, tunakusihi ugenini hapa sisi wana wa Eva” Maandiko Matakatifu yanasema, “wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani, yanaongeza kusema, Hapa maandiko matakatifu yamesema kitu kizuri sana, “Kama wangalikuwa wanaifikiria nchi waliyotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko” (Ebr. 11:15). Tukumbuke daima kuwa maisha ni kufa na kuishi, tumwombe Mungu atufundishe kuzihesabu siku za maisha yetu hapa duniani na kujua kuwa ni chache ili zinapoisha tuwe tayari tumejiandaa kurudi kwetu Mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo, Laudetur Iesus Christus!