Jumatano ya Majivu! Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Kipindi cha Kwaresima huanza na jumatano ya majivu na hudumu kwa muda wa siku 40 mpaka siku inayotangulia siku tatu kuu zinazotangulia Pasaka; yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo = KIINI CHA FUMBO LA WOKOVU WETU. Katika kipindi hiki, wakristo wanaalikwa kutafakari sana fumbo la wokovu wa Kristo na kuishi ubatizo wao kwa undani kabisa. Ni siku 40 za utakaso. Zaidi ya hayo, twakumbuka siku 40 alizokaa Yesu jangwani – akisali na kufunga – kabla ya kuanza utume wake. Leo tunaungana na wakristo wenzetu kufuata njia ya msalaba, ile ya Kalvari, tukitafakari kwa kina maana ya imani yetu na tukiishi katika matendo kile tunachokiamini. Leo tunapakwa majivu. Katika kitabu cha Mwa. 3,19 tunasoma hivi; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa, kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.
Siku ya Jumatano ya majivu tunapakwa majivu utosini au kisogoni. Maana yake nini? Alama hii yatukumbusha kuwa mwili wa mwanadamu u katika hali ya uharibifu na ukomo. Alama hii ikituelekeza kwenye matumaini makuu. Tunaishi tukitambua kuwa sisi si kitu na ulimwengu huu ni mahali pa kupita tu. Tunakiri na kukubali waziwazi mbele ya Mungu Baba Muumba wetu na mbele ya wenzetu kuwa sisi tumepungukiwa. Ni majivu tu. Lakini huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi zetu. Tunakiri dhambi zetu. Mtu mmoja anafanya tafakari hii: majivu ni masalio ya moto, makazi yake jalalani. Ila yakisugua sufuria yenye masizi huifanya kuwa nyeupe pe. Japo tu dhaifu, tuna thamani zaidi ya majivu.
Majivu yatufanye tuwe weupe. Alama ya pili ni sauti ya Yesu. Katika Mk. 1,16 – tunasoma - tubuni na kuiamini Injili. Na hapa Yesu anaanza safari yake ya kitume na unakuwa mwaliko kwetu, mwaliko wa kuelekeza matumaini yetu katika Neno la Mungu. Kipindi hiki kama tulivyosikia hapo juu – tunaalikwa kuwa karibu zaidi na Neno la Mungu kwa imani na matendo. Maisha ya mkristo ni maisha ya imani, yenye msingi wake katika Neno la Mungu – na anayelishwa na Neno la Mungu anao uzima wa milele. Njia kuu ya kushinda vishawishi na dhambi ni kusikiliza Neno la Mungu – ili kuwa na uwezo wa kukataa vishawishi vya shetani.
MHIMILI WA KWARESIMA: Kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Ikumbukwe kwamba, Neno la Mungu ni neno la ukweli, kuishi, kusema na kutenda ukweli na kukataa uongo ambao ni sumu kali inayoharibu ubinadamu wetu na mahusiano yetu na Mungu na wenzetu na ambao pia ni mlango wa dhambi zote. Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha toba katika kanisa Katoliki cha siku zipatazo 40 tangu Jumatano ya majivu mpaka siku kabla ya siku 3 kuu zinazotangulia Jumapili ya Pasaka au Jumapili ya ufufuko wa Bwana. Tunapofunga tunatakiwa kuzuia vilema vyetu na kuviacha kabisa, tunaomba kujaliwa moyo wa toba, tunainua mioyo yetu na tunaomba Mungu atujalie nguvu na tuzo.
Haitoshi tu kukiri makosa yetu bali tunahimizwa kuungama na kutubu hayo makosa na kuwa tayari kuanza upya. Kipindi cha Kwaresima huanza tangu Jumatano ya majivu. Mwanzoni mwa kazi yake ya kuhubiri Habari njema Yesu anaanza kwa kusema tubuni na kuiamini Injili – Mk 1,15. Maneno haya haya tunayasikia/tumeyasikia kila tunapopakwa majivu. Mwaliko huu wa Yesu unatuingiza katika kipindi cha toba – tubuni na kuiamini Injili. Huu ni mwaliko wa uzima. Ni mwaliko ili tuongoke, tuanze maisha mapya, maisha ya sala, kufunga na kutoa sadaka.
SALA: Kwa kifupi kusali kwa mkristo maana yake ni kuruhusu upendo wa Mungu utawale ndani ya mioyo yetu na hivyo kuwa katika mwelekeo wa kusikiliza sauti za ndani ya mioyo ya mwanadamu na kujiweka mbele yake na vyote tulivyo navyo. Kusali kwa mkristo ni kuishi maisha ya sala kama sadaka na sifa kwa Mungu Muumba wetu. Sala pia inatuunganisha na Yesu, kanisa na historia yake kwa ujumla na inatusaidia kufunua mioyo yetu mbele ya Roho Mtakatifu ambaye anafanya kila kitu kuwa kipya. Kwa ufupi sala katika utatu Mtakatifu ndiyo jambo ambalo kila mwanadamu anapaswa kulitambua na kuligundua kipindi hiki.
KUFUNGA: Kufunga kwa asili ya kiroho ina maana kubwa katika elimu ya mambo ya mwisho hasa inapotokea kuwa kuna jambo kubwa linalosubiriwa. Ni kama vile mahitaji ya mwanadamu ya kula yanashika nafasi ya pili kwa vile mwanadamu analishwa na hamu hiyo na matarajio hayo. Hicho ndicho chakula chake. Utamaduni wa kikristo wa kufunga unawakilisha zaidi ya yote ukomo wa matarajio ya kumngoja bwana na kufungua mioyo yao, na kujinyima kwa kila kitu ambacho kinaonekana kuwa ni kikwazo kuwa karibu na Mungu. Ni kungojea kwa hamu kubwa, chukua mfano wa mtu anayeshinda njaa akipata chakula atakavyokifurahia. Kwa kufunga tunatengeneza nguvu za kutawala miili yetu, vionjo vyetu n.k.
Kwa kufunga tunakuwa na uwezo wa kuiambia miili yetu kile tutakacho kufanya. Mfano tunajinyima chakula fulani kitamu, kizuri au kitu kitamu na kizuri tukipendacho na katika kujinyima huko tunatoa msaada au kujinyima huko tunawasaidia wengine ili nao washiriki nasi upendo huo. Au kwa kutoendeleza mapenzi yetu tu, tukijinyima kufanya hilo tulipendalo tunapata muda wa kufanya jambo fulani jema kwa ajili ya wengine. Na hapa wakristo wanaalikwa kuwa makini – huwezi kufunga na kufaidi tena hicho hicho unachopenda kukiacha. Kwa tendo la kufunga tunapata uwezo wa kuiambia miili yetu kile tupendacho kufanya na si miili yetu ituambie kile cha kufanya. Kwa maana hiyo basi, kufunga kunamaanisha ni hija kuelekea kipindi cha pasaka na hivyo mwanadamu anapaswa kutambua kuwa tunamhitaji Mungu kama chanzo cha uwepo wetu na pia kujiweka wazi ili Mungu aweze kuwa ndani yetu.
MATENDO YA HURUMA – KUTOA SADAKA: Matoleo mengineyo mema zaidi ya utoaji wa sadaka pia ni mwelekeo wa moyo. Moyo ambao ni mpole, wa toba, wenye huruma na wa faraja ambao unatafuta mahusiano na wengine katika kuhurumia wengine ili kukuza mahusiano na Mungu. Kwa hiyo au sadaka yaonesha kujali, kufanya kitu halisi, zawadi ambayo waamini wanatoa wanapojaribu kuwazia upendo wa Mungu ambao unawakubali na kuwasamehe. Je Mungu ametujalia mambo mangapi mema? Sisi tumemrudishia nini? Kwa asili na maana ya kutoa sadaka ni kupoteza pia. Huwezi kutoa sadaka na kutarajia hapo hapo kufaidi yote pia. Mfano mzuri ni Bwana wetu Yesu Kristu – alitoa uhai wake kwa ajili yetu. Hii ndiyo changamoto iliyo mbele yetu leo hii. Ni wangapi tuko tayari kutoa sadaka kwa ajili ya wengine? Kujitoa kweli kwa hali na mali? Bila manung’uniko. Bila kudai faida?
Hakika kipindi hiki cha Kwaresima ni muda wa kuangalia upya thamani ya sadaka ndogo, alama ya upendo, inayotolewa kwa unyenyekevu, kwa siri na ambayo ni halali, ambayo inakugharimu, na inafanywa katika kumtukuza Mungu katika wale wanaotaabika, na wahitaji. Tukijenga tabia au mazoea ya kutoa kwa ajili ya wahitaji tunajenga pia mazoea ya kuwa huru na mambo ya dunia hii yanayopita. Kila mmoja wetu ana hitaji fulani katika maisha yake, hakuna tajiri kabisa kwamba hana cha kupokea au maskini sana kwamba hana cha kutoa. Kutoa ni moyo na si utajiri. Tuonje tena katika kipindi hiki furaha ya kutoa kuliko ile ya kupokea.
Hakuna upendo bila sadaka, hivyo hivyo upendo bila sadaka inakuwa kama alama ya nje tu. Sadaka ni matoleo ya upendo na tusisahau mfano mkubwa alioutoa Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu alitupenda sana hata akamtwaa mwanae wa pekee kwa ajili yetu sisi sote. Kama Mungu amejitoa kwetu je sisi tunamrudishia nini? Ndugu zangu, kufunga kwaonesha heshima yetu mbele ya Mungu, kutambua na kukubali udhaifu wetu mbele ya Mungu na wenzetu (kujipaka majivu), kwamba tu wadhambi na na kwamba tuko tayari kufuata njia ya Bwana, yaani njia ya wokovu. NASI TUINGIE KATIKA NJIA YA BWANA ILI TUWEZE KUPATA WOKOVU WA MUNGU.