Liturujia Neno la Mungu: Kwaresima IV: Baba Mwenye huruma!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 4 ya Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Tunasukumwa kuzama zaidi katika Injili ya Baba mwenye huruma, maarufu kama Injili ya Mwana mpotevu, ili kugusa na kuonja huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa wale wote wanaotubu na kumwongokea kutoka katika undani wao!
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Yos 5:9, 10-12) ni kutoka Kitabu cha Yoshua. Ni somo ambalo linatupeleka katika maisha ya waisraeli mara tu baada ya kuvuka mto Yordani na kuingia katika nchi ya ahadi. Ni tukio lililokamilisha safari yao ya miaka 40 jangwani baada ya kutoka utumwani Misri. Linaanza na maneno ya Mungu mwenyewe kwa Yoshua kuwa “siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu”. Ndiyo kusema Mungu amekamilisha tukio la kuwakomboa watu wake. Amewaondoa moja kwa moja toka mikono ya wamisri na amewaongoza hadi kuwaingiza katika nchi aliyokuwa amewaahidia.
Wakaadhimisha kwa mara ya kwanza katika nchi ya ahadi sikukuu ya Pasaka, sikukuu ambayo kwao ilikuwa ni kuadhimisha ukombozi wao kutoka Misri. Hii ilifuatiwa na matukio mengine mawili makubwa; kwanza ile mikate iliyokuwa ikishuka kutoka mbinguni kama chakula chao walipokuwa jangwani ilikoma na pili wakaanza kula mazao ya nchi (mazao ya mashamba). Haya ni matukio yanayoonesha mwendelezo wa wema wa Mungu kwa watu wake. Mikate iliyowashibisha jangwani ilitoka kwa Mungu na hapa wanaanza kula mazao ya mashamba ambayo hawakuyapanda bali waliyakuta. Mungu aliyewakomboa anawahakikishia kuwa kwa wema wake ataendelea kuwahifadhi.
Somo la pili (2Kor 5:17-21) ni Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho. Paulo anazungumzia hali mpya anayoipata mwanadamu baada ya kujipatanisha na Mungu. Upatanisho huu unamfanya mtu kuwa kiumbe kipya. Kwa mtume Paulo, kama anavyoeleza katika barua zake kwa warumi na wagalatia, kukutana na Kristo ni kuwa tayari kuanza maisha mapya na kuyaacha maisha ya kale yanayopingana na hali mpya ya maisha ndani ya Kristo. Hapa katika somo hili anaendelea kuonesha kuwa upatanisho na hali mpya ya maisha ndani ya Kristo ni kazi anayoianza Mungu mwenyewe ndani ya mtu. Anasema “vyote vyatokana na Mungu na ni Mungu aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo”.
Na anaendelea kuongeza “naye – yaani Mungu- ametia ndani yetu neno la upatanisho. Hapa anaposema ametia ndani yetu, Paulo anajiongelea yeye mwenyewe na mitume wengine na neno la upatanisho analolizungumzia ni huduma ya upatanisho waliyokabidhiwa mitume kuiadhimisha katika sakramenti. Na ni kwa sababu hii, Paulo kama mhudumu wa upatanisho anawasihi wakristo wa Korinto wajipatanishe na Mungu. Anawasihi waipokee neema hiyo ambayo kwa Mungu ipo tayari wazi na inahitaji tu utayari wa waamini wenyewe.
Injili (Lk 15:1-3, 11-32) Injili ya leo inajulikana sana kama Injili ya Baba mwenye huruma, ingawa kwa wengi bado inajulikana kama Injili ya Mwana mpotevu. Tunapoangalia mwanzo wa simulizi lenyewe tunaona kuna makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni la watoza ushuru na wenye dhambi wanaomkaribia Yesu wamsikilize. Kundi la pili ni la mafarisayo na waandishi ambao wanaanza kunung’unika au tuseme wanachukizwa na tendo la watoza ushuru na wenye dhambi kumkaribia Yesu ili kumsikiliza. Ni katika mazingira haya Yesu anatoa mfano huo wa baba aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo aliyeomba urithi, akatoka nyumbani akaenda kutapanya mali aliyopewa na yule mkubwa ambaye daima alibaki nyumbani na baba yake. Kumbe, tunaweza kusema kuwa katika hao wana wawili Yesu alikuwa akichora picha ya makundi hayo mawili ya watu.
Yule mwana mdogo, anayeitwa mpotevu, katika vipimo vyote alifanya kosa. Na ndivyo walivyokuwa wakionwa watoza ushuru na wadhambi. Jina tu lilionesha hukumu ambayo jamii ilikuwa imeshawapa tayari. Polepole katika simulizi tunaona pia kuwa hata yule mkubwa alikuwa ni mkosefu vile vile kama yule mdogo: mdogo aliondoka nyumbani akajitenga na ndugu zake, mkubwa alikataa kuingia ndani na alijitenga na nduguye kwani hakumwita “mdogo wangu” bali “mwanao”. Zaidi ya hayo, kijana mkubwa alijihesabia haki kwa kazi alizokuwa akizifanya. Na wala hakuzifanya kwa upendo bali daima alikuwa na matarajio ya kujinufaisha na kufurahi na rafiki zake. Huyu kijana mkubwa aliwawakilisha Mafarisayo na waandishi.
Ni Injili inayoonesha sote ni wakosefu kwa namna moja au nyingine. Inatahadharisha dhidi ya kishawishi cha kujihesabia haki na kufurahia zaidi maangamizi ya wenye dhambi kuliko wongofu wao. Ni Injili ambayo zaidi ya yote inaonesha huruma kubwa ya Baba aliye tayari kumpokea yeyote yule anayemwendea kwa moyo wa toba akitaka kujipatanisha naye.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Kanisa linatualika katika dominika hii kutafakari juu ya huduma ya upatanisho yaani habari ya ondoleo la dhambi. Bwana wetu Yesu Kristo baada ya ufufuko wake aliwapatia mitume na waandamizi wao huduma hii. Yaani wahubiri kuhusu msamaha na maondoleo ya dhambi kwa njia ya Kristo na pia waadhimishe kwa jina lake ondoleo la dhambi kwa njia ya ubatizo na Sakramenti ya upatanisho ambamo kwa huduma ya Kanisa watawapatanisha watu na Mungu. Kanisa limepokea funguo za ufalme wa mbinguni ili ndani yake ondoleo la dhambi lifanyike kwa njia ya damu ya Kristo na kwa tendo la Roho Mtakatifu. Ndani ya Kanisa hili, ambamo roho iliyokuwa imekufa kwa sababu ya dhambi, inazaliwa upya iweze kuishi pamoja na Kristo Yesu, ambaye neema yake imetuokoa.
Masomo ya leo yametuonesha kuwa sote tunaihitaji huduma hii ya upatanisho kwa sababu kwa namna moja au nyingine, tunamkosea Mwenyezi Mungu na tunawakosea wenzetu. Makosa yetu haya yanatulemea na yanatuondolea hadhi yetu kama watoto wa Mungu kwa sababu yanaiondoa neema ya utakaso iliyo ndani yetu. Masomo pia yanatuonesha pia kuwa wema wa Mungu ni mkubwa mno kwa wakosefu wanaotubu. Yeye kama baba mwenye huruma hutungoja daima bila kuchoka. Huingoja siku tutakayozingatia hali yetu na kuamua kurudi kwake. Hutungoja lakini akituwekea mbele yetu misaada yote tunayohitaji ili kurudi. Unabaki tu utashi wetu wa kusema kama yule mwana mpotevu: nitaondoka, nitakwenda kwa baba na nitamwambia baba nimekosa juu ya mbingu na mbele yako.” Kipindi hiki cha kwaresima kiwe ni kipindi kwetu cha kujipatanisha na Mungu na wenzetu.