Liturujia ya Neno la Mungu: Kwaresima: Amesikia, Ameona, Ameshuka!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 3 ya Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Mwenyezi Mungu ameyaona mateso ya watu wake, akasikia kilio chao na ameshuka ili kuwaokoa! Ni wakati wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuchuchumilia neema, kuambata utakatifu wa maisha! Kipindi cha Kwaresima, kitoe hamasa ya toba na wongofu wa ndani, ili kujiandaa vyema kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa!
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Kut 3:1-8a, 13-15) ni kutoka kitabu cha Kutoka. Ni somo linaloelezea kuitwa kwa Musa na kutumwa kwenda kuwakomboa waisraeli. Musa anatokewa akiwa anachunga katika mlima Horebu, mlima ambao unaitwa pia mlima Sinai. Uwepo wa Mungu unaoneshwa na kutokea kwa malaika pamoja na kuwepo kwa kijiti kinachowaka moto lakini hakiteketei. Mungu anapomwita Musa anautambulisha uwepo wake kuwa ni utakatifu, utakatifu ambao unabadilisha kila kitu hata mahala na utakatifu ambao unahitaji kiwango fulani cha heshima. Ni kwa sababu hii Mungu anamwambia “usikaribie, vua viatu kwa sababu mahali unaposimama ni patakatifu”. Ndipo Mungu anamwambia Musa, nimeyaona mateso ya watu wangu, nimesikia kilio chao nami nimeshuka ili niwaokoe.
Nimesikia, nimeona na nimeshuka ndiyo matendo ambayo tangu hapa yanamhusianisha Mungu na Waisraeli na sio hao tu bali na watu wake wote wanaoteseka: Mungu anawatangazia kuwa daima husikia kilio chao, huyaona mateso yao na kwa wakati wake hushuka kuwaokoa. Jamii ya Misri aliyokuwa anatumwa Musa ilikuwa ni jamii ya watu wanaoabudu miungu wengi, na kila mungu alikuwa na jina lake. Kwa jinsi hii Musa anauliza, nitakapoulizwa ni Mungu yupi amekutuma nisemeje. Mungu anatambulisha jina lake ambalo ndilo utendaji wake. Anasema ni “Mimi niko Ambaye Niko”. Mimi niko ni Mungu aliye hai na anayebaki hai daima – Ambaye Niko ni Mungu anayevipa vitu uhai, sifa inayoonesha nguvu na uwezo wake. Ndiye aliyevifanya vitu viwe hai na ndiye anayeendelea kuvifanya viwe hai. Hiki ni kiashirio cha uaminifu wake.
Somo la pili (1Kor 10:1-6, 10-12) ni waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorinto. Katika somo hili Paulo anawalinganisha wakristo wa Korinto na baba zao waisraeli wakati wa Musa. Kulielewa vema ingefaa kurudi nyuma sura chache kuona ni nini alichokuwa akikizungumzia Paulo. Huko tunaona kuwa Paulo alikuwa akiwakanya wakorinto dhidi ya ibada za sanamu na miungu wengine na dhidi ya mmomonyoko mkubwa wa maadili waliokuwa nao. Katika somo la leo anawaonesha kuwa wao kama wakristo wanaposhiriki mambo hayo wajue kuwa watawajibishwa na Mungu mwenyewe.
Ndipo anawaonesha kuwa baba zao waisraeli wao pia walipopitishwa bahari ya shamu ni kama walibatizwa kwa sababu waliokolewa toka utumwani. Wao pia walipokea jangwani chakula cha kiroho kama ambayo wakristo wa korinto wanakipokea katika Ekaristi na sakramenti nyingine. Pamoja na hayo, Paulo anawaonesha kuwa Mungu hakupendezwa na wengi wao na ndiyo maana aliwaangamiza jangwani wasiifikie nchi ya ahadi. Na aliwaangamiza kwa sababu hawakuenenda kadiri ya ukombozi walioupokea bali walimnung’unikia Mungu. Hapo Paulo anawaambia wakorinto kuwa mambo yote hayo yameandikwa kama mifano ili kuwaonya ili wasiangukie nao chini ya gadhabu ya Mungu siku ya hukumu.
Injili (Lk 13:1-9) injili ya leo, kadiri ya Mwinjili Luka inatoa mwito wa kutubu. Mwito huu unakuja ndani ya masimulizi mawili na mfano mmoja ambao Yesu anautoa. Katika masimulizi mawili ya mwanzo kuna tukio ambalo Pilato aliwaangamiza wagalilaya waliokuwa wakitoa dhabihu hekaluni. Aliwaua akachanganya damu yao na zile dhabihu walizokuwa wakizitoa. Simulizi la pili ni lile la watu 18 walioangukiwa na mnara wakafa. Tafsiri ya jumla kadiri ya Agano la Kale juu ya ajali au majanga kama hayo yaliyokuwa yakiwakuta watu ilikuwa inayahusisha majanga hayo na dhambi. Na Yesu alielewa watu wa nyakati zake wangekuwa pia na mtazamo huo. Yeye lakini hayaoni majanga hayo katika mtazamo huo, bali anaenda zaidi ya hapo na anawauliza – Je, mnadhani hao waliokumbwa na majanga hayo ndio walikuwa wadhambi kuliko wengine wote waliosalia? Kwa kweli jibu ni hapana, japo wasikilizaji wake hawakulitoa.
Kama ni hivyo sasa tunayaelezeaje hayo yaliyotokea? Hapo Yesu anatoa mfano wa mtini tasa. Mtini ambao kwa miaka 3 tangu upandwe haukuwa umetoa matunda na mwenye shamba akaazimia kuukata. Kwa mtini kutoa matunda huchukua hadi miaka 6 japo ipo mitini inayoanza kutoa matunda baada ya miaka 2. Ndiyo maana mtunzaji wa shamba anaomba auongezee mwaka. Kumbe miaka 3 ni kipindi kifupi. Ni kwa miaka hiyo hiyo 3 ambayo Yesu alifanya utume wake na kuwaalika wote kuipokea Habari Njema. Kwa mfano huu Yesu anaalika watu kutambua kuwa muda uliobaki ni mfupi: watu watubu na zaidi ya toba wajitahidi kuzaa matunda ya matendo mema. Kila nafasi Mungu anayomjalia mtu ni nafasi ya kurekebisha uhusiano wake na Mungu.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tulikianza kipindi hiki cha Kwaresima kwa kupakwa majivu na kwa mwaliko wa kutubu na kuiamini Injili. Maandiko Matakatifu katika dominika ya leo yanaleta upya mwaliko huo wa Kwaresima, mwaliko wa kufanya toba. Tunaalikwa kufanya toba kwa sababu tayari Mungu amekwisha tuonesha nguvu zake na uwezo wake wa kuokoa. Katika somo la kwanza Mungu mwenyewe amejifunua kwa Musa na kwa njia yake amejifunua kwetu sote kuwa ni Mungu anayeona mateso ya wamwombao, ni Mungu anayesikia kilio chao na ni Mungu anayeshuka kuwaokoa kwa sababu anao uwezo, yupo, ndiye huvipa uhai na neema vitu vyote na ni Mungu mwaminifu. Ufunuo huo wa Mungu mwenyewe ni mwaliko na kichocheo cha kutokuona haya kumrudia kwa toba.
Maandiko Matakatifu yanatualika pia kufanya toba kwa kuwa ipo hukumu ya mwisho, hukumu ambayo kila mmoja wetu atawajibika kwa vile alivyoishi na kutenda katika mahusiano yake na Mungu na jirani. Mtume Paulo anaonesha uwepo wa hukumu hii akirejea ile hukumu ya awali ambayo Mungu aliwapa waisraeli waliomwasi jangwani, hakuwaruhusu waingie katika nchi ya ahadi – waliangamia wote. Na anaongeza kusema kuwa yote hayo yalitokea kama mfano kwetu. Kristo katika injili anaonesha kuwa upo uharaka wa kutubu kwa sababu muda tulionao ni mfupi. Na kuwa kila nafasi ya uhai tunayopewa ni nafasi ya neema ya kutusaidia siku kwa siku kujisogeza kwa Mungu. Kama Kanisa linavyotufundisha kuwa toba na wongofu ni kazi ya neema ya Mungu anayefanya mioyo yetu imrudie (KKK 1432), tuiombe neema hiyo ili kipindi hiki cha kwaresima kiwe ni wasaa wa kuiishi toba na kumrudia Mwenyezi Mungu kutoka hali zisizofaa katika maisha yetu.