Neno la Mungu Jumapili VIII: Linda Moyo wako kitovu cha utu wako!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 8 ya Mwaka C wa Kanisa. Changamoto kubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kuhakikisha kwamba, wanalinda moyo wao kwa ni moyo ni kitovu cha utu na heshima ya binadamu! Watu wenye moyo mwema, wanatambulikana kwa maneno na matendo yao!
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Ybs 27:5-8) ni kutoka Kitabu cha Hekima ya Yoshua bin Sira. Kama jina lenyewe linavyodokeza, hiki ni kitabu ambacho kimo katika kundi la vitabu vya Agano la Kale vinavoitwa vitabu vya Hekima. Navyo ni kitabu cha Ayubu, cha Mithali, cha Mhubiri cha Hekima ya Sulemani na hiki cha Hekima ya Yoshua bin Sira. Kwa ujumla vitabu hivi vinalenga kuanza kutoka katika uzoefu na mang’amuzi ya maisha na kufika katika kweli zile zile za kimungu kadiri ya ufunuo.
Katika mazingira hayo, somo la kwanza la leo linazungumza juu ya utu wa mtu. Na linalenga hasa kuonesha ni nini kipimo cha thamani ya utu wa mtu. Na hapo linatuonesha kuwa ni maneno yake. Mwandishi anasema usimsifu mtu kabla ya kumsikia anachoongea. Ni maneno yake yataonesha kama matunda yanavyoonesha mti uliopandwa vizuri au kama chekecheo inavyoruhusu mbegu nzuri zipite na kubaki juu na makapi. Maneno ya mtu ni zaidi ya kile anachokisema, humfunua mtu mwenyewe jinsi alivyo. Ni ujumla wa namna yake ya kufikiri, mtazamo wake juu ya maisha, namna yake ya kukabiliana na hali mbalimbali za maisha, mwono alionao juu ya wenzake, misimamo yake n.k. Kumbe kwa namna fulani somo hili linatualika tuyaangalie mambo haya na kuyapatia mwelekeo unaofaa kwani ndiyo hasa yanayoonesha thamani ya utu wetu.
Somo la pili (1Kor 15:54-58) ni Waraka kwa kwanza wa Mtume Paulo kwa wakorinto. Mtume Paulo anahitimisha fundisho kuhusu ufufuko wa wafu kwa wakristo wa Korinto. Anahitimisha kwa kuonesha kuwa ufufuko wa wafu upo kwa sababu Kristo kwa sadaka yake Msalabani amekiangamiza kifo. Amekibadili kutoka adhabu kama ilivyotolewa baada ya anguko la Adamu na Eva (Rej. Mwa. 3:19) kuwa mlango wa maisha mapya. Na maisha haya yanaanza baada ya ufufuko. Anahitimisha fundisho hili kwa kuonesha kuwa ufufuko wa wafu utakuwa ni kudhihirisha kuwa kifo nacho kitaangamizwa. Kile kilichoonekana kumeza maisha ya watu sasa chenyewe kinamezwa; kile kilichoonekana kushinda sasa chenyewe kinashindwa na kilichoonekana kutia watu uchungu sasa kinaondolewa uchungu wake. Uchungu unaobaki ni dhambi kwa maana dhambi huua, humtenga mtu moja kwa moja na furaha ya ushindi wa Kristo dhidi ya mauti. Ndiyo maana Mtume Paulo mwishoni anawasihi wakorintho wazidi kuimarika, wasitikisike na wazidi kuitenda kazi ya Bwana ili wasijiruhusu kuanguka katika dhambi.
Injili (Lk 6:39-45) injili ya leo, kadiri ya Mwinjili Luka, inaendeleza mafundisho ya Yesu kwa umati uliokuwa ukimsikiliza. Yesu anahama kutoka mafundisho ya moja kwa moja na sasa anaanza kuwafundisha kwa mifano. Anatoa mifano mitatu: wa kwanza ni kuhusu kipofu, kwamba aliye kipofu awezaje kuongoza kipofu mwenzake kama si wote wawili kutumbukia shimoni? Mfano wa pili wa yule aliye na boriti katika jicho lake na anamwambia mwenzake aliye na kibanzi kwenye jicho “niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako”. Mfano wa tatu wa mti na matunda: kwamba hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya wala mti mbaya uzaao matunda mazuri.
Kipofu ni mtu anayehitaji msaada. Hawezi katika hali yake kumuongoza mwingine anayehitaji msaada. Kumbe kwanza anahitaji apate kiongozi, yeye afuate nyayo za kiongozi na ndipo anapoweza kumshika mkono kipofu mwingine amuongoze. Mfano huu unawaelekea kwanza mitume, watakaochukua nafasi ya kutangulia mbele ya wafuasi, lakini pia unawaelekea wafuasi wote wa Kriso kwamba wamweke daima mbele yao Kristo kama kiongozi na mwalimu na wote pamoja wafuate nyayo zake ili wasiingie shimoni. Katika safari hiyo ya kumfuasa Kristo, mfano wa pili unawaalika wafuasi kuchukuliana. Lipo hitaji la kurekebishana pale mmoja anapokosea na huu ni wajibu wa msingi.
Kristo anataka yule anayechukua wajibu wa kumrekebisha mwingine amrekebishe akijua kuwa na yeye anayo mapungufu yake na inawezekana yakawa makubwa kuliko ya yule anayerekebishwa. Si mfano unaozuia maonyo au kukosoana. Ni mfano unaozuia kuwahukumu wengine. Mfano wa tatu, sambamba na miwili iliyotangulia, unalenga kuonesha utu wa ndani na utu wa nje wa mtu. Matendo ya mtu daima ni matokeo ya undani alionao katika utu wake, kutoka katika hazina njema ya utu wa ndani hufuata matendo mema na kutoka katika hazina mbaya ya utu wa ndani hufuata matendo mabaya.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News tunaweza kuufupisha ujumbe wa leo katika mstari mmoja: “linda moyo wako, ndio kitovu cha utu wako”. Tunasema hivyo kwa sababu masomo ya dominika hii yanatualika tuyaone matendo ya mtu na yote anayofanya kuwa ni kama matokeo tu ya kile kilicho ndani yake. Ndani ya mtu ni katika moyo wake. “Moyo ndipo mahali ambapo nipo, ndipo mahali ninapoishi” inatuambia Katekisimu ya Kanisa Katoliki na kuendelea kuwa “moyo ndipo kiini chetu kilichofichika, kisichoweza kufikiwa na akili yetu wala na akili ya wengine.
Moyo ni mahali pa uamuzi, penye kina zaidi kuliko maelekeo yetu ya kiroho na ndipo mahali pa kweli pale ambapo tunachagua uhai au kifo (Rejea. KKK n. 2563). Moyo ukiwa mwema, kutoka katika wema wake maneno ya ulimi na matendo ya mtu yatakuwa mema. Ni kama ule mti mzuri ambao kwake hutoka matunda mazuri. Moyo ukiwa mwovu, kutoka katika uovu wake maneno ya ulimu na matendo ya mtu yatakuwa maovu. Katika uwiano kati ya moyo wa mtu na matokeo ya maneno na matendo yake yafaa kutambua kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kuwa mwema na kuonekana mwema. Kuonekana mwema, ni sifa ya nje ambayo mtu anaipata kutoka kwa wale wanaoyapima maneno na matendo yake.
Huku hakutoshi kama hakuna msukumo wa wema kutoka ndani ya mtu. Kwa wenyewe, kusisitiza tu kuonekana mwema ni kujidanganya mwenyewe na ni kama ulaghai kwa nafsi yako mwenyewe. Mwaliko wa leo wa kulinda moyo ni mwaliko wa kujenga dhamiri; kuilea na kuilinda ili idumu kuwa hai na sahihi. Dhamiri iliyo hai na sahihi ni ngome imara dhidi ya mivuto isiyofaa, dhidi ya vishawishi na dhidi ya ukaidi ambapo hata kama mtu ataona ukweli na kuutambua kuwa ni kweli bado kwa kupendelea hukumu binafsi ataukataa. Mwaliko wa kujenga dhamiri ni mwaliko endelevu na hudumu maisha yote.
Na katika malezi ya maadili ya kikristo, Kristo ndiye mfano wa pekee wa kufuata. Katika maisha yake ametuonesha namna ifaayo ya kuhusiana na watu na akatufundisha namna pia ya kuhusiana na Mungu Baba. Kulisikiliza Neno lake, kuziadhimisha na kuzipokea sakramenti zake na kukubali kuongozwa naye aliye Njia, Ukweli na Uzima ndiko kuulinda undani wa mioyo yetu dhidi ya uovu.