Alhamisi Kuu: Ekaristi: Sadaka, Shukrani, Kumbu kumbu & Uwepo
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, siku ya Alhamisi kuu, siku ya kwanza kati ya siku tatu kuu za Pasaka, alhamisi kuu, ijumaa kuu na jumamosi Takatifu. Hizi ni siku tunazoadhimisha fumbo la wokovu wetu, yaani Mateso, Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda huo wa siku tatu, na sio maadhimisho matatu yanayotofautiana. Leo kanisa linaadhimisha mambo makuu matatu aliyoyaweka Bwana wetu Yesu Kristo; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Amri Kuu ya mapendo na Sakramenti ya Daraja Takatifu. Hivi alhamisi kuu ni siku ya mapadre tuwaombee na kuwapongeza pia.
Fumbo Kuu la Pasaka tunaloliadhimisha linaanza rasmi na adhimisho la Karamu ya Mwisho mlo aliokula Yesu na wanafunzi wake muda mfupi kabla ya kukamata, kuteswa na kufa msalabani. Kitabu cha kutoka kinatupa simulizi jinsi Wayahudi walivyoadhimisha mlo wa Kipasaka, wakikumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri. Sherehe hii iliadhimishwa kifamilia. Baba wa nyumba ndiye aliyeongoza maadhimisho haya. Maandalizi yalifanywa kwa kuandaa chumba cha sherehe, mwanakondoo aliyeokwa, mikate isiyotiwa chachu, mboga chungu na vikombe vinne vilivyojaa divai. Mikate isiyotiwa chachu iliwakumbusha haraka yao walipoondoka Misri na mboga chungu iliwakumbusha mateso waliyopata walipokuwa utumwani Misri.
Wakati sherehe mzee wa familia, alichukua kikombe cha kwanza kilichojaa divai na kumshukuru Mungu kisha kukirudisha mezani, alielezea sababu ya upekee wa mlo huo, baada ya kuulizwa swali na mtoto nini maana ya mlo huu. Baada ya kuotoa maelezo, alichukua kikombe cha kwanza cha divai na kunywa, kisha aliwapa na wengine wanywe. Waliimba zaburi ya 113, zaburi ya aleluya, kisha walikunywa kikombe cha pili cha divai. Baba wa familia alikibariki chakula na wote walikula pamoja. Kisha kikombe cha tatu cha divai kililetwa, na wote walikunywa na kuimbwa zaburi za 115 hadi118 kishwa walikunywa kikombe cha nne cha divai na sherehe ilifungwa.
Yesu na wanafunzi wake waliadhimisha sikukuu hiyo kwa mlo huu wa Kipasaka. Lakini mlo huu ni tofauti na ule waliokula wayahudi. Kwanza, Kristo ndiye Mwanakondoo mwenyewe, hivyo hawakuwa na haja ya kuchinja na kuandaa mwanakondoo. Mtume Paulo anatuambia “Bwana wetu Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu (1Kor.11:23-25). “Maana kila mlapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo” (1Kor 11:26). Namna hii Yesu aliweka Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho.
Katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Yesu yupo mzima, mwili wake na Damu yake, ubinadamu na Umungu wake katika maumbo ya mkate na divai. Amefanya hivyo ili akae nasi, tuongee naye tumueleze hali zetu, shida zetu, matatizo yetu, furaha na huzuni zetu. Yupo nasi katika neno lake, yupo nasi katika Ekaristi, yupo nasi katika Makasisi wake, yuko tayari kutusikiliza wakati wote. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unatufundisha kuwa kila Sadaka ya Ekaristi inapoadhimishwa, kazi ya ukombozi wetu inafanyika kwa ukamilifu wake (SC 2). Huu ndio utajiri tulionao katika Ekaristi kwamba tunasamehewa dhambi zetu na kurudishiwa uhusiano na urafiki wetu na Mungu katika Sadaka ya Misa Takatifu. Ekaristi, hutuunganisha na Kristo, hudhoofisha nguvu ya dhambi na ni amana ya uzima wa milele. Kwa hiyo, tuipende Ekaristi, tushiriki maadhimisho ya Misa Takatifu na Kupokea Ekaristi. Hii ndiyo amana aliyotuachia Yesu Kristo.
Alhamisi kuu Yesu alituchia wosia wa kupendana, akisema pendaneni kama mimi nlivyowapenda ninyi. Yesu anatoa mfano rahisi sana lakini ni mgumu kuuelewa. Yesu aliye Bwana na mwalimu, mfalme, masiha, mwokozi, Mungu kweli katika nafsi ya pili, anajishusha, anajinyenyekeza, kwa upendo na utii anawaosha wanafunzi wake miguu. Petro hakuelewa mapema jambo hili na Yesu anamwambia nilifanyalo sasa huwezi kulielewa. Kisha anawaambia kama mimi niliye mwalimu nimefanya hivi ninyi nanyi fanyeni vivyo hivyo. Upendo ni utambulisho wetu ndiyo maana Yesu anatuambia mkipendana ninyi kwa nini watu watawatambua kuwa mu wafuasi wangu. Upendo ni kuiweka nafsi ndani ya nafsi nyingine na hivyo unayempenda anaweza kuhisi kile unachohisi, iwe ni uchungu, furaha, au maumivu, kwani uko ndani yake naye ndani yako.
Ndiyo maana Yesu anasema “Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu” (Yn.15:4), “mtu akinipenda atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda nasi tutakuja kwake na kukaa naye” (Yn. 14:23). Upendo ni kutoa, Yesu amejitoa mwenyewe ili akae nasi katika Ekaristi. Upendo ni kumwambia siri zako umpendaye, Mungu ametuambia siri za umungu wake kwa njia Yesu Kristo. Upendo ni kuteseka kwa ajili ya umpendaye, Yesu ameteseka kwa ajili yetu juu ya mti wa Msalaba (Yn.15:13). Upendo hutamani kuungana na umpendaye, Mungu ametuahidi heri ya milele mbinguni. Ndiyo maana mtume Paulo anauliza, “nani awezaye kututenga na upendo wa Kristo? Je ni taabu, au dhiki, au mateso, au njaa, au ukosefu wa nguo, au hatari, au kifo?” (Rum. 8:35), anajibu, hakuna kiwezacho kututenga na upendo wa Kristo: wala kifo, wala uhai, wala malaika au nguvu nyingine za mbinguni, wala yanayotokea sasa, wala yatakayo tokea baadaye; wala mamlaka; wala ulimwengu wa juu, wala wa chini kabisa, (Rum. 8:38-39) maana upendo daima huvumilia, ni mpole, hauna wivu, haujidai, haujivuni, una adabu, tena hautafuti faida yake binafsi, haufurahii maovu, bali ukweli. (1Kor. 4-6). Hii ndiyo hali halisi ya upendo na hii ndiyo amri ya mapendo na wosia aliotuachia Yesu siku ya alhamisi kuu.
Alhamisi kuu Yesu aliweka Sakramenti ya Daraja Takatifu yaani Upadre. Padre ni nani? Padre ni mtu ambaye amejitoa maisha yake kwa ajili ya kuwahudumia watu. Padre ni mwanadamu aliyetwaliwa kati ya watu kwa mambo yamuhusuyo Mungu. (Ebr. 5:1-4). Padre ni kuhani. Padre ni Kristo mwingine. Padre ni kiongozi wa dini, ni mhubiri, ni mwana-mageuzi katika jamii, ni mkurugenzi wa mustakabali wa kijamii, ni mwalimu, ni mlinzi na mdhamini wa maadili na ustaarabu, ni mhariri wa kuenzi na kutathimini demokrasia na ni mwezeshaji na mtagulizi kwa mambo ya imani. Padre yuko na taifa la Mungu nyakati zote, kipindi cha kuzaliwa na kufa, wakati wa furaha na huzuni. Katika uchanga wetu, Padre yupo ili apate kutubatiza. Kwa uwezo aliopewa na kwa mikono yake, dhambi ya asili inaondolewa, na mbatizwa anafanywa kuwa mtoto mteule wa Mungu na wa kanisa.
Katika uchipukizi na ujana wetu, Askofu ambaye ni Kuhani hutupatia sakramenti ya Kipaimara ambayo kwayo tunajazwa mapaji ya Roho Mtakatifu. Aliyeimarishwa anapewa nguvu na kuwa askari amini wa Bwana. Kila siku Padre hutupatia Ekaristi Takatifu kwa ajili ya ustawi wa roho zetu, kwani wakati maisha yetu yanapokuwa katika hatari, vishawishi na wasiwasi, tunahitaji mkate wa mbingu ili roho zetu ziimarike. Jitihada kubwa, kazi za ukarimu na sadaka mbalimbali ndiyo majitoleo yake katika jumuiya. Tunapokuwa wadhambi, tumezama katika dimbwi la utumwa wa shetani, sauti tulivu ya Padre yenye nguvu ya Mungu inatufariji ikituambia, nenda na amani umesamehewa dhambi zako. Maeneo haya humfukuza shetani na kutupatia utulivu na amani rohoni. Padre hubariki na kushuhudia makubaliano ya mume na mke wanapoahidi uaminifu katika sakramenti ya ndoa.
Familia mpya, kiini msingi cha jumuia inapata baraka ya Mungu na kukua katika misingi ya imani kwa malezi elekezi ya Padre. Padre huunganisha jitihada zake na za wazazi katika kuelimisha watoto katika mambo ya imani na kuwaandaa kupokea sakramenti. Padre hachoki, hata wakati wa magonjwa tayari yuko pembeni mwa vitanda vyetu akitupatia mpako mtakatifu kwa kututuliza, kutuimarisha na kutuponya na uovu na magonjwa. Tukifa tuna muunganiko na Kristo, kwenye mazishi yetu Padre yupo tayari kupumzisha miili yetu. Na kila siku katika misa husali kwa ajili ya roho za marehemu walioko toharani. Palipo na huzuni Padre huleta furaha, pasipo na haki hutetea haki, kwa vijana huwatia moyo na kuwafundisha fadhila mbalimbali, utii, uaminifu, moyo wa uwajibikaji na heshima kwa wat una kwa Mungu. Huwakumbusha matajiri juu ya wajibu wao wa kusaidia wahitaji na waajiri kulipa ujira unaostahili.
Kwa kuwa wito wake ni kazi ya ukweli, Padre ni chumvi ya dunia. Padre hutoa zaidi lakini hupokea kidogo, zaidi hulipwa chuki na minong’ono. Huyu ndiye Padre. Hali ya kibinadamu ni hali ya unyonge, uchovu, kushawishika kukata tamaa. Kama Kristo mwingine padre anayependwa sana na kuchukiwa sana. Padre yuko katikati ya kila tatizo. Mtu anapoanguka kwa sababu ya ubinadamu husamehewa, lakini kwa Padre ni tofauti, hupigiwa kelele na kuhukumiwa hapo hapo tena na wale anaowahudumia kila siku. Tuwapende mapadre, tuwaombee, tuwafariji na kuwatia moyo ili wawe na nguvu ya kutuhudumia vizuri pia tusali kuombea miito mitakatifu katika kanisa ili tupate mapadre wema na waaminifu wanaojitahidi kumfuasa Kristo. Tumsifu Yesu Kristo, Laudetur Iesus Christus.