pasaka ya Bwana: Tafakari ya Mkesha wa Sherehe ya Pasaka: Historia ya wokovu wa mwanadamu pasaka ya Bwana: Tafakari ya Mkesha wa Sherehe ya Pasaka: Historia ya wokovu wa mwanadamu 

PASAKA YA BWANA 2019: Tafakari Mkesha wa Sherehe ya Pasaka

Mkesha wa Pasaka umegawanyika katika sehemu kuu nne: Liturujia ya Mwanga inayopambwa kwa Mbiu ya Pasaka. Pili: Liturujia ya Neno la Mungu linalosimulia historia nzima ya wokovu. Tatu ni Liturujia ya Ubatizo, waamini wanarudia ahadi za Ubatizo na Wakatekumeni wanabatizwa na kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu. Nne, Liturujia ya Ekaristi Takatifu: chakula cha njiani!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, mkesha wa Sherehe ya Pasaka. Kwa kawaida, ibada ya kesha la Pasaka inafanyika usiku, na haianzi kabla ya jua kutua, na inapaswa kumalizika kabla ya jua kutoka siku ya Jumapili. Mkesha huu una sehemu kuu nne, kwanza ni Liturujia ya Mwanga inayopambwa kwa mbiu. Kanisa linatafakari maajabu ambayo Bwana Mungu alilifanyia taifa lake tangu mwanzo. Pili ni Liturujia ya Neno yenye masomo tisa. Tatu ni Liturujia ya Ubatizo: Adhimisho la Sakramenti ya Ubatizo wa Wakatekumeni na nne ni Liturujia ya Ekaristi: Kanisa pamoja na wanachama wapya waliozaliwa katika mkesha huu linaitwa kula chakula alicholiandalia Bwana taifa lake kwa kufa na kufufuka kwake, ndiyo kuumega mkate, Ekaristi Takatifu.

Masomo tisa katika vijilia vya mkesha wa pasaka yanatupa simulizi kamili la historia ya wokovu wa mwanadamu tangu alipoanguka katika dhambi baada ya kuubwa. Simulizi la uumbaji katika kitabu cha mwanzo linatufundisha kuwa asili na chanzo cha mwanadamu ni Mungu katika Utatu Mtakatifu. Katika viumbe vyote vilivyoumbwa, ni binadamu tu peke yake ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ili amjue, ampende, amtumikie na mwisho afike kwake mbinguni. Mungu kabla ya kumuumba mwanadamu aliumba vitu vingine vyote kama maandalizi ya mazingira ya kuishi mwanadamu. Baada ya kumwumba mwanadamu alimkabidhi vyote ili avitiishe na kuvitumia, lakini kwa sharti moja tu asile matunda ya mti wa katikati (Mw. 1 :1-2 :2). Maana yake jukumu la lipi ni jema na lipi ni baya sio jukumu lake bali la Mungu. Lakini ikawa ni kinyume kwani mwanadamu hakutii maagizo ya Mungu. Kwa kosa la kutotii amri na maagizo ya Mungu dhambi iliingia duniani.

Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva la kukaidi maagizo na amri za Mungu, walipoteza neema ya utakaso, sura na mfano wa Mungu ndani mwao na mahusiano mazuri na Mungu yakatoweka kwa sababu ya kiburi na ukaidi, ndipo taaabu, mahangaiko na mateso yakamwandama mwanadamu kwa kujitenga kwake na Muumba wake. Hivyo walichokipoteza Adamu na Eva ndicho tulipokipoteza nasi kwani ubinadamu wetu ulikuwa tayari kwao. Hata hivyo Mungu kwa upendo wake kwa mwanadamu aliyemuumba kwa sura na mfano wake na kwa huruma yake hakumwacha apotee na kuangamia kabisa. Mungu kwa nyakati mbalimbali na tofauti, mara nyingi na kwa namna nyingi na njia mbalimbali alizitumia ili kumwokoa mwanadamu (Waeb.1:1-4). Kwanza aliwaangamiza kwa gharika wakati wa Nuhu, akafanya agano na Ibrahimu Baba wa imani (Mwa.22:1-18).

Taifa la Israeli si kwa sababu ya ubora wake ila kwa mpango na makusudi ya Mungu likawa taifa teule liliandaliwa ili kumpokea mwokozi. Kila walipomkosea Mungu waliadhibiwa kwa kupelekwa utumwani na walipotubu na kuomba msamaha, Mungu aliwasamehe na kuwaokoa. Kwanza aliwapeleka utumwa wa Misri, akawatoa kwa mkono wa Musa akawavusha bahari ya shamu (Kut. 14:15 –15:1). Mungu akawatuma waamuzi, wakaja pia wafalme na manabii wakati wa utumwa wa Babeli. Walipotubu na kumrudia, Mungu aliwasamehe na kuwarudisha katika nchi yao ya ahadi. Pamoja na juhudi zote alizofanya Mungu kwa njia ya waamuzi, wafalme na manabii ili kuturudisha kwake, kwa mioyo yetu migumu na ukaidi wetu hawa wote tuliwatenda jeuri na wengine kuwaua kabisa.

Nabii Isaya akatabiri ujio wa masiha, mtumishi wa Mungu atakayetupatanisha naye. Hatimaye muda ulipotimia, Mungu akaamua kumtoa na kumleta kwetu mwanaye wa pekee ndiye Mkombozi wetu Yesu aliyemtambulisha kwetu siku ya ubatizo wake mtoni Yordani na alipogeuka sura mlimani Tabor kuwa ndiye mwanaye mpendwa tumsikilize yeye. Huyu ndiye Kristo tuliyetesa mateso mengi tukampiga mijeledi, tukamvika taji ya miiba kichwani, tukampiga kwa mwanzi, tukamtemea mate, akiwa amechoka kabisa yuko hoi  tukambebesha msalaba mzito, alipoanguka kwa udhaifu wa kimwili tulimpiga bila huruma, hatimaye tukatumndika juu ya msalaba kwa kumpigilia misumari kama mhalifu, alipokufa hatukuamini, tukaona haitoshi tukamtoboa ubavu wake kwa mkuki ikatoka damu na maji chemchemi ya sakramenti za kanisa, watu wema wakamchukua wakazimka, siku ya tatu akafufuka ili arudishe tena uhusiano wetu Mungu Baba.

Leo hii tunashangilia amefufuka kwelikweli tumefurahi kwelikweli, tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Ufufuko wa Yesu Kristo, ni ukweli kabisa wa imani yetu. Imani tunayoisadiki na kuiishi kama msingi wa jumuiya ya kwanza ya Kikristo. Ufufuko wa Yesu ni ishara ya matumaini, ni nguvu katika safari yetu ya maisha ya kiroho. Ufufuko wa Yesu Kristo ni uthibitisho mkubwa kabisa wa Umungu wake. Ufufuko wa Yesu sio tu ni muujiza mkubwa kupita yote aliyofanya kuthibitisha kuwa yeye ni Mungu, lakini pia ni utimilifu wa fumbo la wokovu wetu. Ufufuko wa Yesu ni sehemu ya wokovu wetu. Tumekombelewa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu. Kifo na ufufuko wake havitenganishwi, ingawa hayo ni matukio mawili ya kihistoria.

Kwa kifo chake pale Mlimani Kalvari, katika upendo kamili, na utii kwa Mungu Baba (Phil.2:8), kazi yake ya ukombozi haikukamilika. Kazi yake ya kuwakomboa wanadamu, ilikamilishwa kwa ufufuko na kupaa mbinguni kurudi kwa Baba. Ni kwa ufufuko tu, safari ya mbinguni, safari ya kwenda kwa Baba yetu inakamilika. Hivyo ni jambo la muhimu kutambua kwamba, tumekombolewa sio tu kwa mateso na kifo cha Yesu, bali pia kwa ufufuko wake. Ndio kusema, ufufuko ni ishara ya kupokelewa kwa sadaka ya Yesu Kristo na Mungu Baba. Pasaka ni mabadiliko, neno pasaka asili yake ni lugha ya kiebrania Pesach, Passover, kupita juu, ni sikukuu kubwa katika liturujia ya mwaka ya wayahudi walipokumbuka Siku ambapo Malaika alipita juu ya nyumba za waisraaeli alipokuwa akiwapiga wazaliwa wa kwanza wa Wamisri na kuwaua ili Farao awaachie wana waisraeli. Hii ndiyo siku ambapo Waisraeli walitoka kutoka utumwa wa Misri wakaanza maisha mapya kama watu huru.

Kwetu sisi Pasaka ni mabadiliko ya kiroho kutoka katika utumwa wa dhambi, utumwa wa shetani na kuwa watu huru. Kutoka katika maisha ya zamani, kwenda maisha mapya, basi tusibaki katika maisha ya zamani tubadilike katika Kristo Yesu mfufuka. Ukristo wetu usiwe ni ukristo wa jina bali ukristo unaoishi tubadilike kutoka utu wa kale kwenda utu mpya. Usiku wa Kesha la Pasaka ni usiku Mtakatifu, uliopamba kwa nuru na mwanga wa mshumaa ambao sifa zake huimbwa katika mbiu. Mshumaa huu unakuwepo katikati yetu ukitumulika na kutuangazia nuru ya kweli ndiye Kristo, ni usiku wa wokovu wetu. Ni usiku wa kuuutangazia ulimwengu kuwa Kristo amefufuka yu hai, ni usiku wa kuepuka nafasi za dhambi. Ni usiku wa upendo, furaha, amani, uvumilivu, unyenyekevu, utii, uchaji wa Mungu. Ni usiku wa kwenda mbio kuutangazia ulimwengu habari za ufufuko wa Bwana, kuwa kaburi li wazi, Kristo amefufuka, yu mzima, kusudi nao pia wakimbie kwenda kumshuhudia Kristo Mfufuka ili tuweze kumwona na kumtambua katika kuumega mkate.

Mkesha wa Pasaka
20 April 2019, 15:26