Jumapili ya Matawi: Mwanzo wa Juma Kuu: Mateso ya Kristo!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya matawi. Zimetimia siku 40 tangu tuanze kipindi hiki cha kujipatanisha na Mungu. Leo tunaadhimisha matukio mawili msingi; kuingia kwa shangwe Yerusalemu na mwanzo wa Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Tunaingia juma kuu ambapo tutaadhimisha siku kuu tatu za Pasaka yaani Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu. Tunazama katika tafakari ya fumbo la Msalaba, fumbo la wokovu wetu, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda huo wa siku tatu.
Alhamisi Kuu, tutaadhimisha karamu ya mwisho yaani mlo wa mwisho aliokula Yesu na wanafunzi wake muda mfupi kabla ya kukamatwa na kuteswa hadi kufa Msalabani. Ni siku aliyoweka sakramenti za Ekaristi Takatifu na upadre na amri ya mapendo. Ijumaa kuu kanisa linaadhimisha kifo cha Kristo msalabani na jumamosi kuu kanisa linaomboleza kwa masikitiko makuu likingojea ufufuko wake katika vigilia vya pasaka ambapo kunakuwa na ibada ya mwanga na kupigwa mbiu ya kumshangilia Kristo mfufuka.
Katika somo la kwanza, Nabii Isaya anamwonesha Yesu Kristo kuwa ni mfalme wa amani sio mfalme wa vita, ni mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na hana makuu. Ili kudhihirisha hili anaingia Yerusalemu kwa shangwe na furaha akiwa juu ya mwanapunda, mnyama mpole na mtaratibu asiye na makuu ambaye kwa wayahudi alikuwa ni mnyama aliyetumiwa na watu duni, maskini na wanyonge kwa safari na kazi, tofauti kabisa na farasi aliyetumiwa na wafalme na majemedari wa vita. Punda ambaye hajatumiwa bado kwa kazi au safari za kawaida, alitumika kwa mambo matakatifu. Ndiyo maana Yesu aliagiza mwanapunda ili kuonyesha kuwa yeye ni Mtakatifu na yote anayoenda kuyafanya ni Matakatifu.
Tukio hili linatimiza utabiri wa Nabii Zekaria ukisema; “Furahi sana Ee binti Sayuni, piga kelele ee binti Yerusalemu! Tazama Mfalme wako anakuja kwako. Ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana punda, mtoto wa punda” (Zek.9:9). Watu waliochukua matawi kama ishara ya ushindi na matumaini kwa Masiha wanatandika nguo zao huku wakiimba nyimbo za furaha. Kundi hili la watu linalomshangilia Yesu ni la wanyonge, watu toka mashambani, watu duni, wenye kipato cha chini, nao wanafanya mji wote wa Yerusalemu utikisike kwa kelele za shangwe na hivyo kuamsha hasira za wakuu wa Makuhani, Mafarisayo na Waandishi ndiyo maana wakaanza mikakati ya kumkamata Yesu tena wakati wa usiku, wakati wa giza, wakiwa na taa na mienge, marungu na mikuki na silaha za kivita huku wamejaa hofu na mashaka.
Kristo anakamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali, naye bila ubishi anaanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa. Safari yenye mateso makubwa, anabebeshwa msalaba mzito, anafanyiwa dhihaka njiani, anapigwa mijeledi, anatemewa mate, anatukanwa na pale msalabani anapigiliwa misumari mikononi na miguuni hatimaye anakufa kwa sababu ya dhambi zetu. Tendo hili la kufa Msalabani, liliwakwaza wayahudi na kupigwa bumbuazi, na kuona kuwa Yesu Kristo sio masiha waliomgonjea bali ni mtu aliyelaaniwa na Mungu, kwani Kitabu cha Kumbukumbu la Torati kiliwafundish: “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utazikwa siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu, asije akatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana, Mungu wako iwe urithi wako” (Kum.21:22-23). Hawa waliotandaza nguo zao, wakapeperusha matawi na kuimba nyimbo za shangwe, wanamgeuka Yesu na kupaza sauti zao msulubishe, msulibishe, msulubishe, wamesahau kabisa utabiri wa manabii kuwa masiha atasalitiwa, atafedheheshwa, atateswa na kuuawa, lakini atafufuka kwa ushindi na utukufu mkuu siku ya tatu utabiri waliousubiri kwa miaka mingi.
Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, wasioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Je, sisi tunasadiki kuwa Kristo ni mwana wa Mungu aliyetukomboa kwa njia ya Mateso? Je, tunayatazamaje mateso ya Yesu Kristo? Je, ni uupuzi, ni kikwazo kwa imani yetu? Tukumbuke kuwa hakuna utukufu pasipo mateso na hakuna Pasaka bila Ijumaa kuu. Yesu kwa upendo na hiari anayapokea hayo yote. Anakwenda njia ya mateso hayo makali, anayapokea matusi, dharau, kutemewa mate, kupigwa mijeledi, kupigiliwa misumari na hatimaye kufa msalabani ili tukombolewe, hivyo hakika hakuna utukufu bila mateso.
Utukufu umefikiwa baada ya mateso, hivyo pande zote mbili ni muhimu na za lazima kwa wokovu. Kwa kujua ukweli huu kanisa linahimiza waamini kuvumilia mateso na magumu yanayowapata katika kumfuata Kristu ili waufikie ule utukufu wa milele. Tujifunze kuyapokea mateso katika maisha yetu kwa imani na uvumilivu mkubwa kwani maisha yetu ya ukristo hayawezi kukwepa mateso. Badala ya kunung`unika, tuyapokee na kumwambia Yesu kuwa, Bwana kwa mateso haya unisaidie kuingia katika ufalme wako. Lakini tutambue kuwa majukumu yanayotukabili katika maisha ya kila siku sio mateso; pia tutambue kuwa mateso na mahangaiko tunayojisababishia wenyewe kwa kukiuka amri na maagizo ya Mungu hayawezi kutuletea wokovu bali yatatupeleka kwenye moto wa milele kwani yanazidi kumtesa Kristo.
Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema asulubishwe, asulubishwe. Kwetu sisi kwa mawazo yetu, maneno yetu, matendo yetu maovu tunatoa mlio na makelele hayo hayo. Petro anajaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Kristo anapambana na kumshinda shetani si kwa mapanga na vitisho bali kwa uvumilivu wake, unyenyekevu wake, upole wake na utii wake kwa Baba yake. Je sisi leo wanakanisa wakristo hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani na Ibilisi kwa nguvu za giza, maseng’enyo, malumbano, kwa nguvu ya pesa, mapigano, visasi na fitina.
Tukumbuke ufalme wa Kristo si wa dunia hii hivyo hatupaswi kumpigania kwa jeshi bali kwa ushuhuda wa maisha. Tuwe werevu kama nyoka na wapole kama njiwa. Petro hakuishia hapo bali mara tatu amemkana Kristo akisema mimi si mfuasi wa mtu huyu, akasisitiza mimi simjui mtu huyu. Sisi pia tunafanya jambo hili katika maisha yetu pale tunapoionea aibu Injili, jogoo amekwisha wika mara ya tatu tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya msalaba kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu ni nguvu ya Mungu, tuutazame sasa msalaba kwa imani kuu na moyo wa toba. Tumwombe Mungu atujalie moyo thabiti na wa ujasiri wa kuyapokea mateso kama Kristo alivyoyapokea na hata pale tunaposikia hatumjui huyu! Mwondoshe! Msulubishe! Tusikatishwe tamaa au kukwazwa, bali maneno na mateso hayo yatuimarishe na kutuunganisha zaidi na Kristo aliyevumilia mateso kwa ajili yetu sisi wadhambi.