Tafakari Neno la Mungu: Jumapili V: Kwaresima: Injili ya uhai
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, katika dominika ya tano ya kipindi cha Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Kadiri ya utamaduni na mapokeo ya Kanisa, kuanzia Dominika hii misalaba inafunikwa, mpaka ijumaa kuu wakati wa kuadhimisha mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa, mpaka wakati wa maaadhimisho ya kesha la Pasaka. Dominika hii huadhimishwa takaso la tatu la wakatukumeni watakaobatizwa wakati wa mkesha wa Pasaka!
Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima, zinatuhimiza kwa kurudia tena na tena, mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, kutenda matendo mema na kuwahudumia wahitaji. Zimepita siku 33 tangu tuanze kipindi hiki na zimebaki siku 7 tuingie juma kuu linalofunguliwa na jumapili ya matawi. Ni mda mwafaka kujitafakari na kujiuliza: Je, ile dhambi ninayoipenda kuliko zote nimeiacha, tendo gani la huruma nimetenda tangu kwaresma ianze, ni nini nilichojinyima kwa ajili ya wenye shida na nimesaidia wahitaji wangapi kwa siku hizi 33 tangu Kwaresima ianze?
Leo katika somo la kwanza Nabii Isaya anatoa utabiri kuwa Mungu atatuletea ukombozi mkubwa zaidi kuliko ule aliowakomboa waisaraeli utumwani Misri. Utabiri huu unatizwa kwa mateso, kifo cha msalabani na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo yaani Pasaka. Paulo katika somo la pili anatuambia kuwa tukiwa na imani juu ya nguvu ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, tutayaona mambo ya dunia hii si kitu ni ya kupita, hivyo tutafunua mioyo yetu kwa makuu ambayo mwenyezi Mungu ametutendea kwa njia ya Kristo na kuwa tayari kuacha dhambi, kutenda mema na kuukaaza mwendo ili tulipate tuzo la uzima wa milele.
Injili ya leo inatupa mfano ambao unasisimua sana hisia za watu. Ni mfano wa mwanamke mzinzi mwenye aibu ya kufumaniwa, alimejaa hofu ya kupigwa mawe mpaka afe. Ni mfano unaosisimua kwani kwa fikra za mwanadamu dhambi ya uzinzi yaonekana kuwa kubwa na ya ajabu zaidi licha ya kuwa katika ulimwengu wa sasa uzinzi na uasherati unazidi kuwa jambo la kawaidi. Lakini kiuhalisia, mfano huu unaonyesha zaidi chuki kali ya wayahudi kwa Yesu na mafundisho yake, na hivyo wanafanya kila namna kwa mawazo, maneno na matendo yao ya hila ili wamwangamize, wateketeze uhai wake.
Uhai ni mali ya Mungu. Uhai ni zawadi na tunu pekee ambayo Mungu ametupatia sisi wanadamu, hivyo ni jukumu letu kuupokea, kuutunza na kuulinda. Thamani ya maisha yetu mbele za Mungu ni kubwa mno kwa kuwa tumeumbwa kwa sura na mfano wake. Thamani ya tunu hii, Kristo anaidhihirisha kwa kuwafanya mafarisayo na waandishi watambue kuwa hukumu ya kifo ni ukatili na uovu dhidi ya tunu hii ya uhai hata kama sheria ya Musa iliruhusu uovu huo na kusema, “Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa”(Wal 20:10; Kumb 22:22).
Walimu wa sheria na mafarisayo walikuwa watu wanaozingatia kwa ushupavu sana sheria za Musa na Manabii. Hivyo walijiona kuwa wao ni watu wenye maarifa, haki na waadilifu. Waliwachukia mno watu waliovunja sheria na watenda dhambi. Waliona kuwa Mungu hawezi kumsamehe mtu aliyetenda dhambi na ndivyo walivyofundisha. Yesu aliyefundisha msamaha wa dhambi na kujihusisha daima na wadhambi alikuwa adui kwao. Kwa hiyo lengo lao hasa la kumleta kwake mwanamke huyu aliyefumaniwa ni kutafuta sababu ya kumshitaki Yesu ili auawe.
Tukumbuke kuwa kipindi hiki Wayahudi walikuwa chini ya ukoloni wa Warumi na hawakuruhusiwa kutekeleza adhabu hii ya kifo. Hivyo Yesu angesema watekeleze sheria ya Musa wampige kwa mawe mpaka kufa, kwanza yeye mwenyewe angekuwa na hatia ya kuuwa kadiri ya sheria ya serikali ya warumi, pili angepingana na mafundisho yake juu ya huruma, upendo na kutowahukumu wengine pia angepoteza wafuasi. Lakini pia angesema wasimuue angepingana na sheria ya Musa. Yesu anatoa jibu la kuwashitaki wao akisema, “Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe” (Yn 8:7), lakini tumeambiwa, kimya kimya, wakaondoka mmoja mmoja, wakitanguliwa na wazee hata wa mwisho wao. Kisha Yesu anamwambia huyu mwanamke “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; usitende dhambi tena” (Yn 8:11).
Sababu ya kupelekwa huyu mwanamke peke yake ina maana kubwa zaidi inayopita uelewa wa Mafarisayo na Waandishi. Mungu alimwambia Hosea. “Nenda tena ukampende mwanamke anayependwa na mume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama mimi Mwenyezi ninavyompenda Israeli, ingawa yeye anaigeukia miungu mingine” (Ho.3:1). Tunapotenda dhambi tunakosa uaminifu kwa Mungu. Ubaya wa kukosa uaminifu kwa Mungu ni sawa na kuzini, hivyo Israeli alizini kwa kumwacha Mungu na kuitumikia miungu mingine. Na sisi kila tunapotenda dhambi tunakosa uaminifu kwa ahadi zetu za ubatizo tulizoziweka mbele za Mungu, maana yake tunazini. Ndiyo maana mwanamume hakuletwa katika tukio hili la kufumaniwa, ili kutuonyesha kuwa sisi sote tu wazinifu kwa dhambi zetu mbele za Mungu. Huyu mwanamke ni Ishara ya Israeli aliyeasi na ni ishara kwetu sote tunaoishi katika dhambi. Hivyo kila tunapotenda dhambi tunakuwa sawa na huyu mwanamke na hivyo tunapswa kupigwa kwa mawe mpaka tufe.
Lakini lengo la Mungu kutuumba si kuangamia bali kutushirikisha uzima wa milele. Dhamani ya uhai wa mwanadamu ni kubwa mno na iko mikononi mwa Mungu peke yake. Ndiyo maana kwa upendo, Mungu aliamua kumtoa mwane wa pekee ili atudhihirishie dhamani ya tunu hii. Yesu mwenyewe alikubali kuutoa uhai wake, tena kwa hiari ili afe kwa ajili yetu sisi tuliostahili kufa ili atukomboa. Alikubali kufa kwa hiari kifo cha msalabani ili kwamba kusiwepo tena adhabu za vifo. Kifo cha Kristo ni ishara na alama ya kukomesha adhabu za vifo, manyanyaso ya wale wasio na hatia. Lakini bado vifo na mauaji ya watu wasio na hatia yanaendelea. Katika ulimwengu wetu wa sasa dhamani ya mwanadamu ni ndogo kuliko vitu. Mwanadamu anatumiwa na vitu vinapendwa.
Ni watoto wangapi wanuawa kwa utoaji mimba na hata wengine waliokwisha kuzaliwa wanatupwa, watu wangapi wanahukumiwa kunyongwa katika mahakama zetu, wangapi wanauwa kwa sababu za ushirikina na uchawi na ni roho ngapi zinaangamizwa katika vita na ugaidi. Hii haimaanishi kuwa kifo cha Kristo msalabani hakikuwa na nguvu bali ni kwasababu mioyo yetu imefungwa wala haijaguswa bado kwa kifo chake na hivyo hili fundisho bado hatujalielewa. Imani yetu juu ya nguvu ya mateso, kifo na ufufuko wake ni haba. Hatuamini. Lakini tukichunguza vyema dhamiri zetu, tutatambua kuwa ni kwasababu tu wazinzi na tutaona hitaji la kuondoka mmoja mmoja kwenda kutubu.
Tunaalikwa kutowahukumu wengine na kutojihukumu mwenyewe bali kufanya toba ya kweli. Wakati mwingine tukiangalia historia ya maisha yetu tunajiona sisi hatuna thamani yoyote. Kabla watu hawajatupiga kwa mawe, sisi wenyewe tunajipiga kwa mawe. Tunaona kabisa Mungu hawezi kutusamehe. Paulo amesema nayasahau ya zamani nikichuchumilia yaliyo mbele, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria bali ile ipatikanayo kutoka kwa Mungu kwa Imani. Anatambua akijingalia alivyolitesa kanisa kwa kuwaua wakristo asingeweza kuhubiri injili lakini kwa imani anatambua kuwa “nguvu ya kufufuka kwa Kristo imemkomboa.
Tusikate tamaa. Tunaalikwa kuanza maisha mapya yasiyo na dhambi, maisha ya uadilifu. Tusifikiri kuwa kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha kuacha kwa muda matendo maovu ambayo tutayaendeleza baada ya kuisha kipindi hiki. Tubadilike kabisa toka ndani. Tumepewa onyo la kutoendelee kuishi katika dhambi wala mimi sikuhukumu, nenda zako usitende dhambi tena. Tuwaoneshe huruma wale wote waliokata tamaa kutokana na kuishi katika dimbwi la dhambi za kukatisha uhai wa wengine. Tuwatie moyo tusiwalaumu na kuwahukumu bali tuwasaidie waweze kutambua dhamani ya huruma ya Mungu na kufanya toba ya kweli.