Tafuta

tafakari ya Neno la Mungu Jumapili V ya Kipindi cha Kwaresima: Udhaifu na huruma: "Misera et misericordia" tafakari ya Neno la Mungu Jumapili V ya Kipindi cha Kwaresima: Udhaifu na huruma: "Misera et misericordia" 

Liturujia Neno la Mungu: Kwaresima V: Huruma na Upendo!

Maandiko Matakatifu yanatualika kuutafakari upendo unaojimwilisha katika msamaha, mahali ambapo nadharia ya upendo inachukua mwili, inapata mashiko. Anayesema ninakusamehe anasema ninakupenda na anayesema anapenda awe tayari kusamehe. Msamaha una lengo la kuunda upya, kuboresha ubinadamu na kuimarisha mahusiano kati ya mtu na mtu na kati ya mtu na Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika ya 5 ya Kwaresima mwaka C wa Kanisa. Maandiko Matakatifu katika siku hii ya leo yanatualika kuutafakari upendo unaojimwilisha katika msamaha. Msamaha ndio mahali ambapo nadharia ya upendo inachukua mwili, inapata mashiko.

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Is 43:16-21) ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya. Ni somo linalowajia Waisraeli wakiwa utumwani Babeli kama sehemu kubwa ya ujumbe wa matumaini kwao kuwa atawakomboa. Kuwapa ujumbe huo, Mungu anaanza kuwakumbusha alichokifanya kwa babu zao alipowakomboa kutoka utumwani Misri. Anasema ni yeye aliyetengeneza njia wakapita baharini na ni yeye aliyewaangamiza farao na majeshi yake yote akawazima kama kuzima utambi. Basi wakikumbuka matendo hayo makuu aliyoyafanya wazidi kutumaini kuwa hata sasa atawakomboa kutoka utumwani Babeli kwani atatengeneza njia jangwani na atawarudisha katika ardhi yao.

Katika ujumbe huu Mungu anawaambia atafanya mito ya maji nyikani katika jangwa. Aliwatoa Misri Mungu alifanya ishara kama hii. Aliwapa maji kutoka katika mwamba. Ishara hii hii Mungu anawaambia atairudia lakini sasa ataenda zaidi. Atafanya mito ya maji itiririke jangwani. Hii ni ishara kuwa ukombozi huu utakuwa ni mkubwa kuliko ule wa kwanza. Ni hapa tunaona kidokezo cha ukombozi mkubwa zaidi atakaoukamilisha kwa njia ya Kristo katika Agano Jipya. Katika somo hili, Mungu anawaambia pia “msiyakumbuke mambo ya kwanza wala msiyatafakari mambo ya zamani”. Ni yapi hayo mambo ya kwanza? Na ni yapi yaliyo ya zamani? Hapa Mungu anawakumbusha kuwa wameenda utumwani kama adhabu aliyowapa kwa kushindwa kushika agano na kushindwa kufuata maagizo yake. Anawaambia wasikumbuke adhabu ya hasira yake, wawe tayari kupokea wema wa ukombozi anaowaahidia.

Somo la pili (Fil 3, 8-14) ni Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Katika somo hili, Paulo analinganisha maisha yake ya mwanzo kabla ya wongofu na maisha yake ya sasa baada ya wongofu. Kama tunavyofahamu Paulo hapo awali aliupinga sana ukristo kwa sababu aliona ni kama usaliti kwa imani yake katika dini ya kiyahudi. Aliwatesa wakristo na kuwaangamiza akiamini kuwa kwa kufanya hivyo anatekeleza mapenzi ya Mungu hadi pale Kristo alipomtokea na kumwambia anapowatesa wakristo anamtesa Yeye Kristo mwenyewe. Katika somo hili anaeleza kuwa sasa ameanza maisha mapya na ameyaacha yale ya zamani. Anakiri kuwa katika maisha ndani ya Kristo anaona thamani kubwa sana ambapo anapolinganisha na maisha yake ya awali anayaona yale kama uchafu. Anakiri kuwa ameyaacha maisha na vitu ambavyo kwa sasa havipi thamani tena.

Pamoja na hayo Mtume Paulo anatambua kuwa maisha ya ufuasi daima ni safari. Kumbe pamoja na kuyapokea maisha mapya ndani ya Kristo haoni kuwa amekwishafika au kwamba amekamilika bali anazidi kukaza mwendo ili alifikie taji Kristo ameawekea waaminifu wake. Ukristo sio tukio la kufanya mara moja na kumaliza: sio tu kubatizwa, sio tu kupokea Ekaristi, sio tu kupewa Kipaimara, sio tu kufunga ndoa, kuweka nadhiri au kupokea sakramenti ya daraja, Ukristo ni maisha. Ni maisha yanayohitaji kurutubishwa, kulindwa, kuendelezwa na kuyaishi.

Injili (Yoh 8: 1-11) Katika Injili ya leo, waandishi na mafarisayo wanamleta kwa Yesu mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi. Wanamweleza kuwa kadiri ya torati ya Musa inabidi mwanamke huyo apigwe kwa mawe hadi auwawe na kisha wanamuuliza “nawe wasemaje”. Waandishi na mafarisayo wanamletea Yesu kesi ili ahukumu lakini mbele kidogo katika simulizi tunaona kumbe ni wao walikuwa wanatafuta sababu ya kumhukumu. Sheria ya Musa wanayoiongelea, wanainukuu kimakosa. Katika kitabu cha Mambo ya Walawi 20:20 na kitabu cha Kumbukumbu la Torati 22:22 Sheria inasema katika tukio hilo wote wawili mwanaume na mwanamke inabidi waangamizwe kwa kupigwa kwa mawe. Wao walimleta mwanamke tu, hawakumleta na mwanaume.

Kumbe sheria ya Musa pamoja na mwanamke waliyemleta ilikuwa ni namna tu ya kutimiza lengo lao. Yesu hakuwajibu neno bali aliinama akaandika chini kwa kidole chake. Hakupenda kuingia katika malumbano ya hoja kwa sababu tayari hoja zao zilikuwa na uovu. Kuandika chini ni kuugusa udongo uliomuumba mwanadamu, mwanadamu ameumbwa kwa udongo, na hivi Yesu alitaka watoke katika hoja zao za nadharia na wautazame undani wa ubinadamu wao na wa huyo mwanamke wanayetaka apigwe mawe. Anawataka wauangalie ubinadamu na uhai kwa ujumla kuwa si kama kitu cha kutolea maamuzi kutoka katika ufundi wa hoja ulio nje ya uhalisia.

Na kutoka hapo, walipozidi kumhoji anawaambia “asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe”. Kisha anaimana tena na kuandika chini sheria hii mpya anayotaka sasa ndiyo iongoze maisha na mahusiano ya wote walio ndani ya Kristo. Alipokuwa anaandika, mafarisayo na waandishi wakaanza kuondoka mmoja mmoja na akabaki Yesu na yule mwanamke. Hakuna aliyemshitaki. Na Yesu anamwambia “wala mimi sikuhukumu, enenda zako; wala usitende dhambi tena”.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika tafakari ya injili ya leo, Mtakatifu Augustino anasema wafarisayo na waandishi walipompeleka yule mwanamke mzinzi kwa Yesu waliukutanisha “udhaifu”  na “huruma” –misera et misericordia. Na hata baada ya mashitaka kwa Yesu baada ya mafarisayo na waandishi kuondoka mmoja mmoja kuanzia yule aliyekuwa mzee hadi yule wa mwisho wao, alipobaki Yesu na yule mwanamke vilibaki hivyo viwili – huruma na udhaifu. Baba Mtakatifu Francisko aliyatumia pia maneno hayo katika ujumbe wake wa kuhitimisha mwaka wa Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu kuonesha fumbo la upendo wa Mungu pale anapokutana na mdhambi. Alieleza kuwa msamaha ndio tendo linaloonesha moja kwa moja na kwa uwazi zaidi upendo wa Mungu kwa wanadamu.

Maandiko Matakatifu katika siku hii ya leo yanatualika kuutafakari upendo unaojimwilisha katika msamaha. Msamaha ndio mahali ambapo nadharia ya upendo inachukua mwili, inapata mashiko; anayesema ninakusamehe anasema ninakupenda na anayesema anapenda awe tayari kusamehe. Injili ya leo inatuonesha pia kuwa msamaha huu una lengo la kuunda upya, una lengo la kuboresha ubinadamu na una lengo la kuimarisha mahusiano kati ya mtu na mtu na kati ya mtu na Mungu. Ni kwa jinsi hii Yesu anamwambia mwanamke “enenda zako wala usitende dhambi tena”. Kamwe msamaha si kivuli cha kufunika mambo wala hauombwi kuficha uwajibikaji bali ni hatua madhubuti ya kujikosoa na azimio la kujisahihisha.

Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumeingia katika  dominika hii ya 5 ya Kwaresima, dominika inatusogeza karibu kabisa na juma la Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo na tayari kuanzia dominika hii tunafunika Misalaba na sanamu zote. Tunakiri kuwa ni kwa sababu ya dhambi zetu Kristo ameingia katika mateso hayo makali na hilo ni “tendo-ishara” la kufunika nyuso zetu kwa kuona uchungu kwa dhambi zetu, uchungu unaotupeleka kufanya toba. Mwaliko wa upendo na msamaha wa Kristo utusaidie kuyaingia vema mafumbo haya tunayoaadhimisha.

Liturujia J5 Kwaresima
05 April 2019, 17:38