Jumapili ya Huruma ya Mungu 2019: Huruma na upendo!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 2 ya Pasaka, ambayo pia ni adhimisho la dominika ya Huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu katika mwanga wa Pasaka ni kielelezo cha ufahamu ambao unaweza kuchukua mtindo mbali mbali katika maisha ya mwanadamu yaani: kwa kutumia milango ya fahamu, kwa kufundishwa, lakini kubwa zaidi ni kwa njia ya mang’amuzi ya huruma ya Mungu inayofungua akili na nyoyo za watu ili kuweza kufahamu kwa kina na mapana zaidi Fumbo la maisha ya Mungu na maisha ya mtu binafsi. Huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba: vita, chuki, uhasama na ubaya wa moyo ni mambo ambayo hayana msingi kabisa na kwamba, waathirika wakubwa ni wale watu wanaofungwa katika hali kama hizi, kwani ni mambo yanayowapokonya utu wao.
Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anaendelea kusema Baba Mtakatifu Francisko, inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kwa furaha.
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 5: 12-16) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Somo hili linaeleza maisha ya jumuiya ya mitume na waamini mara baada ya ufufuko wa Kristo. Kwa jina la Kristo Mfufuka mitume waliweza kufanya ishara na maajabu mengi kwa watu. Walijaliwa uwezo wa kuendeleza nguvu za kinabii na za uponyaji alizokuwa nazo Kristo. Tunaona pia kuwa ufufuko wa Kristo uliwaunganisha. Wakawa jumuiya moja iliyo na nia moja. Kwa jinsi hii watu waliwaadhimisha, waliwapa heshima na idadi ya walioamini ilizidi kuongezeka.
Somo la pili (Ufu 1,9-11a, 12-13, 17-19 ) ni kutoka kitabu cha Ufunuo. Katika somo hili, Yohana anaeleza jinsi alivyokutana na Kristo mfufuka. Alikuwa Patmo, kisiwa ambacho kilitumiwa na warumi kama gereza la wafungwa. Akiwa huko anapata maono. Maono haya anayapata katika siku ya Bwana. Hii ni siku ya ufufuko wa Kristo, siku ya dominika. Kuitaja siku kwa jina hili ni kuonesha kuwa jumuiya anayoiandikia ilikuwa ni jumuiya ya kikristo inayoiheshimu siku ya dominika kama siku inayopambanua uwepo wao ikihusisha na kile kilichotokea katika siku hiyo yaani ufufuko wa Kristo.
Katika maono yake aliona vinara vya taa saba za dhahabu. Vinara hivi viliwakilisha makanisa saba au jumuiya saba za makanisa ambazo hapo awali alikuwa ameambiwa ayaandikie na kuyapelekea maono yake. Katikati ya vinara hivyo ndipo alimwona mtu mfano wa mwanadamu. Na huyo mwanadamu akajitambulisha kwake kuwa ndiye wa kwanza na wa mwisho – yaani alfa na omega, aliyekuwa amekufa na sasa yuko hai hata milele. Jina alilojitambulisha nalo ni jina lenye hadhi ya kimungu. Na kiashirio cha yule aliyekuwa amekufa ni kiashirio cha Kristo mfufuka ambaye sasa anaishi milele. Katika maono haya Yohane anamwona Kristo mfufuka kama msingi na mhimili wa yale makanisa saba. Na kimsingi ni Kristo anayejifunua kama msingi na mhimili wa makanisa yote hai, yaani nafsi za wote wanaomuamini.
Injili (Yoh. 20:19-31) injili ya leo ni kutoka kwa mwinjili Yohane. Baada ya ushuhuda wa kukuta kaburi wazi, injili ya leo inatoa ushuhuda mwingine juu ya ufufuko wa Kristo. Nao ni Yesu mwenyewe kuwatokea wanafunzi wake. Huu ndio ushuhuda unaofuta mashaka kuwa huenda mwili wake ulichukuliwa au uliibwa. Yesu anaingia katikati yao japokuwa milango imefungwa. Anawasalimu “amani iwe kwenu”. Hili ni tangazo na hapo hapo ni zawadi. Anawatangazia kuwa ile amani iliyokuwa imekosekana duniani kwa sababu ya dhambi sasa kwa ufufuko wake ameishinda dhambi na sasa anawapatia amani hiyo kama zawadi, kama tunda la ufufuko wake.
Kisha akawavuvia Roho Mtakatifu ili Roho yuleyule aliyetenda kazi pamoja naye sasa awape mitume nguvu ya kuendeleza kazi yake. Uwezo anaowapa ni ule wa kuendelea kuleta amani ipatikanayo kwa maondoleo ya dhambi. Anawapa uwezo wa kuondolea dhambi. Mwinjili anatumia lugha ya “kufungua na kufunga” kumaanisha kuwa Yesu amewapa uwezo na mamlaka yote kuhusu maondoleo ya dhambi. Hakuna dhambi ambayo mitume hawataweza kuiondoa. Injili inaunganisha tukio hili la maondoleo ya dhambi na lile la Tomaso aitwaye asiyeamini, kuonesha kuwa kupokea nguvu hii aliyoitoa Kristo Mfufuka kunahitaji imani hai. Bila imani mafumbo ya kipasaka ambayo Kristo aliwaaminisha mitume wake hayatakuwa na matokeo katika nafsi ya mwamini. Ndivyo Yesu mwenyewe anavyohitimisha akisema “wana heri wale wasioona wakasadiki”.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, dominika hii ya pili ya Pasaka tunapotafakari tendo kubwa la Yesu kulikabidhi Kanisa lake uwezo wa kuondolea dhambi, tunaadhimisha dominika ya Huruma ya Mungu. Kwa Mtakatifu Sr. Faustina ambaye Yesu alimchagua kuwa mjumbe wa huruma, kuamsha ibada ya huruma ya Mungu katika nyakati zetu alisema “Dominika inayofuatia dominika ya Pasaka ninataka iadhimishwe Sherehe ya Huruma ya Mungu. Mwanangu, utangazie ulimwengu wote juu ya Huruma yangu isiyo na kikomo. Katika siku hiyo nitafungulia milango yote ya Huruma yangu na roho itakayopokea Maungamo na Ekaristi Takatifu siku hiyo itapata maondoleo ya dhambi pamoja na adhabu zake zote.”
Ni dominika inayotukumbusha, kama anavyofundisha Papa Francisko, kuwa Huruma ndilo jina jingine la Mungu - “Bwana amejaa Huruma na Neema” (Zab. 103:8). Na katika kipindi hiki cha Pasaka tunapomshangilia Kristo Mfufuka tunaalikwa kuiona Huruma ya Mungu katikati ya fumbo la ukombozi wa Mwanadamu. Huruma inaita huruma, na mwitikio kwa huruma ni huruma. Tunapojifunza huruma hii kuu ya Mungu, tunaalikwa nasi kuwa vyombo vya huruma.