Jumapili ya Matawi: Fumbo la Mateso ya Yesu & Wokovu wa binadamu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Siku ya leo tunatafakari Masomo ya dominika Matawi mwaka C wa Kanisa. Huu mwanzo wa Juma Kuu ambamo Mama Kanisa anatafakari kuhusu Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kama sehemu ya mchakato wa wokovu wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi mauti kadiri ya mpango wa Mungu, jambo la kushangaza sana!
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Is 50:4-7) ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya. Nabii Isaya anamzungumza mtumishi aliyeteseka vikali. Na katika somo hili, mtumishi mwenyewe aliyeteseka anaeleza namna alivyoyakabili mateso yake. Mtumishi anaeleza kuwa mbele ya mateso yake hayo hakujificha, hakuona aibu na wala hakuwa mkaidi. Aliutoa mwili wake upigwe na ufanyiwe fedheha na watesi wake. Mtumishi anaeleza kuwa sababu za kufanya hivyo ni kwamba alikuwa na uhusiano wa karibu na Mungu. Ni kwa ukaribu huo Mungu alimfundisha na alizibua sikio lake akampa usikivu. Na kwa sababu ya ukaribu huo, mtumishi hakutahayari, alijipa uhakika kuwa Mungu hatamwacha.
Tunapolitafakari somo hili katika juma la mateso, tunaona mwendelezo wa tafakari nzito ya Agano la Kale kuhusu fumbo la mateso katika maisha ya mwanadamu. Kutoka kwa Ayubu ambaye mbele ya mateso alihitimisha “Bwana alitoa, Bwana ametwaa Jina lake na libarikiwe (Ayu 1:21) kwenda kwa Yeremia ambaye mbele ya mateso alilalama “na ilaaniwe siku niliyozaliwa” na kisha “Ee Bwana uniokoe” (Yer 17:14) kilichokuwa pia kilio cha mzaburi, hapa tunamwona mtumishi ambaye mbele ya mateso makali anasema “sikuwa mkaidi na wala sikurudi nyuma”. Mtumishi anatupa mwono mpya katika kulitafakari fumbo la mateso kuwa nguvu ya mteseka ni ukaribu wake na Mungu.
Somo la pili (Fil 2, 6-11) ni Waraka wa wa Mtume Paulo kwa Wafilipi. Ni somo linaloeleza fumbo la unyenyekevu wa Kristo. Somo hili limjaa mafundisho msingi sana kuhusu fumbo la Kristo na wokovu wa mwanadamu. Kristo hakuuona umungu wake kuwa ni kitu cha kukitumia kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya ubinadamu uliokuwa umeharibiwa na dhambi. Kwa utashi wake aliuachilia utukufu akatwaa namna dhaifu ya wanadamu na tena akajinyenyekeza na kutii hadi kufa msalabani. Kinachoweza kuonekana hapa ni kwamba labda Kristo alijitenga na umungu wake au labda aliuficha. Pasipo kujitenga wala kuuficha umungu wake, kwa tendo hili Kristo ndio aliufunua umungu wake. Alionesha sura ya Mungu si yule anayekaa katika utukufu tu bali Mungu anayeshuka na kuingia katika hali dhaifu ya ubinadamu ili aiokoe na kuiinua.
Katika mistari hii michache, Mtume Paulo analeta fundisho kubwa la umwilisho wa Kristo, yaani fumbo la Mungu kujifanya mtu ili amfanye mtu afanane na Mungu. Jambo la pili analoeleza Paulo ni fumbo la utii. Ni kwa kutokutii kwa Adamu dhambi iliingia ulimwenguni na kwa kutokutii huko ubinadamu ulianguka, yaani ulipungua katika hadhi ile ambayo Mungu aliuumba. Kristo katika kuurudishia ubinadamu hadhi yake anapita katika mlango uleule wa Adamu na alirekebisha kosa kwa kutii ili kama anavyosema Mtume Paulo, palepale dhambi ilipoingilia pale pale wokovu upatikane. Na hivi anaonesha kuwa ubinadamu utaweza kuitunza hadhi yake mbele ya Mungu pale utakapoendeleza utii kwa Mungu. Somo hili pia linagusa fumbo la mateso. Mateso ni njia aliyoamua Kristo kwa uhuru na utashi wake kuitumia ili kumkomboa mwanadamu. Kwa somo hili, Paulo anaalika kuyaona mateso katika sura ya ukombozi.
Injili (Lk 22:14-23:56) Injili ya leo kwa kufuata desturi ni ya Historia ya Mateso ya Kristo. Kwa mwaka huu inasomwa injili ya Luka. Simulizi hili refu tunaweza kuona kuwa linajikita katika maeneo matatu. Eneo la kwanza ni mezani wakati wa mlo wa Pasaka, eneo la pili ni katika mlima wa Mizeituni ambapo Yesu alikwenda kusali na eneo la tatu ni katika mashitaka, mateso na kifo chake. Maeneo yote haya matatu yanahusiana na yanafafanua maana ya kile ambacho kinatendeka. Mlo wa Pasaka ilikuwa ni sherehe ambayo Wayahudi waliifanya kila mwaka kukumbuka kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri. Yesu na wanafunzi wake pia kwa kuwa walikuwa wayahudi waliifanya sherehe hiyo.
Katika sherehe hiyo Yesu anafanya kitu kipya. Anatoa mkate kuwa mwili wake na divai kuwa damu yake. Hili ni tendo analolifanya mezani lakini linakuja kudhihirishwa na kukamilishwa pale msalabani anapoutoa mwili wake kama sadaka safi na isiyo na doa mbele ya Baba na kumwaga damu yake kwa ajili ya wote. Hapo Yesu anaibadili pasaka ya wayahudi na kuisimika Pasaka mpya ambayo tangu wakati huo inakuwa sio kukumbuka ukombozi kutoka utumwani Misri bali ni kuadhimisha ukombozi wa ulimwengu mzima kutoka utumwa wa dhambi.
Eneo la pili ambalo ni katika mlima wa mizeituni Yesu alikwenda kusali. Uchungu wa mateso yaliyokuwa mbele yake ulimuelemea akaomba “Ee Baba ikiwa ni mapenzi yako uniondolee kikombe hiki walakini si mapenzi yangu bali mapenzi yako yatimizwe”. Hili ni tukio linaloonesha kuwa kweli Yesu aliteseka. Mateso yake hayakuwa kitu cha kufikirika au alama tu. Yalikuwa ni mateso yaliyougusa mwili wake, yaliyomsonga na yaliyomuumiza. Aliteseka kwa maana halisi ya kuteseka. Pamoja na hayo aliyatanguliza mapenzi ya Mungu na alitaka kuteseka akiwa na muungano kamili na Baba. Eneo la tatu ambalo linaanza na usaliti wa Yuda, mmoja wa wanafunzi wake na linaendelea kwa mashitaka ya wazee, wakuu wa makuhani na waandishi na hatimaye hukumu ya kifo cha aibu msalabani. Ndipo hapo alipokamilisha yote yaliyokuwa yametabiriwa na kuhitimisha kazi ya ukombozi iliyomleta duniani.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Dominika ya Matawi ni dominika ambamo Kanisa linaadhimisha tukio la Yesu kuingia mjini Yerusalemu. Aliingia akishangiliwa “hosana, hosana” maana yake “utuokoe, utuokoe” . Watu walikuwa na matumaini ya muda mrefu ya kumpata mkombozi na waliona matumaini yao yanatimia kwa njia yake. Njia aliyoitumia na ukombozi alioulenga vilimfanya Yesu aonekane yuko kinyume na matumaini ya wengi. Alilenga kumkomboa mwanadamu kutoka utumwa ulio kiini cha utumwa mwingine wowote ule ambao ni dhambi, na alitumia njia ambayo haifikiriki hata kidogo kuwa ni njia ya ushindi, ambayo ni mateso na kifo Msalabani.
Kwa hakika si kwa Wayahudi wa wakati wa Yesu tu bali hata kwetu leo bado tunaona ugumu. Si wakati wote tunakubali kuwa dhambi ndio msingi wa utumwa unaoukandamiza ubinadamu katika namna mbalimbali na kuwa tunahitaji kukombolewa kwanza kutoka utumwa wa dhambi na maelekeo yake ili mahusiano yetu mengine yawe huru. Si wakati wote pia tunakubali kuteseka pamoja na Kristo katika kutekeleza mpango wa ukombozi wetu. Katika juma hili Kuu tunalolianza tuombe neema ya kuingia katika undani wa tafakari katika mafumbo haya na kuyapokea ili kuupokea ukombozi aliutuletea Kristo kwa mateso, kifo na ufufuko wake.