PASAKA YA BWANA 2019: Fumbo la Pasaka: Kutangazwa & Kushuhudiwa
Na Padre William Bahitwa, - Vatican,
Utangulizi: Kristo amefufuka, Aleluya Aleluya! Heri nyingi kwa Sherehe ya Pasaka kwako ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News na karibu katika tafakari ya Neno la Mungu kwa Sherehe hii kubwa ya Ukombozi wetu. Ni hiki tunachokikiri tunaposema “akafufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko”. Mtume Paulo naye katika waraka wake wa kwanza kwa wakorinto anakiri na kusema “kama Kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure”.
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 10: 34a, 37-43) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Somo hili linawasilisha kilichokuwa kiini cha mafundisho ya mitume kumhusu Kristo na kuhusu ukristo kwa ujumla. Mafundisho haya yaliitwa “Kerygma”, neno la kigiriki linalomaanisha “kutangaza”.Yaliitwa hivyo kwa sababu yalitolewa kama mahubiri ya hadhara. Kiini cha mafundisho hayo kilikuwa ni kutangaza hadharani na kwa nguvu zote kuwa Kristo, yule ambaye Wayahudi walimkataa, wakamsulubisha na kumuua msalabani sasa amefufuka. Hii ndiyo Habari Njema ambayo Mitume popote walipoenda waliitangaza na kuitetea na mafundisho mengine yoyote, yawe ni maelekezo au ufafanuzi waliyatoa kutoka katika msingi huu.
Mtume Petro katika somo hili anatoa hotuba katika tukio ambalo Kornelio, mcha Mungu ambaye hakuwa myahudi, alishukiwa na Roho Mtakatifu. Lilikuwa ni tendo lililomfumbua macho Petro na wayahudi wengine kuwa Kristo hakuja kwa ajili ya wayahudi tu bali kwa ajili ya watu wote wenye mapenzi mema. Katika siku hii ya Pasaka, somo hili linatuonesha kuwa matunda ya Habari Njema, yaani matunda ya Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo hayana mipaka. Yeyote anayemfungulia Kristo moyo wake na kuenenda kadiri ya mfano wa maisha mema aliyoyaishi na kuyafundisha atayapokea matunda ya ufufuko wake.
Somo la pili (Kol 3, 1-4 ) ni waraka wa mtume Paulo kwa Wakolosai. Paulo katika somo hili anauelezea ubatizo kama Sakramenti ya kipasaka. Ubatizo ni sakramenti ya kipasaka kwa sababu inamuunganisha mbatizwa na fumbo la kifo na ufufuko wa Kristo. Kila anayebatizwa katika Kristo anaingia katika mauti yake na kufufuka pamoja naye. Ubatizo ni kupitishwa katika mauti ya Kristo na kufufuka pamoja naye. Kwa sababu hiyo Paulo anawaalika wakristo wa Kolosai waliobatizwa na hivi kufufuliwa pamoja na Kristo, wayaelekeze maisha yao kulingana na hali yao mpya ya maisha. Kwa maneno mengine, Mtume Paulo katika somo hili anaonesha kuwa ufufuko wa Kristo umempatia mwanadamu hali na hadhi mpya ya maisha. Katika hali na hadhi yake hiyo mpya, mkristo anatambua kuwa maisha yake yanayoanzia hapa duniani hayakomei hapa chini bali yanaekea juu Kristo aliko. Na ni huko utakapofunuliwa uhai ambao ufufuko wa Kristo unadokeza utukufu wake.
Injili (Yoh. 20:1-9) Injili ya dominika hii ya Pasaka ni kadiri ya mwinjili Yohane. Ni Injili ambayo imejaa lugha ya alama. Mwinjili Yohane anapenda kwa lugha hii ya alama kufikisha fundisho kuhusu fumbo la kifo na ufufuko wa Kristo. Alama ya kwanza ni ya kaburi, kaburi ambalo linawakilisha kifo. Katika hatua ya kwanza, Maria Magdalena, Petro na yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda wanaoneshwa wakielekea kaburini. Lakini wote watatu, kila mmoja kwa wakati wake, wanapofika kaburini wanasita na kupatwa na hofu. Maria Magdalena alipofika na kuona jiwe limeondolewa alipatwa hofu kuwa Bwana ameondolewa.
Yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, aliyekwenda mbio kuliko Petro, alipofika kaburini mbio ziliisha akasita, akainama na kuchungulia tu. Petro naye alipofika injili inasema “akaja akimfuata”. Hakukuwa kumfuata kwa kuja nyuma yake bali kulikuwa kumfuata katika kusita, kuinama mbele ya kaburi na kuchungulia. Hii ni alama inayoonesha namna ubinadamu ulivyo mbele ya fumbo la kifo. Mbele ya fumbo la kifo ubinadamu husita na huinama kwa hofu. Hatua ya pili inaanza pale Petro anapoingia kaburini. Na hapo ndipo alipoingia pia yule mwanafunzi aliyekuwa wa kwanza kufika kaburini. Ndani ya kaburi Petro anaona vitambaa vya sanda aliyozikiwa Yesu vimekunjwa na ile leso iliyokuwa kichwani imezongwazongwa mbali. Vitambaa haviwezi kujikunja vyenyewe.
Hii ni alama kuwa yupo aliyevikunja. Yupo aliye na nguvu kuliko nguvu za kifo zilizokuwa zimemfunga Yesu kaburini na ni huyo aliyemfungua na kumwondoa kaburini. Na hili lisingeweza kuwa tendo la kibinadamu kwa sababu mbele ya nguvu ya kifo ubinadamu husita na huinama kwa hofu. Kuona hivi yule mwanafunzi aliamini. Alichikiamini katika hatua hii si kuwa Kristo amefufuka bali kuwa hayumo kaburini. Hii ni kwa sababu injili inaongeza kusema kuwa “kwa maana hawajalifahamu bado andiko ya kwamba imempasa kufufuka”. Ushuhuda wa ufufuko wa Yesu kwa mitume ulikuwa hasa katika mambo mawili: kukuta kaburi wazi na Yesu kuwatokea na kuwafunulia Maandiko. Kumbe, Injili ya leo inaeleza na kufafanua msingi wa kwanza wa ushuhuda wa ufufuko wa Kristo yaani kukuta kaburi wazi.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Pasaka ndiyo sherehe ya sherehe zote linazoziadhimisha Kanisa katika mzunguko wa mwaka mzima wa liturujia. Ni katika fumbo hili maadhimisho mengine yote yanatoka na katika fumbo hili yanapata kilele chake. Ni sherehe ya umuhimu na umaana mkubwa sana kwa ukombozi wa mwanadamu. Katika sherehe ya Pasaka tunaadhimisha utimilifu wa ahadi za Agano la Kale na za Yesu Kristo mwenyewe wakati wa maisha yake duniani. Ni ufufuko wa Yesu unaothibitisha ahadi hizo za kale na unaothibitisha kazi zote na mafundisho yote aliyoyatoa Kristo mwenyewe. Ni hiki tunachokikiri tunaposema “akafufuka siku ya tatu kadiri ya Maandiko”.
Mtume Paulo naye katika waraka wake wa kwanza kwa wakorinto anakiri na kusema “kama Kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure” (1Kor 15:14). Ufufuko wa Kristo haukuwa kurudi katika maisha ya kidunia kama ilivyokuwa ufufuko mwingine alioufanya kabla ya Pasaka: kama ule wa binti Yairo au wa Lazaro. Hawa waliyarudia maisha ya kawaida ya ubinadamu na baadaye iliwapasa kufa kama binadamu wengine wowote. Ufufuko wa Yesu ulikuwa tofauti. Ulikuwa ni kupita kutoka hali ya kifo na kuingia katika maisha mengine, maisha ya umilele yasiyofungwa na mipaka ya wakati au mahali na maisha yasiyokufa kamwe.
Na ni kwa njia hiyo ametufungulia nasi waamini wake njia ya kuyaendea hayo maisha. Ufufuko wake unakuwa ni msingi na asili ya ufufuko wetu pia. Kwa kufuata mafundisho ya masomo ya leo, tumwombe Mungu atujalie neema ili kwa ufufuko wa Kristo tutwae jukumu la kuwa mashahidi wake, tuishi kwa kuyatafuta yaliyo juu Kristo aliko na kwa nguvu ya kimungu iliyomfufua Kristo tuzishinde hofu mbalimbali zinazoyasonga maisha yetu ya kibinadamu. Heri ya Pasaka!