Tafuta

Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya Kuombea Miito Duniani: Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya Kuombea Miito Duniani: Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu 

Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema: Vijana iweni na ujasiri

Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Mchungaji Mwema, Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani. Kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Miito Duniani ni "Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu" Baba Mtakatifu anawataka vijana kuthubutu kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya pasaka. Inaitwa Dominika ya Mchungaji Mwema, Siku ya 56 ya kuombea Miito mitakatifu. Maneno ya Yesu; Mimi ndimi mchungaji mwema, kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele kwa kuutoa uhai wangu, ndiyo kiini cha maisha ya miito kwa wale ambao Yesu anawaita wayatoe maisha yao kwa ajili yao na kwa ajili ya wengine kwa kushiriki kazi yake yeye aliye mchungaji mwema. Hapa ndipo linazaliwa wazo la wito wa kujisadaka, kujitoa bila kujibakiza kwa ajili ya ufalme wa mbinguni.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa siku hii ya kuombea miito alioutoa 31/01/2019 katika kumbukumbu ya Mtakatifu Yohane Bosco.  Kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani kwa Mwaka 2019 ni: ”Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu”.Wito ni nini? wito ni neno linalotokana na kitenzi ita. Kuita kunaonesha uhusiano kati ya anayefanya kitendo cha kuita na yule anayeitwa/anayepokea mwaliko huo. Wito ni mwaliko wa ndani ya nafsi ya mtu kutoka kwa Mungu kwa kusudi la kumjua, kumpenda, kumtumikia na hatimaye kufika kwake mbinguni. Kwa uumbaji Mungu ametuita ili tukashiriki naye utukufu wake mbinguni.

Aina mbali mbali za miito: Wito wa ujumla: Sote tunaitwa kuwa watakatifu kama Mungu alivyo mtakatifu. Papa Fransisko anasema; katika wito huu wa ujumla sote tunaitwa kujenga familia ya kikristo kuishi pamoja ndani ya Kristo maisha ya kitakatifu katika mazingira ya kazi zetu mfano Ualimu, udereva, upishi, ujenzi, udaktari au ukulima. Kuzifanya kazi hizi kitakatifu, kwa umoja na uwajibikaji wa kijamii na kisiasa katika misingi ya haki, upendo na wema ndiko tunajipatia utakatifu kwa kuyatakatifunza malimwengu kwa maisha na kazi zetu.

Wito wa pekee. Huu ni wito wa kutumika na kutumikia wengine kwa namna ya pekee zaidi. Huu ni wito kwa ajili ya Mungu na watu wake, wito wa Daraja Takatifu ukisindikizwa kwa karibu zaidi na maisha ya wakfu- Utawa na wito wa upweke. Chimbuko la miito hiyo yote ni Mungu mwenyewe. Mungu anaita na kuchagua yeye anayemtaka katika miito hii. Hakuna awezaye kujitwalia zawadi hii mwenyewe. Wajibu wetu ni kuitikia: “Mimi hapa nitume Bwana” (Is.6:8).

Wito  wa  upadri: Kwa njia ya ubatizo waumini wote wanashiriki ukuhani wa Kristo. Lakini kwa ajili ya huduma katika Kanisa kuna ukuhani wa Daraja Takatifu unatolewa kwa sakramenti ya Daraja Takatifu ambayo kazi yake ni kutumikia katika jina na nafsi ya Kristo mchungaji mwema anayeyatoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wake nao pia wanaoitika wanapaswa kuwa wachungaji wema. Papa Fransisko anasema wakiyatoa maisha yao kwa ujasiri kwa ahadi za Mungu. Huyu kuhani wa daraja (Padri) kwa jinsi ile alivyotiwa wakfu, anawezesha kumwilisha na kuliongoza taifa la kihuhani, akitenda kwa niaba ya nafsi ya Kristo mchungaji mwema.

Padri huyo huyo huipokea sadaka ya Ekaristi Takatifu na kumtolea Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya watu wote, kondoo aliokabidhiwa awachunge. Kazi ya Padri ni kumtambulisha Mungu kwa binadamu. Mungu ndiye kilele cha lengo la maisha yake. Yeye peke yake ndiye anayeshiriki upadre wa Kristo na ndiye awezaye kuwasaidia waamini washiriki ukuhani wa jumla wa Kristo ili waweze kumfikia Mungu. Huyu ndiye mchungaji mwema ambaye Kristo mchungaji mkuu mwema anafanya kazi ndani ya nafsi yake.

Wito  wa  utawa unawaita wanaume na wanawake wajitolee maisha yao kwa Mungu kwa namna ya pekee wakiafuata mashauri ya injili kwa nadhiri za ufukara (kutokuwa na mali ya binafsi), utii (kuwatii wakubwa wa Shirika na Askofu mahalia wanapofanya kazi) na usafi kamili wa moyo/useja/ubirika kwa wanawake (kujinyima kabisa uhusiano wa kimwili-kijinsia). Watawa wanayatolea maisha yao kwa ujasiri mkuu kwa ahadi za Mungu wakidumu katika sala wakiliombea kanisa linalosafiri duniani na lililoko toharani. Kwa maisha yao ya kijumuiya wanafanya kazi za kuwahudumia watu wakifuata karama za waanzilishi wao. Hivyo wanashiriki kwa karibu zaidi kazi ya kichungaji wakiwa na Kristo Mchungaji wao Mkuu katika kuutakatifuza ulimwengu.

Wito wa upweke: Huu ni wito ambao Mungu anawaita anaowataka yeye ili wayatoe maisha yao kwa ajili ya watu wengi. Hawa hawapokei sakramenti ya daraja, sio watawa na wala hawajifungamanisha na maisha ya ndoa bali wanatoa maisha yao, vipaji vyao na muda wao kwa sala na majitoleo yao wanawahudumia wengine mf. waalimu, wauguzi, watoaji wa huduma za kijamii, makatekista au walezi wa vijana na watoto yatima. Kwa moyo wa Ukristo wanajenga Ufalme wa Mungu na wanashiriki kwa karibu kazi ya Kristo mchungaji mwema.

Wito  wa  ndoa na familia: Wito wa ndoa ndiyo kiini cha miito yote. Wito wa ndoa ni wa kwanza kuwekwa na Mungu ili kuendeleza kazi ya uumbaji. Hivyo ni kiwanda cha miito yote. Wito huu umeandikwa na kusimikwa katika maumbile ya mwanaume na mwanamke kwa namna ya ajabu. Mungu aliyabariki na akakusudia yadhihirishe na kuendeleza kazi ya uumbaji: Na Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia: zaeni mkaongezeke, mkajaze nchi na kuitiisha. Hivyo ni katika familia ndiko wanakotoka Wachungaji wema kwani mtini hujulikana kwa matunda yake. Bila malezi bora fungamano katika familia ambayo ni kanisa la nyumbani na shule ya amani na upeendo hatuwezi kupata wachungaji wema wanaomfuasa Yesu mchungaji mkuu mwema.

Wajibu wa kila mkristo: Baba mtakatifu Fransisko anahitimisha ujumbe wa siku ya kuombea miito akisema tuungane kwa pamoja katika sala na kumwomba Mungu atusaidie kutambua na kung’amua mpango wake wa upendo kwa maisha yetu na atupe na kutujalia ujasiri wa kufuata na kutembea katika njia ya wito aliyemjalia kila mmoja wetu.  Kumbe wajibu wa kila mmoja wetu ni kuomba na kuombea miito hii hasa wito wa upadre kwani Kristo mwenyewe anatuhimiza akisema; Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake, kwani mavuno ni mengi watenda kazi ni wachache (Mt.9:38).

Pili tutie mkazo malezi ya awali katika familia kuhusu miito mitakatifu na maisha ya sala ili kupata wachungaji wema kwani mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Baba Mtakatifu Francisko anasema tuwasaidie vijana waweze kuisikia, kutambua na kung’amua sauti ya Mungu ili wawe na uwezo wa kuchagua kwa uhuru wito ambao Mungu anawaita waufuate bila kusita, watoe maisha yao kwa ahadi za Mungu, kwani katika ulimwengu wa utandawazi kuna sauti nyingi zinazowafanya vijana washindwe kutambua wito wa Mungu na hivyo wanajikuta wameingia katika maisha hatarishi.

Tuwasaidie wanaoitikia miito hii kwa hali na mali, kutowakwaza kwa maneno na matendo yetu, kutowatia katika vishawishi na kutowazuia kumtangaza Kristo kama Wayahudi walivyofanya kwa Mitume katika somo la kwanza la Matendo ya Mitume. Walifanya nini? wao walipowaona makutano waliomwamini Kristo, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana, wakalisukumia mbali Neno la Mungu, wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.

Yohane katika somo la pili kutoka Kitabu cha Ufunuo aliona watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao, wametoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwan-kondoo, yeye aketiye katika kiti cha enzi ametanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari ile yoyote. Kwa maana huyo Mwana-kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchem za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao. Hawa ndio walioisikia sauti ya Mchungaji mwema, wakamfuata, wakapata uzima tele.

Inatupasa tujiulize; Je, tunamfuata Yesu mchungaji mwema kokote anakotuongoza au tunafuata njia zetu sisi wenyewe kwa kusikiliza sauti za wachungaji mbwa mwitu ambao ni wezi na wanyanyanyi wasiopita mlangoni? Yesu anatuambia; Mimi ni njia, ukweli na uzima, akasisitiza mimi ndimi nuru ya ulimwenguni yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe bali atakuwa na uzima wa milele. Tuisikilize sauti ya Kristo mchungaji wetu mwema katika nafsi za wachungaji aliotuachia kupitia kwa mtume Petro akisema; “Wewe ndiwe Petro na juu mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda” ili nasi tusishindwe katika maisha yetu ya hapa duniani.  Tumsifu Yesu Kristo.

Jumapili: Miito 2019

 

09 May 2019, 16:03