Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Utukufu na Ushindi wa Kristo!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Kupaa Mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo. Ni sherehe tunayoadhimisha kila mwaka siku ya arobaini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ni siku ambapo Kristo mfufuka alitoweka rasmi katika upeo wa macho ya Mitume wasimuone tena, baada ya kuwatokea mara nyingi akiwaimarisha kiimani baada ya kufufuka kwake, zaidi ya kumtokea Saulo katika barabara ya Damasko. Neno linalosikika masikioni leo ni kupaa. Kiitikiko cha wimbo wa katikati kutoka Zab. 47:5 kinatuhabarisha kuwa: “Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu” Mwinjili Luka katika injili anasema; “Ikawa katika kuwabariki, alijitenga nao akachukuliwa juu mbinguni na wingu likamficha wasimwone tena Lk.24:51.
Tunapoadhimisha sherehe ya Kupaa mbinguni Bwana wetu Yesu Kristo, swali la msingi hapa ni kupaa maana yake nini? Katika lugha ya kawaida ya Kiswahili neno kupaa ni kitenzi kikimaanisha kwenda juu, kutoka katika mzizi paa yaani sehemu ya juu. Katika lugha ya kibiblia neno kupaa ni kuhama kwa mwili wa utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, kutoka duniani na kuingia Mbinguni. Ni hali ya kutukuzwa kwa Yesu, kuwa mkuu na mmiliki wa vitu vyote mbinguni na duniani. Ni kuwa juu ya vitu vyote. Ni kurudia utukufu aliokuwa nao kabla ya umwilisho, yaani kuchukua mwili kwa mama Bikira Maria. Ni kuvikwa taji ya ushindi. Kristo ni mshindi ameshinda dhambi na mauti [Mk 16:19].
Ni lini Kristo alipaa mbinguni? Tunakiri katika kanuni ya Imani kuwa “akafa, akazikwa, akashukia kuzimu na siku ya tatu akafufuka katika wafu na akapaa mbinguni ameketi kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi”. Yohane anatuambia; Kisha akalifungua pazia la Mbingu na kuingia pamoja na roho za watakatifu [Uf. 7:14; 14:2]. Mmojawapo wa wale wahalifu waliosulibiwa pamoja na Yesu alimwambia, “Ee Yesu unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako,” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mahali pema peponi” [Lk 23:42-43]. Hivyo hakukuwa na wakati fulani uliopita kutoka ufufuko mpaka kupaa katika maana ya kuwa na hali ya utukufu.
Kwa ufufuko Yesu alitoka kaburini akiwa na mwili wa utukufu, usiofungwa na nguvu za maumbile ndiyo maana aliweza kuingia na kuwatokea Mitume hata milango ilipokuwa imefungwa. Kwa hiyo mara baada ya ufufuka Yesu aliishi mbinguni na kutoka huko aliwatokea wafuasi na mitume wake mara nyingi kwa muda wa siku arobaini, akiwaimarishe ili wapate kuamini kuwa ni kweli amefufuka ili waweze kuwa na ujasiri wa kuwatangazia wengine ili nao waweze kuamini [1Cor 15:14]. Tunaposema Yesu mfufuka alipaa mbinguni siku ya arobaini, tuna maana kwamba hiyo ni siku ambapo alionana ana kwa ana, uso kwa uso, macho kwa macho na wanafunzi wake kwa mara ya mwisho mpaka atakapokuja mara ya pili katika utukufu wake.
Na siku arobaini zina maana ya muda wa kutosha, kwa Wayahudi huu ndio ulikuwa mtindo wa kuongea kwa njia ya namba kuwakilisha mda wa kutosha [Kut 34:28] ambao Yesu mfufuka aliwatokea wanafunzi wake akiwaandaa kumpokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, siku hamsini baada ya kufufuka na siku kumi baada ya kupaa kwake, yaani kuacha kuwatokea na kuonekana kwa mitume wake lakini nguvu zake zikaendelea kufanya kazi kwa mitume hata leo katika mapadre wake, katika sakramenti zake, katika neno lake na katika sala zetu.
Katika simulizi la tukio la kupaa Bwana wetu Yesu Kristo mbinguni, tunaambiwa kwamba, “Wingu likampokea wasimwone tena.” Wingu katika Maandiko Matakatifu ni alama ya uwepo wa utukufu wa Mungu na ni fumbo la utukufu wa Mungu. Ni wingu lile lile la giza kuu alimokuwamo Mungu alilolikaribia Musa (Kut. 20:21). Ni wingu lile lile lililoelea juu ya hema ya kukutana na Mungu (Kut. 40:34). Ni wingu lile lile ambalo mwenyezi Mungu aliwatangulia katika mnara wa wingu kuwaonesha njia, na usiku aliwatangulia katika mnara wa moto kuwaangazia Waisraeli ili waweze kusafiri mchana na usiku (Kut. 13:20–22). Ni wingu lilelile ilimotoka sauti ya Baba baada ya ubatizo wa Yesu mtoni Yordani na baada ya Yesu kugeuka sura mlimani Tabor ikisema huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye.
Kupaa kwa Yesu mbinguni maana yake ni kwenda kwa Mungu Baba. Neno la kiswahili mbinguni kwa kiebrania ni shamayim ni neno mbadala kwa jina la Mungu. Ndiyo maana Yesu alisema “kheri walio maskini wa roho kwa maana ufalme wa mbinguni ni wao” akimaanisha ufalme wa Mungu ni wao (Mt. 5:3). Ni kwanini mbinguni, liwe jina mbadala la Mungu? Kwa Wayahudi juu mawinguni/juu mbinguni ni makao ya Mungu na milimani ni sehemu ya kukutana na Mungu. Kilele cha mlima ni sehemu ya karibu zaidi na Mungu.
Hivyo mlimani ilikuwa sehemu ya kukutana, kumuabudu na kumsikiliza Mungu. Ndiyo maana Mungu alimtokea Musa katika kichaka kilichowaka moto katika mlima Horebu ujulikanao kama mlima Sinai (Kut.3:1-6) ndipo alipopokea Amri kumi za Mungu/Torah (Kut.24:12-18) na mfalme Sulemani alijenga hekalu la Mungu juu ya mlima Sayuni, mlima huo ukawa mahali pa pekee pa kukutana na Mungu. Baadaye Sayuni ukawa mji wa mfalme/Masiha, ambapo mataifa yote yatakusanyika (Isa.2:1-3, Zek.14:16–19; Ebr.12:22; Uf.14:1). Katika Agano Jipya matumizi ya maneno juu au mbinguni yameendelea kutumika kama jina mbadala la Mungu. Malaika Gabriel anapompasha habari Bikira Maria anamwambia usihofu, kwa maana “Roho Mtakatifu atakujia juu yako na nguvu zake aliye juu zitakufunika kama kivuli (Lk. 1:35).
Zakaria katika wimbo wa kinabii anasema “naye mtoto ataitwa nabii wake aliye juu” (Lk. 1: 76). Yesu katika kuhubiri anasema, tubuni kwa maana ufalmwe wa Mbinguni umekaribia. Yesu kabla ya kupaa mbinguni anawachukua wanafunzi wake na kwenda nao juu ya mlima na baada ya kuwaasa wasitoke Yerusalem mpaka watakapovikwa uweza na nguvu kutoka juu ndipo akachukuliwa kwenda juu mbinguni. Hatimaye alipokua akienda zake mbinguni (yaani kwa Mungu) malaika walitokea wakawaambia kwamba wasishangae kwani jinsi hiyo hiyo walivyomuuona akienda zake mbinguni ndivyo atakavyokuja. Kumbe maneno juu, mbinguni, angani, wingu yanaashiri uwepo wa utukufu wa Mungu, utukufu alionao Yesu mfufuka. Hali hii mpya ya utukufu inamfanya Kristo asifungwe na sheria za maumbile, wakati au mahali.
Kupaa mbinguni kwa Kristo Yesu ni uthibitisho kwamba maisha ya hapa duniani siyo ya umilele, tuna maisha ya umilele mbinguni Kristo aliko, ndiyo maana anasema anaenda kutuandalia makao ili aliko nasi tuwepo, hili ndilo tumaini letu. Kama ndivyo hivyo, tufanye nini tuweze kufafanana na Kristo mfufuka na kushiriki utukufu pamoja naye mbinguni baada ya maisha ya hapa duniani? Kwanza yatupasa tufuate Agizo la Yesu Kristo “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu (Mt. 28: 19). Kuihubiri Injili kwa maneno na matendo yetu. Tukiishi kulingana na amri za Mungu na za Kanisa, na kwa kupokea sakramenti kwa kustahili nasi tutashiriki utukufu wa Kristo mbinguni.
Msafiri daima anajiandaa na kutayarisha masurufu ya njiani. Swali la kujiuliza Je, unayo masurufu ya kutosha? Masurufu yetu tunayapata katika sala, neno la Mungu, sakramenti za kanisa na katika kutenda matendo mema, hasa kuwahudumia wahitaji kwani ni katika hao tunakutana na Yesu. Swali, Je, kama Kristo akishuka kutuchukua, utakuwa mmojawapo wa kupaa mbinguni pamoja naye? Kupaa kwa Yesu mbinguni, kutusaidie kuungama imani yetu bila woga na kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo mpaka miisho ya dunia ili tukashiriki naye utukufu wa Mungu mbinguni. Hayo ndiyo masurufu yetu ya njiani. Tumsifu Yesu Kristo.