Tafuta

Jumapili IV ya Pasaka ni Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, Siku 56 ya Kuombea Miito mbali mbali ndani ya Kanisa: Utakatifu wa maisha, Familia, Upadre na Maisha ya Wakfu. Jumapili IV ya Pasaka ni Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, Siku 56 ya Kuombea Miito mbali mbali ndani ya Kanisa: Utakatifu wa maisha, Familia, Upadre na Maisha ya Wakfu. 

Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema: Siku ya Kuombea Miito!

Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, ni Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu”. Yesu ndiye mchungaji mwema, ni njia ukweli na uzima. Viongozi wa Kanisa na familia waige mfano wa Kristo Yesu!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Mama Kanisa anaadhimisha Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Kristo Yesu Mchungaji mwema, sanjari na Siku ya 56 ya Kuombea Miito Duniani. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa maadhimisho haya unaongozwa na kauli mbiu “Ujasiri wa kuthubutu kutekeleza ahadi ya Mungu”. Yesu ndiye mchungaji mwema, ni njia ukweli na uzima. Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake ni vielelezo vya Kristo Mchungaji mwema kama ilivyo pia kwa Mapadre. Sifa kuu za mchungaji mwema, ni kusikiliza kwa makini na kujibu kwa huruma na mapendo mahitaji msingi ya kondoo wake. Mchungaji mwema, yuko tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya kundi lake!

Dr. David livingstone alikuwa mmisionari, tabibu na mvumbuzi hodari. Stanley alimpata baada ya kumtafuta kwa muda mrefu. Stanley alisikia habari na umaarufu wa mmisionari huyu akiwa kwao Scotland. Akafunga safari ndefu kumtafuta. Akampata Ujiji, huko Kigoma. Baada ya kukaa naye kwa muda wa kutosha, Stanley aliomba abatizwe na kuwa mkristo. Stanley anashuhudia kuwa namna Livingstone alivyohudumia wale watu aliokaa pamoja nao na kuwatibu magonjwa yao ilitosha kugusa maisha yake. Yote aliyoyaona na kushiriki ilikuwa ni katekisimu iliyokamilika.

Wito na ujumbe tuupatao leo ni kutafakari juu ya maana ya wito wa Mungu na hivyo kusali kwa ajili ya kuombea miito mbali mbali ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha! Katika somo la injili Yoh. 10:27 – Yesu anatamka wazi – mimi ni mchungaji mwema. Hakika kwa Waisraeli tamko kama hili liliwashtua sana kwani kadiri ya mafundisho na imani yao mchungaji wao ni mmoja tu naye ni Bwana Mungu – Zab. 23,1 – Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu. Zaidi sana katika Yoh. 10:30 – anasema  - Mimi na Baba tu umoja. Hakika tamko kama hilo si la kawaida na lataka mtazamo mpya – ni kama vile mtu afike hapa leo na aseme – tangu leo mahali hapa ni pangu – hali tukijua wazi kuwa ni mali ya parokia au nyumba ya malezi au ardhi ya fulani au chuo chetu n.k.

Katika mpango wa ukombozi wa mwanadamu, Mungu alimtuma Mwanae wa pekee, Kristo Yesu, tena kwa mamlaka, naye Mwana anawatuma wale aliowachagua, tena anawatuma kwa mamlaka – Yoh. 20:21-23 – Basi Yesu akawaambia tena amani iwe kwenu, kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi, naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, pokeeni Roho Makatifu, wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa, na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Hii ni aina mpya kabisa ya maisha ya kiroho. Mwenyezi Mungu anampatia mwanadamu msamaha wa dhambi. Hakika mtazamo wa kibinadamu tu hautoshi.

Si rahisi namna hiyo kama vile wawili wanaogombana wanavyoweza kusema – haya basi nakusamehe. Pengine mmoja anasema hivyo ili yaishe tu kwa nje ila moyoni bado uchungu unabaki. Jicho la imani katika somo hili na neno hili la Mungu siku ya leo lahitajika. Mungu anatuma na anatoa zana za kazi – Mt. 28,18 – Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Halafu Yesu anachukua hatua za kuita wale aliowachagua – Yoh. 15,16 – si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa, ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awaapeni – na zaidi sana akaweza kusema awapokeaye ninyi, anipokea mimi, naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenituma - Mt. 10:40. Hili ndilo fumbo la wito wa Mungu. Katika Yoh. 10:11 tunaambiwa kuwa mchungaji mwema ni yule atoaye uhai wake kwa ajili ya kundi.

Ndiyo maana tunaposali leo kwa ajili ya miito tunasali pia ili tuweze kuelewa vizuri maana ya wito wa Mungu ili tuweze kutofautisha wito wa Mungu na wito toka kwa mwanadamu. Neema ya Mungu husikilika na kupokeleka tukitoa nafasi na muda kutafakari juu ya mapenzi yake kwetu. Katika Rum. 10:17 twaambiwa kuwa imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo. Huu ufahamu ndio uliomsukuma Paulo na wengine kwenda kwa mataifa, Yohani kushuhudia na sisi tulioko hapa leo kuendelea kuamini na kusadiki juu ya upendo huo wa Mungu. Somo la kwanza linatusaidia pia kutafakari sana wito wa leo. Kanisa la kwanza linaishi huo ushuhuda – wanatangaza na kuteseka. Wametambua upendo wa Mungu na wanautangaza.

Ili kuitangaza Pasaka hatuna budi kuutangaza na kuishi ushindi wa Kristo Mfufuka. Kuishi maisha ya furaha na utukufu. Ushindi wa makundi mbalimbali katika somo la ufunuo ni uthibitisho wa hilo. Wanashinda kwa sababu wanaishi hilo pendo la Mungu. Wanashinda wakitangaza utukufu huo mpya. Katika Waraka wa 1Kor. 9:22, Paulo anasema kwa wanyonge nilikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Huu ndio wito anaotuita Mungu ili tumfuate. Wakati mwingine ili kuwapata kondoo hatuna budi kuvaa ngozi ya kondoo. Mungu si mwanadamu, lakini alijifanya mtu ili apate kutukomboa. Kila aisikiaye sauti ya Mungu na kumwamini na kumsadiki anaalikwa kulichunga neno hilo la Mungu. Sote tunaalikwa kusali ili wapatikane wengi wanaojitoa kueneza ufalme wa Mungu na kuwaombea na kuwatunza wale wote waliojitoa kueneza Habari Njema kwa sala, maneno na matendo. Tumsifu Yesu Kristo.

08 May 2019, 14:52