Jumapili ya V ya Pasaka: Saa ya Ushindi & Upya wa maisha!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari masomo ya dominika ya 5 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa. Pasaka inatukumbusha kuwa hali ya ubinadamu wetu iliharibiwa na dhambi na uharibifu huu uliathiri ulimwengu mzima na uliharibu mahusiano yetu na Mungu. Fumbo la Pasaka na ukombozi aliotuletea Kristo ndio uliotutoa katika uharibifu huo na kuanzisha Agano Jipya na Mungu, Agano la uzima na neema.
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mdo. 14:21b-27) ni kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume. Somo hili linahitimisha safari ya kwanza ya kitume ya Paulo ambapo yeye pamoja na Barnaba wanapitia tena makanisa mahalia waliyoyaanzisha ili kuendelea kuyaimarisha katika imani. Ujumbe wanaowapa ndio huu “imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi”. Polepole ujumbe huu ndio uliokuwa kama kauli mbiu ya wakristo wa mwanzo, kauli mbiu iliyowapa ujasiri wa kukabiliana na dhiki, manyanyaso hadi kufia dini. Badala ya kurudi nyuma na kuogopa, kauli mbiu hii iliwafanya wakristo wa mwanzo kuona fahari kubwa pale walipoteswa kwa sababu ya imani yao.
Somo hili pia linatuonesha baadhi ya desturi ambazo zimekuwapo tangu mwanzo wa Kanisa, desturi ambazo kwa njia ya Mapokeo zinaendelea hadi sasa katika kanisa. Tunaona desturi ya mitume kuwachagua wazee wa makanisa. Paulo na Barnaba waliwachagua wazee katika makanisa hayo waliyoyaanzisha, wakawawekea mikono na kuwakabidhi kundi. Mahalifa wa mitume ndio maaskofu. Nao huendeleza jukumu hilo la kuwachagua na kuwawekea mikono mapadre kwa ajili ya kulichunga kundi wanalowakabidhi. Ni mwaliko wa kutambua kuwa kanisa letu limejengwa pia juu ya nguzo imara ya desturi na mapokeo. Ni wajibu wa msingi sana kuzingatia desturi na mapokeo ya kanisa katika kuendeleza utume wa kanisa kwani desturi na mapokeo hayo vimefungamana kwa karibu sana na utambulisho wa kanisa lenyewe.
Somo la pili (Ufu 21:1-5a ) ni kutoka kitabu cha Ufunuo na linahusu maono ya mbingu mpya na nchi mpya. Nabii Isaya alitabiri ujio wa Yerusalemu mpya na ulimwengu mpya. Katika Isa. 65:17 anasema “maana tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya na mambo ya kwanza hayatakumbukwa”. Maono haya ya Yohane ni kuonesha kutimia kwa utabiri huu wa kinabii. Katika lugha ya kibiblia, upya haina tu ile maana ya kitu kinachokuja baada ya kingine. Upya humaanisha ukamilifu, kitu kilichofikia ukomo wa thamani yake au ukamilifu usio na doa.
Kwa hiyo ulimwengu mpya au Yerusalemu mpya ni ulimwengu au Yerusalemu ni ile iliyo kamili: iliyojaa fadhili za Bwana na utukufu wake na isiyo na chochote kinachokinzana na utukufu huo. Ndiyo maana katika maono haya Yerusalemu hii mpya inashuka kutoka mbingumi, yaani ukamilifu huu wa ulimwengu ni kazi yake Mungu mwenyewe. Yohane anaona pia kuwa ukamilifu huu utakuwa pia ni juu ya ubinadamu wote ambao sasa utastahili au utastahilishwa kuingia katika umoja na Mungu mwenyewe. Ubinadamu utakuwa kama bibi arusi aliyekwisha kupambwa tayari kumlaki mumewe. Ndipo Yohane anapata maono na kusikia sauti kuwa Mungu mwenyewe atafanya maskani na watu wake, atafuta kila chozi katika macho yao na wala mauti, wala maombolezo wala kilio havitakuwapo tena.
Somo hili ni mojawapo ya sehemu katika kitabu cha Ufunuo zinazotupa ufunguo wa kuelewa maono ya Yohane katika kitabu kizima. Ni hapa tunaona kuwa maono ya Yohana katika kitabu hiki si ya kulenga kuogopesha watu kuhusu mambo yajayo au kuwatisha kuhusu uharibifu wa ulimwengu. Badala yake ni maono yanayowajaza watu wa Mungu matumaini na kuwaanda kwa ajili ya muungano na Mungu, muungano ambao unakuwa ni nguvu na kichocheo cha kutia bidii katika harakati za sasa za imani na changamoto zake.
Injili (Yoh. 13:21-33a, 34-35) Injili ya leo kadiri ya mwinjili Yohane inaturudisha katika ile karamu ya mwisho ya Yesu na wanafunzi wake ambapo baada ya chakula Yuda aliondoka akabaki Yesu na wanafunzi kumi na moja waliosalia. Hapo ndipo kadiri ya mwinjili Yohane, Yesu alipoanza kuzungumza kwa kirefu na wanafunzi wake na kuwapa maelekezo ya mwisho akiwafafanulia mambo ambayo polepole tutaanza kuyasikia katika sura hizi. Anapoondoka tu Yuda, Yesu anatamka kuwa imetimia saa ya kutukuzwa mwana wa Adamu, saa ambayo Mungu anatukuzwa ndani ya nafsi ya mwana wa Adamu. Hii ni saa ya ushindi.
Ushindi ambao anakwenda kuupata Kristo kwa njia ya Msalaba na ni ushindi ambao Mungu anakwenda kuupata kwa njia ya mwana wa Adamu. Imetimia saa ya Yesu kuchukua njia ambayo ni yeye tu anaweza kuipitia na wala si yeye pamoja na wanafunzi wake bali yeye peke yake na hivyo anawaambia wanafunzi wake “bado kitambo kidogo niko pamoja nanyi”. Katika kuielekea saa hii ya ushindi na katika kuuingia na kuushiriki ushindi huu wa Mwana wa Adamu, Yesu anawaachia wanafunzi wake amri mpya ya mapendo. Inarudi ile dhamira ya upya tuliyoiona katika tafakari ya somo la kwanza, upya kwa maana ya ukamilifu, na hivi anawapa amri ya mapendo kamili.
Na mapendo haya kamili si yale ya mtu kumpenda mwingine kama anavyojipenda mwenyewe kwa maana kwa kufanya hivi yeye ndio anakuwa kipimo cha upendo. Katika ukamilifu au upya wa mapendo kipimo cha upendo ni Yesu. Ndio maana anawaambia pendaneni kama mimi nilivyowapenda. Huu ni mwaliko wa kudumu wa kila mfuasi wa Kristo kuutafakari upendo alionao Kristo kwake, namna Kristo anavyompenda na hivi naye ajibidiishe kuwapenda wengine kwa upendo ambao Kristo anao juu yake.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Pasaka ni adhimisho linalotufungulia mlango wa upya wa maisha. Linauangazia upya wa ubinadamu, upya wa ulimwengu mzima na upya wa mahusiano kati ya viumbe vyote na Mungu muumbaji. Pasaka inatukumbusha kuwa hali ya ubinadamu wetu iliharibiwa na dhambi na uharibifu huu uliathiri ulimwengu mzima na uliharibu mahusiano yetu na Mungu. Fumbo la Pasaka na ukombozi aliotuletea Kristo ndio uliotutoa katika uharibifu huo na kuanzisha Agano Jipya na Mungu, Agano la uzima na neema. Hii ndiyo furaha ambayo tunaiadhimisha katika kipindi hiki cha siku 50 za Pasaka.
Maandiko Matakatifu katika dominika hii ya 5 ya Pasaka yametuingiza katika tafakari hiyo ya upya wa maisha. Katika lugha ya kibiblia yametuonesha ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuunda upya ulimwengu ulioathiriwa na dhambi. Yametuonesha pia matumaini ya waana wa Mungu kuifikia siku hiyo ambayo ulimwengu utaumbwa upya, siku itakapopita mbingu ya kwanza na nchi ya kwanza inayosongwa na mahangaiko ya kila aina na giza la dhambi na kuja ile mbingu mpya na nchi mpya iliyojaa wingi wa neema ya Mungu na inayodhihirisha ukamilifu na umoja wa ubinadamu na muumba wake kama alivyokusudia tangu mwanzo wa uumbaji.
Ahadi hii imetimia kwa njia ya Kristo na kwa tukio lake la Kipasaka. Na sasa anatualika sote kuuishi upya huu na kuudhihirisha kwa amri mpya aliyotuachia, amri ya mapendo. Upendo ndio ufunguo wa kuingia katika upya wa maisha ndani ya Kristo na kama alivyotuonesha katika injili ya leo upendo ndio utambulisho wa kuwa mwanafunzi wake. Tujitafakari leo juu ya namna tunavyouishi upendo huu katika maisha yetu ya kila siku, tujibidiishe katika upendo na tumwombe Mungu azidi kuwasha ndani yetu moto wa upendo wake; tupendane kama Yeye anavyotupenda.