Tafuta

Wito wa kumfuasa Kristo Yesu ni sadaka ya maisha inayotolewa kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu! Wito wa kumfuasa Kristo Yesu ni sadaka ya maisha inayotolewa kwa unyenyekevu, ari na moyo mkuu! 

Tafakari: Jumapili XIII: Wito wa kumfuasa Kristo Yesu!

Ni katika kumtumikia Mungu kwa uaminifu tunaitwa kuwa watakatifu kushiriki furaha ya milele mbinguni. Wito sio wa shuruti. Kila mmoja yuko huru kuitika na kukubali kwa hiari yake mwenyewe kwa kuwa binadamu amejaliwa mwili, roho, akili, utashi na uhuru kamili ili awajibike kikamilifu. Ni kwa njia ya mwili tunamtumikia Mungu kwa kuwahudumia wenzetu na kuutiisha ulimwengu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, karibu katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 13 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Dominika hii inatukumbusha kuwa kumfuasa Kristo ni kujitoa sadaka, kuacha yote kwa ajili ya uzima wa milele. Na sadaka iliyo safi sio ya shuruti bali ni ya kujitoa kwa uhuru kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kama anavyotuambia Mtume Paulo katika waraka kwa Warumi akisema, “Basi ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana” 12:1. Mungu amemwandalia kila mmoja wetu namna ya maisha ambayo kwayo tunapaswa kumtumikia.

Mpango huu wa Mungu ni kwa kila mwanadamu na unaanza hata kabla ya kuzaliwa ndivyo anavyomwambia Yeremia, “Kabla hujachukuliwa mimba, mimi nilikujua, kabla hujazaliwa, mimi nilikuweka uwe nabii kwa mataifa” (Yer.1:5). Ni katika kumtumikia Mungu kwa uaminifu tunaitwa kuwa watakatifu kushiriki furaha ya milele mbinguni. Wito huu sio wa shuruti. Kila mmoja yuko huru kuitika na kukubali kwa hiari yake mwenyewe kwa kuwa binadamu amejaliwa mwili, roho, akili, utashi na uhuru kamili ili awajibike kwa matendo yake mwenyewe. Ni kwa njia ya mwili tunamtumikia Mungu kwa kuwahudumia wenzetu na kuutiisha ulimwengu.

Roho ndiyo itiayo uzima katika mwili na ni kwa njia ya roho tunaweza kuwasiliana na Mungu Baba yetu aliyetuumba. Ni kwa njia ya akili tunaweza kunga’amua, kufahamu, kutambua na kujua kati ya lililojema na baya na kwa utashi tunachagua kutenda kwa uhuru kile tunachokijua. Uhuru unaweza kutumika vizuri au vibaya. Adamu na Hawa walikuwa na uhuru wa kuchagua kula tunda au kutolila kama Mungu alivyokuwa amewaamuru. Wao wakachagua kula tunda. Walichagua kwa uhuru wao wenyewe kwani maandiko matakatifu yanatuambia “Basi, mwanamke alipoona kuwa mti huo ni mzuri kwa chakula, wavutia kwa macho, na kwamba wafaa kwa kupata hekima, akachuma tunda lake, akala, akampa na mumewe naye pia akala” (Mwa.3:6).

Kumbe, hawakulazimishwa bali walichagua walichokipenda wao. Kwa kufanya hivyo walitumia vibaya uhuru wao kwani kuchagua kwa uhuru si kuchagua unachokipenda. Kuchagua vizuri na kwa uhuru ni kuchagua mapenzi ya Mungu bila kulazimishwa au kushurutishwa. Ni kuyatambua, kuyapenda, na kuyatimiza mapenzi ya Mungu Baba kwa moyo wa upendo. Ndiyo maana Paulo katika somo la pili la waraka kwa Wagalatia anasema, “Ninyi ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za dunia” (Gal.5:13). Paulo anasisitiza na kusema, “uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo,” Gal 5:13b. “Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako,” Gal 5:14.

Huku ndiko kuenenda kwa roho na kuvidhibiti vilema vya mwili, ikiwa ni pamoja na tamaa zake, Gal 5:16.  “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zinapingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka,” Gal 5:17. Lakini dereva wa maisha yako akiwa Roho wa Mungu, utaruhusu ndani yako moyo usio na ubaguzi na kujitoa kwa upendo bila kujibakiza. Na huu ndio ukweli kwamba, tukiongozwa na Roho hatupo tena chini ya sheria, Gal 5:18. Huko ndiko kuitika wito wa kumpenda, kumjua na kumtumikia Mungu kwa uhuru, ni kumfuasa Krsito na ndiyo sadaka iliyo hai na ya kupendeza.

Elisha katika somo la kwanza ni mfano hai wa kuitika wito wa kumtumika Mungu bila shuruti. Elisha anapoitwa na Mungu kupitia Elia, mara anaacha yote na kuanza safari ya utumishi kwa ajili ya wokovu wa watu wake wakati ambapo Ahabu na Yezebeli waliwatesa waisraeli wakiwashurutisha wamkane Mungu wao wa kweli na wamwabudu Baali. Tunaambiwa, Eliya alipopita karibu na Elisha, akatupa vazi lake juu yake, Elisha akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata na kukutumikia. Elia akamwambia, enenda, urudi naye akaenda akamrudia. Ndiyo ya Elisha inakuwa ndiyo kweli, akainuka, akamfuata Eliya akamhudumia na Mungu akapendezwa naye.

Injili inaeleza kuwa maisha ya kikristo ni ya sadaka. Ni kujitoa bila kujibakiza na bila kigeugeu kwani lengo la Kristo kujimwilisha na kukaa nasi sio ushindi wa kidunia bali kujitoa sadaka yeye mwenyewe kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Yesu akielekea Yerusalemu kutimiza fumbo la ukombozi, njiani anakutana na watu wanaomwomba kuwa wafuasi wake. Lakini Yesu hatoi jibu la ndio au hapana. Anachokifanya anawaambia nini maana ya kumfuata yeye na nini cha kufanya. Kwa mtu wa kwanza anambwambia, mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Maana yake kipaumbele cha kumfuata Kristo sio maisha ya raha bali ni kujikatalia malimwengu kwa ajili ya ufalme wa mbinguni.

Ni kujitoa sadaka iliyo hai na ya kumpendeza Mungu. Kwa mwingine anamwambia waache wafu wawazike wafu wao. Ni jibu gumu na la kukatisha tamaa, lakini linatufundisha kuwa kifo ni kweli isiyopingika na hivyo shughuli zake na mazingira yake, isiwe sababu ya kuiacha na kuikana imani yetu, tuwe tayari kuacha yote kwa ajili ya ushuhudi wa imani yetu. Kwa wa mwisho anamwambia, mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu. Tunafundishwa kuwa na msimamo thabiti katika imani na kutokuwa ndumilakuwili au kigeugeu katika maisha ya imani. Tunalopaswa kufanya ni kujenga uaminifu na utayari wa kutimiza kile tulichoitiwa na kukubali bila shuruti kwa sifa na utukufu wake Mungu.

Kwa Ubatizo wetu tuliitwa kuacha yote na kumfuata Kristo. Ubatizo si lelemama bali ni wajibu msingi na wa kwanza katika maisha yetu ya kuujenga muunganiko na Mungu wetu mtakatifu sana. Ni kukubali kujitoa sadaka sisi wenyewe. Sakada ni nini? Ni kile kinachotolewa na kuteketezwa kwa heshima ya Mungu, ili laana zifungwe, neema na baraka zifunguliwe. Sadaka kubwa na halisi ni ya Kristo msalabani (1Kor 5:7). Misa Takatifu ndilo tambiko kubwa na la pekee kwa maisha ya Kikristo. Ndiyo maana Padri Kabla ya kuanza mageuzo (kabla ya kutolea tambiko hili kwa ajili ya dhambi zetu) anatualika sote akisema: “salini ndugu ili sadaka yangu na yenu ikubaliwe na Mungu Baba mwenyezi.”

Hivyo ili tuzipate baraka na neema zitokanazo na sadaka hii, tambiko hili takatifu, ni lazima katika azimisho la misa kwanza tuwe makini katika sala, pili lazima tuwe na moyo wa ibada kwa Mungu, tukijitoa kabisa mwili na roho, kujitoa nafsi zetu pamoja na Kristo kwa Mungu kama anavyotuambia mzaburi, “sadaka yangu Ee Mungu ni moyo mnyoofu na uliopondeka” (Zab 51:17). Moyo mnyoofu na uliopondeka ndicho anachoangalia Mungu. Katika Sadaka ya Misa Takatifu tunapaswa kutoa mioyo yetu pamoja na yote tuliyonayo yaani sehemu ya mali yetu kama ishara ya nje ya sadaka yetu ya moyo. Pesa au sehemu ya mali tunayotoa inaitwa sadaka kwa sababu ni kile kinachotolewa kuwakilisha kilicho ndani Moyo mnyoofu na uliopondeka.

Sadaka hii haipimwi kwa wingi bali kwa moyo. Ndiyo maana Yesu alimsifia Mjane aliyetoa vyote alivyokuwa navyo kwa moyo mnyoofu na nafsi yake, vyote analimtolea Mwenyezi Mungu na kumtegemea yeye peke yake Mk 12:41-44. Katika maisha yetu ya kumfuasa Kristo daima tusikilize maneno ya Paulo akisema, “Basi ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu na ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Dhabihu hii iliyo hai katika miili yetu ni kujitoa kwa kila namna na kuruhusu miili yetu itumike mbele za Mungu kwa ajili ya utukufu wake. Kuitoa miili kuwa dhabihu ni kuruhusu miili yetu kutii na kufuata makusudi ya Mungu, na pia ni kukubali kuishi kwa ajili ya injili.

Tunapojitoa katika kufanya kazi ya Mungu kwa moyo na upendo tunatoa dhabihu iliyo hai. Tunapofanya kazi za Kanisa kwa majitoleo bila shuruti, tunajitoa sadaka. Paulo anaongezea kusema sadaka hii itakuwa takatifu na ya kumpendeza Mungu, na ndiyo itakayotupa hadhi ya kuvikwa taji ya utukufu mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

J13 ya Mwaka
29 June 2019, 17:46