VATICAN-POPE-MASS VATICAN-POPE-MASS 

Sherehe ya Pentekoste: Kuzaliwa kwa Kanisa; Ushuhuda & Walei!

Kanisa linasadiki na kufundisha kuhusu Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii! Katika Sherehe ya Pentekoste, Kanisa liadhimisha siku ya kuzaliwa kwake, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakatoka kutanga Habari Njema. Ni Siku ya Waamini Walei Duniani.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Ndugu msikilizaji wa radio Vatikani, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu, katika Domenika ya Pentekoste. Ni siku ya “Kuzaliwa kwa Kanisa.” Ni adhimisho la mwanzo mpya. Ni sikukuu ya kushuka kwa Roho Mtakatifu. Ni sikukuu ya vitu “kuumbwa” upya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Pentekoste maana yake ni “ya hamsini”. Ni siku ya hamsini tangu tulipo sherehekea Jumapili ya Pasaka, domenika ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Sherehe hii tunaadhimisha ujio wa Roho Mtakatifu, tunakumbuka kuzaliwa kwa Kanisa na mwanzo wa utume wa Kanisa. Ni sherehe ya waamini walei wote. Sherehe hii inakamilisha fumbo la Pasaka kwa kuhitimisha kipindi cha Pasaka, tunaacha kusali sala ya Malkia wa Mbingu na kuanza kusali sala ya Malaika wa Bwana.

Mwanzo na asili ya sherehe ya Pentekoste. Katika Agano la kale kwa asili sherehe hii ilikuwa ni sikukuu ya wakulima wakaanani. Ilikuwa sikukuu ya kumshukuru Mungu baada ya kuvuna mazao yao ya kwanza na papo hapo kumwomba Mungu awajalie tena mavuno mema msimu ufuatao. Ndiyo maana iliitwa sikukuu ya mavuno au sikukuu ya wakulima (Kut. 23:16), au sikukuu ya mavuno ya kwanza (Hes 28:26). Shughuli kuu ya Waisraeli walipotoka Misri ilikuwa ni ufugaji. Walipoingia Kaanani waliiga mila na desturi za wakaanani ikiwemo shughuli za kilimo pamoja na sikukuu zao na kuziingiza katika sikukuu ya imani yao ikiwemo hii ya kumshukuru Mungu kwa mavuno mapya. Mwanzo, sikukuu hii haikuwa na tarehe hasa ya kusheherekea. Baadae Makuhani waliihusianisha na historia ya Wokovu wao yaani Pasaka na kupokelewa kwa amri kumi za Mungu mlimani Sinai.

Pentekoste iliitwa pia Sikukuu ya majuma kwa vile ilisherehekewa majuma saba baada ya Pasaka ya Wayahudi na hivyo Pentekoste huitwa siku ya hamsini baada ya pasaka, (2Mak 12:31ff; Tob 2:1). Hivyo ina maana kwamba Sherehe hii ilianza baada ya kuwekwa rasmi tarehe maalumu ya Pasaka ya Wayahudi, kwani wahusika wa Sherehe hii walikuwa ni Wayahudi au Waisraeli. Kadiri muda ulivyoendelea, sikukuu ya pasaka na mikate isiyotiwa chachu ziliunganishwa pamoja na kufanya jumla ya majuma 7 ambapo sasa walifanya sherehe siku moja baada ya majuma saba 7x7+1 = 50 ndivyo sherehe ya Pentekoste ilivyopata maana mpya ambayo ni ya kidini na huo ukawa mwisho wa kipindi cha furaha ambapo kufunga kulikuwa hakuruhusiwi, na walisali wakiwa wamesimama.

Waisraeli walianza kuadhimisha sherehe ya Pentekoste kukumbuka siku Musa alipopewa amri kumi za Mungu mlimani Sinai. Ni siku hiyo ambapo Taifa la Israeli lilizaliwa kwa kupewa katiba au kanuni rasmi za kuwaongoza, yaani Amri za Mungu. Sherehe hiyo sasa ilichukua sura mpya ikiwakumbusha tukio kubwa na la maana sana kwao yaani kuzaliwa kwa Taifa lao la Israeli. Namna ilivyosherekewa: Sherehe ya pentekoste ilikuwa ni siku ya hija ambapo, wakulima wa Kiyahudi na waongofu toka sehemu mbalimbali walimiminika mjini Yerusalemu wakiwa wamechukua makapu yaliyojaa mazao mapya. Makuhani na walawi walisimama nje ya hekalu tayari kuwapokea watu. Halafu wote pamoja waliandamana kuingia hekaluni. Wakulima walibeba makapu yao hadi ndani ya hekalu kwa nyimbo na vifijo. Humo hekaluni Makuhani walipokea mazao na kusali sala ya kumshukuru Mungu. Halafu kuhani kwa niaba ya waamini alitolea na kuinua mikate miwili isiyotiwa chachu, iliyotengenezwa kutokana na nafaka ya mavuno mapya ya mwaka huo.

Desturi hii ya kutoa shukrani ya mazao ilienea katika nchi nyingi kuzunguka bahari ya kati, na watu kutoka nchi mbalimbali, walikuja Yerusalemu kwa lengo la kutoa shukrani ya mavuno. Katika hali hiyo ya sherehe na kusanyiko la mkutano huo mkubwa siku ya Pentekoste ya Kiyahudi, na Yesu akiwa ameshapaa mbinguni, Mitume kwa hofu ya Wayahudi walikuwa wamejifungia katika chumba, wakidumu katika kusali, wakisubiri ahadi ya Kristo, yaani ujio wa Roho Mtakatifu, humo ndani ghafla kukaja upepo toka mbinguni, ukaijaza nyumba ile walimokuwamo, zikatokea ndimi za moto zilizogawanyika zikiwakalia kila mmoja. Wote wakajawa Roho Mtakatifu, wakapata ujasiri wakatoka nje, wakaenda hekaluni ambapo walikuwapo watu wa kila lugha, kila jamaa na kila taifa ambayo majina yao yanatajwa katika kitabu cha matendo ya mitume, watu wa mataifa yaliokuja kuhiji na kumtolea Mungu shukrani za mazao yao. Mitume wakaanza kuwahubiria kwa nguvu habari za Yesu Kristo mfufuka na wote wakasikia na kuelewa.

Leo tunasherehekea Pentekoste ya Kikristo, yaani siku hamsini baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo na ni siku chache tu baada ya Bwana wetu Yesu Kristo kupaa mbinguni. Ni siku ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume na mwanzo wa Kanisa la kwanza. Kama vile Wayahudi walivyosherehekea sikukuu ya mavuno ya kwanza, na baadaye kusherehekea sikukuu ya kupewa amri kumi za Mungu na kuundwa kwa Taifa lao la Israeli, vivyo hivyo na sisi tunasherehekea mambo matatu yanayofanana na hayo katika sherehe yetu hii: Mosi, tunasherehekea mavuno makubwa ya Kanisa. Mavuno haya ni zawadi ya wakristo waliobatizwa mara ya kwanza siku ile ya Pentekoste, watu wapatao elfu tatu. Sisi tunasherehekea mavuno ya wakristo waliobatizwa katika mkesha wa Pasaka ambapo mbiu ilipigwa tukisherekea usiku ule Mtakatifu tulipokombolewa kutoka utumwa wa dhambi. Wote hawa wamejazwa Roho Mtakatifu na wanatenda matendo makuu ya Mungu.

Pili, tunasherehekea ujio wa Mungu Roho Mtakatifu, nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, asiye na mwanzo wala mwisho, yeye ni kiongozi wa Kanisa kama vile ilivyokuwa amri za Mungu kwa taifa la Israeli. Wote wanaoshukiwa nae hujazwa mapaji yake saba ili tutende kazi kwayo. Hivyo, Roho Mtakatifu, ndiye anayeliongoza kanisa kuwachagua viongozi wa kanisa, kuwapeleka anakopenda Mungu wakafanye utume, anawajalia hekima katika utume na kuwasaidia katika maamuzi, anawasaidia wahubiri wa Injili kuhubiri vema, na kuongoza usomaji wa Maandiko Matakatifu. Tena Roho Mtakatifu anawajalia watu vipaji mbalimbali kwa ajili ya kanisa lote na kwa ajili ya wanakanisa wote, kwa ajili ya wokovu wa wote na kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu. Vipaji hivyo ni kama vile hekima, akili, shauri, nguvu, elimu, ibada na uchaji kwa Mungu. Karama zingine ni kama vile unabii, Uponyaji, ualimu, kunena kwa lugha na nyingine nyingi. Hivyo basi, yatupasa kutambua karama hizo zote.

Katika ulimwengu wa leo kutokana na matatizo yanayotuzunguka baadhi ya waamini wa Madhehebu mbalimbali, hata ndani ya Kanisa moja, Takatifu Katoliki na la Mitume wanaonekana kukazia zaidi karama mbili tu za Roho Mtakatifu yaani uponyaji na kunena kwa lugha. Huko ni kumfanya Roho Mtakatifu kuwa fukara wa vipaji. Vipaji vya Roho Mtakatifu ni vingi na humjalia kila mmoja kwa ajili ya kuhudumiana, kujengana na kufaidiana sisi kwa sisi. Yatupasa kutambua kuwa vipaji tulivyonavyo ni kazi ya Roho Mtakatifu. Imani inayotegemea miujiza tu haina nguvu, tena ni imani isiyo ya kweli na ndiyo inayotuingiza katika utapeli wa ile tudhaniyo kuwa ni miujiza. Vipaji tulivyonavyo viwe kwa manufaa ya wote. Na tujue kuwa karama kubwa kuliko zote ni upendo. Tujihadhari na hili; “kwa sababu hiyo nawaambieni, watu watasamehewa dhambi na kufuru zao zote, lakini hawatasamehewa dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu” (Mt.12:31) Yesu alisema haya.

Tatu, tunasherehekea kuzaliwa kwa Kanisa. Taifa la Israeli lilizaliwa siku ya kusanyiko kuu mlimani Sinai. Siku ya mkutano wa kusanyiko la Yerusalemu Taifa la Mungu la Agano jipya, Israeli mpya ndilo Kanisa jumuiya ya waamini lilizaliwa. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu wakanena matendo makuu ya Mungu. Utume rasmi wa Kanisa ulianza.  Muujiza wa Pentekoste ulirudisha umoja uliopotea huko Babeli kwa sababu ya majivuno ya watu waliotaka kujenga mnara mpaka ufike Mbinguni kwa Mungu. Mungu akawachafulia lugha yao wakashindwa kuelewana. Muujiza huu unatuita tuishi bila ubaguzi wa rangi, jinsia, kabila, utaifa, ukanda, ujimbo, ujumuiya, ukazi, ukipato, uanafunzi, uanakwaya, ukarismatiki, uwanamoyo, uanalejio, ukachero, undoa, utawa, upadre, ushemasi hata useminari ili watu wote wapate kulisikia Neno la Mungu, ili wapate kuliishi na kuokoka.

Kwa Ubatizo wetu na Kipaimara sote tumejazwa Roho Mtakatifu yatupasa kuongea lugha moja tu, lugha ya upendo kwa wote, lugha ambayo hakuna asiyeielewa. Upendo haufifii kamwe kwani wadumu mpaka Mbinguni. Ni fadhila ya Kimungu iliyotofauti na nyingine kwani mwisho wake si hapa Duniani. Hakuna mtu wa rangi, kabila, au taifa lolote ambaye haelewi lugha ya upendo. Tumsifu Yesu Kristo.

Pentekoste
05 June 2019, 11:58