Hija ya Kitume Romania: Ias: Shuhuda wa imani na matumaini!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Askofu Petru Gherghel wa Jimbo Katoliki la Ias anasema “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Romania. Katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuzungumza na waamini waliokusanyika kwenye mkutano wa familia na vijana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Ias, Romania, Jumamosi, tarehe 1 Juni 2019.
Hawa ni vijana wanaonesha upendo mkubwa kwa Baba Mtakatifu, hali ambayo wameishuhudia wao wenyewe bila kusahau uwepo wa wazazi, wazee na wagonjwa, ambao pia wameonja faraja na baraka za uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao. Familia nyingi kutoka Jimbo Katoliki la Ias ni zile za watu wanaoishi ughaibuni, lakini kwa tukio hili zimeamua kurejea tena Jimboni mwao, ili kuonesha umoja na mshikamano wa watu wa Mungu, lakini zaidi, kusikiliza wosia wa Baba Mtakatifu katika mchakato wa ujenzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya utakatifu, haki na amani; mahali pa kurithisha tunu msingi za maisha na utu wema.
Askofu Petru Gherghel anaamshukuru Mungu kwani kwa hakika Kanisa ni familia kubwa ya familia zote Jimboni humo na linataka kuendelea kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia imani, mapendo, furaha na matumaini kwa watu wa Mungu. Waamini wamejiandaa kwa ajili ya kuadhimisha tukio hili kwa sala na sadaka pamoja na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake, ili anapokuwa miongoni mwao, aweze kuwaimarisha katika imani, tayari kuimwilisha katika matendo, kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu amepata fursa ya kusikiliza shuhuda zilizotolewa na wanafamilia, lakini familia moja imebahatika kupata zawadi ya watoto 11. Kati yao kuwa watawa wawili na mapadre wawili, matendo makuu ya Mungu. Vijana wamekumbusha kwamba, wao ni leo ya Mungu katika ulimwengu mamboleo!