Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVI ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa kusikiliza kwa makini na kujifunza kutoka kwa Yesu, ili kutenda kwa huruma na upendo! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVI ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Umuhimu wa kusikiliza kwa makini na kujifunza kutoka kwa Yesu, ili kutenda kwa huruma na upendo! 

Tafakari Jumapili XVI: Jifunzeni kuwa wanafunzi wasikivu wa Yesu

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XVI ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inaleta mbele ya macho yetu ya imani umuhimu wa sala, tafakari na Ibada ya kuabudu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Waamini wajifunze kuchota nguvu kutoka katika Neno la Mungu na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa ili watende kwa huruma na upendo pasi na manung'uniko.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Simulizi la Martha na Maria ni moja kati ya masimulizi yanayotushangaza mara ya kwanza tunapolisikia na hasa iweje Yesu haoni juhudi za ukarimu na makaribisho ya Marta dhidi ya umbu lake yaani Maria aliyeketi miguuni kwa Yesu na kumsikiliza. Hata baadhi ya wataalamu wa Maandiko mara nyingi wanatumia sehemu hii ya Injili kujaribu kueleza aina mbili ya maisha yaani yale ya taamuli na maisha ya kiraia. Watawa wakaa pweke au watawa wa ndani kwa ajili ya maisha ya sala na tafakari wao wamechagua fungu lililo jema. Na kinyume chake mapadre mfano wa jimbo na wale wa mashirika ya kazi za kitume wanaobaki nje na kujishughulisha na mambo mengi ya kitume na kichungaji na hata pia walei wanaojitoa kwa sadaka zao mbali mbali katika kueneza ufalme wa Mungu, kundi hili basi wamechagua fungu lisilo jema kama lile la Maria.

Tafsiri hiyo au hata zile zifananazo na hizo si sahihi kwa sababu nitakazojaribu kuzieleza hapa chini. Dominika iliyopita tulisikia mfano au simulizi lile la Msamaria na Yesu anatualika nasi kuenenda na kutenda kama Msamaria yule. Ila kinyume chake Yesu anamsifu mwanamke aliyekuwa ameketi miguuni pake bila kufanya lolote. Ni Yesu anajipinga katika mafundisho yake? Mwinjili Luka anatuonesha kuwa Yesu anasifu fungu alilochagua Maria kuwa amechagua fungo lililo jema na wala haoneshi kuwa Yesu alipinga au alikuwa kinyume na kile alichokuwa anafanya dada yake Martha.  Martha alifanya akiwa na malalamiko na hivyo kupoteza umaana wa kile alichokuwa akikifanya. Na hata Martha mwenyewe hakuona umaana wa kile alichokiwa akikifanya na ndio maana anaenda kwa mgeni wao yaani Yesu na kumshitaki dada yake mdogo Maria.

Mwinjili Luka mara kadhaa huwa anatuonesha Yesu akiwa ameketi mezani katika nyumba za watu fulani fulani, iwe ni wale wenye haki au wema na hata kati ya Mafarisayo. (Luka 7:36; 11:37; 14:1) lakini pia alifika katika nyumba za watoza ushuru na wadhambi (Luka 5:30; 15:2; 19:6). Na leo tunamuona katika nyumba ya hawa ndugu au dada wawili, nyumbani kwa Martha na Maria kadiri ya Mwinjili Luka. Martha aliyekuwa dada mkubwa, hivyo mara moja anajituma na kufanya kitu fulani kwa ajili ya makaribisho ya ukarimu kwa mgeni wao. Ni kawaida kabisa hata katika familia zetu mgeni anapofika basi akina mama wanajibidiisha kwa ukarimu kumwandalia kitu fulani na katika muktadha huu ni hakika Yesu alifuatana pia na wanafunzi wake na hivyo walikuwa wageni wanaume idadi ya kutosha iliyomtaka si tu Martha peke yake bali hata na umbu lake aungane naye katika maandalizi yale.

Maria aliye mdogo kiumri na hapa badala ya kuona haja ya kuungana na dada yake katika maandalizi yale anabaki miguuni mwa Yesu akimsikiliza bila kufanya kitu kwa mtazamo hata wetu pia. Maria alikuwa ameketi miguuni pa Yesu. Kuketi miguuni mwa mwalimu kwa lugha ya kibiblia ina maana ya kuwa mfuasi na hivyo aliyeruhusiwa kuketi miguuni ni mwanafunzi au mfuasi aliyetaka kujifunza kutoka kwa Rabi au Mwalimu. Katika Kitabu cha Matendo ya Mitume tunamwona Mtume Paolo anatuambia aliketi miguuni mwa Gamalieli, aliyekuwa mwalimu mashuhuri wa nyakati zake. (Matendo 22:3) Hivyo Mwinjili Luka kwa makusudi mazima anatueleza mkao wa Maria ndio kusema Maria alichagua kuwa mwanafunzi wa Yesu. Labda nyakati zetu hatuoni shida kuona Maria anaketi miguuni na hivyo kuwa mwanafunzi wa Yesu, kwa nyakati zile kilikuwa ni kitu kigeni na kushangaza kwani hakuna Rabi wala mwalimu yeyote angekubali na kumpokea mwanamke kuwa mwanafunzi wake.

Marabi walikuwa na msemo: “Ni heri kuichoma Biblia kuliko kuiweka mikononi mwa mwanamke.’’ Na hata wanawake wasingeruhusiwa kusali au kuombea chakula mezani na hata akienda kwenye Sinagogi basi ilibidi ajifiche na sio kukaa waziwazi. Mtazamo huu ulikuwepo si tu kati ya Wayahudi bali hata katika Jumuiya za Wakristo wa Kanisa la mwanzo, wanawake katika mikusanyiko ya kiibada hawakupaswa kuongea chochote wala kuuliza na kama walikuwa na maswali basi walipaswa kuwauliza waume zao warejeapo nyumbani. (1Wakorinto 14:34-35). Hivyo Yesu ni mwanamapinduzi wa fikra na tamaduni za namna hiyo, kwani anampokea Maria na kumfanya mmoja kati ya wanafunzi wake. Na ndio Yesu anatualika nasi leo kupokea mwaliko wake wa kuwa wanafunzi wake, kuketi miguuni pake na kumsikiliza na kujifunza kutoka kwake kabla ya kutoka na kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili katika maisha!

Hata Mwinjili Luka pia anatuonesha kinyume na utamaduni wa nyakati zile kwani anaanza sehemu ya Injili ya leo kwa maneno kuwa: mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Haikuwa inakubalika kwa mwanamke kumwalika nyumbani kwake mwanaume na kupokea mwaliko huo.  Na ndio unaona Mwinjili Luka tofauti na Mwinjili Yohana hamtaji hapa kaka yao akina Marta na Maria yaani Lazaro. (Yohana, 11;12:1-8) Mwinjili Luka ni mmoja kati ya waandishi wanaoonesha kinagaubaga juu ya mapinduzi ya tamaduni na fikra aliyotuletea Yesu. Yesu analeta mapinduzi makubwa ya kitamaduni na ya kifikra kwani mbele yake la muhimu ni kuwa wanafunzi wake na siyo jinsia au rangi au kabila au taifa au tofauti zetu zozote zile. Na vema pia kukumbuka kuwa Injili haisemi kuwa Maria alikuwa amezama katika sala au tafakuri, bali alikuwa akisikiliza Neno la Yesu, na sio maneno kama baadhi ya tafsiri zinavyosomeka.

Maria anabaki kuwa mfano wa kusikiliza Neno la Yesu Kristo.  Hayakuwa mazungumzo ya kawaida kama yale tunayokuwa nayo tunapotembeleana majumbani bali ni juu ya Neno la Mungu. Na moja linatutafakarisha zaidi leo ni ukimya wa Maria kwani Mwinjili Luka kuanzia mwanzo wa simulizi hili mpaka mwisho hatusikii hata neno moja kutoka kinywani mwa Maria. Ni ajabu! Ila ni fundisho kwetu tunaotaka kuwa wanafunzi wa Yesu. Ni katika nguvu ya ukimya nasi tunakutana na Mungu anaandika Kardinali Robert Sarah katika Kitabu chake ‘’The Power of Silence’’. Itoshe leo kutolea mfano mazungumzo ya Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta na Padre kijana kabisa ambaye leo hii ndiye Kardinali Angelo Comastri, Mhudumu mkuu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kardinali Robert Sarah katika Kitabu chake anamuelezea Mtakatifu Mama Theresa kama mwanamke wa ukimya na tafakari na katika ukimya huu daima aliunganika na Mungu. Kwake kusali na kubaki katika ukimya huo mkubwa ni sawa na kumpenda Mungu kwa moyo wote na kwa roho yote hivyo kutenga muda wa kukaa naye na kumsikiliza. Kardinali Angelo akiwa Padre kijana alifika kumuona Mtakatifu Mama Theresa si tu kuongea naye bali hasa kuomba sala zake. Mama Theresa akamjibu kuwa daima anasali kwa ajili ya mapadre na hapo pia akamuuliza Padre kijana Angelo Comastri kuwa anasali masaa mangapi kila siku? Pamoja na jibu ambalo labda wengi wetu tungelijibu lakini naomba hapa ninukuu sio kwa tafsiri sahihi sana maneno ya Mtakatifu Mama Theresa kwa Padre Angelo: ‘’haitoshi mwanangu!

Katika upendo tunafanya kila linalowezekana…wadhani naweza kufanya tendo lolote la upendo na huruma bila moyo wangu kujazwa na upendo wa Yesu? Waamini kuwa naweza kwenda mitaani na kuwakusanya maskini na wahitaji bila moyo wangu kuwaka na mapendo ya Yesu mwenyewe?... Soma vizuri Injili: Yesu katika sala alitolea sadaka hata matendo ya huruma. Wajua kwa nini? Ni kwa nia ya kutufundisha kuwa bila Mungu tunakuwa maskini kiasi cha kushindwa kuwasaidia maskini! Bila Mungu sisi ni maskini na katika umaskini huo hatuwezi kutoka na kuwasaidia wengine. Hatuwezi kutoa kitu ambacho hatuna, upendo wetu lazima uangazwe na moto wa upendo wa Mungu kwanza. Kinyume chake tunabaki kama Marta wenye mahuzuniko na malalamiko katika utendaji wetu.

Sasa turejee katika Injili yetu ya leo na hasa jibu la Yesu kwa Martha ambalo mara kadhaa linatusumbua kupata ujumbe hasa wa Yesu kwetu leo. Yesu hamkalipii Martha kwa kuwa anafanya kazi la hasha na badala yake ile hali yake anayokuwa nayo, ndio hasa tunaweza kusema hasira na ghadhabu yake ya kihisia kuona anatumika peke yake bila msaada wa ndugu yake. Na hii inatokana na yeye kuamua kutenda kabla ya kuketi miguuni mwa Yesu na kulisikiliza Neno la Mungu. Ni hali hiyo tunajikuta nayo hata nasi katika kutekeleza majukumu yetu ya kila siku na hata utume wetu tusipo mtanguliza kwanza Mungu, kupata wasaa wa kuketi miguuni mwake na kumsikiliza. Tutafakari utume wetu wa kila siku iwe maparokiani kwa wachungaji wetu au katika familia zetu kwa walei au katika jumuiya zetu kwa watawa.

Ikiwa hatutaanza kwa kumsikiliza Mungu, kwa sala na tafakari ya ndani daima mwisho wake ni uchovu na malalamiko na manung’uniko na kuishia kurusha lawama kwa wengine. Iwe ni makasisi parokiani ni vema kuchunguza majitoleo yetu chimbuko na chanzo chake ni nini? Ni bidii na nguvu na akili zetu au tunachota kwa Mungu mwenyewe? Ikiwa katika familia au jumuiya yeyote ile tujiulize na kama sio nawaalika daima turejee maneno ya Mtakatifu Mama Theresa kwa Padre Kijana ambaye leo ni Kardinali Angelo Comastri, tunachota wapi nguvu za kutenda mema kama sio kwa Kristo mwenyewe. Tukumbuke sisi bila Mungu ni maskini kiasi kwamba hatuwezi kusaidia maskini wengine! Pamoja na kwamba Yesu hapingi bidii zetu ila anatukumbusha kabla ya yote la kwanza ni ulazima wa kuketi miguuni mwake na kusikiliza Neno lake na ni baada ya hapo tunaweza kutoka na kwenda kutenda.

Na hapo tutatenda bila lawama wala malalamiko wala kughadhibika kwani matendo yetu yataongozwa na moto wa Neno na upendo wake wa Kimungu. Tusithubutu kutenda lolote bila kwanza kuketi miguuni mwake! Mazungumzo ya Yesu na Martha na Maria ni kama yanakosa hitimisho kadiri ya Injili ya leo. Ila Mwinjili Luka mpaka mwisho anazidi kutuonesha ukimya wa Maria. Maria hasemi wala hatamki neno lolote iwe la kujitetea ua kujieleza kwa nini anafanya hicho anachofanya na hivyo kuweka wazi nia yake iliyojificha ndani mwake. Ni ishara tosha kuwa ukimya wake ni baada ya kuelewa Neno la Yesu hivyo linabaki katika moyo na kuwa mwongozo wa maisha yake akibaki akilitafakari. Kila anayelisikiliza Neno la Yesu na kuongozwa naye anabaki bila maneno mengi kwani anabaki na amani na utulivu wa ndani kinyume chake ni malalamiko yasiyokuwa na mwisho na kutupia kila mtu lawama.

Tujitafakari hata nasi mara nyingi tunakuwa wa maneno mengi na lawama na manung’uniko kwa kuwa hatujapata wasaa wa kuketi miguuni mwa Yesu kwanza kabla ya kutenda. Sasa ni Martha anayepaswa kuketi miguuni pa Yesu na kusikiliza Neno la Yesu ili naye apate utulivu wa ndani na amani ya ndani na hivyo kuondokana na malalamiko na lawama na hasira. Martha ni mkarimu na mchapakazi kweli kweli ila anakosea nini kianze katika maisha yake, na ndio daima tunakumbushwa na kufundishwa na Injili ya leo daima maisha yetu yaongozwe na sala na kwa kutafakari Neno la Mungu. Neno la Mungu na sala ya tafakari haina budi kupewa kipaumbele katika maisha yetu ya siku kwa siku kama kweli tunataka kuenenda na kutenda kama rafiki zake Yesu. Mtakatifu Tomaso wa Akwino kadiri ya masimulizi ya msaidizi wake Reginald anasema maandiko mengi ya Mtakatifu Tomaso hayakutokana na kusoma sana bali kutafakari sana. 

Mtakatifu Tomaso wa Akwino alikuwa anajihoji maswali mengi na magumu hata kuna wakati alikuwa anafika analaza kichwa chake katika Tabernakulo ili Yesu wa Ekaristi amfunulie siri za mbinguni.  Akili zake hazinabudu kuangaziwa na Yesu mwenyewe, hivyo Taalilimungu makini ni ile inayotokana na Mungu mwenyewe kujifunua na kuziangaza akili zetu ziweze kumjua vema na hivyo kumpenda kweli kweli! Na ndio hata leo wanataalimgu mahiri sio wale wanaotumia saa nyingi kubukua maktaba na kusoma vitabu bali hasa wanaokuwa na muda wa kukaa kimya na kutafakari Neno la Mungu. Hakika kila anayechukua wasaa wake katika siku na kusali na kutafakari Neno la Mungu huyo atatenda kwa upendo bila malalamiko na bila lawama. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hawa ndio wale wanaoandika taalimungu kwa kupiga magoti yao na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI ni mfano bora wa kuigwa!

Nawatakia tafakari njema na Dominika njema na huku tukijitahidi kila mmoja wetu kutenga muda wa kutafakari Neno la Mungu, Kuabudu Ekaristi Takatifu na kuyamwilisha yote haya katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji!



20 July 2019, 12:36