Jumapili XVII ya Mwaka: Baba Yetu: Muhtasari wa imani & Maisha!
Padre Gaston George Mkude, - Roma.
Amani na Salama! Ukimya ni mwanzo wa sala: Tunaishi katika ulimwengu wa kiimla wa makelele mengi na hivyo wengi wetu tunakosa nafasi ya kubaki na kuwa wenyewe na Mungu katika majadiliano na maongezi ya kirafiki kabisa, ni maongezi kati ya baba na mwana. Yesu anatufundisha tusalipo daima tunamuita Mungu ni Baba. Hivyo sala kwa lugha nyepesi kabisa ni mazungumzo ya baba na mwana. Ni ulimwengu wa teknolojia ya mawasiliano yanayokua kwa kasi sana, ni ulimwengu ambapo mwanadamu anajikuta ametekwa na maendeleo yake mwenyewe. Mwanadamu anapoteza uhuru na ujirani kwa matakwa yake mwenyewe. Mathalani simu leo hii inamfanya mwanadamu awe mtumwa wa teknolojia, hapa tuna mifano mingi na hasa inayoakisi maisha ya kila mmoja wetu kuanzia asubuhi tunapoamka mpaka saa ile ya kwenda kulala. Ni mara ngapi tumekuwa watumwa wa simu au computer au vitu vya aina hiyo?
Zaidi ya ulimwengu huo wa kiimla wa makelele yatokanayo na maendeleo ya kiteknolojia, mwanadamu anasongwa tena na ufinyu wa maana ya sala. Sala ni kueleza shida zetu mbele ya Mungu, ni kutaka Mungu atende tutakavyo sisi, ni kumshawishi Mungu abadili mapenzi yake, ni kutaka na kuongea sisi bila kumpatia Mwenyezi Mungu naye atuoneshe mapenzi yake kwetu na hivyo kumsikiliza. Sala kwa wengi imebaki kuwa ni mawasiliano ya upande mmoja tu yaani mwanadamu anataka na kuongea. Sala haina budi kuwa na masikilizano ya pande mbili yaani mwanadamu na Muumba wake. Ni mawasiliano na mazungumzo ya pande mbili, hata kama tunamlilia Mungu, tunamlalamikia Mungu lazima nasi tutoe nafasi ya kumsikiza Mungu. Mwinjili Luka ni kati ya wainjili wanaotuonesha maana na umuhimu wa sala na kusali. Ni mara 7 katika Injili ya Luka anatuonesha umuhimu huo wa sala. Labda tunashangaa iweje mitume wa Yesu waliokuwa wayahudi na kukulia katika utamaduni wa kidini na kiimani wasijue jinsi ya kusali.
Kwa hakika mitume walisali na hata walikuwa wanaenda kwenye masinagogi na hata hekaluni kule Jerusalemu kwa ajili ya mikusanyiko ya sala na hata kutolea sadaka wakati wa Pasaka ya Kiyahudi. Mitume wanaona namna na jinsi tofauti ya kusali na ile waliyojua na kuizoea kabla. Mitume wanavutiwa na namna mpya ya Yesu ya kusali na ndio wanasukumwa kumuomba awafundishe nao kusali kama Yohana Mbatizaji alivyowafundisha wanafunzi wake. Ni kwa Yohana Mbatizaji na wanafunzi wake kwani baadhi walikuwa hapo awali wanafunzi wa Yohana wanaguswa na kuona kuna haja zaidi ya kujifunza namna hii ya Yesu ya kusali. Mitume hawaridhiki sana na namna zile walizozijua awali bali sasa nao wanataka kusali kama Bwana na Mwalimu wao anavyosali. Ni Yesu anayekuwa kielelezo chetu cha nini maana ya sala na jinsi ya kusali.
Sala ni kioo cha kujiona sisi wenyewe, ni katika sala tunakuwa sisi wenyewe mbele ya Mungu, hakuna jambo au kitu tunaweza kuficha mbele ya Mungu wetu. Ni nafasi ya kujikusanya na kubaki wakweli bila unafiki au usiri wa aina yeyote. Ni mazungumzo ya kirafiki kati yangu na Mungu anayeona sirini. Sehemu ya Injili ya leo ni katekesi juu ya sala na hivyo hatuna budi kuitafakari vema kama nasi tunataka kujua maana na jinsi ya kusali. Inatuonesha kama nilivyoonesha hapo juu mazingira ya wanafunzi kufanya ombi la kufundishwa kusali, Yesu anawafundisha Sala ya Baba Yetu na inafuata na mfano na jinsi Mungu daima anasikia sala zetu na kuzijibu. Sala ya Baba Yetu kwa wengi labda ni sala kama mojawapo ya kanuni za sala kama Salamu Maria, Salamu Malkia wa Mbingu, “Requiem aeternam” na kadhalika, tofauti na kanuni za sala nyingine ni mhutasari wa imani yetu na maisha ya kikristo. Katika Kanisa la Mwanzo tunaona Wakatekumeni walifundishwa Sala ya Baba yetu na kuipokea kutoka kwa Askofu kabla ya Ubatizo wao.
Ilikuwa ni zawadi kutoka kwa Mchungaji mkuu kwa kila aliyeomba kubatizwa. Hivyo waliipokea siku nane kabla ya ile siku ya Ubatizo ambao ulifanyika katika kesha mama la Pasaka. Kwa mara ya kwanza waliisali Usiku ule wa mkesha wa Pasaka pamoja na Jumuiya nzima ya waamini. Na ndio tunaona Kanisa la mwanzo hata lilikuwa na desturi waamini kusali Sala hii karibu na kisima cha ubatizo. Toleo ya Sala ya Baba yetu kadiri ya Mwinjili Luka ni fupi na tofauti na ile tunayoitumia mara nyingi katika ibada na maadhimisho yetu itokanayo na Injili ya Mathayo. Pia sala ya Baba yetu inanukuliwa kuwepo tangu mwanzo katika Maandiko ya Mababa ya Didake. Kwa kweli kadiri ya Mtakatifu Agostino anasema Sala ya Baba yetu ni ufupisho wa mafundisho ya imani ya mkristo. Tertuliani anasema ni kioo ambacho mbele yake mmoja anajiona mwenyewe mbele ya Mungu. Hivyo sala ya Baba yetu inabaki kuwa si tu kanuni ya sala bali pia inabeba katekesi juu ya maisha ya mwamini.
Baba: Mungu ni Baba, hivyo tunaposali ni kuwa mbele ya Baba yetu wa mbinguni. Ni kuwa na imani na matumaini kuwa tunaingia katika mahusiano ya ndani na ya kipekee na Baba yetu. Ni Baba mwema na anayetupenda bila mashaka wala wasiwasi wowote, hivyo tunasali kwa imani na matumaini. Ni maongezi ya upendo kwani Mungu Baba anatupenda. Ni kuingia pia katika umoja wanadamu wengine wote kwani tusalimu hatusemi Baba yangu bali Baba yetu, ni kukubali na kukiri kuwa Yeye ni Baba wa wanadamu wote. Sala inatuunganisha na kutukumbusha undugu wetu kama wanadamu. Sala inatualika kutoka katika ubinafsi wetu. Juna lako litukuzwe: Ni Mungu alitukuze Jina lake kati yetu, ili ukuu wake uweze kuonekana si tu kwangu ninayesali bali kwa ulimwengu mzima. Jina lake linatukuzwa kwa sisi kuenenda na kutenda kama wana wa Mungu, kwa kumpenda Mungu kwa moyo, kwa roho, kwa akili na nguvu zetu zote. Ufalme wako uje: Ni kumuomba Mungu awe mtawala na kiongozi wa maisha yake ili Ufalme wake wa Upendo, haki na amani utawale ulimwenguni kote. Sio ufalme wa dunia hii bali wema na upendo wake ukatawale mioyoni na maishani mwetu.
Utupe Mkate wetu wa kila siku: Katika ulimwengu wa mashariki ya kati, mkate ulikuwa mlo mtakatifu na hivyo ulipaswa kuliwa si tu na mwenye mkate bali hata na wale wenye njaa na shida ya mkate. (Isaya 58:7) Mkate ulikuwa ni mlo mtakatifu hivyo haukupaswa kutupwa jalalani, au kukatwa kwa kisu kama tufanyavyo leo bali kumegwa kwa mikono ya mwanadamu, ni matunda ya kazi ya mwanadamu na baraka ya Mungu aliyetujalia ardhi na mvua hata kupata mkate huo. Mana haukuwa mkate wetu maana ni kutoka mbinguni ila mkate ni wetu kwani ulitokana na matunda ya kazi na jasho la mwanadamu kwa upande mmoja na Mungu kwa upande mwingine. Ni mkate wetu pia kwa maana ya kuwa si kwa ajili yangu tu bali na wengine wanaokuwa wahitaji wanaonizunguka. Hivyo katika sala hii tunaomba mahitaji yetu si kwa ajili yetu tu bali na wenzetu wanaokuwa na uhitaji huo.
Ni mkate wa leo na si wa kesho na keshokutwa kwani kila mkate unaobaki na kuwa wa ziada kwangu leo ni kumnyima mwingine anayelala na njaa leo kwa kukosa mkate. Ni kuomba sio kwa kujilimbikizia na kuwa wabinafsi bali daima kuishi kwa kujali shida na mahitaji ya wengine. Ni sala inayotualika kuwa wakarimu kwa yale yote ambayo Mungu amependa kutukirimia katika maisha yetu. Utusamehe dhambi zetu kama nasi tunavyowasamehe: Mwenyezi Mungu daima anatusamehe na kutuhurumia makosa na madhambi yetu ila nasi kama wakristo tukumbuke katika sala hii tunaomba kusamehewa kama nasi tunavyosamehe, ndio kusema jinsi Mungu alivyo mwema na mwenye huruma nasi tunaalikwa kuwa wema na wenye huruma. Kuwa watu wa rehema daima. Ni wajibu wetu wa lazima kuwa watu wa rehema kwa wengine. Sala daima inatubadilisha na kutufanya tufanane na Mungu.
Usituache kuanguka majaribuni: Majaribu yanayoongelewa hapa haswa ni kumuomba Mungu asituache kupotoka na kuacha kuishi Neno lake, Injili yake bali daima atuongoze kuishi na kushika Neno lake. Ni kuomba kuongozwa naye katika hali zote katika maisha yetu. Tusali bila kukoma: Yesu anaendelea kutupa mfano wa rafiki anayeomba bila kukoma mpaka rafiki yake alipojibu ombi au hitaji lake la mikate mitatu. Si kwamba Mungu hasikii sala au maombi yetu, ila kama nilivyotangulia kusema hapo awali, sala hazibadili mapenzi ya Mungu ambayo daima ni mema kwetu bali zinatusaidia na kutuandaa kupokea mapenzi yake katika maisha yetu. Ni kwa kudumu katika sala daima nasi tunajaliwa neema na nguvu za kukubali mapenzi yake katika maisha yetu. Naomba tukumbuke sala zetu sio kumshawishi Mungu atende kama tutakavyo sisi bali ni sisi kunyanyua mioyo yetu na kukutana na Mungu ili kupokea mpango wake katika maisha yetu (Fiat voluntas tua)
Mwenyezi Mungu daima anajibu sala zetu: Daima sala zetu zinapokelewa na Mwenyezi Mungu. Pamoja na kwamba si kazi rahisi kukubali mapenzi na mpango wa Mungu katika maisha yetu. Utakalo lifanyike duniani kama mbinguni. Yesu anatuhakikishia leo wema wa Mungu kwetu, ombeni, tafuteni na bisheni. Hatuna budi kusali tukiwa na imani na matumaini na tukijikabidhi daima katika wema wa Mungu. Anayesali daima anapata nguvu na neema za Mungu za kuweza kupokea mpango wa Mungu katika maisha yake hata ikiwa ni kupokea msalaba na magumu. Tunaweza kuwa na mifano ya watu wengi wema na wenye imani na wenye kusali waliopokea msalaba katika maisha yao bila manung’uniko wala kumlaani Mungu, ni nguvu itokanayo na sala na hivyo kuweza kupokea kwa utulivu mateso yao.
Maana ya Sala kadiri ya Mtakatifu Yohane Damascene: Mtakatifu Yohane Damascene anatukumbusha kuwa kusali ni kunyanyua mioyo yetu kwa Mungu. Ni kutoka katika uduni wetu na kuongea lugha ya Mungu, na ndio kusali si tu tendo la mwanadamu bali ni kwa njia na msaada wa Roho Mtakatifu kuweza nasi kuingia katika lugha hiyo isiyokuwa ya kibinadamu. Ni kujadiliana na Mungu, ni kukaa mbele ya Mungu, hivyo daima kama tunataka kusali vema hatuna budi kwanza kumuomba Roho Mtakatifu atufundishe jinsi ya kusali na hapo sala zetu zitakuwa na maana. Ni Mungu daima anataka kuwa katika mahusiano na mwanadamu, ni Mungu basi anapaswa kutufundisha lugha yake ya kimungu kila tusalipo. Na ndio mitume leo wanamwendea Yesu na kumuomba awafundishe jinsi ya kusali, bila Mungu hatuwezi kusali, bila Mungu hatuwezi kuongea lugha ya kimungu.
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI katika mahubiri yake siku ya kumbukumbu ya miaka 800 ya kuzaliwa kwa Papa Celestino V (04 Julai, 2010) anatukumbusha kuwa, tunaishi katika jamii ambayo kila nafasi, kila muda lazima ijazwe na shughuli fulani, kiasi kwamba tunakosa kabisa muda wa kusikiliza na kujadiliana. Anatualika tusiwe na uoga wa kuwa na ukimya nje na ndani mwetu, kama tunahitaji kweli kumsikiliza Mungu, na hata pia kuisikiliza sauti ya mtu anayekuwa karibu yangu, sauti za wengine. Hatuwezi kuwepo mbele ya Mungu na hata jirani kama hatutakuwa na wasaa wa kubaki katika ukimya, katika sala. Ukimya ni mwanzo wa sala! Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.
Pax Christ!