Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XV ya Mwaka C wa Kanisa: Matendo ya huruma ni utimilifu wa sheria na torati yote! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XV ya Mwaka C wa Kanisa: Matendo ya huruma ni utimilifu wa sheria na torati yote! 

Tafakari Jumapili XV ya Mwaka: Utimilifu wa Torati na Unabii!

Matendo ya huruma ni utimilifu wa sheria na torati yote, yanapita sheria. Kutenda matendo ya huruma ni kwenda zaidi ya sheria. Mlawi na kuhani, walipomwona mtu aliyekuwa anajeruhiwa na kuachwa nusu mfu, kwa kufuata sheria walipita pembeni. Msamaria mwema akisukumwa na upendo kwa Mungu na jirani anatimiza sheria kwa ukamilifu na anapata dhawabu machoni pa Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 15 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe wa domenika hii ni kwamba matendo ya huruma kwa jirani ni utimilifu wa sheria na torati yote, ndiyo amri kuu ya mapendo. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha kumbukumbu la Torati linatueleza kuwa sheria hazitoki nje ya mtu, haziko mbali hata tuseme nani ataenda kutuletea, zi karibu tena zinatiririka kutoka ndani ya moyo wa mtu na wala si ngumu kuzifuata, jambo moja tu linahitajika nalo ni upendo. Swali la mwalimu wa sheria kwa Yesu katika Injili linalosema Mwalimu, nifanye nini ili niweze kuurithi ufalme wa mbinguni ni swali ambalo lipo katika kila nafsi ya mwanadamu.

Mwanasheria anajibu wazi kuwa imeandikwa, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wote na kwa roho yote na kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote na jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe.  Lakini, jirani yangu ni nani? Ni swali jingine la mwanasheria. Yesu hatoi jibu la kumuonesha aliko jirani yake. Anatoa mfano maarufu wa msamaria mwema aliyemsaidia mtu aliyeangukia katika mikono ya watu waovu, wanyang’anyi, waliomtenda jeuri, wakampiga, wakamvua nguo zake, wakamnyang’anya vyote alivyokuwa navyo wakamwacha nusu mfu. Msamaria alipomwona huyu mtu nusu mfu, tendo la kwanza alimuonea huruma, akashuka juu ya mnyama wake, akamkaribia, akampa huduma ya kwanza, kisha akampeleka nyumba ya kutunza wagonjwa na kulipa gharama zake huku akiahidi atalipa pia gharama zitakazoongezeka.

Kwa mfano huu wa Msamaria mwema Yesu anatuonesha jinsi ya kuziishi amri za Mungu katika uhalisia wa maisha yetu ya kila siku. Anatuambia nasi tufanye kama msamaria ili tuweze kuishi. Jibu la swali, na jirani yangu ni nani, liko wazi kuwa jirani, ni mtu yeyote yule anayehitaji msaada. Jibu hili ni la mwana sheria tena anasema wazi jirani ni huyo aliyemwonea huruma mtu aliye nusu mfu. Hivyo mtu yeyote unayemuonea huruma na kumsaidia ndiye jirani yako. Yesu akamwambia, enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo. Nasi hatuna cha kufanya zaidi ya kufanya alichofanya msamaria mwema. Kadri ya historia, wayahudi na wasamaria walikuwa maadui.

Wayahudi waliwadharau na kuwachukia wasamaria, ndiyo maana Yesu alipoongea na mwanamke Msamaria pale katika kisima cha Yakobo (Yn 4:). Wanafunzi wake hawakumuelewa na pia wakati wasamaria walipokataa kumpokea kwa kuwa aliukaza uso wake kuelekea Yerusalemu, wanafunzi wake Yakobo na Yohane wana wa ngurumo waliomba ashushe moto toka mbinguni uwaaangamize. Yesu ni kinyume kabisa juu ya huu ubaguzi na dharau kwa wengine ndiyo maana alimsifia mkoma Msamaria aliyetakaswa na kurudi kutoa shukrani (Lk17:) na mfano huu wa Msamaria mwema aliyemhudumia kwa upendo Myahudi aliyekuwa katika hatari ya kufa ili kutufundisha kuwa upendo unapita sheria na uadui wote na kipimo chake ni matendo ya huruma.

Matendo ya huruma ni utimilifu wa sheria na torati yote, yanapita sheria. Kutenda matendo ya huruma ni kwenda zaidi ya sheria. Mlawi na kuhani, walipomwona mtu aliyekuwa anajeruhiwa na kuachwa nusu mfu, kwa kufuata sheria walipita pembeni. Kisheria hawakuwa na kosa lolote kwani walitimiza sheria ya kutojitia unajisi kama ilivyo katika Kitabu cha Mambo ya Walawi sura 21.  Msamaria mwema kwa tendo lake la huruma, akisukumwa na upendo kwa Mungu na jirani anatimiza sheria kwa utimilifu wake na anapata dhawabu machoni pa Mungu. Jamii yetu ya sasa ina majeruhi wengi wa kimwili, kiakili na kiroho. Wapo watoto waliotelekezwa, vijana wa mitaani wanaooishi katika dimbwi la dawa za kulevya na pombe, wapo wanaofanyishwa kazi zisizo halali tena kupita uwezo wao bila malipo.

Kuna wajane walionyimwa haki zao, wapo yatima wa wazazi wanaoishi na yatima wa wazazi waliokufa, wapo wagonjwa ambao wanataabika kwa kukosa matibabu, wapo wakimbizi, wapo maskini na vilema, hawa wote wapo katika jamii zetu, tunaishi nao, wako karibu, hawako mbali wanahitaji huruma yetu inayotiririka kutoka ndani ya mioyo yetu, wanahitaji msaada wetu. Tunao wajibu wa kuwasaidia. Jambo hili halihitaji ushuhuda wa waandish wa habari bali moyo wa upendo wa msamaria mwema wenye kauli mbiu tenda wema enenda zako. Kuna matendo ya huruma ya kimwili ambayo ni kuwaona wagonjwa na walioko gerezani, kuwavika nguo walio uchi, kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu na kuwakaribisha wageni (Mt. 25:31-46).

Pia kuna matendo ya huruma ya kiroho ambayo ni kufundisha wasiojua, kushauri wenye mashaka, kuonya wadhambi, kuvumilia mabaya, kusamehe makosa bila kusita, kufariji wanaoteseka na kuwaombea wazima na wafu. Haya ndiyo matendo ya huruma ambayo ni utimifu wa sheria na torati ambayo yanatustahilisha kuuridhi ufalme wa mbinguni. Hivyo kukosa kuingia mbinguni kwa kushindwa kushika sheria na torati ambazo haziko mbali, tena si ngumu ni uzembe wa makusudi. Huruma ni upendo unaolekezwa katika kumsaidia mtu katika taabu au uhitaji. Huruma hii lazima iwe katika ukweli kwa wanostahili, katika jambo jema, kwa njia halali na kwa nia njema.

Huruma ni moyo wa msaada. Ni kufariji pale penye taabu au huzuni, kusaidia palipo na shida au uhitaji, ni kuonyesha hisia ya kuumia kwa sababu ya uwepo wa taabu fulani na kuwa tayari kusaidia. Kwa maneno ya Mtume Paulo “Lieni na wanaolia” (Rum 12:15). Kuna muunganiko wa pekee kati ya upendo, haki na huruma. Upendo ni kumtakia mema au kutafuta mema kwa ajili ya mwingine. Upendo, ndio husukuma mtu awe na huruma na upendo hudhihirishwa kwa namna ya pekee katika huruma. Kwa hiyo, huruma ni upendo uliolekezwa katika kumsaidia mtu mwenye shida au taabu. Haki ni kile kilicho halali ya mtu. Huruma ikisukumwa na upendo humfanya mtu atende haki. Kwa hiyo, mtu hawezi kuwa na huruma bila mapendo na hawezi kutenda haki kama hana huruma na upendo.

Hivyo, katika kutimiza haki lazima tuzingatie huruma na mapendo hasa haki inapohusisha adhabu. Haki pia itatufanya tuwe na huruma kwa wakosaji kwa sababu kwa kuwatendea haki hatutawadai zaidi ya uwezo wao. Tutatambua kuwa wao ni dhaifu kama sisi hivyo, tutawachukulia katika udhaifu wao na kuwahurumia wanapokosea; tukiwaonya inavyostahili ili kuwasaidia warekebike. Huruma na adhabu: Kwa hakika adhabu halali ni tendo la huruma. Lakini kusisitiza na kutetea sheria kama Mafarisayo inaweza kuonekana kukosa huruma pale ambapo sheria zinakuwa ni kandamizi na si halali au zinatolewa kwa upendeleo. Tunahitaji busara na hekima ili kutambua mazingira ambapo matendo ya huruma yanataleta faida zaidi ya kushika sheria kwani sheria haina maana kama haitamsaidia mlengwa kuwa mkamilifu katika kuwasiaidia wengine.

J15 Mwaka C
10 July 2019, 17:15