Jumapili XVI ya Mwaka: Ukarimu na Usikivu: Chanzo cha neema na baraka katika maisha!
Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa radio Vatikani katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 16 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatuasa tuwe na moyo wa ukarimu kwa wenzetu hasa wageni na usikivu kwa neno la Mungu ili tuweze kupata neema na baraka kutoka kwa Mungu. Somo la kwanza na injili yanaunganishwa kwa ujumbe wa ukarimu kama alama ya huduma na utumishi kwa wengine hasa wageni. Ukarimu wa Ibrahimu kwa wageni katika somo la kwanza ni mfano wa huduma inayompatia mtu neema na baraka machoni pa Mungu kwani ni ukarimu unaotoka ndani ya moyo uliojaa upendo. Simulizi la Maria na Martha linasisitiza kuwa huduma na utumishi kwa wengine visitufanye tushindwe kusikiliza neno la Mungu na Paulo ni mfano wa utumishi bora kwa wengine kwa kuyatoa maisha yake kwa kuvumilia taabu na mahangaiko ili upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo uweze kudhihirishwa kwa njia yake.
Ndiyo maana anasema wazi katika somo la pili, sasa nayafurahia mateso niliyo nayo kwa ajili yenu; tena nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua ya mateso ya Kristo, kwa ajili ya mwili wake, yaani, Kanisa lake. Na hii ndiyo siri iliyofichwa kwa wamchao Mungu, yaani Watakatifu wake. Ni siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, na sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake. Ni kwa siri hii, nimefanywa mhudumu wake, sawasawa na uwakili wa Mungu, niliyopewa kwa faida ya watu, nikilitimiza neno la Mungu, Kol 1:25. Haya yote yanaunganishwa kwa neno moja ukarimu unaoongozwa kwa upendo. Mungu ni upendo na Mungu ni ukarimu. Ukarimu ni uwepo wa kimungu ndani yetu. Unapofanya tendo la ukarimu unaakisi uwepo wa Mungu ndani yako. Tunapowakirimia wenzetu wenye mahitaji mbalimbali twafanya tendo la Kimungu.
Kitabu cha Mithali 22:9 kinatuasa kikisema, mwenye jicho la ukarimu atabarikiwa na Mungu, maana huwapa maskini chakula chake. Ibrahimu anapewa hakikisho hilo na baraka hizo mbele ya Mungu kwa ukarimu alionyesha kwa wageni nao wakamwambia, Bwana asema, hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Ni baraka toka kwa Mungu kwa ukarimu wake. Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto barua yake ya pili anasema, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu (2Kor 9:6-7). Ni kwa maana hii Ukarimu hugeuka kuwa neema na baraka ambazo ndiyo hazina yetu tunayojiwekea mbinguni kama anavyotuambia Yesu, Jiwekeeni hazina mbinguni ambako nondo na kutu hawawezi kuharibu, wala wezi hawaingii wakaiba. Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako, (Mt. 6:19-21). Na mzaburi anatuambia, heri amkumbukaye mnyonge, maana Bwana atamwokoa siku ya taabu (Zab. 41:1).
Kujikusanyaji na kujiwekea hazina ya mbinguni kunafanyika kwa kujikusanya mali za duniani na kuzitoa kwa kuwapa watu wenye shida, wanyonge na wahitaji kwa moyo wa ukarimu na upendo, na ni katika kuwasaidia wahitaji wa aina hii muujiza hufanyika, vitu hugeuka kuwa neema, na neema hizo huwekwa mbinguni kwenye hazina yako, ambapo ndipo utakuwa moyo wako (Mt. 6:21). Kwa hiyo kadri ulivyo na neema hizo kwa wingi mbinguni, wakati utakapokuwa umekwenda kuzimiliki, nawe utaweza kuwagawia wanaokuomba msaada wa neema hizo, neema hizo haziishi tena, ni kama ule unga wa mjane wa Sarepta aliyemsaidia mwenye shida Nabii Elia, na baada ya tendo hilo la ukarimu, unga wake haukupungua, wala mafuta katika chupa hayakwisha (1 Fal. 17:16), kwa sababu mjane huyu alikuwa tayari kutoa na kutumikia kwa ukarimu.
Neema hizo za mbinguni, ndizo zinaweza kufanya miujiza hapa duniani wakati tuombapo sala zake, yeye akiwa mbinguni. Hii ndiyo maana, wakati Kanisa linapofanya mchakato wa kumtangaza mtu kuwa ni Mtakatifu, linaomba muujiza unaopatikana kutokana na maombezi yake yenye nguvu za neema alizonazo mtumishi wa Mungu mwenye kufanyiwa mchakato huo. Ombi la mtu aliyejaa neema husikilizwa haraka mbele ya kiti cha Mungu, halikataliwi, majibu yanatokea mara moja. Kwa hiyo kadri mtu alivyo na neema hizi kwa wingi katika hazina yake, ni kadri hiyohiyo anavyoweza kutusaidia kwa msaada wa sala zake. Kama neema ni kidogo hataweza kutupatia, maana hataweza kutoa zaidi ya alichonacho. Na hii ndiyo sababu kanisa katika kufanya mchakato wa kumtangaza mtu kwamba ni mwenyeheri na baadae kwamba ni mtakatifu.
Kwa wengine miujiza inakuwa ni ya haraka kama kwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kama mfano kati wa watu walio na neema hizi kwa wingi, ndiyo maana mchakato wake ulienda haraka. Kwa wengine unachelewa au hata wengine kukosa kabisa; kwa sababu hazina aliyojiwekea mbinguni ni ndogo. Haya mambo ni mazuri sana tufanye hima kuwa na moyo wa ukarimu ili tujiwekee hazina mbinguni lakini haya yote yafanyike kwa upendo, na sio kwa woga kwamba, nisipofanya matendo ya huruma sitaenda mbinguni au kwamba nitatupwa katika moto wa milele. Mt. Basil anasema, Kama tukiacha kutenda dhambi kwasababu ya woga, tuko katika hatari ya kuwa watumwa; kama tukishikilia ushawishi wa mishahara tutafanana na mamluki au askari wa kukodiwa; mwisho kama tukitii kwa ajili ya uzuri wenyewe na kwasababu ya upendo kwake, tuko katika nafasi ya wana na watoto wa Mungu. Hivyo upendo ndio utawale katika kutenda matendo haya ya huruma, maana ajuaye ni Mwenyezi Mungu, yeye atayapima matendo yote (1Sam. 2:3), kwa kipimo sahihi.
Usiyafanye matendo haya ili watu wakuone na kukusifu, kwani watu wafanyao hivyo kwamba watu wawasifu, hawapati na wala hawatapata thawabu mbinguni wamekwisha kupata thawabu yao (Mt. 6:5). Kama lengo la kufanya matendo ya ukarimu, ni kuonekana na kupata sifa kwa watu, usifiwe na kumshangiliwa, basi umekwisha kupata thawabu yako yaani, zile sifa na mashangilio ya watu waliyokupatia na hivyo usitegemee thawabu mbinguni kwani umezipata hapahapa duniani, huna chochote mbinguni. Bali katika kufanya matendo ya ukarimu iwe ni kwamba mapendo ya Kristo yatumiliki (2Kor. 5:14), Mungu Baba aonaye sirini atakujazi (Mt. 6:6). Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anasema, baada ya ugeni hapa duniani, natumaini kwenda na kukufurahia wewe, lakini, sitaki kujiwekea akiba ya mafao ya mbinguni. Nataka nitumikie pendo lako tu mwishoni mwa maisha haya, nitatokea mbele yako nikiwa na mikono tupu, kwani sikuombi uhesabu kazi yangu.
Haki yetu yote inalawama machoni pako. Nataka tu, nivikwe katika haki yako mwenyewe na nipate kutoka kwenye pendo lako miliki yako ya milele. Mambo ya kusema kwamba nimefanya matendo mengi ya huruma; kwamba nimesaidia maskini wengi, nimelisha wenye njaa wengi, nimenywesha wenye kiu wengi, nimehudumia wagonjwa wengi na kazi nyingi sana nimefanya; hayo si hoja kwa Mungu, kwani, sawa umefanya hayo yote tena kweli ni mengi, lakini kama huna upendo, si kitu, yote ni bure. Jambo la msingi ni kwamba, usitumikie haki, bali upendo, kwani upendo ni kila kitu.