Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa: Umuhimu wa sala katika maisha ya mwaamini pamoja na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa: Umuhimu wa sala katika maisha ya mwaamini pamoja na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. 

Tafakari Jumapili XVII ya Mwaka: Umuhimu wa sala katika maisha!

Sala ya mwenye haki ni sala inayotoka ndani ya mtima wa moyo wake, haina hila wala mawaa ndani yake nayo inaelekezwa kwa Mungu ambaye ni Baba mwenye haki, nasi tunapaswa kuwa na matumaini kwake kwani chochote tumwombapo kwa kweli na haki atatupatia. Sala inasimikwa katika imani, matumaini na mapendo! Sala inatabia ya udumifu pasi na kuchoka!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 17 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Bibilia inatuasa kusali bila kuchoka, kila mara na kila wakati, tukimshukuru Mungu kwa kila jambo (1Thes. 5:17-18). Sala ya mwenye haki ni sala inayotoka ndani ya mtima wa moyo wake, haina hila wala mawaa ndani yake nayo inaelekezwa kwa Mungu ambaye ni Baba mwenye haki, nasi tunapaswa kuwa na matumaini kwake kwani chochote tumwombapo kwa kweli na haki atatupatia. Somo la kwanza kutoka kitabu cha Mwanzo linatuonyesha nguvu ya sala ya mtu mwenye haki. Abrahimu baba wa imani, mtu mwenye haki anasali na kuomboleza mbele za Mungu kwa sababu ya dhambi za watu Sodoma ili Mungu asiwaangamize.

Ni wazi kuwa Mungu ndiye mwanzo na mwisho wa maisha ya mwanadamu. Tumetoka kwake na kwake tutarudi. Yeye ndiye ametuweka hapa duniani tumjue, tumpende, tumtumikie na mwisho tupate kufika kwake mbinguni. Na ili tuweze kuyatekeleza haya kikamilifu, Mungu ametupatia mwongozo wa kufuata. Na kwa kuufuata mwongozo huo tunaweza kutembea salama hapa duniani mpaka kufika kwake mbinguni. Mwongozo unadai tufuate kanuni za maadili na kuitii dhamiri njema. Lakini kwa dhambi zetu kama za watu wa Sodoma tunapoteza hadhi ya kuwa watoto wa Mungu, tunajistahilisha kuangamizwa milele kwa sababu, dhambi humtenga mtu na Mungu. Dhambi inaua mahusiano kati ya mtu na Mungu. Kwa kutenda dhambi yaani kwenda kinyume na sheria ya Mungu, urafiki kati ya Mungu na mwanadamu unaingia dosari.

Mtu anakuwa mbali na muumba wake; mwunganiko alionao na muumba wake unapotea (Mwanzo 3). Nabii Isaya anasema, “Dhambi zenu ndizo zinazowatenga na Mungu wenu, dhambi zenu zimemfanya Mungu ajifiche mbali nanyi hata asiweze kuwasikieni” (Isaya 59:2). Dhambi humtenga mtu na wengine na huathiri mahusiano yake na wengine. Aidha, tunapowadhuru wengine kwa mwenendo wetu mbaya tunamgusa pia Mungu mwenyewe kwani kila mtu ameumbwa kwa sura na mfano wake Mungu. Dhambi pia humtenga mtu na nafsi yake mwenyewe. Ukitenda dhambi hadhi ya kuwa mtoto wa Mungu anayestahili kupendwa na kuheshimiwa inashuka. Unaishi chini ya viwango kama mwana wa Mungu. Unaanza kutamani kula makombo, karibu unafanana na nguruwe kama mwana mpotevu (Luka 15), unaingia katika taabu na magumu ya kila aina. Maisha mazuri, furaha na amani vinapotea na unaanza kusota (Mwanzo 3-4).

Taabu, mateso na mahangaiko vinakuandama unasongwa na maumivu ya kimwili kama ni dalili tu za uozo uliomo ndani, anakuwa mkorofi, mgomvi, msingiziaji kwani ili kujipatia faraja lazima mdhambi awapakazie wengine maovu yake, akijihami kwani anadhani anaonewa daima, hapendi upatano na wenzake, kwake amani ni kama mwiba ndani mwake. Mwisho wa yote huingia kifo cha mwili na cha roho maana mshahara wa dhambi ni mauti, ni kifo (Warumi 6:23; Luka 15:32). Kama Abrahamu baba wa imani, mtu mwenye haki alivyosali kuiombea Sodoma isiangamizwe kwa dhambi zake, vivyo hivyo nasi tunapaswa kusali na kujiombea sisi wenyewe kwa dhambi zetu na za wengine ili Mungu asituangamize. Kwa kuwa tu wadhambi ili sala zetu zisikilizwe lazima kwanza tutubu kweli dhambi zetu na tusiyarudie matapishi ya dhambi yetu, tutoe msamaha kwa waliotukosea, kufanya malipizi na kujisamehe sisi wenyewe. Tukijiwekea hazina katika utu wema na mahusiano mema na watu pamoja na Mungu na pia tuwe wepesi wa kujirekebisha kasoro zetu.

Somo la pili kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai linatueleza kuwa mkristo wa kweli ni mtu yule ambaye kwa ubatizo amekuwa sehemu ya Fumbo la mwili wa Krsito yaani Kanisa. Paulo anasema, kama vile tohara, katika Agano la Kale, ilivyokuwa alama ya kuwa mshiriki wa taifa la Mungu, vivi hivi ubatizo hutufanya washiriki wa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ameifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani, Kol 2:14. Ukombozi huu ni wa dhamani sana ndiyo maana Mtume Petro katika barua yake ya kwanza kwa watu wote anasema, (1Pet 1:18-19), “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na hila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,”.  Kwa hiyo tuwe kielelezo cha Kristo mfufuka, katika maisha yetu ya kila siku kwa maneno na matendo tukiyavumilia mateso na msumbuko yanatupata tukiishuhudia imani yetu.

Katika Injili ya leo kama ilivyoandikwa na Luka inatufundisha kuwa wakristo tunapswa kusali kama Kristo ambaye sala na maisha yake havikutengana hata mara moja. Katika kila jambo alilolifanya alianza kwa sala ndiyo maana mitume wake walivyoona hivyo wanamuomba awafundishe kusali. Katika sala ya Baba yetu aliyowafundisha mitume wake, Yesu anatufunulia kuwa Mungu ni Baba mwenye huruma anayetutunza, siyo hakimu anayedai kutulizwa kwa sala. Hivi tumwombe kwa imani na matumaini atujalie ridhiki kwa maisha yetu. Yesu anasisitiza, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa. Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Lakini sharti ni moja lazima nasi tuwapatie wanaoomba, tuone mahitaji ya wanaotafuta, tuwafungulie wanaopiga hodi, tuwasaidie wahitaji, tuwasamehe wanaotukosea na kuomba msamaha kwa kuwa nasi tu wakosefu tunahitaji kusamehe kama anavyosema Mt. Agustino, basi ni hivyo hivyo masharti ya kusamehewa ni kusamehe bila masharti. Tujitahidi kuwa watu wa haki na kweli siku zote katika maisha yetu ili tuwe kweli wana wa Mungu walio huru kwani ukweli unatuweka huru.

Jumapili 17 Mwaka C
25 July 2019, 12:07