Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVIII ya Mwaka C wa Kanisa: Rasilimali, utajiri wa dunia na karama mbali mbali ziwe ni nyenzo za huduma kwa Mungu na jirani! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVIII ya Mwaka C wa Kanisa: Rasilimali, utajiri wa dunia na karama mbali mbali ziwe ni nyenzo za huduma kwa Mungu na jirani! 

Tafakari Jumapili XVIII: Mali ya dunia na changamoto zake!

Mali nyingi inaleta kiburi na kumfanya mtu amsahau Mungu kama chanzo cha mali yake na kama lengo la maisha yake. Kiburi hiki kinamfanya tajiri awadharau watu wengine na kuwaona hawana thamani yoyote na kama vile wamelaaniwa na Mungu. Mali zetu zisitufanye tuwe na ubinafsi. Tajiri katika Injili hakuona zaidi ya nafsi yake. Mali ilipoongezeka hakuona kuwa kuna wahitaji wengine.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 18 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatufundisha namna tunavyopaswa kutumia mali za ulimwengu huu ili kwazo tuweze kuurithi ufalme wa Mungu. Katika Somo la kwanza kutoka kitabu cha Mhubiri tunaelezwa kwamba, kwa mwanadamu mambo yote ulimwenguni yanakoma na kifo chake. Ya hapo baadaye hayajui. Ni Mungu peke yake anayejua yote. Kwa hiyo mwanadamu yampasa amtegemee Mungu katika yote. Ndiyo maana aseme, Ubatili mtupu ubatili mtupu. Mambo yote ni ubatili. Maana kuna mtu ambaye kazi yake ni kwa hekima, na kwa maarifa, na kwa ustadi; naye atamwachia mtu asiyeshughulika nayo kuwa sehemu yake. Hayo tena ni ubatili, nayo ni baa kuu. Kwa maana mtu hupata nini kwa kazi yake yote, na kwa juhudi ya moyo wake alivyojitahidi chini ya jua? Kwa kuwa siku zake zote ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni, hata usiku moyoni mwake hamna raha.

Hayo ni ubatili. Kumbe, pesa au mali au vitu vya ulimwengu visipotusaidia kumjua na kumpenda Mungu ili tuweze siku moja kuuridhi ufalme wa Mbinguni havina maana ni ubatili na ni kama kufukuza upepo. Somo la pili kutoka waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai linatufundisha kuwa katika ubatizo tumekufa na Kristo na tumefufuka naye, tukapata uzima mpya. Basi sasa tuishi kadiri ya uzima mpya. Tufishe hali ya dhambi inayodumu ndani yetu hata kufa. Paulo anatuasa tuyatafute yaliyo juu, Kristo aliko, na siyo yaliyo katika nchi. Hii ni pamoja na kuvifisha viungo vyetu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, ibada ya sanamu na kuambiana uongo. Tuuvue kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake na kuuvaa utu mpya kwa kumfanya Kristo ambaye ni yote, na katika yote.

Injili ilivyoandikwa na Luka inatukumbusha kuwa wingi wa mali si uhakika wa wokovu wa maisha yetu. Maana halisi ya maisha ni jitihada ya kumfikia Mungu kwa kumfuasa Kristo. Uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo ndiyo maana Mungu anamwambia mkulima tajiri aliyejikinai, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako. Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Mzaburi naye anatuasa kuwa nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Hivyo tunapojimilikisha yale ambayo kwa asili siyo yetu, mwisho wa siku huwa ni ubatili na masikitiko makubwa. Kwa kuwa siku zake zote tajiri ni masikitiko, na kazi yake ni huzuni; naam, hata usiku moyoni mwake hamna raha. Hayo nayo ni ubatili (Mhu 2:23). Kumbe sisi ni mawakili wa yale Mungu atupayo. Wazo hili la uwakili huanza na utambuzi wa kuwa Mungu ndiye mmiliki wa kila kitu na kila mtu duniani.

Yesu anatutahadharisha akisema, agalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo, kwani wingi wake havituhesabii haki mbele za Mungu Lk 12:15. Hivyo mwisho wa maisha yetu duniani utatathiminiwa kulingana na tulivyotumia mali za Mungu alizotukabidhi na kutuambia, "vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako mbinguni," Mt 25:21. Lakini tuchukue tahadhari, kuwa na mali si vibaya. Masomo haya yanatuasa namna tunavyopaswa kujihusianisha nazo ili kuepuka hatari ya kumsahau Mungu. Hii ni kwa sababu: Mali nyingi inaleta kiburi na kumfanya mtu amsahau Mungu kama muumba wake, kama chanzo cha mali yake na kama lengo la maisha yake. Kiburi hiki kinamfanya tajiri awadharau watu wengine na kuwaona hawana thamani yoyote na kama vile wamelaaniwa na Mungu.

Mali zetu zisitufanye tuwe na ubinafsi. Tajiri katika Injili hakuona zaidi ya nafsi yake. Mali ilipoongezeka hakuona kuwa kuna wahitaji wengine. Alijifikiria tu yeye binafsi na kutaka kujiwekea akiba wakati wengine wanakufa njaa. Hukumu aliyoipokea sio kwa sababu alilima akavuna mazao mengi bali kwa ubinafsi uliokidhiri hata kusema, kisha nitaiambia nafsi yangu, pumzika basi ule, unywe, ufurahi”. Tukumbuke kuwa kuna maisha mengine zaidi ya hapa duniani. Lazima katika kutafuta kwetu tukumbuke kwamba kuna maisha mengine ambayo yanategemea tutakavyokuwa tumeishi hapa duniani. Duniani si mahala pa kupumzika. Ni wakati wa kuandaa mapumziko yetu Mbinguni. Ndiyo maana Paulo anatuambia, “ndugu nataka kusema hivi: muda uliobaki ni mfupi. Na tangu sasa wale waliooa waishi kama hawakuoa; wenye kulia wawe kama hawalii, na wenye kufurahi wawe kama hawafurahi; wanaonunua wawe kama hawana kitu; nao wenye shughuli na dunia hii wawe kama vile hawana shughuli sana nayo. Maana ulimwengu huu kama tuujuavyo unapita” (1Kor.7:31).

Mtu mwingine anaweza kusema kwa vile mimi sina mali basi masomo ya leo hayanihusu. Hapana hata maskini huyu yanamhusu. Inawezekana hatuna mali, lakini mahusiano yetu na Mungu yakawa ni afadhali ya wale wenye mali kwa kuwa: tuna tamaa kubwa ya mali na utajiri kiasi hata cha kuwaza njia na namna mbaya zaidi ya kuzipata hata kwa kukatisha uhai wa wengine. Haturidhiki kwa vichache Mungu alivyotujalia. Tunakuwa na choyo na wivu. Tunakuwa na maumivu makali wengine wakifanikiwa hata kutamani kuharibu mafanikio yao. Kila mara sala zetu mbele za Mungu ni za malalamiko na manunguniko na hata pengine tunawaombea wengine wafe ili sisi tufaidike na mali zao. Tujifunze kuacha. Tusipojifunza kuacha kwa hiari tutapaswa kuacha kwa lazima na hapo itakuwa ni kilio. Tukumbuke kuwa maisha ni zaidi ya pesa, maisha ni zaidi ya mali, maisha ni zaidi ya madaraka maisha ni zaidi ya kujulika na maisha ni zaidi ya tamaa za mwili.

Tukumbuke kuwa muda wetu hapa duniani, nguvu zetu, akili, nafasi, mahusiano na mali zetu zote ni zawadi toka kwa Mungu ambazo ametukabidhi tuvitunze na kuvitumia vizuri. Tumwombe Mungu, ambaye ametupa mamlaka juu ya mali ya dunia hii, atujalie hekima na busara katika matumizi ya riziki ya dunia hii, na hivi lengo lake la kutuumba, yaani kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho kufika kwake mbinguni liweze kutimia. Tumsifu Yesu Kristo!

Jumapili 18 ya Mwaka C
31 July 2019, 16:05