Tafakari Jumapili XV ya Mwaka: Upendo kwa Mungu na Jirani!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa kwa waamini kurejea tena katika mpango wa maisha unaodai juhudi, mpango unaoleta furaha na amani ya ndani! Yaani iweni wenye huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kanisa limeagizwa kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu inayopenya katika moyo na akili ya binadamu. Huu ni mchakato wa kupyaisha juhudi za kichungaji, ili kweli Kanisa liweze kuwa ni chemchemu ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!
Padre Munachi, mhubiri maarufu anaandika hivi juu ya mhubiri mmoja maarufu wa dhehebu la Jeshi la Wokovu kwa jina la Catherine Booth. Kila alipohubiri watu wengi na wa kaliba mbalimbali walifurika. Ujumbe wake ulikuwa ni ujumbe wa matumaini. Usiku mmoja baada ya mahubiri, mwanamke mmoja tajiri katika mji ule alimwalika chakula cha jioni. Alipofika tu nyumbani alipokelewa kwa maneno haya – Mama Catherine, “ule mkutano sikuupenda kabisa”. Catherine akamwuliza mwenyeji wake sababu ya kusema hivyo. Yule mwenyeji akajibu, niliwaangalia sana wale watu karibu yangu na sidhani kama nitapata usingizi usiku huu. Nyuso zao zimechoka, wachafu na wamekata tamaa ya maisha. Catherine akamwuliza kwani huwafahamu watu wale? Yule mwenyeji akasema siwafahamu. Catherine akashangaa sana. Lakini akamwambia kumbuka kuwa sikutoka nao London. Wote wale ni majirani zako na watu wanaoishi katika mazingira na maeneo yako.
Kwa uhakika Mwenyezi Mungu anatudai mengi, lakini pia ametujalia mengi. Hakuna lililo kuu zaidi ya upendo wake kwetu wa kutujajliwa kushiriki utukufu wake wa milele. Na kwa kawaida Mungu hatudai zaidi ya uwezo wetu. Ndiyo maana akatupatia Mwanae mpendwa. Neno la Mungu jumapili ya XV ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa linatuwajibisha sana. Mtakatifu Theresa wa Avila anasema kuwa ingawa hatuna Bwana wetu kati yetu katika hali ya kimwili, tunaye jirani, ambaye kwa ajili ya upendo na matendo mema, ni mzuri kama angekuwa Bwana wetu mwenyewe. Somo la kwanza linatoa mwito wa watu kumrudia Mungu na kushika sheria zake. Hakika hazikuwa rahisi lakini inawezekana kuzishika. Mwandishi anasisitiza lakini sheria hizo si fumbo na haziko mbali nao. Tena anasema zipo tayari mioyoni mwao na midomoni pao. Zipo karibu sana nao. Ukweli waonekana kwa upendo wa Mungu usio na mipaka kwao. Uwezekano huo ni mkubwa zaidi kwani Mungu ndiye anayechukua jukumu la kuwapenda na hivyo yote yamerahisishwa.
Katika somo la pili twaona jinsi wimbo huu unavyotukuza ukuu wa Mungu juu ya viumbe vyote. Yeye ndiye Bwana na muumba wa vyote na Kristo ndiye mwanzo na mwisho wa kila kitu. Katika ukuu huo ndipo sisi tunajikuta tukiwajibishwa. Yote ni kwa ajili ya sifa na utukufu wake na hivyo sisi tunawajibishwa kumrudishia Mungu sifa, utukufu, ukuu na enzi. Mungu ametujalia akili, uhuru, utashi na neema ya kuishi wito huo. Katika Injili tunasikia habari ya yule mwanasheria akimwuliza Yesu juu ya sheria iliyo kuu. Uzuri wa mfano wa Msamaria ni kuwa Yesu anampa nafasi mwuliza swali atoe jibu yeye mwenyewe. Na tunaona hili mwishoni mwa somo letu. Yesu anajua kuwa tunajua ila sisi tunasita kutenda. Jibu rasmi hapa ni kuishi na kushika ile sheria ya dhahabu – Mpende Mungu na jirani.
Mfano wa Msamaria mwema watuonesha wazi kuwa hata watu wema au wanaodhani kuwa wema wanavyoweza kushindwa kufanya jema. Yule kuhani na mfarisayo wanajua sheria vizuri lakini wanaijua juu juu tu na kwenye maadishi lakini hawakutoa msaada wo wote katika uhalisia wa jambo au tukio lile. Na yapo matukio mengi katika maisha yetu ambayo tunashindwa kuyatolea majibu sahihi. Wanafugwa zaidi na sheria na kadiri ya sheria ilikuwa kama yule angekuwa mfu na kama wangemgusa basi wangekuwa najisi kwa siku saba. Katika kipindi hiki wakiwa najisi kuna vitu vingine vizuri zaidi kadiri yao wangeshindwa kuvifanya. Kwa hiyo wanapita pembeni. Katika kitabu ‘Yesu wa Nazareti’ cha Papa Mstaafu Benedikto XVI tunaona akitoa maelezo na uwezekano wa kuishi changamoto hii katika uhalisia wake. Mahali fulani anasema kuwa ili tuweze kuishi neema hii hatuna budi kubadili mtazamo toka kujiuliza jirani yangu ni nani na kujiuliza mimi ni jirani wa nani hapa na sasa.
Na sisi pia tujiulize jirani ni nani? Katika somo la Injili ni yupi jirani wa mwenzake. Ni yule msamaria au aliyeshambuliwa na majambazi? Bibi mmoja alimkumbusha mjukuu wake juu ya amri ya dhahabu – mpende Mungu na jirani akimwambia kumbuka kuwa tuko hapa kuwasaidia majirani/wengine. Mjukuu akavuta pumzi na akamjibu bibi yake, sawa bibi, lakini hao wengine wapo hapa kwa ajili ya nini? Hatuna budi kujiuliza usamaria wetu ukoje. Ni wangapi kati yetu hapa wana shida, mahangaiko, majanga, wamedanganywa au kudanganyika, maumivu ya mwili na roho, wamepoteza mwelekeo na dira, wamekata tama kwa namna mbalimbali. Tunawagangaje hawa? Ni mara ngapi tunapita pembeni ingawa tunajua kinachoendelea au tunatazama tu na kuendelea na shughuli zetu?
Tunapiga picha matukio kama ya ajali n.kili tuwe wa kwanza kusambaza picha za maiti na majeruhi badala ya kutoa msaada unaohitajika mara moja? Hakika yapo mengi ambayo tunayafumbia macho na mioyo yetu. Tuna deni kubwa sana ndugu zangu. Mhubiri maarufu Padre Munachi anaongelea uwezekano wa kuwa katika mtindo wa maisha unaofanana na ule wa waendao kuzika. Kuishi kwa mazoea au kutojali. Kwa kawaida msafara wa mazishi hausimamishwi njiani na kila mtu huupisha upite. Katika injili ya Lk. 7:11-17, tunasikia habari ya binti wa Naim aliyefariki na watu wanapita kwenda kuzika. Yesu anafanya kinyume. Alikuwa na msafara wake na wao walikuwa na msafara wao. Anatambua hali ya yule mama. Yesu anaweka mkono wake juu ya lile jeneza. Yule mama anatambua nguvu ya Yesu na anasimama. Anashiriki katika lile tendo takatifu.
Yesu anasema acha kulia – Lk. 7:11. Kama yule mama asingeshiriki tendo hili, hakika mwanae asingepata uzima. Aliamini na kutambua uzima uliokuwepo na akampatia Mungu nafasi ya kugusa maisha yake. Ndugu zangu Mwenyezi Mungu ametupatia nafasi ya kushiriki utakatifu wake. Tuna uwezo wa kufanya miujiza tukiwa upande wake Mungu. Mt. Teresa wa Avila anasema kuwa ingawa hatuna Bwana wetu kati yetu katika hali ya kimwili, tunaye jirani, ambaye kwa ajili ya upendo na matendo mema, ni mzuri kama angekuwa Bwana wetu mwenyewe. Ufahamu wetu na maisha yetu au ushiriki wetu au ufahamu wetu wa neno la Mungu utapata maana na ushuhuda wa kweli kama tutaweka katika matendo neno la Mungu tulilosikia leo. Tusipoteze muda kuuliza jirani yangu ni nani bali tutumie muda wetu kuwa majirani wema na wanaotenda mema kwa wengine
Mtakatifu Maximillian Maria Kolbe anaenda mbali zaidi. Anaokoa maisha kwa kutoa yeye maisha yake. Alikuwa Padre, mwana habari na mpinzani mkubwa sana wa utawala wa kinazi. Hii ilipelekea kufungwa gerezani. Katika gereza lao alitoroka mfungwa mmoja na ikatoka amri kuwa wafungwa kumi wauawe. Wakachaguliwa watu 10 na kati yao alikuwapo kijana mmoja. Padre Kolbe alimfahamu vizuri na akamwonea huruma. Yeye aliamini kuwa unazi utashindwa. Padre Kolbe akajitolea kufa akichukua nafasi ya yule kijana kwa vile alisema huyu bado mdogo, ana familia changa na bado ana muda wa kutengeneza maisha yake. Walihukumiwa kufa kifo cha njaa. Wa mwisho kufa kwa kuchomwa sindano alikuwa padre Kolbe. Katika gereza ambalo ukuta wake umejengwa kwa mawe walikuta alama ya msalaba mkubwa ukutani iliyochorowa kwa vidole vya padre Koble. Leo hii ni mtakatifu shahidi wa upendo. Hakika huyu ndiye jirani wa kweli.
Tumsifu Yesu Kristo.