Tafakari Jumapili XVII ya Mwaka: Sala ya Bwana & Sala ya Mkristo!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Sala ya Bwana yaani “Baba Yetu” ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni sala inayofumbatwa katika moyo safi, imani thabiti na dumivu; pamoja na ujasiri wa kimwana. Huu ni mwaliko wa kukesha na kwa njia ya Kristo Yesu, maombi yao yataweza kupelekwa kwa Baba wa milele. Hii ni sala yenye matini mafupi ambayo yameendelezwa na Mwinjili Mathayo na kufikishwa maombi saba, alama ya utimilifu katika Maandiko Matakatifu. Ni mwaliko wa Yesu kwa wafuasi wake kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kwa kuvunjilia mbali woga na mashaka yasiyokuwa na mvuto wala mashiko, kwani daima Mwenyezi Mungu yuko kati na karibu na watu wake. Jambo la msingi ni kwa waamini kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa na ujasiri wa kimwana!
Katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika’ cha Padre Joseph Healey uk. 87 tunakutana na sala hii ya kiafrika: Ee Bwana, uwe kwetu mwenzi wa furaha na shangwe, uwawezeshe vijana wapate nguvu, na mtu mzima atunze nguvu zake. Umwezeshe mwenye mimba kujifungua, na mwananke aliyejifungua amnyonyeshe mtoto wake. Umwezeshe mgeni kufika kwenye ukomo wa safari yake, wale wanaobakia waishi salama nyumbani mwao. Uyawezeshe makundi ya mifugo kwenda kwenye malisho na kurejea yakiwa yameshiba. Ee Bwana, uwe mwenzi wa mavuno na mitamba. Uweze kuwa mwenzi wa ukarabati na wa afya njema. Amina. Bila shaka katika sala hii tunaona uwezo wa mwanadamu kutambua nafasi ya muumbaji na uwezo wa kuendelea kutambua ukuu huo wa Mungu.
Yote ni mali yake Bwana na sala inatoa ombi ili vyote viendelee kuwa na uzima. Wale wafuasi walimwomba Yesu awafundishe kusali. Wanatambua ukuu wa Mungu juu ya hali zao na vile walivyo navyo. Kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele ‘Ufunuo’ tunasoma kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, aweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Lile ombi la Mitume limelala hapa, yaani huu uwezo wa mwanadamu kumtambua Mungu. Ile sala ya kiafrika hapo juu inatambua hilo pia. Na sisi leo tunaendelea kusali na kumwomba muumba kwa vile twaweza kufahamu ukuu huo wa Mungu. Katika somo la kwanza toka kitabu cha Mwanzo tunaona kuwa tabia ya Abrahamu anapotoa ombi, anaomba Mwenyezi Mungu awaokoe watu wote – wema na wabaya.
Kwa kifupi utu wa mtu hubaki hata kama ni mwenye dhambi. Mungu humpenda mwanadamu lakini huchukia dhambi. Abrahamu anatumia nafasi yake ya uaminifu kwa Mungu kuwaombea msamaha wenye kosa na hivyo anaokoa wenye dhambi. Hapa tunatambua pia kuwa heshima ya mwenye haki haipo katika utakatifu wa maisha yake ya kila siku bali katika Mungu anayempenda. Hivyo kosa litendwalo na mtu haliondoi utu wake pamoja na kwamba ni mkosaji. Wokovu wetu bado upo katika upendo wa Mungu ambao haupungui daima. Tunatambua pia kuwa upendo wa Mungu huzidi kosa la mwanadamu. Sasa kama mtu anaishi maisha ya utakatifu, basi mimi na wewe tunafurahi au tunawajibu wa kufurahi kwa vile Mungu anapendwa na upendo wa Mungu unadhihirishwa katika utakatifu wa maisha ya mtu fulani. Nasi tunawajibishwa kuishi utakatifu huo.
Katika somo la pili tunapata tena nafasi ya kukumbuswa kuhusu ubatizo wetu na haja ya kuishi kama watu wake Mungu. Kwa njia ya ubatizo tumekuwa viumbe vipya na mali yake Mungu. Kila tufanyacho hakina budi kuwa kipya na katika Kristo. Katika Kristo maisha yetu yote yanaanza upya. Na hata sala zetu na namna yetu ya kusali. Wale wafuasi katika somo la injili walitambua hili. Katika somo la injili tunaona mitume wakiwa pamoja na Yesu katika mazingira ya kusali na kuomba. Kile walichokiona na kuwa tofauti katika maisha na namna yake ya kusali mbele ya Baba yake kinawafanya watoe ombi rasmi kwake. Tufundishe kusali. Tukumbuke kuwa walikuwa Wayahudi na maisha yao ya sala yalikuwa yanaeleweka wazi – kumbuka yule farisayo aliyejidai mwenye haki mimi nasali mara tano kila siku, natoa sadaka n.k – lakini wanaona tofauti kwake Yesu. Ni kitu gani hicho/ni tofauti gani hiyo? Tofauti kubwa hapa ni hii; katika sala zao walijitukuza wenyewe. Katika sala ya Yesu Mungu anatukuzwa na mwanadamu anakombolewa!
Leo tunapata tena nafasi ya kutafakari kuhusu maisha yetu na Mungu pamoja na wenzetu:
1. Mimi/sisi/wewe husema – Baba yetu na si baba yangu – tamko hili latufanya tujisikie sote watoto wa Mungu. Je tuko hivyo kweli katika maisha yako/yangu? Sisi sote ni watoto wa Baba mmoja?
2. Misi/sisi/wewe huomba – jina lako litukuzwe – yaani Ee Mungu utukuzwe na ufahamike. Je, ndivyo ilivyo? Maisha yangu/yako/yetu yanamtukuza Mungu? Yanamwakilisha Mungu?
3. Mimi/wewe/sisi – husali ufalme wako ufike – hapa huomba kuwa ufalme wa Mungu uwe ndio ufalme wa mwanadamu. Je juhudi zako ni zipi ili hilo litimie? Mimi/wewe/sisi hatuna viufalme vingine tofauti na huo ufalme wa Mungu tunaoutamka?
4. Husema – mapenzi yako yatimizwe mbinguni na duniani – maana yake tunakubali utashi wetu uwe mali yake Mungu. Ndivyo ilivyo?
5. Husali utupe mkate wa kila siku – huu ni wajibu tunajipatia na unatuwajibisha pia. Kutoka jasho, kuwajibika. Tunatoka jasho kweli kupata mkate wetu wa kila siku kwa halali?
6. Utusamehe makosa yetu kama tunasamehevyo wengine – ni kweli hivyo na huwa tunafanya hivyo? Tunasameheana makosa yetu?
7. Usitutie majaribuni – tunajikabidhi kwake Mwenyezi Mungu na kuomba kubaki katika usalama wake. Mbona tunaendelea kujiingiza katika majaribu mbalimbali ya maisha. Kama utendaji wa dhambi bila wasiwasi au woga wo wote? Mbona maisha ya dhambi yamekuwa ni sehemu ya mazoea yetu? Sisi leo tunadaiwa nini? Kuomba tena Yesu atufundishe kusali? Hapana. Tunatakiwa kutafakari mahusiano yetu kwanza na Mungu halafu na watu wake. Je sala tusalizo zinatoa changamoto kwa wengine? Wanapotuona tunasali, wanaguswa? Kuna kipya katika maisha yetu ya sala? Je wale waliorudi nyuma kiimani, kimaadili, waliokata tamaa n.k wakituona tunavyosali leo hii na siku nyingine – watajihoji, watavutwa waje kusali na sisi na kuomba tuwafundishe sala zetu?
Katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, No. 1, tunasoma hivi; Mungu ametuumba ili tumjue, tumtumikie, tumpende na mwisho tufike kwake mbinguni na katika Zab. 139:13-19 – tunaona kuwa mtu/mwanadamu ni kiumbe cha Mungu na mwanadamu anaweza kutambua hilo na kumshukuru Mungu muumba wake. Mtu/mwanadamu huyo ameumbwa kwa mfano na sura yake Mungu – Mwa. 1:27. Tuendelee kuomba neema zake Mungu ili akili yetu iweze kumfahamu na utashi wetu umtumikie. Jibu la ombi la mitume kwa Yesu linapata maana hapa. Nasi baada ya kufundishwa na Yesu hiyo sala, wajibu wetu ni kuishi mapenzi yake Mungu na si mapenzi yetu. Tumsifu Yesu Kristo.