Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XVIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Jitajirisheni mbele ya Mungu kwa kutumia utajiri wa mali na karama zenu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya XVIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Jitajirisheni mbele ya Mungu kwa kutumia utajiri wa mali na karama zenu kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVIII: Jitajirisheni mbele ya Mungu

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ua XVIII ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa ni mwaliko kwa waamini kujitajirisha mbele ya Mungu kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema urajiri wa rasilimali fedha, vitu pamoja na karama mbali mbali walizojaliwa na Mwenyezi mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao! Uchu wa fedha na mali visiwe ni kikwazo cha kiroho!

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.

Katika kitabu ‘Hadithi za Kiafrika” kilichoandikwa na Padre Joseph Healey tunakutana na simulizi hili – padre Jack hakujisikia vizuri katika parokia yake kwani alijiona kuwa na vitu vingi kama umeme jua, tanki la maji, nyumba ya bati n.k. Siku moja alipokuwa anakwenda kigangoni na Katekista Charles, padre huyu mmisionari alikiri jinsi alivyojisikia vibaya kwa kuishi kama tajiri miongoni mwa maskini. Katekista Charles alikunja uso wake kwa mshangao. Halafu akamwambia Padre, wewe ni maskini zaidi yetu hapa kijijini. Huna watoto wala wajukuu. Ndugu zangu dhana ya utajiri/mali na umaskini inaweza ikapata maana na sura mbalimbali pengine kadiri ya mila, desturi, mahali na wakati na pengine mahitaji ya watu. Mtazamo huu unaweza pia kugusa uelewa wetu juu ya utajiri na umaskini wa kiroho. Katika injili tunasikia juu ya heri, heri maskini wa roho – Mt. 5:1.

Na pia tunasikia habari jinsi ilivyo vigumu kwa tajiri kuingia mbinguni – Mt. 19:16-30. Je, utajiri na umaskini wa kweli ni upi? Biblia yatuambia nini? Jibu la kibiblia kuhusu utajiri wa kweli liko wazi. Tajiri wa kweli na mwingi wa fadhila ni Mungu Baba peke yake. Yote tuliyo nayo yatoka kwake na ni mali yake. Neno la Mungu katika Mdo. 3:1-10 laweza kutupa jibu halisi na mwongozo mzima katika tafakari yetu ya leo. Kutoka Andiko hili tunasikia habari ya muujiza wa uponyaji wa kiwete tangu kuzaliwa na ambaye alikuwa anawekwa kwenye lango la kuingilia hekaluni ili kuomba. Akawaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni na anaomba. Alitegemea kupata kitu kutoka kwao. Petro anamwambia wazi sina dhahabu wala almasi, bali nitakupa nilicho nacho. Kwa jina la Yesu wa Nazarethi tembea. Wakamshika mkono na mara miguu yake na viungo vikafunguka, akaruka, akasima na kutembea na akaingia hekaluni na Petro na Yohane kuabudu.

Sehemu hii ya Andiko yaweza kutupa jibu ambapo mwandishi wa Somo la kwanza aongea juu ya ubatili mtupu. Yule kiwete alikuwa anaomba pesa. Kumbe hakuhitaji pesa ila uzima wa kimwili, yaani kuweza kujitegemea na kumudu maisha yake mwenyewe. Sisi tunaombana nini kati yetu? Pengine mahitaji yetu ya wakati huu ni yapi? Ukiwete wetu ambao twatamani kuondokana nao wakati wetu huu ni upi? Sisi tuna kitu gani cha kutoa ili ukiwete uondoke kabisa katika maisha yetu ya kimwili na kiroho? Somo la pili laongelea haja ya kuwa na mtazamo mpya na kutambua uzima mpya uliopatikana kwa njia ya ubatizo. Somo latoa wito kwa mwanadamu kuona utukufu wa Mungu uliopo kati yetu. Ni mwaliko kuvuka hali zetu za kawaida na kuuishi huo uzima mpya. Huo ndio utajiri kamili. Hili ni deni kubwa kati yetu sisi tunaoamini. Tunadaiana uzima huu mpya. Katika somo la injili twaona wazi kuwa wingi wa mali au vitu havimpatii mtu uhakika wa uzima wa milele.

Tunasoma kutoka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele ‘Ufunuo’ kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, aweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Hakika fundisho hili lamtaka mwanadamu kuutambua ukuu wa Mungu na uweza wake. Hakika yule anayefahamu hilo basi katika maisha yake atakiwa kumchagua Mungu. Kwa kutumia akili aliyojaliwa na yenye uwezo wa kujua na kufahamu basi anaweza kumchagua huyo ambaye ni asili na chanzo cha utajiri wote. Mtakatifu Jerome anasema ni tajiri wa kutosha yule aliye maskini katika Kristo. Ushuhuda huu ni mkubwa sana kwani Kristo ndiye mrithi wa hayo yote na yule amfuataye Kristo atapata yote yaliyo yake Mungu. Sote twatambua kuwa ufalme wa Mungu haununuliwi kwa fedha wala dhahabu. Sisi hatukukombolewa kwa fedha wala dhahabu bali kwa damu yake Kristo.

Tutafakarishwe na mfano huu wa bibi tajiri aliyekuwa na vitu vingi sana hapa duniani. Alipofariki dunia alibahatika kuingia mbinguni. Alipokelewa na Malaika na kupelekwa sehemu yake ya kukaa. Huku akiongozana na Malaika wake aliona watakatifu wenzake wakiwa wamekaa katika ufahari mkubwa. Mwisho akafika katika sehemu yake na kumbe kulikuwa na vitu vidogo sana na vichache. Malaika kwa unyenyekevu akamwonesha mahali pake pa kukaa. Mahali hapo hapakumfurahisha kabisa kwani hapakuwa na ufahari mkubwa kama alivyozoea duniani. Malaika akamwambia hana budi kuridhika na mahali hapa kwani vifaa vya ujenzi alivyotuma toka dunia vilitosha kujenga hicho kibanda. Malaika akaondoka akaenda zake. Mwandishi mmoja anasema ‘fedha yaweza kununua kila kitu isipokuwa furaha, kulipa gharama zako zote isipokuwa mbingu’. Tumsifu Yesu Kristo.

30 July 2019, 16:36