Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVI ya Mwaka C wa Kanisa: Upendo kwa Mungu: Ukarimu kwa wageni! Kuvumilia mateso kwa sabauri na Kusikiliza Neno la Mungu Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XVI ya Mwaka C wa Kanisa: Upendo kwa Mungu: Ukarimu kwa wageni! Kuvumilia mateso kwa sabauri na Kusikiliza Neno la Mungu 

Tafakari Jumapili XVI: Upendo kwa Mungu: Ukarimu, Mateso, Neno!

Upendo kwa Mwenyezi Mungu unajionesha kwa namna ya pekee kabisa kwa ukarimu na utu wema kwa jirani na wageni! Pili ni kuvumilia kwa saburi na udumifu mateso na mahangaiko kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na tatu. Tatu ni kusikiliza kwa umakini na utulivu mkubwa Neno la Mungu ambalo ni taa na dira ya maisha kwa waja wake: Ukarimu, Mateso & Neno!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari Masomo ya Liturujia ya dominika ya 16 ya mwaka C wa Kanisa. Upendo kwa Mwenyezi Mungu unajionesha kwa namna ya pekee kabisa kwa njia ya ukarimu kwa wageni, maskini na wahitaji zaidi, kama alivyofanya Msamaria mwema, Abrahamu na Martha. Pili ni kuvumilia mateso kwa saburi, imani na matumaini kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume. Tatu ni kuhakikisha kwamba, unasikiliza, unatafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuwa ni dira na mwongozo wa maisha!

Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mwa 18: 1-10a ) ni kutoka katika kitabu cha Mwanzo. Babu yetu wa imani Abrahamu, katika somo hili anakuwa ni mfano pia wa ukarimu wa kibinadamu. Wageni watatu wakiwa katika njia zao, mchana katika nchi yenye joto, Abrahamu anajitoa kwa ukarimu kuwakaribisha wakae kwake wapumzike kivulini hadi walau jua lipungue. Anawakarimu pia kwa chakula wapate nguvu ya kuendelea na safari yao. Wageni hawa wa Abrahamu kumbe walikuwa ni wajumbe wa Mungu. kwa ukarimu wake wajumbe hawa wanampa habari njema ya kutimia ahadi ya Mungu kwake, ahadi ya kumpatia mtoto. Agano Jipya linanukuu tendo hili la ukarimu wa Abrahamu na kulisifu. Waraka kwa Waebrania 13:2 unataja kuwa “kwa ukarimu wengine waliwapokea malaika bila kujua” na Injili ya Mathayo 25:43 inataja kuwa kukosa ukarimu ni mojawapo ya sababu ya hukumu katika siku ya mwisho.

 

Somo la pili (Kol 1:24-28 ) ni kutoka waraka wa mtume Paulo kwa Wakolosai. Paulo aliuandika waraka huu akiwa kifungoni na sasa anawaandikia wakolosoa kuhusu kifungo chake akisema anayafurahia mateso anayoyapata. Tena anayatimiliza katika mwili wake yale yanayopungua ya mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake yaani Kanisa. Ni nini anachokimaanisha hapa Paulo? Je mateso aliyoteseka Kristo hayakutosha au hayakukamilika hadi Paulo ayakamilishe? Kwa hakika mateso ya Kristo yalikamilika na yalitosha kabisa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu. Paulo anazungumza kurejea mafundisho yake juu ya mateso ya wanaomwamini Kristo. Mateso ambayo kanisa na wote wanaomwamini Kristo wanapaswa kuteseka katika kumshuhudia Kristo. Haya ni mateso ambayo kila mtu mmoja anapoteseka ni Kanisa zima linateseka na anapoteseka mmoja anateseka kwa ajili ya kanisa zima. Kumbe Paulo anaposema anakamilisha mateso yaliyopungua kwa mateso ya Kristo anamaanisha kuwa mateso anayoteseka anateseka kwa ajili ya Kristo. Na mateso yake kwa hakika yanajumlishwa katika mateso yale ambayo kanisa zima linapaswa bado kuteseka mpaka pale atakaporudi Kristo, mateso kwa ajili ya kuendeleza utume.

Injili (Lk 10:38-42) Katika injili ya dominika ya leo, Kristo anakaribishwa katika familia. Ni katika mji wa Martha na Mariamu. Simulizi hili linakuja mara tu baada ya ule mfano wa Yesu kwa mwanasheria kuhusu “jirani yangu ni nani”? Mfano ule ulijikita katika upendo wa mtu kwa jirani, simulizi hili linakuja kukamilisha msisitizo juu ya upendo wa mtu kwa Mungu. Maria anayeketi miguuni pa Yesu na kumsikiliza anatoa mfano wa kumpenda Mungu kwa kusikiliza Neno lake na kushika maagizo yake. Yesu anausifu moyo huo wa Mariamu na anasema anapomjibu Martha “martha , Martha unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi lakini kinatakiwa kitu kimoja tu na Mariamu amelichagua fungu lililo jema ambalo hataondolewa”.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, kutoka katika tafakari pana na ya jumla katika dominika iliyopita juu ya upendo kwa Mungu na kwa jirani, Masomo ya leo yanajikita na kuufafanua zaidi upendo kwa Mungu katika namna tatu tofauti. Namna ya kwanza ni ile aliyoionesha Abrahamu kwa kuwakirimu wageni na kuwatendea mema. Tendo la Abrahamu linaudhihirisha upendo kwa Mungu kwa njia ya kuwatendea mema wengine hasa wahitaji. Kristo mwenyewe alisema “yoyote mliyomtendea mmojawapo wa wadogo hawa mlinitendea mimi”. Tendo la ukarimu, tendo la wema, liwe dogo au kubwa, ni tendo linalomfikia Mungu na udhihirisho wa upendo kwa Mungu.

 

Namna ya pili ya upendo kwa Mungu ni ile anayoidhihirisha Mtume Paulo, kuyapokea kwa saburi na kuyavumilia mateso tunayoyapata katika kuishika imani na katika kuuishi upendo kwa Mungu. Upendo kwa Mungu ni sadaka ambayo mara nyingi hutuingiza katika magumu na hata mateso. Kuushuhudia upendo bila kuogopa magumu yanayotokana nayo ni tendo la ushujaa na alama kubwa ya kumpenda Mungu. Namna ya tatu ni ile anayoionesha Mariamu katika injili, kuketi miguuni pa Yesu na kumsikiliza. Kuketi miguuni pake kwa njia ya sala na tafakari na kulisikiliza Neno lake ndiyo msingi wa upendo halisi kwa Mungu.  Mungu aliye asili ya upendo na aliye upendo wenyewe atuimarishe na kututhibitisha katika upendo wake.

Liturujia J16
19 July 2019, 12:20