Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 21 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Jibidiisheni kupitia kwenye mlango mwembamba kwa njia ya matendo mema na adili! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 21 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Jibidiisheni kupitia kwenye mlango mwembamba kwa njia ya matendo mema na adili! 

Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka: Wokovu: Mlango mwembamba!

Mwinjili Luka leo anawaalika wasikilizaji wake kubadili mtazamo na hata namna zao za kufikiri na kuenenda kwani wengi waliona inatosha kuwa na dini ya mazoea au wengine wanaiita dini ya maumbile. Inatosha kuwa nina sali kila siku au kwenda kanisani kila Domini au kutoa zaka na kuudhuria jumuiya ndogo ndogo bila kuhusianisha maisha yangu na tunu msingi za Kiinjili! Uadilifu!

Padre Gaston George Mkude, - Roma

Amani na Salama! Katika Injili ya Mathayo tunakutana mara nyingi na lugha ya kutisha kutoka kwa Yesu kwa wadhambi na wakosefu, mathalani moto wa jehanamu,  juu ya siku ya hukumu ambapo Mungu atatenga mbuzi na kondoo na hata mara sita Mwinjili Matayo anazungumzia juu ya kulia na kusaga meno. Lakini kwa Mwinjili Luka kinyume chake tunakutana na Sura tofauti ya Yesu kwani ni mwenye huruma na rafiki wa wadhambi kiasi aliweza hata kula na kunywa nao walipomwalika. Hivyo, sehemu ya Injili ya leo inatupa sura tofauti sana na ile tunayoizoea kutoka kwa Mwinjili Luka na hapo ni vema tukatafakari vema kusudi na lengo lake. Yesu leo haonekani kuwa ni mganga aliyekuja ili kuwaponya walio wagonjwa, si yule anayewaacha tisini na kenda na kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea, si yule anayeamka usiku kutoka usingizini ili ampe rafiki yake mkate kwani amefikiwa na mgeni, si yule anayefanana na Baba mwenye huruma aliyempokea kwa furaha na hata kufanya karamu kubwa baada ya kumpata tena mwanaye.

Leo Kristo Yesu anatualika kujibidisha na kupitia mlango mwembamba, na kinyume chake basi ni kutupwa nje kwenye kilio na kusaga meno. Mwinjili Luka anapoandika sehemu hii ya Injili ya leo lengo na shabaha yake ni kuwahimiza wakristo wa jumuiya yake kutambua wajibu wao wa kushika imani si kwa mazoea tu bali kwa maisha halisi ya siku kwa siku. Ni kuwaalika kubadili mtazamo na hata namna zao za kuenenda kwani wengi waliona inatosha kuwa na dini ya mazoea au wengine wanaiita dini ya maumbile. Inatosha kuwa ina sali kila siku au kwenda kanisani kila Domini au kutoa zaka na kuudhuria jumuiya ndogo ndogo bila kuhusianisha maisha yangu na Injili ya Yesu Kristo. Ni katika muktadha huo basi nawaalika turejee kuitafakari vema sehemu ya Injili ya leo. Mtu mmoja anaenda kwa Yesu na kumuuliza juu ya idadi ya wale watakaookoka. Yesu hamjibu swali lake kwani mtu yule alitaka kujua idadi na badala yake Yesu anatualika leo tutafakari nini tufanye kwa ajili ya kuurithi uzima wa milele.

Jibidisheni, lazima kutoka jasho, lazima kufanyia kazi wokovu wetu ndio jibu la Yesu si tu kwa yule mtu bali kwa kila mmoja wetu. Kushiriki karamu ya Kristo hatuna budi kutoka jasho. Walioko karamuni ndio wale waliojibidisha kwa kupitia mlango mwembamba. Katika sura ya 9 ya Injili ya Luka tunakutana na mabishano kati ya  wanafunzi wa Yesu juu ya nani ni mkubwa kati yao. Yesu anawakumbusha ulazima na umuhimu wa kuwa wadogo kama watoto wadogo. Hivyo hatuwezi kuwa wafuasi wa Yesu kama hatujibidishi kuwa wadogo kwani kwa kukomaa na ukubwa wetu basi hapo itakuwa ni ngumu kupita katika mlango mwembamba. Na ndio mwaliko wa kuwa watumishi wanyenyekevu katika maisha yetu bila kujikweza na kujikuza na kusaka sifa na utukufu wetu. Mdogo ni yule anayetambua kuwa hana mastahili yeyote mbele ya Mungu, anayekiri kuwa ni mdhambi na mkosefu hivyo anaikimbilia Huruma na Upendo wa Mungu. Ni kwa kuwa wadogo tu hapo tunahakika ya kuweza kuingia karamuni kwa kupitia mlango mwembamba.

Kundi la pili ni wale wanaobaki nje na mlango kufungwa na huko wanakuwa kwenye kilio na kusaga meno.  Hao si wapagani ni wale waliomjua Yesu hata kusikiliza Neno lake, na kula na kunywa naye. Ndio kutukumbusha kadi ya kushiriki karamu ile haitoshi kujua mafundisho juu ya imani yetu bali lazima kuishi Injili katika maisha yetu.  Haitoshi kushiriki Misa iwe kanisani au jumuiyani au sala kila siku bila kuiweka imani yetu katika maisha. Ni mwaliko wa kubadili mtazamo wetu kuwa maisha yetu hayana budi kuongozwa na Injili. Mwinjili Luka anatuonesha tena kundi la wale walio karamuni wapo hata na watu wasio mjua Yesu! Wapo pia wapagani na watu wa mataifa kutoka kila rangi na kabila na taifa. Hivyo karamu ni kwa ajili ya watu wa ulimwengu mzima. Nawatakia tafakari njema na Dominika njema.

26 August 2019, 11:57