Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka wa C wa Kanisa: Imani na matumaini kwa maisha na uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Mwaka wa C wa Kanisa: Imani na matumaini kwa maisha na uzima wa milele! 

Tafakari Jumapili 19 ya Mwaka C: Imani & matumaini ya uzima wa milele!

Imani ni ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Imani ni ile hali ya akili ya mtu kupokea ukweli uliofunuliwa na Mungu. Imani ni mwambatano wa nafsi ya mtu kwa Mungu. Imani ni kukubali kwa hiari ukweli wote ambao Mungu ameufunua kwetu (KKK, 150). Imani ni neema ya Mungu ndani mwetu (KKK, 153). Imani ni zawadi ya Mungu, fadhila ya kimungu inayomiminwa naye mioyoni mwetu.

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 19 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Tafakari ya leo imebeba ujumbe wa imani ambayo ni msingi na chanzo cha tumaini la kweli na mwanzo wa uzima wa milele kwani hutujalia kuonja furaha na mwanga wa heri ya mbinguni.  Somo la kwanza kutoka kitabu cha Hekima ya Sulemani linatoa mwangwi wa jinsi Mungu alivyowatayarisha Waisraeli kwa safari ya ukombozi kutoka utumwani Misri, usiku ule alipowaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri. Kama vile Waisraeli walivyokesha usiku ule kwa imani wakingoja ukombozi wao kutoka kwa Mungu, sisi nasi kwa imani tunapaswa daima kuwa tayari kwa saa ya kifo chetu na kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo kwa utimilifu wa ukombozi wetu kama injili inavyotuambia tukeshe, tuwe tayari mda wote.

Somo la Pili kutoka waraka kwa Waebrania linawaimarisha wakristo Waebrania waliovunjika moyo sababu ya madhulumu na mateso kwa ajili ya imani yao kwa Kristo mfufuka likiwaasa wawe na imani kwa uzima wa milele kama aliyowaahidi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo wakifuata mfano wa babu zao Ibarahimu, Isaka na Yakobo. Kwa imani Ibrahimu alikaa ugenini katika nchi ya ahadi, katika hema pamoja na Isaka na Yakobo. Kwa imani Sara alipokea uwezo wa kuwa na mimba katika uzee wake akiwa na umri wa miaka 90, na Ibrahimu akiwa na miaka 100, Mwa 17:17. Hivyo imani inatujalia uhakika wa mambo yajayo. Injili kama ilivyoandikwa na Luka, yatueleza kuwa wakristo, daima tutabaki kuwa kundi dogo na dhaifu hapa duniani, lakini tukidumu katika imani tutapokea tuzo na kufurahi milele yote mbinguni tukionana uso kwa uso na Mungu Baba kama Yesu, anavyotufariji akisema, msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa Baba yenu ameona vema kuwapa ule ufalme.

Lakini kwa sharti la kuviuza tulivyo navyo, kuvitoa sadaka ili tujifanyieni mifuko isiyochakaa na kujiwekea akiba isiyopungua mbinguni, mahali ambapo mwivi hawezi kukaribia, wala nondo kuharibu, kwa kuwa hazina yetu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yetu. Angalisho ni daima tuwe waaminifu na kuwa tayari kwa ujio wake, tukikesha na kuomba daima kwani hatujui saa ajapo Lk 12:40. Kukesha huku kwawezekana tukiwa na imani ya kweli. Lakini imani ni nini? Imani ni fadhila ya kimungu. Imani ni “Kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (Ebr. 11:1). Imani ni ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu. Imani ni ile hali ya akili ya mtu kupokea ukweli uliofunuliwa na Mungu. Imani ni mwambatano wa nafsi ya mtu kwa Mungu. Imani ni kukubali kwa hiari ukweli wote ambao Mungu ameufunua kwetu (KKK, 150). Imani ni neema ya Mungu ndani mwetu (KKK, 153). Imani ni zawadi ya Mungu, fadhila ya kimungu inayomiminwa naye mioyoni mwetu.

Uhakika wa ukweli wa imani ya Kikristo ni Mungu mwenyewe anayejifunua kwetu ili tumjue, tumpende, tumtumikie, tuokolewe naye na mwisho wa yote ni kuonana naye uso kwa uso huko mbinguni aliko yeye pamoja na malaika na watakatifu wake wote. Hivyo imani haitegemei ufahamu wa akili ya kibinadamu, bali yamtegemea Mungu mwenyewe. Twaamini ukweli wa mafumbo ya Kimungu, si kwa mamlaka ya akili zetu, bali kwa mamlaka ya Mungu anayejifunua na kutufunulia ukweli wa mafumbo hayo. Twajua na kuamini kuwa yote yatokayo kwa Mungu ni kweli kwa sababu Mungu ni ukweli na uaminifu, hadanganyi, wala hadanganyiki. Kwa kuwa Mungu ni fumbo, na ukweli wa Kimungu ni fumbo kama Mungu mwenyewe, fumbo hili linaeleweka na kuhakikishwa na Mungu mwenyewe, si kwa mamlaka ya akili ya kibinadamu. Lakini hata hivyo, uelewa wa kina zaidi unaleta imani kubwa zaidi. Neema ya imani inafungua “macho ya moyo” kwa ajili ya ufahamu hai wa yale yaliyo katika ufunuo.

Hivi ndivyo asemavyo Mtakatifu Augustino: “Nasadiki ili kufahamu, na nafahamu ili kusadiki vizuri zaidi”. Kanisa Katoliki linaungama mafumbo makuu ya imani ambayo ni fumbo la Utatu Mtakatifu, fumbo la Ukombozi, fumbo la Yesu kujifanya Mtu (Umwilisho), fumbo la Ekaristi Takatifu, fumbo la Umama wa Bikira Maria, fumbo la Bikira Maria kukingiwa dhambi ya asili pia fumbo la Bikira Maria kupalizwa mbinguni mwili na roho. Haya yote yamefunuliwa na Mungu na imani tu yaelewa. Faida za imani: Imani inatupatia utambulisho wetu. Kubatizwa na kupokea Imani Katoliki kunatufanya watoto wa Mungu. Imani inatuunganisha na wengine na hivyo kutusaidia kujua namna ya kuhusiana na wengine na kunufaika na misaada ya sala na kijamii kutoka kwa wengine. Imani inatuweka na kutupatia njia ya uhakika ya kufika mbinguni. Imani ni namna ya maisha. Kwa hiyo, inatusaidia kujua jinsi tunavyopaswa kuishi maisha yetu, jinsi ya kuielewa na kuitika miito mbalimbali kama vile upadre, utawa, ndoa na namna ya kuendesha kazi zetu kama biashara, kilimo, kazi ya ajira hata jinsi ya kuipenda, kuitunza na kuiheshimu miili yetu inategemeana na imani tuliyonayo.

Imani inatusaidia kujua namna tunavyopaswa kusali. Tunasali kadiri ya imani na tunaamini kadiri tunavyosali. Sala ni chazo cha imani na sala inaonyesha imani ya mtu. Imani ni sababu ya matumaini yetu. Imani yatusaidia kujua malengo ya maisha yetu na hivyo kutupatia mwelekeo wa maisha yetu na jinsi tunavyopaswa kuishi kwa sasa na baadaye. Imani inatupatia maelezo ya mambo ambayo hatuyaelewi kwa akili zetu za kibinadamu mfano uwepo wa matatizo, magonjwa, mateso hata uwepo wa kifo. Katika jamii zetu hata miongoni mwa waliopokea ufunuo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo bado tunashikilia dhana potofu ya imani za kishirikina. Ukatili wa kinyama wa watu wenye ulemavu wa ngozi, biashara ya binadamu na viungo vyake, mauaji ya vikongwe, safari za ungo, imani katika tiba za masharti ya kishirikina kama vile kutoa kafara za watu, au kufanya tendo la ndoa kinyume na maumbile au na watoto au vikongwe hata wanyama, imani kwa mafuta ya upako.

Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, kuna hata maji au chuvi ya upako, pete, medali au mikufu hata nguo na viatu vya upako ni matokeo ya imani potofu kuwa kwa njia hiyo mtu atafanikiwa katika maisha mfano katika biashara, kupata ajira au kufanikiwa katika kuchimba madini, kufaulu mitihani au kupata mchumba au watoto. Masharti kama hayo ni uvunjifu wa amri ya kwanza ya Mungu, ni kinyume na imani aliyotufunulia Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, pia yanamuathiri mtu mzima kiroho na kimwili. Dhana ya uwepo wa wataalamu wa kufanya mvua inyeshe au isinyeshe, ahadi za kutajirika kimiujiza, maombezi ya kufuta nuksi, kuvunja mti wa ukoo na kumaliza matatizo ya kiroho au kimwili, hofu ya kinachoitwa “freemasoni” na dini ya waabudu shetani (devil worship) ni dalili za ukosefu wa imani kwa Mungu mmoja katika nafsi tatu aliyejifunua kwetu kama Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Haya ni matokeo ya kukosekana kwa elimu-dini ya kweli juu ya imani ya kweli na elimu-dunia iliyo bora na yakutosha kutuwezesha kusimama imara na kutolea uamuzi fumbuzi na sahihi kwa changamoto za maisha yetu. Basi ndugu nawasihi“simameni imara katika imani ya kweli” ya Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume ili mpate kulifikia tumaini letu la kweli Mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

J19 Mwaka C wa Kanisa
09 August 2019, 15:24