Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 21 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa watu wote! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili 21 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa watu wote! 

Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka: Wokovu ni zawadi ya Mungu!

Tusipouishi ukristo wetu, tusipozishika amri na maagizo ya Mungu hatutaingia kamwe katika ufalme wa Mungu hata kama tumebatizwa na kuwa Taifa teule la Mungu. Ushuhuda wa imani yetu kwa maneno na matendo yetu ndiyo yatakayotustahilisha kuingia katika ufalme wa milele mbinguni. Wokovu ni zawadi ya Mungu kwa watu wote, lakini wanapaswa kuutafuta katika haki na kweli!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 21 ya mwaka C wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya leo yanatukumbusha kuwa ubatizo sio kibali cha urithi wa ufalme wa mbinguni, kuwa mkristo au taifa teule la Mungu sio kibali cha kuingia mbinguni na kuuridhi uzima wa milele. Tusipouishi ukristo wetu, tusipozishika amri na maagizo ya Mungu hatutaingia kamwe katika ufalme wa Mungu hata kama tumebatizwa na kuwa Taifa teule la Mungu. Ushuhuda wa imani yetu kwa maneno na matendo yetu ndiyo yatakayotustahilisha kuingia katika ufalme wa milele mbinguni. Katika somo la kwanza Mungu kupitia kinywa cha Nabii Isaya anawafariji na kuwatuliza Waisraeli waliorudi toka utumwani Babeli akiwaambia kuwa siku za mbele utukufu wake utahubiriwa kwa mataifa yote. Utabiri huo umetimia katika Agano Jipya kama anavyotuambia mtume Paulo, “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana,” Gal 4:4-5.

Mwinjili Yohane anasisitiza akisema, “Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Yesu anathibitisha ukweli huu kwa kusema, “Mimi ndimi njia, ukweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Somo la pili kutoka waraka kwa Waebrania linatukumbusha kuwa kuishi daima katika imani, kama anavyotaka Mungu, ni wajibu wa kila mkristo. Hata tukipata mateso, tusikate tamaa kwani madhulumu na mateso ni malezi ya Mungu Baba kwetu sisi wanae. Tukumbuke wosia huu, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye; maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi. Naye humpiga kila mwana amkubaliye. Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa si kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.

Injili kama ilivyoandikwa na Luka inatufundisha kuwa kusikiliza mahubiri na mafundisho ya Kanisa, kushiriki sadaka ya Misa Takatifu na kupokea Ekaristi Takatifu yaani kula mwili wa Kristo na kuinywa damu yake hakutoshi kwa ajili ya kuurithi ufalme wa mbinguni. Watakaoingia mbinguni ni wale walioishi amri ya mapendo, waliofanya yale aliyoamuru Yesu Kristo. Ukweli huu Yesu anaueleza baada ya kuulizwa swali Je! Bwana, watu wanaookolewa ni wachache? Maneno ya Kristo kuwa watakuja watu toka mashariki na magharibi, na toka kaskazini na kusini, nao wataketi chakulani katika ufalme wa Mungu ni mwangwi wa utabiri wa Nabii Isaya katika somo la kwanza aliposema, wakati unakuja nitakapokusanya mataifa yote na lugha zote; nao watakuja, nao watauona utukufu wangu, nitawatuma hao waliookoka kwa mataifa, wauhubiri utukufu wangu. Utabiri huu unaweka wazi kuwa sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, sote tunaitwa kuwa watakatifu, sote tunaitwa kushiriki furaha ya uzima wa milele lakini kwa sharti la kuzishika na kuziishi amri na maagizo ya Mungu.

Bila kuishi maisha ya kumtukuza na kumsifu Mungu, bila kuwa na muunganiko na Mungu wetu aliyemtakatifu sana hatuwezi kuuona utukufu wake katika Maisha yajayo. Na huku ndiko kuingia katika mlango ulio mwembamba kuishi kadiri ya amri na maagizo ya Mungu. Kumbe katika kuuridhi ufalme wa mbinguni haitoshi kuwa mingoni mwa Taifa teule la Israeli, kama walivyoamini wayahudi. Hata kwetu sisi kubatizwa na kuitwa mkristo haitoshi kuuridhi ufalme wa mbinguni yatupasa kuiishi Imani yetu, kuwa kweli mashahidi wa Kristo kwa watu wote. Ushuhuda wa kiimani sio jambo rahisi yahitaji kujitoa sadaka kuvumilia mateso ndiyo maana Yesu anasema, Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. Kuna uwezekano kuwa tumebatizwa, tunaitwa wakristo lakini hatuuishi ukristo wetu, hivyo tusije kushangaa siku ya mwisho wa Maisha yetu Bwana atakapomtuma mjumbe wake kutuita kila mmoja kwa mda na nafasi yake yakasikika maneno haya, siwajui mtokako; ondokeni kwangu ninyi nyote mlio wafanyaji wa udhalimu. Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno.

Ni wazi ubatizo ni mlango wa sakramenti zingine zote, ubatizo ni sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika sakramenti hii. Licha ya haya yote, bado tuna wajibu wa kuishi kweli kama Watoto wa Mungu, tuna wajibu wa kuishi kama watoto wa Kanisa. Si jambo rahisi kwani latutaka kwenye kinyume na fikra za kiulimwengu, kuishi kinyume na mtazamo wa wana wa ulimwengu huu, kujinyima kwa ajili ya wengine, kuachana na tamaa za kidunia na kuyakaza macho yetu kuelekea mbinguni. Huu ni mlango mwembamba, hivyo tumuombe Mungu atujalie neema na baraka zake tuwe kweli Watoto wake, tuuishi kweli ukristo wetu ili mwisho wa siku ukifika tuweze kuokolewa na kuingia katika ufalme wa uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo. 

Jumapili 21 Mwaka C
20 August 2019, 15:57