Tafakari Jumapili 21 ya Mwaka: Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa watu wote!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. – Dodoma.
Mama Kanisa anafundisha kwamba, wokovu wa Mungu unafumbatwa katika Sheria na neema. Mwanadamu akiitiwa heri, lakini amejeruhiwa na dhambi, anahitaji wokovu wa Mungu. Msaada wa Mungu unamjia katika Kristo Yesu kwa njia ya sheria inayomwongoza na katika neema inayomtegemeza. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu ambayo ni zawadi kwa watu wote bila ubaguzi. Lakini unapaswa kupokelewa kwa njia ya unyenyekevu, toba na wongofu wa ndani. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni mpango unaoonekana wa upendo wa Mungu kwa ajili ya binadamu, kwa sababu Mwenyezi Mungu anataka binadamu wote waweze kuwa ni Taifa moja la Mungu, wakikusanyika katika mwili mmoja tu wa Kristo Yesu, wajengwe katika hekali moja la Roho Mtakatifu. Kwa ufupi, Kanisa katika ulimwenguni ni Sakramenti ya wokovu, alama na chombo cha umoja na ushirika wa Mungu na waja wake!
Historia ya wokovu kadiri ya Maandiko Matakatifu yaonesha mpango wa Mungu kwa ukombozi wa ulimwengu. Tangu sura ya 12 ya kitabu cha Mwanzo na kuendelea tunaona jinsi historia hii inavyoendelea na inavyokumbwa na vikwazo vingi. Kwa wito wa Abrahamu Mungu anateua mtu atakayemtumia ili mpango wake uweze kuonekana na kukamilika na kwa njia yake mataifa yote yatabarikiwa. Mpango huu upo wazi katika maandiko matakatifu na kupitia taifa la Israeli, Mungu anajidhihirisha kwa ulimwengu. Historia hii inakamilika kwa ujio wake Kristo. Hakika historia hii ina mchanganyiko wa mambo mengi mazuri na mabaya, mepesi na magumu lakini iliyokamilika. Kwa mantiki hii, watu wote wataokolewa kama tu watabaki katika mpango wa ukombozi na katika kutimiza mapenzi yake Mungu.
Somo la kwanza la leo limeandikwa kama ushuhuda wa hilo. Sehemu hii ya maandiko ilifanywa baada ya kutoka utumwani. Watu walikata tamaa. Walipoteza yale maisha ya utukufu. Kwa njia ya mateso, Mungu anajifunua tena kwao na kuwahakikishia ushindi. Mungu anajifunua tena kwao na kwa nguvu kubwa. Ataleta pamoja mataifa yote na lugha zote. Sasa hiyo ahadi ni kwa mataifa yote na si kwa Israeli tu. Wigo wa wokovu unapanuliwa kwa mataifa yote. Hivyo jibu la swali kwamba watakaokolewa ni wachache au wengi linapata ufumbuzi. Tena huongea wazi kuwa wokovu utawafikia hata walio nje ya Taifa teule. Huu mkazo wa wokovu kwa wote unasisitizwa kuliko ilivyokuwa kabla. Israeli anakumbushwa kuwa nafasi yake katika historia ya wokovu ilikuwa ni ya huduma kwao na kwa wengine na si kwa ajili yao tu. Ufunuo huo unawekwa wazi na Yesu kwamba wokovu ni kwa watu wote. Injili ya leo yasema kuwa wokovu huo ni kwa mataifa yote.
Tukumbuke swali katika Injili, Je, e ni watu wote wataokoka? Na jibu la Yesu ni kuwa ni watu wote. Na Yesu anapojibu anahamisha swali toka ni wangapi na jibu linaonesha ni jinsi gani wokovu utapatikana. Na kwamba ni kupitia mlango mwembamba. Katika sala ya Nasadiki tunasali ‘Nasadiki kwa Yesu Kristo, aliyeshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu”. Kuokolewa ni kupata maisha ya umilele. Katika Yoh. 3:15 tunasoma ‘ili kila amsadikiye awe na uzima wa milele”. Hivyo hakuna haja ya kuwa na wasiwasi au idadi au nani. Uhakika wa wokovu upo. Kwa ujumla injili ya Luka yaongelewa juu ya safari ya kitume ya Yesu ambapo Yesu anaonekana akiwa safarini kuelekea Yerusalemu. Tunamuona Yesu akitembea katika miji na vijiji vyao akielekea Yerusalemu. Yerusalemu ni mahali ambapo Yesu alichukuliwa mbinguni – Lk. 24:51. Utukufu huu ulitanguliwa na kifo na mateso – Lk. 17:25. Hali Yesu akitambua hali hii anaangalisha mataifa uwezekano wa kupata utukufu huo lakini kupitia njia ya mateso na kifo. Na hii ndiyo historia ya kanisa.
Uwepo wa Kristo unakamilisha historia hiyo. Ni historia ya mapambano lakini ikifanyika pamoja na Kristo basi utukufu hupatikana kwa mataifa yote. Mtume Paolo katika waraka kwa Wafilipi 2:6-11 anaeleza vizuri mpango huu wa wokuvu unaoonekana katika unyenyekevu wa Kristo hata kufa msalabani. Huku kujitoa kwake Kristo – “kenosis”, yaani kujishusha, kujimwaga, kujitoa, hata kuacha utukufu wake wa kimungu na kibinadamu na kukubali kifo, tena cha msalaba. Hakuna upendo zaidi ya huu. Na kwa njia ya mateso, ametuinua na Mungu akamkweza juu kabisa na huu ukuu ukatuletea sisi wokovu. Kile kilichofungamanishwa na dhambi, yaani mateso, kinapewa maana mpya. Upendo wa Mungu unageuzwa kuwa utukufu. Mateso yanageuzwa kuwa wokovu. Wokovu ni kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, kuyatenda na kufanya uongofu wa kweli. Katika kujibu swali la mitume wakati wa ujio wake wa pili na itakuwaje, Yesu anawaelekeza jinsi ya kuishi na kujiandaa kwa huo ujio wa pili na kitu gani cha kufanya wakiwa wanasubiri huo ujio – Mt. 24:3-4.
Baadaye alipoketi katika mlima wa Mizeituni, wafuasi wake wakamjongelea, wakamwuliza kwa faragha, utuambie hayo yatatendeka lini? Na nini itakuwa ishara ya kuja kwako na mwisho wa dunia? Yesu akajibu akawaambia, angalieni, asiwapotoshe mtu. Wokovu wetu utapatikana tukiwa na uhusiano mwema na Kristo. Katika Mt. 7:13-14 tunasoma ‘ingieni mlango mwembamba. Kwa maana mlango ni mpana na njia ni pana iendayo katika upotevu. Tena ni wengi wanaoifuata. Bali mlango umebana na njia ni nyembamba iendayo katika uzima. Tena ni wachahe wanaoifuata’. Mtakatifu Agostino anasema ‘tumeumbwa bila hiari yetu na kwa mapenzi yake Mungu. Lakini wokovu ni juhudi binafsi”. Tumsifu Yesu Kristo.