Tafakari Jumapili 22 ya Mwaka: Unyenyekevu na Upendo wa dhati!
Na Padre Reginald Mrosso, - Dodoma.
Neno la Mungu Dominika ya 22 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, linatupatia changamoto kuangalia tena utengano unaoweza kuwepo kati yetu sababu ya mali, hali tulizonazo au nafasi zetu za kiuchumi katika jamii. Mwandishi wa somo la kwanza na kama ilivyo katika somo la Injili asema kuwa mtu mnyenyekevu na mnyofu hajikuzi bali huwa tayari kwa ajili ya wengine. Sote tunaalikwa kutambua kuwa mwenye yote na mweza wa yote ni Mwenyezi Mungu peke yake. Utukufu na utajiri halisi wa Mungu waonekana katika mwanae na Bwana wetu Yesu Kristo. Mtakatifu Jerome anatusaidia kuelewa hili anaposema ni tajiri wa kutosha yule aliye maskini katika Kristo. Ushuhuda huu ni mkubwa sana kwani Kristo ndiye mrithi wa hayo yote na yule amfuataye Kristo atapata yote yaliyo yake Mungu. Ampataye Kristo, basi amepata utajiri wa kweli. Ufahahamu huu unagusa uhalisia wote wa maisha ya mwanadamu. Kifo cha Bwana wetu Msalabani ni dhihirisho la ufahamu huu wa ukuu na uweza wake Mwenyezi Mungu. Kwamba yote tuliyo nayo na maisha yetu yote ni mali yake Muumba, yaani Mungu.
Tunasimuliwa na Sr. Regina Opuku, OLA wa Jimbo kuu la Cape Coast kutoka kitabu ‘Hadithi za Kiafrika’ Ghana habari juu ya unyoofu na unyenyekevu wa Askofu mkuu John K. Amissah wa Jimbo kuu la Cape Coast Ghana ambaye alipata ajali mbaya ya gari akiwa na abiria wengine kwenye gari lake. Ikapita gari ndogo na wakawa tayari kutoa msaada. Gari hili lilikuwa na uwezo wa kubeba baadhi ya majeruhi na wakataka kutoa upendeleo kwa askofu. Yule askofu akasema wengine wamejeruhiwa zaidi yangu, wapewe msaada kwanza. Yeye akawa tayari kusubiri zamu nyingine. Hata hivyo msaada mwingine haukupatikana kwa haraka. Kati ya majeruhi wote, yeye peke yake akafariki dunia. Alitoa msaada kwa ajili ya wengine. Yeye akapoteza maisha yake. Mfano huu utusaidie kutafakari na kuangalia jinsi tunavyotumia yote aliyotujalia Muumba kwa ajili yetu na kwa ajili ya wengine. Tumewekezaje? Ufahamu wetu wa utajiri wa Mungu ukoje? Hatari kubwa ni kule kujiweka sisi mbele hata kutaka kumtangulia na kumwacha nyuma Muumba na pia kuwaweka wengine pembeni. Inatosha tu kuangalia jinsi mwanadamu anavyoweka mbele tamaa ya mali na fedha na hata kuwa tayari kuhatarisha utu wa mtu mwingine.
Mfano wa injili kuhusu tamaa ya kutaka kukaa mbele au kualika tu rafiki unaweka wazi hali hii. Kuna msemo wa lugha ya Kilatini usemao ‘maskini si yule aliye na vichache, ila yule anayetaka vingi’. Hakika ni katika hali hii ya tamaa kubwa migangano ya mali na fedha imegharimu maisha ya watu wengi duniani. Watu hawagombani katika kuishi maadili mema au katika kumtafuta Mungu ila katika kunyang’anyana fedha na mali ya dunia. Tunakumbushwa kuwa kama tunataka kuwekeza basi tuwekeze mbinguni. Tukiangalia uhalisia wa maisha yetu wakati wetu huu na jinsi tunavyoendesha maisha ya kila siku inatosha kutafakari mambo mengi ambayo yanajitokeza kati yetu. Tutafakari kuhusu michango mbalimbali tunayotoa kwa mfano kuchangia harusi. Hivi lengo la kuchangia ni lipi. Lengo ni kumsaidia mwenye tukio au ni kuwekeza ili tuweze kula na kunywa vizuri siku ya tukio? Je mwenye tukio anafaidikaje na mchango ili umsaidie katika kuanza au kuendeleza maisha yake baada ya tukio? Inasikika kuwa fedha ikichangwa inasimamiwa kikamilifu ili imalizike yote katika vyakula na vinywaji.
Sasa ni kwa nini msaada kwa mwenye tukio umalizike katika tukio hilo tu? Na pengine ugomvi huweza kutokea katika kuvunja kamati kama pengine mwenyekiti au mmoja wa wanakamati aliingiza mtu ambaye hakuchangia fedha. Na sheria zinakuwa kali kiasi kwamba hata mwenye tukio hawezi kuongeza mtu hata kama amekuja kwa dharura. Je, huu utamaduni wa kualikana kwa kadi ni tunu ya utamaduni wa kiafrika? Mbona tangu zamani za kale shughuli ya mmoja iwe furaha au kilio iliwahusisha wote? Inakuwaje leo kilio kiwe cha wote na furaha iwe ya wachache? Inakuwaje eti ili kushiriki tukio la furaha kama harusi ni lazima uwe umepata kadi na uwe umetoa mchango? Na aliyetoa mchango mkubwa anapata meza ya upendeleo. Na kama hukutoa mchango basi huwezi kushiriki. Katika mtazamo huu hatuna budi kumshukuru Bwana wetu ambaye ametupatia meza ya Ekaristi ambapo sote tumealikwa kushiriki. Tumsifu Yesu Kristo!