Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XX: Yesu alionekana kuwa tishio!
Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. - Dodoma.
Mfalme Napoleon aliiteka Urusi na kati ya wafungwa Warusi, alikuwepo mfungwa mmoja mkulima. Alishurutishwa kutumikia jeshi la Napoleon na mkononi aliwekewa alama N kama alama ya utambulisho wake. Alipotambua lengo la alama ile aliukata mkono wake na hivyo akaondoa alama ya utambuzi na kuwa huru na hali ya utumwa. Huyu alifanya maamuzi magumu na kwa hilo akawa huru. Pengine ndicho tunachotakiwa kufanya katika maisha yetu ya imani baada ya kusikia neno la Mungu jumapili hii ya leo. Somo la Injili ya leo lina sehemu ya maandiko yenye maneno makali sana ya Yesu kuliko sehemu nyingine au maneno mengine katika injili yote. Wadhani kuwa nimekuja kuleta amani? La. Ila mgawanyiko. Mzee Simeoni aliona haya alipompokea mtoto Yesu mikononi mwake – ni alama ya kuinuka na kuanguka kwa wengi katika Israeli – Lk. 2:35. Mama Maria alishiriki katika maisha yake ufunuo huu wa mzee Simeoni.
Aidha, wakati wa kuzaliwa kwake Yesu maneno haya yalisikika – Amani duniani kwa wote wenye mapenzi mema. Wakati wa utume wake alisema heri waletao amani. Yesu alipokuwa anakamatwa, Petro alitaka kutumia silaha kumlinda. Yesu akamwambia Petro aweke upanga alani. – Mt. 26:52. Tuelezeje hapa? Ili kuelewa vizuri ujumbe wa neno la Mungu leo hatuna budi kujua amani na umoja alioleta Yesu na kujua amani na umoja aliouvunja. Kristo alileta amani na umoja wa uzuri, wa uzima wa milele na aliikataa amani na umoja usiyo na tija. Siyo kweli Yesu alikuja kuleta utengano na vita ila kwa uhakika kilichotokea ni kuwa uwepo wake ulileta mtazamo mpya katika maisha. Kwamba ujio wake au uwepo wake ulimweka mwanadamu katika nafasi ya maamuzi thabibiti. Twajua kuwa mwanadamu akitakiwa kutoa jibu au kufanya maamuzi basi uhuru wake hupata changamoto kubwa na maamuzi yaweza kutolewa kwa njia tofauti na namna mbalimbali.
Neno la Mungu katika Injili, Yoh. 8:31 latuambia kuwa ukweli utakufanya huru. Hapa uhuru wa mtu unachagizwa. Yule mzee mfungwa Mrusi aliamua kuwa huru kwa kuukataa utumwa. Akakata mkono wake uliomfanya atambulike kama mfungwa. Yesu anatofautisha aina mbili za amani. Katika Yoh. 14:27 – twaona akiwapa mitume amani yake na anasema wazi amani awapayo si kama utoavyo ulimwengu. Kwa kifo chake aliangamiza amani potofu ya kibinadamu, ya ulimwengu na kuzindua amani mpya na umoja ambalo ni tunda la Roho Mtakatifu. Hii ndiyo amani aliyotoa kwa wafuasi ule usiku wa Pasaka – amani iwe nanyi. Amani hii mpya isipokuwepo katika aina mbalimbali za maisha yetu basi mgawanyiko utakuwepo. Hii inatupata hasa tunapotakiwa kutoa maamuzi ya maisha yetu. Mtu aliyempata Mungu pia aweza kuingia katika mtafaruku huu wa kufanya maamuzi sahihi. Kumchagua Mungu au kubaki na mambo ya dunia.
Mgawanyiko waweza pia kutokea ndani ya nafsi ya mtu – kati ya mwili na roho. Kati ya kutimiza haja za mwili na kutimiza sauti ya dhamiri. Mgawanyiko huanza ndani mwetu. Mt. Paulo katika Wag. 5:17 anasema – ’kwa maana mwili hutamani yasiyotakiwa na Roho, na Roho hutamani yasiyotakiwa na mwili, basi hubishana, kwa hiyo mnashidwa kutimiza mnayotaka’. Mtu huwa na tabia ya kufungwa na amani yake ndogo na uhuru wake, hata kama hapati faida yo yote. Kwa namna hii amani na umoja wa Kristo huweza kuwa tishio kwake ukionekana kama kikwazo na tishio kwa utulivu wake binafsi. Hali hii ya ubinafsi isipoepukika, basi mgongano mkubwa waweza kutokea. Wengi wetu hushindwa hapa. Nabii Isaya aliweza kuvuka hali hii ya ubinafsi na kuwa tayari kutumwa – Isa. 6:8 – kisha nikasikia sauti ya Bwana, akisema, nimtume nani? Nani atakayekuwa mjumbe wetu? Nikaitika, mimi hapa, unitume mimi. Ujasiri huu wa Nabii Isaya utusaidie kuachana na ubinafsi wetu na utusaidie kuelewa wito wa Mungu katika masomo ya leo.
Mgongano au mgawanyiko waonekana wazi katika masomo yetu; jinsi Nabii Yeremia anavyopingwa. Yeremia anaongea kuangamizwa kwa utawala wa Yuda. Wao hawakuwataka kusikia jambo hili. Anatupwa katika shimo la matope. Viongozi wa watu waliziba masikio wasisikie ukweli. Yeremia aliisikia sauti ya Mungu. Hata hivyo Yeremia hakuwa mtu anayetaka mateso – 15:10-18 – si rahisi kuwa mjumbe wa Mungu. Na katika 20:7-9 anaeleza wazi mahangaiko yake ya ndani… umenivuta ee Bwana, nami nimekubali kuvutwa nawe. Umenishinda, ulikuwa na nguvu mno. Nimekuwa sababu ya kicheko kila wakati na dhihaka ya dunia yote. Hata hivyo anakubali yaishe na anamtumikia Mungu. Tunasikia pia habari juu ya mateso ya wakristo au changamoto za imani mpya katika somo la pili. Mwandishi wa barua kwa Waebrania anawakumbusha juu ya mateso ya watakatifu wa zamani na kwamba sasa wanakula matunda yao na anataja wazi ushindi wa Kristo.
Hivyo Wakristo wa sasa wanaitwa kutambua ushindi huo. Kwa hakika akiwepo Kristo ni lazima uwepo ufalme wa Mungu na huu ndo mwisho wa ufalme mwingine. Hapa upo mgawanyiko au mgongano mkubwa. Katika Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo, nje ya kuta, mojawapo ya maandishi yaliyopo Kanisani kuna bango hili – ‘tumefanya kumbukumbu hii ili kuwakumbuka wale waliopigana tayari na kuwafundisha wale watakaopigana sasa na baadaye’. Tumsifu Yesu Kristo