Tafakari Jumapili 22 ya Mwaka: Fadhila ya Ukarimu & Unyenyekevu
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika kipindi hiki cha ufafanuzi wa masomo ya dominika. Leo tunayafafanua na kuyatafakri masomo ya dominika ya 22 ya mwaka C wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee kabisa, Mama Kanisa anatualika kutafakari kwa kina na mapana kuhusu: fadhila ya unyenyekevu, wema na ukarimu mambo msingi yanayofumbatwa katika sheria ya Injili sanjari na kanuni ya dhahabu. Katekesimu ya Kanisa Katoliki inafafanua kwamba, kanuni hii ya mafundisho yaendeleza fundisho la Bwana kwa mamlaka ya Mitume, hasa kwa maelezo ya fadhila zimiminikazo kutokana na imani kwa Kristo Yesu na yanayohusisha upendo, paji kuu la Roho Mtakatifu. “Tendo lenu na lisiwe na unafiki. Kwa pendo la kidugu, mpendane ninyi kwa ninyi, mkitumaini kwa furaha, katika dhiki, mkisubiri, mkifuata kwa ukarimu. Waamini wanapaswa kushughulikia dhamiri kwa mwanga wa uhusiano wao na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake. Unyenyekevu wa matumaini unamrudisha mwamini katika mwanga wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Somo la kwanza (Ybs 3:17-20, 28-29 ) ni kutoka katika kitabu cha Yoshua bin Sira, mojawapo ya vitabu vya Hekima. Somo hili linatoa fundisho juu ya fadhila ya unyenyekevu. Linatuonesha kuwa unyenyekevu ndiyo fadhila inayompatia mtu kibali mbele ya watu. Mwenye unyenyekevu atapendwa kuliko mkarimu: mkarimu hutoa vitu alivyonavyo kwa wengine lakini myenyekevu hujitoa mwenyewe kwa faida ya wengine. Unyenyekevu sio tu fadhila inayompa mtu kibali mbele ya watu bali ni fadhila inayompa mtu kibali mbele ya Mungu. Na tena kadiri mtu anavyozidi kupanda juu katika madaraka ndivyo anavyotakiwa kuzidi katika unyenyekevu. Mafundisho haya ya hekima kuhusu unyenyekevu yameendelea kuchukua nafasi hata katika Agano Jipya. Kilele chake ni Yesu mwenyewe anayejitambulisha kuwa ni mnyenyekevu wa moyo: “jitieni nira yangu mjifunze kutoka kwangu kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11:29)
Somo la pili (Ebr 12:18-19, 22-24a) ni kutoka katika waraka kwa Waebrania. Somo hili linalinganisha Agano la Kale lililofungwa mlimani Sinai na lile Jipya kwa njia ya Yesu Kristo. Linaonesha kuwa Agano la Kale lilifungwa katika mazingira ya kuogofya; Mungu alionekana kuwa mbali na watu na tena kama Mungu wa kutisha. Mlima wenyewewe wa agano, mlima Sinai ulikuwa ni mlima usioweza kukaribiwa wakati wa uwepo wa Mungu. Hata mnyama angeugusa tu angepigwa mawe hadi kufa. Agano Jipya limejionesha tofauti. Si tena Agano la alama bali ni halisi kwa njia ya Kristo na Mungu amewasogelea watu na kukaa kwao ili awaokoe. Utoafauti huu unaelezwa ili kuonesha ukuu wa imani ya kikristo na matunda ya muungano wa mwamini na Kristo.
Injili (Lk 14:1, 7-14) Katika injili ya dominika ya leo Yesu Yesu yupo chakulani pamoja na wageni wengine waalikwa. Tangu enzi, wakati wa chakula ni wakati unaoheshimiwa sana. Na kwa tamaduni nyingi mlo wa sherehe husindikizwa na hotuba mbalimbali kuhusu dhamira ya sherehe yenyewe. Yesu anapopata nafasi hiyo ya kuzungumza, bila shaka kama mmojawapo wa waalikwa, yeye hazungumzii tukio bali anajikita kuwazungumzia watu wale waliomzunguka. Kwa wageni waalikwa anawafundisha unyenyekevu. Anasema “ukialikwa arusini usiketi katika kiti cha mbele”. Anawaonesha kuwa heshima ya mtu haiji kwa kujichukulia nafasi ya kwanza. Heshima, mtu hajipi mwenyewe bali heshima mtu hupewa na watu baada ya kuona namna anavyoenenda na namna anavyohusiana nao.
Baada ya kuongea kwa wageni waalikwa, neno la pili Yesu analielekeza kwa mwenyeji wa sherehe. Kwake anamwambia ufanyapo sherehe usialike watu kwa kigezo kuwa wao pia waje wakualike katika sherehe zao. Yesu anatambua kuwa kuwaalika watu ni tendo jema na la ukarimu. Tendo hili basi kama lilivyo tendo lingine lolote la wema lisifanywe kwa lengo la kutegemea malipo. Wema unaofanywa kwa kutegemea malipo si wema, ni biashara.