Tafakari Jumapili XVIII: Athari za tamaa ya mali na utajiri!
Na Padre William Bahitwa, - Vatican.
Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunatafakari Masomo ya Liturujia ya dominika ya 18 ya mwaka C wa Kanisa. Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM wanasema, utandawazi ni mchakato unaogusa maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili; unagusa na kutikisa maisha ya mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Utandawazi una tabia ya kujielekeza zaidi katika masuala ya kitamaduni, kiuchumi, kisiasa na hata kidini. Kimsingi, utandawazi unagusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Kwa upande mwingine, jamii ikijenga na kukuza utandawazi wa umoja, udugu na upendo, kunakuwepo na mafungamano ya watu wa familia ya Mungu duniani; watu wanaweza kujizatiti na kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu kwa kujikita katika mchakato wa haki, amani na maridhiano kati ya watu!
SECAM inasema, utandawazi wenye mvuto na mashiko, unawawezesha watu kushirikishana na kugawana amana na utajiri wa maisha ya kiroho; kwa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, urithi mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya! Utandawazi unapotea na kuogelea katika dhambi na ubinafsi kama inavyojionesha sehemu nyingi za dunia, unakuwa ni “jamvi” la uchu wa mali na madaraka; uchoyo na ubinafsi; mapambano kati ya nchi maskini na tajiri; kati ya wenye nacho na “akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi”. Utandawazi katika mwelekeo huu, unakuwa ni “kichaka” cha kutaka kuchuma rasilimali na utajiri asilia kwa mafao binafsi; kwa kujikita katika raha, starehe na kupenda mno anasa kiasi cha kutoguswa na shida wala mahangaiko ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Utandawazi wa namna hii unabomoa na kuvuruga misingi ya utamaduni, maisha ya kiroho, utu na heshima ya binadamu na matokeo yake ni kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Utajiri wa mali, fedha na karama mbali mbali vitumike kwa ajili ya huduma upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kamwe isiwe ni sababu ya uchoyo na ubinafsi, kwani mali bila kujali na kumthamini Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wa maisha ni ubatili mtupu!
Ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza (Mhu 1:2, 2:21-23 ) ni kutoka katika kitabu cha Mhubiri. Hiki ni mojawapo ya vitabu 7 vya Agano la Kale vinavyoitwa vitabu vya Hekima, vitabu vinavyochota kutoka katika uzoefu wa maisha kanuni na miongozo ya kuwasaidia watu kuishi vizuri. Kwa upande wake, Mhubiri anaziangalia kanuni hizi, anayaangalia maisha ya mwanadamu tangu mwanzo hadi mwisho wake hapa duniani, anapima jitihada zake na yote anayopitia na kuhitimisha kuwa yote ni ubatili. Haoni kanuni inayoelezea maisha katika ukamilifu wake. Jitihada za mtu, maelekezo na ushauri kuhusu maisha vyote hufika mahala vinakwama. Kwa hakika somo hili pamoja na kitabu chote cha Mhubiri hakilengi kufundisha kuwa maisha ni ubatili. Badala yake ni kitabu kinacholenga kurekebisha fikra za watu juu ya maisha na juu ya ulimwengu. Kinalenga kuonesha ni wapi fikra za mwanadamu, kama zikiachwa zenyewe bila ufunuo wa kimungu, zinaweza kufikia. Bila ufunuo wa kimungu, hekima ya mwanadamu huishia kumuonesha kuwa yote ni ubatili kwa sababu haiendi zaidi ya kile kinachoonekana.
Somo la pili (Kol 3:1-5, 9-11 ) ni kutoka waraka wa mtume Paulo kwa Wakolosai. Mafundisho ya Mtume Paulo juu ya ufufuko wa Kristo hayakukomea tu kuonesha kuwa Kristo ameyashinda mauti na sasa ni mzima. Zaidi ya hapo aliwaonesha wakristo kuwa ufufuko wa Kristo ni tendo la kuinuliwa kwao kutoka hali duni ya ubinadamu unaosongwa na dhambi kwenda katika hali ya kimungu ya utukufu. Wanabaki ni binadamu lakini wenye hali ya kimungu, kwa maana wanauelekea umungu. Paulo anauonesha uhusiano huu anapowakumbusha wakolosai akiwaambia “yatafuteni yaliyo juu” – zidini kuishi kwa kuulekea umungu. Na tafsiri ya kuishi kwa kuyatafuta yaliyo juu ndiko huku anakoeleza Paulo: kuuvua utu wa kale na kuuvaa utu mpya; kuvifisha viungo vinavyomrudisha mwanadamu katika utumwa ule wa dhambi aliokombolewa: uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, tamaa na ibada ya sanamu yaani ushirikina.
Injili (Lk 12:13-21) Katika injili ya dominika ya leo, Yesu anatahadharisha dhidi ya tamaa ya mali na hatari ya kuweka tumaini lote la maisha katika mali na utafutaji wake. Tunaona mtu mmoja anamwomba Yesu amwambie ndugu yake amgawie urithi wake. Yesu anakataa. Sheria ya Musa ilikuwa wazi kuhusu ugawaji wa urithi (Rej. Kum 21:17, Hes 27:1-11) na Yesu angeweza kabisa kuirejea. Yesu alikataa kuwa mwamuzi kwa sababu alijua hataweza kuitimiza tamaa ya mali iliyosukuma ombi hilo. Badala yake anatoa mfano ambao ndani yake unaonesha ni wapi tamaa ya mali inaweza kumfikisha mtu.
Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, masomo ya dominika ya leo yanatupatia nafasi ya kutafakari juu ya tamaa katika maisha yetu hasa tamaa ya mali. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inatufundisha kuwa hamu ya vionjo inatufanya tutamani vitu vinavyopendeza ambavyo hatuna. Hivyo ipo tamaa iliyo nzuri lakini mara nyingi tamaa zetu zinapita mipaka ya akili na kutusukuma tutamani bila haki kile ambacho si chetu na kilicho cha mwingine au kinachotakiwa na mwingine. Amri ya kumi ya Mungu inakataza tamaa ya mali inayotokana na uchu wa utajiri na nguvu yao. Inakataza pia tamaa ya kukosa haki kwa kumdhuru jirani kwa sababu ya mali zake za kidunia. Kiu ya mwanadamu ya mali wakati mwingine ni kubwa sana, haina mipaka, haizimiki kamwe na ndiyo maana imeandikwa “yeye apendaye fedha, hana fedha za kutosha kamwe” (KKK 2535-36). Kuishi kwa namna hii ni kuishi kana kwamba hatima yetu ipo hapa duniani. Mtume Paulo ametuonesha leo kuwa sisi ni wa duniani lakini hatima yetu ipo mbinguni. Tusiruhusu kumezwa na dunia tukaisahau hatima yetu.