Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Uaminifu na urafiki wa kweli ni mambo msingi badala ya kung'angania mali na utajiri! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Uaminifu na urafiki wa kweli ni mambo msingi badala ya kung'angania mali na utajiri! 

Tafakari Jumapili 25 ya Mwaka: Jengeni urafiki, msikumbatie mali

Sisi sote hatuna budi kutambua kuwa kila tulichonacho si mali yetu bali tumewekwa kuwa mawakili tu hivyo hatuna budi kutumia daima kwa kuwahudumia maskini na kujenga urafiki na wengine. Hatuna budi kuwa mawakili waaminifu, tukikumbuka umuhimu wa kujenga urafiki na Mungu na jirani ili tuweze kuja kukaribishwa nao si tu katika ulimwengu huu bali katika maisha ya umilele.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mfano wa wakili mjanja na asiyekuwa mwaminifu unakuwa na ukakasi mwingi kwani si mfano mzuri hasa kwetu tulio rafiki na wafuasi wake Yesu Kristo tunaoalikwa kila mara kuwa waaminifu katika maisha. Hivyo kuupata ujumbe wa Injili ya leo nawaalika tutafakari kwa pamoja na kwa makini maana kinyume chake tunaweza kuukosa ujumbe kusudiwa na Bwana wetu Yesu Kristo.Baadhi ya wataalamu wa Maandiko wanatueleza kuwa wakili mjanja alikuwa ameweka mahesabu ya uongo kwa wadeni wake ili baada ya kupoteza kazi aweze kukaribishwa nao na wengine wanasema kuwa alifanya mahesabu ya uongo na wizi kabla na hivyo kupelekea kufukuzwa kazi na mmiliki wa shamba.  Ilikuwa ni desturi nyakati zile za Yesu kwa matajiri wakubwa kumiliki ardhi kubwa na kuweka chini ya mawakili au waangalizi wa mashamba yale na wao waliishi sehemu za mijini, hivyo hawa mawakili walipaswa kila mwaka kutoa hesabu na faida kwa wamiliki wa mashamba yale na wao walibaki na ile ziada kama sehemu ya ujira wao.

Kwa ujanja wao mara nyingi hawa mawakili walitoa hesabu za uongo iwe kwa wamiliki wa mashamba lakini zaidi sana kwa kutoa ujira mdogo kwa maskini waliotumika kama vibarua wa mashamba yale. Hivyo waliweza kufanya ujanja au wizi iwe kwa matajiri wamiliki wa mashamba lakini pia hata kwa watu maskini waliotumika kuzalisha kwa ujira mdogo sana kama ambavyo tumesikia katika somo la kwanza la leo kutoka Nabii Amosi, nabii na mtetezi wa haki ya wanyonge. Hivyo yafaa kusoma Injili yetu ya leo kwa kurejea muktadha wa nyakati zile za Yesu ambazo pia si tofauti sana na hata nyakati zetu za leo. Wakili sio mmiliki bali kuna mwenye shamba, na hivyo anatuhumiwa kwa matumizi mabaya ya mali za mmiliki. Na hata wakili tunaona katika tafakari yake anajiuliza maswali mengi kichwani na moyoni mwake. Ni mmoja anayekubali makosa yake na hivyo mara moja kufikiri nini atafanya akiwa hana tena kazi ile ya kuwa mwangalizi au wakili wa shamba.

Nifanye nini? Ni swali la msingi na zuri tunalokutana nalo mara kadhaa katika Injili ya Luka na Kitabu cha Matendo ya Mitume. Makutano, watoza ushuru, maaskari wanamuuliza Yohane Mbatizaji tufanye nini?  Mkulima tajiri tuliyemsikia Dominika kadhaa zilizopita naye baada ya mavuno mengi anajiuliza nifanye nini? (Luka 12:17) Na hata wasikiliza wa Mtume Petro siku ile ya Pentekoste wanajiuliza, ndugu tufanye nini? Ni swali la msingi sana kila mara unapojikuta mbele ya uchaguzi wa maisha. Wakili asiye mwaminifu anajua kuwa hana muda mrefu kabla ya kuachishwa kazi yake. Kama mkulima tajiri aliyetafakari moyoni mwaka afanye nini kuhusu mavuno yake mengi ndivyo hivyo naye anatafakari moyoni mwake la kufanya baada ya kufukuzwa kazi.  Yeye anajua kufanya kazi hiyo na hivyo anatambua udhaifu wake kuwa hawezi kulima na hata kuombaomba anaona aibu.

Mara moja linakuja kichwani mwake wazo, anatambua nini cha kufanya kwani kabla ya kuacha kazi hana budi kufunga na kukabidhi mahesabu kwa mmiliki wa shamba lile na hivyo anawaita wadeni wake wote.  Wakili huyu mjanja hakuomba ushauri kwa mtu yeyote au wale waliokuwa wanafanyakazi kama yake na badala yake anang’amua yeye mwenyewe nini cha kufanya katika hali ile, ni matokeo ya tafakari yake na hasa kuzingatia uzoefu wa ile kazi yake. Anatambua jinsi gani aliweza kukosa uaminifu kwa wadeni wake kama nilivyotangulia kusema kuwa mara nyingi waliwapa mahesabu ya uongo iwe kwa wadeni lakini pia hata kwa wamiliki wa mashamba yale. Angeliweza kwa hakika kujipatia tena mali kwa njia ile ile ya uongo na wizi lakini safari hii hachagui kuwaibia zaidi mali bali kujenga nao urafiki! Ni uchaguzi wa urafiki na si wa mali! Ni uamuzi sahihi ambao Yesu anausifu na ndio uamuzi tunaopaswa kuufanya kila mmoja wetu, kutumikia na kujenga urafiki na wale wote tunaokutana nao katika maisha ili kujiwekea akiba ya kudumu na si mali za ulimwengu huu ambazo zote ni za kupita na za muda tu. Urafiki wa upendo ni thamani na mali ya milele.

Hivyo wadeni hawa kwa hakika hawatamsahau kamwe wakili yule mjanja kwa jinsi alivyowafanyia wema na ukarimu na urafiki. Yesu anausifu uamuzi wake wa kuunda urafiki na watu na si na mali. Ni vema kujiuliza sisi mara nyingi tunajali watu au mali/vitu/ pesa na hata kuna wakati tunafikia kuvipa nafasi ya kwanza bila kujali wengine. Labda sisi tulitegemea hitimisho tofauti la Yesu kumkaripia na kumuonya vikali wakili yule mjanja kwa kukosa kuwa mwaminifu kwa bwana wake na wadeni wake. Tulitarajia kumsikia Yesu pia akituonya nasi kutokufuata mfano wa wakili yule. Yafaa pia tukumbuke kuwa hasifu kwa kukosa kuwa mwaminifu bali anasifu ujanja wake, kwa jinsi anavyofanya uchaguzi ulio sahihi wa kujenga urafiki na watu na si na mali kama nilivyosema angeweza kufanya ujanja wa kujilimbikiza mali kwa njia ya wizi na uongo bali kinyume chake anaamua kufanya ujanja wa kujenga urafiki. Na si tu Yesu anayemsifu wakili yule mjanja bali hata mmiliki wa shamba na ndio kusema hakuwa ameibiwa chochote kwani kama nilivyotangulia kusema daima walionufaika kwa njia zisizo za haki hawakuwa tu mawakili au waangalizi wa mashamba yale bali zaidi sana matajiri wamiliki wa ardhi ile waliokuwa wanaishi mijini na kusubiri tu kuvuna kile ambacho hawakukitolea jasho.

Ilikuwa ni dhuluma na wizi na uonevu iwe kwa waangalizi na hata pia wamiliki wa mashamba. Sehemu ya Injili ya leo inahitimishwa na misemo maarufu ya Yesu yote ikiwa na lengo la kutusaidia kupata ujumbe wa Yesu katika Dominika ya leo. Sisi sote hatuna budi kutambua kuwa kila tulichonacho si mali yetu bali tumewekwa kuwa waangalizi au mawakili tu hivyo hatuna budi kutumia daima kwa kuwatumikia na kujenga urafiki na wengine. Hatuna budi kuwa mawakili waaminifu na kutumia yote si kwa ubinafsi bali tukikumbuka umuhimu na ulazima wa kujenga urafiki ili tuweze kuja kukaribishwa nao si tu katika ulimwengu huu bali katika maisha ya umilele. Uhakika wa maisha yetu haupo katika mali bali katika upendo kwa wengine, ni upendo unaodumu na kubaki milele. Mali, vitu, pesa na vyote tunavyokuwa navyo hatuna budi kuvitumia kwa upendo ili tubaki na mali ya milele yaani upendo. Vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu nasi ni waangalizi tu na hivyo hatuna budi kutumia vyote tulivyonavyo kwa kujenga urafiki na si kinyume chake. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

21 September 2019, 11:53