Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIII ya Mwaka C wa Kanisa: Masharti ya Kumfuasa Kristo Yesu: Kuchukia, Kubeba Msalaba & Kutojishikamanisha na malimwengu. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili XXIII ya Mwaka C wa Kanisa: Masharti ya Kumfuasa Kristo Yesu: Kuchukia, Kubeba Msalaba & Kutojishikamanisha na malimwengu. 

Tafakari Jumapili 23 ya Mwaka: Gharama ya ufuasi! Yataka moyo!

Ni katika kupenda bila kujibakiza hapo tunaweza kufikia hatua hata ya kutoa maisha yetu kwa ajili ya Mungu na jirani, ni hapa ndio Msalaba unapata maana kwenye maisha yetu ikiwa tu ni matokeo ya upendo na si kinyume chake. Msalaba kama matunda ya upendo ndio unakuwa ishara ya uzima. Msalaba ni ishara ya ushindi ukiwa ni matunda ya upendo wetu kwa Mungu na jirani. Msalaba!

Na Padre Gaston George Mkude- Roma

Amani na Salama! Msalaba hauna budi kuwa ni matokeo ya upendo wetu kwa mungu na jirani. Kwa nini Msalaba katika maisha ya mkristo; Kwa nini mateso na hata kifo? Ni maswali yanayotusumbua katika tafakari ya ufuasi wetu kwa Kristo. Ni maswali yasiyokuwa na majibu mepesi. Mkristo sio yule anayetafuta mateso na Msalaba maana hata Kristo mwenyewe hakutafuta mateso na Msalaba maana wito wetu wa msingi ni upendo. Ni katika kupenda bila kujibakiza hapo tunaweza kufikia hatua hata ya kutoa maisha yetu kwa ajili ya Mungu na jirani, ni hapa ndio Msalaba unapata maana kwenye maisha yetu ikiwa tu ni matokeo ya upendo na si kinyume chake.  Msalaba kama matunda ya upendo ndio unakuwa ishara ya uzima. Msalaba ni ishara ya ushindi ukiwa ni matunda ya upendo wetu kwa Mungu na jirani. Ushindi wetu ni katika kupenda ikibidi hata kutoa maisha yetu kama rafiki zake Yesu Kristo.

Mpaka karne ya tatu ishara ya Ukristo ilikuwa ni picha ya mvuvi na samaki na kamwe haikuwa Msalaba kama leo hii.  Ni kuanzia karne ya nne baada ya Mt. Helena aliyekuwa Mama wa Konstantino ndio msalaba ukaanza kutumika kama ishara ya ushindi. Hivyo kwa kuchagua msalaba, hapo unachagua maisha, ingawa bado si rahisi kueleweka kirahisi hata leo katika nyakati zetu tunapojaribu kuelezea Teolojia ya msalaba. Msalaba unapata maana tu ikiwa tunauangalia kama matokeo ya upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Dominika iliyopita tuliona Yesu akiwa mezani katika nyumba ya mmoja wa wakuu wa mafarisayo, na leo tunaona yupo njiani akiwa na makutano. Yupo njiani kuelekea Yerusalemu, mahali ambapo atahukumiwa kifo, kuteseka, kufa na siku ya tatu kufufuka.

Ni safari yake ya mwisho akiwa ulimwenguni baada ya kumaliza kazi yake ya kueneza Ufalme wa Mungu hapa duniani. Ni safari ambayo hata wale rafiki zake wa karibu yaani mitume walikuwa bado hawajaelewa mustakabali wa Bwana na Mwalimu wao. Mitume kwao ushindi ni kuona Bwana na Mwalimu wao anakuwa mtawala kama watawala wa ulimwengu huu na sio kuteseka na kufa kwa aibu pale msalabani na siku ya tatu kufufuka. Hilo lilikuwa ni jambo gumu si tu kueleweka bali hata kufikirika katika vichwa vyao. Ni katika mazingira haya Yesu anaona bado wafuasi wake hawajaelewa nini maana ya kuwa mfuasi. Anawageukia na kuanza kuwapa katekesi ya kina ya nini maana ya kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, anatugeukia nasi leo katika Dominika hii ya leo ili tuweze kuelewa nini maana ya kuwa wafuasi wake. Yesu leo anatupa masharti matatu magumu ya kuwa wafuasi wake. Yesu anatueleza kinagaubaga bila kuupaka ukweli sukari maana ya kuwa mfuasi na hata hatari tutakazi kutana nazo katika safari yetu ya ufuasi.

Kuchukia ndio kumpa Yesu nafasi anayostahili katika maisha yetu. Yesu leo anatualika kuchukia (Neno la Kigiriki ni mizein) ni kinyume na kawaida yake kwani daima anatualika kupenda, sasa inawezekanaje leo anatualika kuchukia baba, mama, mke, watoto, kaka, dada, na hata sisi wenyewe ili tuweze kuwa wafuasi wake. Yesu kila mara anapotualika kutafakari juu ya ufuasi wetu anatumia lugha ngumu na kali kwa nia moja tu hivyo tangu awali hatuna budi kufanya maamuzi ya dhati na magumu ili kuwa wafuasi wake. Ni Yesu anayetutaka tufanye maamuzi magumu, kubadili namna zetu za kufikiri na kutenda, ni kukubali kuongozwa sio na mantiki ya ulimwengu huu bali ile ya Kimungu, ni kuwa na hekima na busara ya Mungu mwenyewe. Yesu hatuambii leo tusiwapende au tuwapende kidogo walio wa familia zetu au jamaa na marafiki zetu, hapana.

Kusema hatuna budi kuchukia sio mwaliko wa kutokuwapenda au kuwapenda kidogo bali ni kubadili vichwa vyetu na kuanza kuongozwa na Injili, kuwa na mtazamo mpya na hivyo kutoa nafasi sahihi kwa wazazi, mke, watoto au ndugu na hata nafasi yetu sisi wenyewe kama kweli tunahitaji kuwa wafuasi kweli wa Yesu Kristo. Kuchukia ni kututaka tuwe tayari kuvunja hata mahusiano yetu ya karibu ikiwa yanatuweka mbali na Injili na wito wake Yesu Kristo. Ni kumpa nafasi ya kwanza Yesu Kristo na Injili yake katika maisha yetu ya siku kwa siku. Ni kwa kufanya hivyo hapo kweli tunakuwa na upendo wa kweli kwa Bwana tunayemfuata katika maisha yetu. Kubeba msalaba ni matokeo ya upendo wa kweli. Sharti la pili ndio kubeba msalaba wetu na kumfuasa.  Ni mwaliko si tu wa kukubali kuteseka na kusetwa kwa ajili ya Injili bali ni maisha ya kuwa tayari kuwa mashahidi wa upendo wa Mungu katika maisha yetu, tunateseka na kutaabika kwa sababu moja tu yaani upendo wa Bwana wetu Yesu Kristo na Injili yake.

Lazima kuketi na kujitathmini kabla ya kumfuasa Kristo. Kwa hakika, Yesu pia anatumia fursa hii ya leo kutupa mifano miwili ndio ule wa mkulima anayejenga mnara shambani kwake kwa sababu kubwa ya ulinzi dhidi ya wevi na wanyama waharibifu. Anayeketi kwanza kabla ya kuujenga kuona kama ana pesa na uwezo wa kuukamilisha na ndivyo tufanyavyo kila mara kabla ya kuanza mradi mkubwa katika maisha yetu, lazima kufanya tathmini ya kina kuona kama tunaweza kufikia malengo. Ni mwaliko pia hata katika maisha ya ufuasi kuketi na kujitafakari kabla ya kuanza kumfuasa Yesu Kristo. Ni mwaliko kwa kila mbatizwa na si tu kwa wale wanaoitwa kwa maisha ya wakfu kama mapadre na watawa, kila mmoja wetu hana budi kuketi na kujitathmini katika kumfuasa Yesu Kristo.

Mfano wa pili ndiye mfalme anayeketi na kujitathmini kabla ya kwenda vitani. Maisha ya ufuasi ni vita dhidi ya yule mwovu shetani hivyo hatuna budi kuketi kila mara na kujitathmini kabla ya kwenda vitani. Hivyo maisha ya ufuasi ni maisha ya kufanya maamuzi magumu, huo ndio wito wetu anaotualika Yesu kuutafakari katika Dominika ya leo, si kwamba Yesu anataka kutuvunja mioyo la hasha bali kutuweka wazi tangu mwanzo kuwa maisha ya ufuasi hayana budi kuwa ni matokeo ya maamuzi magumu na ya dhati kabisa ya kila mmoja wetu. Ni wito wa maisha wenye magumu na changamoto zake na hivyo hatuna budi tangu mwanzoni kufanya maamuzi ya dhati.

Lazima kuacha yote ili kumfuasa kweli yesu Kristo Yesu. Sharti la tatu na labda ni gumu kuliko yote ndio kutojishikamanisha na mali au vitu ili kuwa wafuasi wake. Yesu hasemi kuwa tutoe msaada wa pesa kidogo bali yote tuliyo nayo, eeeh sio mchezo ni hitaji gumu na zito. Wengi leo hii wanapenda kuona mwaliko huu ni kwa wachache tu hasa wale wanaoamua kujitoa kwa maisha ya wakfu ila naomba niseme ni mwaliko kwa kila mmoja. Ni mwaliko kama nilivyosema hapo juu wa kubadili vichwa vyetu kwa maana ya kuipa pesa na mali nafasi stahiki na sio kuchukua nafasi ya kwanza ile ya Mungu na Neno lake katika maisha yetu. Yafaa kila mmoja kuketi na kujiuliza katika maisha yangu ni nini kinakuja kwa nafasi ya kwanza, moyo wangu upo katika mali au katika kumpenda Mungu na Neno lake? Nawatakia Dominika na tafakari njema.


11 September 2019, 18:07