Tafakari Jumapili 24 ya Mwaka: Dhambi: Huruma na Upendo
Na Padre Gaston George Mkude, - Roma
Amani na Salama! Injili ya leo inatuonesha Huruma na Wema wa Mungu kwetu wadhambi na wakosefu lakini zaidi sana furaha kubwa ya Mungu kwa kila mdhambi anapofanya toba na kurudi katika njia ya haki. Injili ya Luka ni Injili ya Huruma ya Mungu kwani inatuonesha sura halisi ya Mungu. Mifano anayotumia Yesu leo inatualika na kutusaidia hasa kuweza kuelewa Sura ya Mungu. Mwinjili Luka anamuonesha Mungu si tu Baba Mwema anayetuhurumia na kutusamehe dhambi na makosa yetu bali anayetutafuta bila kuchoka kila mara tunapopotea katika dhambi mpaka atupate na hapo anakuwa na furaha kubwa. Si kwamba sisi tunamtafuta Mungu bali Mungu anatutafuta sisi kwanza tunaokuwa gizani kwa kutuangazia mwanga wa huruma yake na pia kututoa katika wimbi la uchafu na ubaya wa dhambi. Tunaona leo mifano miwili ya kwanza au ya somo fupi la Injili ya leo ikimuonesha Mungu anayetutafuta kama kondoo aliyepotea na ile shilingi iliyopotea.
Na hata katika mfano wa Mwana mpotevu ambao kwa leo sitauongelea, tunaona Mungu anaharakisha na kumkimbilia mwana anayerudi nyumbani na hivyo baba yake kumfanyia karamu kubwa. Injili ya Baba Mwenye Huruma au kama wengine wanavyopenda kuiita ya Mwana Mpotevu tuliitafakari vema Dominika ya 4 ya Kwaresima mwaka 2019, hivyo leo naomba tubaki kutafakari zaidi mifano miwili kama nilivyogusia hapo juu, yaani ya kondoo aliyepotea na Mwanzoni tunaposoma vema Injili ya leo tunabaki na mshangao. Pamoja na kwamba Mwinjili Luka anatuonesha watoza ushuru na wenye dhambi walimkaribia Yesu ili kumsikiliza, mara moja anatuonesha kulikuwepo pia waandishi na mafarisayo walionung’unika kumuona Yesu akila na kunywa na wadhambi. Na hivyo Yesu kwa mifano hii ya leo hadhira au walengwa wa mifano hiyo sio wadhambi bali wale watu waliojihesabia haki na hivyo kidini na kijamii walionekana ni watu safi au wema wasio na madhambi.
Kilichowasumbua Waandishi na Mafarisayo ni jinsi Yesu alivyokuwa rafiki wa wadhambi na watoza ushuru. Yesu hakuwahubiria hawa wadhambi waache dhambi zao? Yesu anawapokea na kula na kunywa nao, ni nini maana yake? Hayo ni maswali waliokuwa nayo mafarisayo na waandishi kwani hata nao walimtambua Yesu na kumuona kama mtu wa Mungu, kwa nini basi hafanyi kitu kuwabadili hawa walioonekana wadhambi na wakosefu? Yesu leo anatoa mifano mitatu kama jibu la maswali ya mafarisayo, ni mwito wake kwa mafarisayo kubadili vichwa na mitazamo yao. Hata nasi leo tunaalikwa pia kubadili mitazamo yetu. Wadhambi ndio wanafananishwa na kondoo aliyepotea au shilingi iliyopotea, lakini cha kushangaza leo wapo ndani pamoja na Yesu wakila na kunywa na kinyume chake wanaobaki nje ni waandishi na mafarisayo waliokuwa ni watu wa haki. Ndio kusema bila kubadili vichwa na mitazamo yetu tunajikuta ni sisi tunaobaki nje na kukosa kushiriki karamu na furaha pamoja na Mungu mwenye huruma.
Hatuna budi kwenda kwake si kama wenye haki bali daima kama wadhambi na wakosefu kama Mtume Paolo anayeshukuru wema na huruma ya Mungu kwake. Kila mara Yesu anatumia mifano iliyokuwa inaakisi maisha yao ya kila siku. Wayahudi kama wachungaji basi mfano wa kondoo aliyepotea ni mfano unaopokelewa na kueleweka kirahisi. Hivyo katika Biblia mara nyingi mfano wa Mungu kama mchungaji na taifa lake kama kondoo unatumika mara nyingi. (Zaburi 23; Isaya 40:11) Na hata Yesu anatumia pia lugha hiyo ya kondoo na wachungaji mara kadhaa katika Agano Jipya. (Marko 6:34) Mifano ya Yesu ya leo tunapotafakari tunakutana na ukosefu wa mantiki iliyo sahihi. Mchungaji anayeacha kondoo tisini na tisa na kwenda kumtafuta moja aliyepotea na kisha kurudi kwa furaha na kupita nyumba kwa nyumba akialika marafiki na majirani kufanya sherehe kwa kumpata kondoo huyo mmoja. Kila tunapojaribu kulinganisha thamani ya huyu kondoo na hiyo sherehe au karamu inayoandaliwa tunakosa uwiano wa mantiki na hata uhalisia. Na hata mfano wa Yesu tunaona anatoa nafasi kubwa kuzungumzia juu ya furaha na karamu kuliko hata ukweli wa kondoo mwenyewe aliyepatikana.
Ni katika muktadha huu tunapata ujumbe wa Injili ya Dominika ya leo. Yesu anatuonesha jinsi gani Mungu anafuraha kwa kila mdhambi anapotubu na kuanza maisha mapya. Furaha ya Mungu ni kubwa hivi hata kualika wengine wote washiriki katika furaha hiyo. Ni furaha isiyoelezeka kwa kila mdhambi kurudi nyumbani kwa Mungu, kuanza tena maisha ya mahusiano ya Baba na mwana. Ni furaha inayoonesha thamani ya mwanadamu, kila mmoja wetu mbele ya Mungu ni wa thamani kubwa hivi hata sisi wenyewe hatuwezi kuielezea. Ni kana kwamba ni mimi tu, au ni wewe tu tunaoishi katika sura ya dunia, sisi ni wa thamani kubwa mbele ya Mungu, kila mmoja wetu ni yule kondoo aliyepotea awali na kupatikana kwa neema na huruma ya Mungu. Huruma na upendo wa Mungu sio kwa wale wanaostahili bali kwa wanaokuwa ni wahitaji wa huruma na upendo wake usio na mipaka wala kipimo. Kwa asili Mungu ni upendo wenyewe, hivyo udhaifu na unyonge wake ni upendo maana Mungu hajui kuchukia wala kuangamiza bali daima anatupenda hata tukiwa wadhambi na wakosefu kiasi gani.
Naomba kusisitiza hili maana kinyume chake ni kufanya kufuru, ni kukosea kuitambua sura ya Mungu. Mifano ya Injili ya leo ni katekesi nzuri na rahisi inayoonesha Sura halisi ya Mungu. Kinyume chake ni kufanya uzushi na kufuru.Kinyume chake tunabaki kuwa na sura isiyo sahihi ya Mungu na hivyo kujikuta tunajiweka nje na kukosa kushiriki furaha na sherehe ya kupokea huruma na upendo wa Mungu kama anavyosema Mtume Paolo katika somo la pili la Dominika ya leo. Marabi walirudiarudia kwa desturi mafundisho yao ili yaweze kueleweka vyema kwa wanafunzi wao na ndio pedagojia anayotumia Yesu pia katika mifano hii ya Huruma ya Mungu, na si kwa makosa Mwinjili Luka anatuonesha pia ni kwa jinsi gani Yesu alitaka fundisho hili lieleweke vema na kwa uwazi juu ya Uso halisi wa Mungu, ni Huruma na Upendo usiokifani, usioelezeka na hata kueleweka kwa mantiki zetu za kibinadamu.
Mfano wa pili ni wa shilingi iliyopotea katika nyumba. Tunaona mwanamke akifanya kila juhudi na bidii ili kuipata pesa ile iliyopotea. Ndio kusema jinsi gani Mungu hawezi kutulia tunapokuwa mbali naye, tunapokuwa tumepotea maanake mbali na macho yake yenye huruma na upendo. Tumeumbwa kukaa na kubaki sote mbele ya macho ya Mungu na si kinyume chake. Mungu anatutafuta tena kwa bidii na uvumilifu mkubwa, anatusubiri kila mmoja wetu kurejea na kubaki katika mahusiano ya upendo naye. Sisi sote ni wadhambi na hivyo tunahitaji huruma na upendo wake ili tuweze kushiriki katika ile furaha na sherehe ya milele. Nawatakia Dominika na tafakari njema.